Thursday, May 18, 2017

VIONGOZI UHAMIAJI WAPEWA SOMO.

A 5
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi  Mhe. Meja Jenerali Projest Rwegasira akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Makamishna wa Idara ya Uhamiaji(waliosimama). Wa pili toka kushoto ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala(wa pili toka kulia  ni Kamishna wa Uhamiaji – Zanzibar, Johari M. Sururu(wa kwanza kulia)ni Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda-TRITA, Kamishna Maurice Kitinusa(Picha zote na:- Kitengo cha Uhusiano Chuo Cha Uhamiaji cha Kikanda-TRITA Moshi, Kilimanjaro).
unnamed
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi  Mhe. Meja Jenerali Projest Rwegasira (Katikati) akiongoza Kikao kazi cha Viongozi Waandamizi wa Idara ya Uhamiaji (hawapo pichani). Wa pili kutoka kushoto ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala(wa pili  toka kulia) ni Kamishna wa Uhamiaji – Zanzibar, Johari M. Sururu(wa kwanza kulia) ni Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda-TRITA, Kamishna Maurice David Kitinusa(wa kwanza kushoto) ni Kamishna wa Utawala na Fedha, Edward P. Chogero.

 A 1
 Maafisa Waandamizi wa Uhamiaji wakifuatilia kwa makini hotuba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala(hayupo pichani)kwenye Kikao kazi hicho kama inavyooneka katika picha.
A 2
 Kamishna wa Pasipoti na Uraia, Gerald Kihinga akitoa ufafanuzi  katika Kikao kazi cha Viongozi Waandamizi wa Idara ya Uhamiaji mbele ya Katibu Mkuu Mhe. Meja Jenerali Projest Rwegasira (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni mjini Moshi.
 A 3
Kamishna wa Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, Samuel R. Magweiga akifafanua jambo kwa mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi  Mhe. Meja Jenerali Projest Rwegasira(hayupo pichani) katika kikao hicho.

MWENYEKITI WA CCM KIBITI AUWAWA KWA RISASI.

unnamed
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) Onesmo Lyanga, wa kushoto,akizungumza na waandishi wa Habari.
.......................


HALI ya sintofahamu bado inaendelea kutanda wilayani Kibiti ,mkoani Pwani ,baada ya kutokea mauaji mengine ya kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi ,ndani ya siku sita.

Kaimu mkuu wa wilaya ya Kibiti ,Juma Njwayo ,alieleza kwamba,mwenyekiti wa (CCM) tawi la Njia nne ,kijiji cha Muyuyu ,ambae pia ni mjumbe wa kamati ya siasa kata ya Mtunda ,Iddi Kilungi ,ameuawa kwa kupigwa risasi.

Aidha alisema , mtoto wa marehemu Nurdin Iddi Kilungi ,amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi ya tumbo na kutokea mgongoni.

Njwayo ,alieleza ,majeruhi alikimbizwa hospital ya mission ya Mchukwi  kwa ajili ya matibabu.

Alisema ,tukio hilo limetokea may 17 majira ya saa 1.40 usiku wakati marehemu akiwa amejipumzisha kimazungumzo nyumbani kwake .

Kaimu huyo  ambae pia ni mkuu wa wilaya ya Rufiji, Njwayo, alibainisha, watu wawili wanaodaiwa kuwa ni wauaji walifika eneo la nyumbani kwa Kilungi na kumpiga risasi na baadae kumpiga mwanae  kisha kutokomea kusikojulikana.

Alisema watu hao waliegesha pikipiki mbali ya nyumba na baada ya tukio walitokomea nayo .


Kwa mujibu wa Njwayo, amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti kumhamisha majeruhi (Nurdin Kilungi)kwenda hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi .

Alipoulizwa matukio hayo kuhusiana na masuala ya kisiasa alisema hawezi kulisemea moja kwa moja jambo hilo kwasasa.

“Siwezi kujua kama ndio chanzo ,mambo haya yanaendelea kuchunguzwa na vyombo vyetu vya kiusalama ,endapo itabainika basi umma utatangaziwa lolote lililopo lakini sio kuhisi”alisema Njwayo.

Kuhusiana na madai ya askari doria na kikosi maalum kilichopo Rufiji,Kibiti kutoingia maeneo ya vijijini ambako ndio kuna athari kubwa ,Njwayo,alieleza ,anachojua yeye ni kwamba kuna askari wanaovaa sare na wasiovaa sare ambao wanafika mijini na vijijini.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga ,alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai ni siku sita tangu kutokea kwa mauaji mnamo may 13 mwaka huu,ambapo katibu wa CCM kata ya Bungu ,Halife Mtulia ,aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana kwani vyombo vya dola bado vinafanya upelelezi ili kubaini kiini halisi cha matukio hayo ya mauaji .

Kamanda huyo alisema wanaendelea kuwasaka wahusika wa matukio hayo yanayoonekana kuhusisha viongozi mbalimbali na askari polisi.

Kamanda Lyanga ,aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kufichua wahalifu ambao wapo miongoni mwao pasipo kuogopa .

“Ni wazi kwamba wahalifu wanaofanya mauaji haya wana wenyeji wanaowakumbatia kwa kuwaficha hivyo yeyote atakaebainika kushirikiana na makundi ya uhalifu huo atachukuliwa hatua kali za kisheria”alisisitiza kamanda Lyanga.


WAKUU WA POLISI KUTOKA NCHI ZA SADC KUKUTANA ARUSHA.

ddddd-1
Mkutano mkuu wa  mwaka wa Shirikisho la wakuu wa Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) unatarajia kufanyika Mei 24, 2017 mkoani Arusha chini ya mwenyekiti wa Shirikisho hilo kipindi hiki ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu. 

Mkutano huo utatanguliwa na mikutano ya kamati tendaji za SARPCCO kabla ya kufunguliwa  rasmi Mei 24, 2017 na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ambapo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya Operesheni za pamoja katika kubaini na kukabiliana na makosa  mbalimbali yakiwemo  dawa za kulevya, wizi wa magari, usafirishaji haramu wa binadamu na ugaidi.

Vilevile, mkutano huo utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na Wakuu wa Upelelezi wa SARPCCO pamoja na kamati tendaji za sheria, Mafunzo na kamati tendaji ya Jinsia na watoto katika mkutano wao uliofanyika mwezi Machi mjini Bagamoyo.

Aidha suala la michezo baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo.

SARPCCO iliundwa mwaka 1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu. 

Shirikisho hilo linaundwa na Nchi kumi na tano ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesoto, Mauritius, DRC, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Madagascar na Syshelis.

Imetolewa na:-
Advera Bulimba-ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.