Thursday, October 19, 2017

UJUMBE WA OMAN WAFIKA BAGAMOYO LEO TAREHE 19 OKTOBA 2017



Waziri wa Mafuta na Gesi kutoka Serikali ya Oman Dkt. Mohamed Bin Hamad Al–Rumhi akitazama jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo wakati wa ziara yake wilayani Bagamoyo leo. 

Waziri huyo ametembelea maeneo ya uwekezaji ya  Mamlaka ya Maeneo ya Uwekezaji Kiuchumi (EPZA), maeneo ya Kihistoria la Kaole na eneo itakapojengwa Bandari, Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo na kulia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stellah Manyanya, nyuma ya Naibu waziri Viwanda ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga.

Waziri wa Mafuta na Gesi kutoka Serikali ya Oman Dkt. Mohamed Bin Hamad Al–Rumh akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maeneo ya Uwekezaji Kiuchumi (EPZA) Kapteni George Simbakalia alipokuwa katika ziara ya kutembelea maeneo ya uwekezaji wilayani Bagamoyo leo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.


Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stellah Manyanya akipokea zawadi toka kwa Waziri wa Mafuta na Gesi wa Serikali ya Oman Dkt. Mohamed Bin Hamed Al–Rumhi wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya uwekezaji wilayani Bagamoyo leo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaj Majjid Hemed.

 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, akipokea zawadi kutoka kwa Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy leo Tarehe 19 oktoba alipotembelea eneo linalotarajiwa kujengwa Bandari Bagamoyo.
Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy (kulia) akimkabidhi zawadi Mkuu wa chuo cha Wakala wa Mafunzo na Elimu ya Uvuvi Mbegani (FETA) Yahya Mgawe, alipotembelea Mbegani Bagamoyo leo katika eneo ambalo litajengwa Bandari ya Bagamoyo, wanaoshuhudia kutoka kushoto ni wa Tanzania nchini Oman Abdallaah kilima na wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo.

Kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, Waziri wa Mafuta na Gesi kutoka Serikali ya Oman Dkt. Mohamed Bin Hamad Al–Rumhy, Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Ali A. Al Mahruqi na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaj Majjid Hemed wakimsikiliza mhifadhi ya makumbusho ya Kaole Bagamoyo walipotembelea eneo hilo leo Tarehe 19 Oktoba 2017.


MAREHEMU SHEIKH MKANGAMBE ATAKUMBUKWA KWA MCHANGO WAKE KATIKA JAMII.



WASIFU WA MAREHEMU SHEIKH ABDALLAH SALUM ALLY MKANGAMBE
KUZALIWA KWAKE.

AMEZALIWA MWAKA 1969 KATIKA KATA YA MWEMBESONGO AKIWA MTOTO WA TATU WA MZEE SALUM MKNGAMBE NA MTOTO PEKEE KWA UPANDE WA MAMA YAKE.

ELIMU YAKE;
SHEIKH ABDALLAH SALUM ALLI MKANGAMBE ALIANZA ELIMU YAKE YA MSINGI KATIKA SHULE YA MTAWALA ILIYOPO MANISPAA YA MOROGORO KUANZIA MWAKA 1978-1984.

AIDHA MWAKA HUOHUO SHEIKH MKANGAMBE AKIWA KIJANA WA MIAKA TISA, ALIANZISHWA ELIMU YA AWALI YA DINI YA KIISLAMU KATIKA ENEO LA MAGUBIKE WILKAYANI KILOSA.

MNAMO MWAKA 1981 ALIANZA RASMI MASOMO YA QUR’AN KWENYE AMANI MADRSA ILIYOKUWA CHINI YA MAREHEMU SHEIKH SAID MUSSA KARIYAT.

SEPTEMBA 27/1985 ALIKWENDA DAR ES SALAAM NA KUJIUNGA NA CHUO CHA MARKAZ MNAMO OKTOBA 1985-1990.

MWAKA 1990 BAADA YA KUFAULU MITIHANI YAKE YA MWISHO, ALIFANIKIWA KUWA MIONGONI MWA WATANZANIA WANNE WALIOPATA NAFASI YA KWENDA NCHINI MISRI KUENDELEA NA MASOMO YA JUU KATIKA CHUO KIKUU CHA AZIHAR-SHARIIF.

OKTOBA 1990-1993 MASOMO YA SEKONDARI (THANAWIY) ALEXANDRIYA, MISRI NA KUFAULU VIZURI.

OKTOBA 1993-1997 ELIMU YA CHUO KIKUU KITIVO CHA SHERIA, CHUO CHA AZHAR-SHARIF KAIRO, MISRI.

KAZI ZAKE;
MWAKA 1984-1985 MWALIMU MADRASA YA AMANI NA UHURU
MWAKA 1997-1998 MAREHEMU SHEIKH MKANGAMBE BAADA YA KUREJEA MASOMONI, ALIANZA KUFUNDISHA CHUO CHA AMANI KILICHOANZISHWA NA SHEIKH WAZIRI MADUGA MWAKA 1996.

MWAKA 1998 MWALIMU WA DINI SHULE YA SEKONDARI JABAL-HIRAH, MOROGORO.

JANUARI 1999 ALIAJIRIWA NA AFRICAN MUSLIM AGENCY NA KUWA MWALIMU WA NIDHAMU (DISCPLINE MASTER) KATIKA SHULE YA SEKONDARI YA KIISLAMU YA WASICHANA YA ATTAWN, MOROGORO.

MWAKA 2009-2010 ALIPANDISHWA DARAJA NA KUWA MKUU WA SHULE YA SEKONDARI YA KIISLAMU YA ATTAUUN.

MWAKA 2011-2012 ALIKUWA MKUU WA SHULE MPYA YA SEKONDARI YA AL SAFFAH YA MJINI MTWARA ILIYOKUWA CHINI YA AFRICAN MUSLIM AGENCY .

MWAKA 2012 ALIREJEA MOROGORO NA KUENDELEA NA KAZI YAKE YA UWALIMU KATIKA SHULE YA SEKONDARI YA ATTAWN KAMA MWALIMU WA NIDHAMU KABLA MWAKA 2013 KUTAKIWA TENA MTWARA AL SAFFAH SEKONDARI KUWA MKUU WA SHULE.

DESEMBA 2013 SHEIKH MKANGAMBE ALIACHA KAZI NA KURUDI MOROGORO NA KUWA MWALIMU MKUU MSAIDIZI KATIKA SHULE YA MSINGI YA KIISLAMU YA AL-HAQABA ILIYOPO MAFISA.

MPAKA MAREHEMU ANAFIKWA NA UMAUTI ALIKUWA MKUU WA IDARA YA ELIMU YA DINI YA KIISLAMU KATIKA SHULE YA SEKONDARI YA JABAL-HIRRAH.

UZOEFU KATIKA UONGOZI;
MWAKA 2005-2010 SHEIKH ABDALLAH SALUM MKANGAMBE ALICHAGULIWA KUWA MJUMBE WA BARAZA LA MASHEIKH MKOA WA MOROGORO.

MWAKA 2010-2015 SHEIKH ALICHAGULIWA KUWA MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA BAKWATA MKOA WA MOROGORO
NA KUANZIA MACHI 27, 2016-OKTOBA 17, 2017 ALIKUWA AKIHUDUMU KATIKA NAFASI YA SHEIKH WA MKOA WA MOROGORO, MJUMBE WA KAMATI YA AMANI NA MJUMBE WA KAMATI YA USHAURI YA SHULE YA SEKONDARI YA JABAL-HIRRAH.

TANGU ACHAGULIWE KUSHIKA NAFASI YA SHEIKH WA MKOA WA MOROGORO MWEZI MACHI, 2016, MAREHEMU SHEIKH MKANGAMBE ALIKUWA MHAMASISHAJI MKUBWA WA WAISLAMU KUMILIKI ARDHI KWA AJILI YA MAENDELEO YAO.

LAKINI PIA NI KIONGOZI PEKEE AMBAE ALIWEZA KUTEMBELEA WILAYA ZOTE ZA MKOA WA MOROGORO NA BAADHI YA VIJIJI VYAKE KATIKA KIPINDI KIFUPI CHA UONGOZI WAKE.

AIDHA KUTOKA MWAKA 2005 MPAKA MUDA MFUPI KABLA YA UMAUTI WAKE, MAREHEMU SHEIKH MKANGAMBE ALIKUWA KIONGOZI MKUU WA UMOJA WA VIJANA WA KIISLAMU MKOANI MOROGORO.

MAREHEMU PIA KWA MIAKA MINGI ALIKUWA AMEJITOLEA KUFUNDISHA ELIMU YA DINI KATIKA MADRASA MBALIMBALI ZA MJINI MOROGORO PAMOJA NA KUTUMIA VITUO VYA HABARI KAMA VILE RADIO MUM NA IMAAN MEDIA KUFIKISHA UJUMBE KWA JAMII.

TUNAMUOMBA MWENYEZIMUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU SHEIKH ABDALLAH SALUM ALLI MKANGAMBE MAHALA PEMA PEPON. AAMIN!
SISI SOTE NI WA MWENYEZIMUNGU NA KWAKE TUTAREJEA.

IMEANDALIWA NA RASHID MTAGALUKA
 ...........................................................
RATIBA YA MAZISHI YA MAREHEMU MKANGAMBE.

TAARIFA  ILIYOTOLEWA JANA NA MSEMAJI WA MUFTI WA TANZANIA
IMESEMA MAREHEMU SHEIKH ABDALLAH SALIM  MKANGAMBE ATAZIKWA LEO ALHAMISI TAREHE 19 OKTOBA 2017.SAA SABA MCHANA NYUMBANI  KWA  MAREHEMU MOROGORO  

MAGAZETI YALEO TAREHE 19 OKTOBA 2017.

OMAN YAAHIDI MAKUBWA KWA TANZANIA.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam jana Oktoba 18, 2017
....................

Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza uchumi kwa kasi zaidi.

Ujumbe huu wa Mfalme wa Oman umewasilishwa kwa Mhe. Rais Magufuli na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al Rumhy aliyeongozana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben Nasser Al Ismaily na Naibu Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Rumhy ambaye ameongoza watu zaidi 300 waliokuja nchini kwa meli ya Mfalme wa Oman amesema ziara hii imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman hususani katika masuala ya uchumi, ambapo Oman inabadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi, itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, itajenga viwanda vya mazao na kununua mazao ya wakulima na itawekeza katika uchakataji wa madini ili kuongeza thamani.

“Mhe. Rais tunataka kushirikiana nanyi kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, tunataka Bagamoyo isiwe eneo la bandari tu, bali pia liwe ni eneo ambalo tutajenga viwanda mbalimbali, tuzalishe mbolea na tununue mazao ya wakulima na kuyasafirisha, sisi tupo tayari na kesho tunakwenda kuangalia eneo hilo ili kazi zianze mara moja” amesema Dkt. Rumhy.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said kwa kutuma ujumbe huo na amemhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Oman.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Rumhy kufikisha ujumbe wake kwa Mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo unaanza mara moja na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Mhe. Dkt. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania, nimefurahi kuona mpo tayari kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.

Amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada kujenga visima vya maji 100 hapa nchini na amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Matogoro Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Alphonce Kolimba.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Oktoba, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsiliza Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy akiongea na wanahabari baada ya kukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam jana Oktoba 18, 2017