Wednesday, July 26, 2017

MBUNGE WA KIBAHA VIJIJINI ATOA MAGARI YA WAGNJWA JIMBONI KWAKE.

SAM_4784
MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa akikabidhi magari matatu ya wagonjwa (ambulance) ambayo yatasaidia kubeba wagonjwa katika jimbo la Kibaha Vijijini.
 ...............
MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa amekabidhi magari matatu ya wagonjwa (ambulance )ambayo yatasaidia kupunguza adha ya usafiri kwa wagonjwa hasa mahututi na warufaa.

Kati ya magari hayo ,mawili yametokana na nguvu zake na moja ni msaada kutoka kwa Rais John Magufuli ikiwa ni kati ya magari ya wagonjwa 67 yaliyogawanywa katika maeneo mbalimbali nchini .

Aidha mbunge huyo ,ameiomba wizara ya afya kukipandisha hadhi kituo cha afya cha Mlandizi kuwa hospitali ya wilaya ombi ambalo waziri wa afya,jinsia ,wazee na watoto Ummy Mwalimu amekubali ombi hilo .

Jumaa aliyasema hayo ,viwanja vya shule ya msingi Mtongani ,Mlandizi wakati Ummy Mwalimu alipokwenda kukabidhi magari hayo kwa niaba yake kwa halmashauri na mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha.

Alieleza ,ameamua kujikita kutatua kero zinazowakabili kwa kwenda sambamba na kauli mbiu yake ya  SISI KWANZA SERIKALI BAADAE .
“Ninamshukuru waziri Ummy kwa dhati ya moyo wangu kwa jitihada zake za kupigania gari moja kuletwa Kibaha Vijijini ,”
“Ni bahati kwetu kwani zilikuwa ambulance 67 ambapo 50 zilielekezwa mikoa ya kanda ya ziwa ambako idadi ya vifo vya mama wajawazito ni kubwa hivyo zilibaki 17 hivyo moja wapo ndio hiyo imekuja kwetu ” alisema Jumaa .

Alibainisha kuwa ,magari hayo ni sehemu ya kupunguza tatizo la usafiri linalokabili vituo na zahanati jimboni hapo .

Alisema ,serikali iangalie uwezekano wa kuwaongezea magari ya wagonjwa katika maeneo ya mbali kama Kwala na Magindu .

Hata hivyo Jumaa akizungumzia ombi la kituo cha afya Mlandizi kupandishwa hadhi ,alisema anaendelea kufanya jitihada za kutimiza vigezo vinavyotakiwa kupandishwa hadhi ikiwemo kujenga uzio .

Alimshukuru makamu wa rais kwa harakati zake za kuhakikisha juhudi hizo zinazaa matunda kwa kuwachangia mifuko ya saruji 500 ,waziri mkuu nae alichangia mifuko hiyo 150 .

Wadau wengine wamechangia kokoto tani 7 kwa sh. mil. 9.1, mchanga mil. 2.4 tofali sh. mil 8.4, nondo tani moja sh. mil. 3.6 na fedha zake mwenyewe na hadi sasa zimeshatumia sh .milioni 50 .

Jumaa aliwaomba wadau wa afya na serikali kuendelea kumuunga mkono ili tatizo hilo libakie historia.

Alichukua fursa hiyo pia ,kukabidhi vitanda 25 na mashuka 50 vilivyotolewa na Rais katika majimbo mbalimbali nchini .

Katika vitanda hivyo 20 ni vya kawaida na vitanda vitano ni kwa ajili ya kujifungulia .

Akikabidhi magari hayo ya wagonjwa ,waziri wa afya ,jinsia ,wazee na watototo Ummy alisema atachangia mifuko ya saruji 100 ili kuunga mkono ujenzi wa uzio.

“Nampongeza Jumaa na mmepata mbunge anaejua kujiongeza ,mtumieni ,mtieni nguvu kwa mambo anayowapigania ” alisema Ummy .

Alisema kutoka na ahadi walizowahi kutoa wakubwa wake kupandisha hadhi kituo hicho cha afya na kwa kuwa ni wakubwa wake amekubali ombi hilo .

Ummy alisema pia kuna fedha anaitegemea ambayo atawezesha kujenga wodi ya uzazi yenye sehemu mbili na maabara ya damu kwa lengo la kuboresha huduma za afya .

“Vigezo vikikamilika kwa namna hiii ,idadi ya watu wanaohudumiwa ,uzio ,idadi ya majengo na mengineyo naamini tutapata hospital ya wilaya iliyo nzuri na iliyokamilika ” alifafanua Ummy .

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Mansoor Kisebengo ,alisema watahakikisha wananchi hawagharamii mafuta kwa magari hayo .

Kisebengo alisema ,halmashauri hiyo itakuwa inachangia gharama za mahitaji ya mafuta ili kuondoa bugudha kwa wananchi .
SAM_4781

Tuesday, July 25, 2017

TCU YAFUTA UDAHILI KWA VYUO 19.

Tume ya Vyuo vikuu Tanzania (TCU) imevifutia udahili vyuo 19 na kufuta kozi 75 katika vyuo  22 kwa kukiuka Sheria taratibu na kanuni za utoaji wa elimu ya juu hapa nchini.

Akitoa ufafanuzi kuhusu Taarifa hiyo Jijini Dar es Salaam  Afisa habari wa Tume hiyo Bw. Edward Mkaku alisema uamuzi wa kuvifutia udahili baadhi ya vyuo ni kutekeleza agizo la serikali lililoitaka Tume hiyo kuvisimamia kwa karibu vyuo ili viweze kutoa elimu bora.

Bw.Makaku amesema kuwa kwa vyuo ambavyo wanafunzi wanaendelea na masomo mabadiliko haya hayatawahusu wanatakiwa kuendelea na masomo kama kawaida, ila vyuo hivyo  haviruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwa mwaka huu wa masomo 2017/2018.

Alizitaja baadhi ya sababu zilizopelekea baadhi ya vyuo kufutiwa udahili wa Shahada, Shahada za Uzamili pamoja na Shahada za Uzamivu kuwa ni kukosa vitendeakazi na wataalam katika kufundisha elimu ya juu.

Aidha Mkaku amesema kuwa TCU imeandaa maonesho yatakayoanza Julai 26, 2017 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam,maalum kwaajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi wanaohitaji kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini, pia kuelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume hiyo.
  
Bw.Mkaku pia amesema baadhi ya vyuo vinavyotoa taaluma za afya kama Kilimanjaro Chritiani medical College (KCMC) cha mkoani Kilimanjaro, Kampala International University (KIU) cha  Jijini Dar es Salaam pamoja na  Hubert Kairuki Memorial University (HKMU) pia cha Jijini  Dar es Salaam ambavyo vilikuwa vikitoa kozi za udaktari, ufamasia pamoja na shahada ya uzamili katika Udaktari wa magonjwa ya kinamama iliyokuwa ikitolewa na Chuo cha Hubert Kairuki  imebainika kuwa hawakuwa na vifaa na wataalam wa kutosha kufundisha kozi hizo.

Alivitaja vyuo  vilivyofungiwa kutokana na kutokuwa na wataalam wa kutosha kuendesha kozi zake kuwa ni, St. Joseph, St. John, Tumaini University pamoja na vyuo vingine kadhaa ambavyo havina waalimu pamoja na vifaa kwa mujibu wa maelekezo ya Tume hiyo.

Bw.Mkaku amebainisha kuwa katika vyuo 22 hapa nchni kuna zaidi ya kozi 75 ambazo hazitakiwi kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2017/2018 na kuwashauri watahiniwa wanaotarajia kujiunga na mwaka huu wa masomo kuingia katika tovuti rasmi za vyuo  ili kujua kozi ambazo zinatakiwa na kozi ambazo zimezuiliwa.

“Tulifanya uhakiki wa vyuo hapa nchni Septemba na oktoba 2016 na kubaini baadhi ya vyuo kutokukidhi mahitaji ya watahiniwa katika baadhi ya kozi kwa hiyo ni muhimu kutoa taarifa mapema kwa umma juu ya  mchakato huu” Alisema.

Katika kuondoa changamoto kwa watahiniwa wa miaka ijayo Mkaku amesema kuwa maonesho ya vyuo yatakuwa yanafanyika kikanda ili kutoa elimu kwa umma katika masuala mazima ya elimu ya juu.TCU ilikabidhi rasmi jukumu la udahili kwa vyuo husika Julai 20,2017 ili waendeshe wenyewe na wao watabaki kuwa wasimamizi wa Sheria na sera za vyuo vya elimu ya juu.

TCU wametoa onyo kwa vyuo vitakavyoendelea kudahili wanafunzi katika kozi zilizofutwa kuwa ni kinyume cha Sheria na wakibainika watashitakiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi na zile za vyuo vikuu.

UMMY -AAGIZA MGANGA MFAWIDHI WA KITUO CHA AFYA MLANDIZI ASIMAMISHWE KAZI

IMG-20170725-WA0076
Waziri wa afya ,jinsia,wazee na watoto Ummy Mwalimu ,akitembelea kituo cha afya Mlandizi ,wa kwanza kushoto ni mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi,dk.Mpola Tamambele,ambae amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi
....................

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

WAZIRI wa afya, jinsia ,wazee na watoto ,Ummy Mwalimu ,amemsimamisha kazi mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi,dk.Mpola Tamambele,kutokana na kushindwa kusimamia maelekezo ya serikali ya kuhakikisha mama mjamzito ,mtoto chini ya miaka mitano na mzee wanapata huduma bure .

Kutokana na kutokuwa na mamlaka ya moja kwa moja amemuagiza kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Beda Mmbaga kumsimamisha kazi mganga mfawidhi huyo mara moja wakati uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili zikiendelea .

Amemuelekeza kaimu mkurugenzi huyo pia kuwafuatilia watumishi wa afya kituoni hapo waliohusika kumuagiza mama aliyejifungua Salma Khalifan kwenda kununua vifaa vya kujifungulia vya sh.180,000 ili apate huduma .
Aliyasema hayo wakati alipokwenda kutembelea kituo cha afya Mlandizi ,kabla ya kukabidhiwa kwa magari ya wagonjwa matatu kutoka kwa mbunge wa jimbo hilo ,Hamoud Jumaa .

Waziri huyo alisema yeye hana mamlaka ya moja kwa moja kumsimamisha kazi mganga mfawidhi huyo hivyo anaiachia mamlaka husika isimamie jukumu hilo.
Alisema hatokubali kuona watumishi wachache kwenye vituo vya afya ,zahanati na hospitali wanachezea maagizo ya serikali.

Alifikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mama aliyejifungua ambae alisema amenunua vifaa vya kufanyiwa operesheni kwa gharama ya sh .180,000 .

Ummy alisema haiwezekani kuona mama wajawazito ,wanalipishwa hadi gloves na pamba ili kujifungua wakati serikali yao ilishasema watahudumiwa bure .

Alieleza kwamba ,kuanzia sasa waganga wakuu wa wilaya ,mikoa na watumishi wa afya wote nchini wahakikishe wanatimiza maelekezo ya serikali kuhudumia akinamama wajawazito na watoto ili kupunguza vifo vya uzazi .

Ummy alisema kuwa ,watumishi na wauguzi wengi wanajituma na kufanya kazi zao kifanisi ila wapo wachache ambao wanakwamisha juhudi hizo .

“Sitokubali mtumishi anakwenda kinyume na serikali ,rais wetu John Magufuli anasisimamia suala zima la kuboresha huduma za afya ,halafu akitokea mtu mmoja mzembe anatuchanganya kwakweli sitoweza kumfumbia macho “
“Wananchi wamekuwa waoga hata kuingia katika suala la bima ya afya kwa sababu ya mambo kama haya ,namsimamisha mganga mfawidhi huyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika .” alisema Ummy .

Mbali ya hayo Ummy alibainisha,bajeti ya dawa katika halmashauri ya  wilaya ya Kibaha imeongezeka ndani ya miaka miwili mfululizo kwenye uongozi wa serikali ya awamu ya tano .

Ummy alisema mwaka 2015/2016 bajeti ya madawa katika halmashauri hiyo ilikuwa mil.24 na 2017 ilifikia mil.70 na bajeti ya sasa 2017/2018 imefikia sh. mil.101 .

Kwa upande wake mama aliyejifungua kituoni hapo ,Salma Khalfani ,alimweleza Ummy kwamba aliandikiwa orodha ya dawa za kununua kwenye maduka ya dawa ya nje .

Alieleza ,alitakiwa kufanyiwa upasuaji na hivyo kutakiwa kununua madawa na vifaaa tiba ,pamba na gloves vya 180,000 akanunue ili aweze kujifungua .

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Mmbaga alisema maagizo aliyopewa na waziri ameyapokea na atayafanyia kazi .

Nae mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaaa alisema kumekuwa na malalamiko mengi juu ya wananchi hasa akinamama kulipishwa fedha za dawa na vifaa tiba .

Alisema baadhi ya wazee wamekuwa wakishindwa kupewa huduma za afya bila malipo .

Jumaa alimuomba Ummy kuendelea kushirikiana nae kuwadhibiti watumishi wazembe wanaodidimiza haki za wananchi .