Saturday, April 1, 2017

AREF NAHDI WA TIF APEWA TUZO MAALUM YA UTENDAJI KAZI.


Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahdi, kulia akikabidhiwa Tuzo na Balozi wa  Pakistani, Amiri Muhammad Khan wapili kushoto, wa  pili kulia ni Meya wa Manispaa ya  ilala Charles  Kuyeko, na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Alhuda Center of Islamic Banking and Economics, ya nchini Dubai Muhammad Zuberi ambao ndiyo waliotowa Tuzo hiyo.
....................................
Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation Aref Nahdi amekabidhiwa Tuzo na Shirika la Kimataifa linalotoa mafunzo  kwa Benki za  kiislamu na kusimamia Uchumi wa  kiislamu  la  Alhuda Center  of Islamic Banking and Economics, (CIBE) ambalo Makao yake makuu  nchini Dubay.


Tukio hilo limefanyika katika Mkutano wa  kujadili Uchumi wa  Kiislamu  na Changamoto zake kwa nchi za Afrika ambao umeandaliwa na CIBE, mkutano uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regence jijini Dar es Salaam
Akizungumza  mara baada ya kupokea tuzo hiyo,  Mwenyekiti wa The  Islamic Foundation Aref Mubaarak Nahdi, amesema zawadi hiyo imetolewa kutokana na kutambua mchango wa The Islamic Foundation katika jamii na kusema kuwa hiyo inatoa fursa kwa  Taasisi ya The Islamic Foundation kuongeza juhudi.

Alisema The Islamic  Foundation  inatekeleza wajibu  wake  kwa kumuogopa Mwenyezimungu na wala  sio kwa kuwaangalia watu na  kwamba juhudi zinazofanywa na The  Islamic Foundation ni kielelezo tosha  kwenye uso  dunia kwamba  The Islamic Foundation inatekeleza wajibu  wake.

Aliongeza kwa kusema kwa kujiangalia  mwenyewe huwezi kujua ukubwa wa mambo unayofanya lakini  sifa na  pongezi zinazotolewa na  watu ndio  zinazopelekea kutambua kuwa TIF  inafanya  mambo makubwa hapa nchini.

Aidha,  aliwataka watendaji  wote  wa The  Islamic Foundation  kwenye  kila kitengo  kuongeza juhudi  ya utendaji kazi  ili  kufanikisha malengo ya  kuutumikia uislamu na kuongeza  kuwa malipo yake hayawezi  kupimwa kwa macho ya kawaida na kwamba faida ya kuitumikia TIF kwa maslahi ya uslamu ni yamilele.

Mwenyekitihuyo wa The Islamic Foundation  amepokea Tuzo  hiyo  kutokana  na kazi  zinazofanywa na Taasisi anayoingoza kutekeleza  majukumu  yake kwa juhudi kubwa ya  kueneza Elimu  kwa jamii  ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla.

Akielezea wakati wa  kukabidhiTuzo hiyo mzungumzaji kutoka shirika  lakimataifa  la Alhuda alisema Tuzo  hiyo inakwenda kwa  Aref  Nahdi  kutokana na  mchango wake  mkubwa  katika  kuupeleka  mbele uislamu  ambao mpakasasa inamiliki  Hospitali, Shule za Msingi na  Sekondari, Gazeti,  Kituo cha Redio na  Tevisheni.

Aliongeza kuwa katika  idara zake za Elimu TIF pamoja na vyombo vyake vya Habari imekuwa  mstari  wa mbele katika kutoa Elimu inayopelekea watu  kujua  ubaya wa riba na kupelekea watu wengi  kuongeza ufahamu kuhusu madhara ya Riba  na kufahamu njia sahihi za kukuza Uchum  kwa mujibu wa uislamu.

Mkutano huo  wa siku mbili wa  kujadili Uchumi wa Kiislamu Afrika umehuduriwa  na  nchi  kumi zaidi ya kumi ambapo kwa  pamoja  wamekubaliana  kuongeza Elimu juu ya  matumizi ya  Benki za  kiislamu, Uharamu  wa Riba  na kuzitaka  Serikali  za nchi za Afrika kutunga Sheria zitakazosimamia uendeshaji  wa Benki  za  Kiislamu.

Miongoni  mwa Taasisi zilizopata Tuzo ni  Amana  Bank, Ibni Jazari, ZIC  Takaful, IFM, NBC ISLAMIC  WINDOW, ICCIU Uganda, Gulf African Bank, Nairobi, FSDT, Dar es Salaam.
Mezani ni tuzo aliyopewa Mwenyekiti wa The Islamic Foundation (TIF) Aref Nahdi.
 Mkurugenzi wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Masoud kulia akikabidhiwa Tuzo na Balozi wa  Pakistani, Amiri Muhammad Khan wapili kushoto, wa  pili kulia ni Meya wa Manispaa ya  ilala Charles  Kuyeko, na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Alhuda Center of Islamic Banking and Economics, ya nchini Dubai Muhammad Zuberi ambao ndiyo waliotowa Tuzo hiyo.
Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahd kulia, akikabidhi cheti kwa Mwenyekiti wa ZIC Takaful, Dkt. Muhammad Hafidhi Khalifa.

MAGAZETI YA LEO TAREHE 01 APRIL 2017.

TANZANIA KUPATA MEGAWATI 400 ZA UMEME KUTOKA ETHIOPIA

A 4
Tanzania inategemea kupata Megawati 400 za umeme kutoka Ethiopia ikiwa ni moja ya makubaliano yaliyofikiwa baada ya ziara ya kikazi ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn.
 
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari juu ya makubaliano na mikataba ambayo nchi za Tanzania na Ethiopia wametiliana saini leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

“Tukitaka kujenga uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na umeme wa kutosha,wenzetu Ethiopia wametuonyesha njia na mimi nimemuomba Mhe.Waziri atusaidie wataalamu kutoka nchini kwake ili  waje  tuwaonyeshe maeneo mbalimbali watusaidie katika kupata umeme wa uhakika kwa kujenga mabwawa ya umeme ambayo yamesaidia sana katika kupatikana kwa umeme wa kutosha nchini kwao.”Aliongeza Rais Magufuli.

Aidha amesema kuwa kupatikana kwa umeme huo kutasaidia kuleta changamoto kwa shirika la umeme nchini katika kuwapatia wananchi bei ya chini na hivyo kuleta ushindani katika upatikanaji wa umeme nchini.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn amesema kuwa wana mengi ya kujifunza kutoka Tanzania kwani nchi hizi mbili zina historia inayofanana na kuongeza kuwa hakuna haja ya wao kwenda nje ya Afrika kupata uzoefu katika masuala mbalimbali.

Ameongeza kuwa lengo kuu la kuja nchini ni kwa sababu anahamini nchi hizi mbili zinaweza kuunganisha nguvu zake na kuwa nguzo kuu katika maendeleo katika eneo la ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

“Tanzania na Ethiopia ni nchi ambazo zina ushirikiano mzuri sana,sisi sio washindani bali tunasaidiana katika masuala mbalimbali kwani tumekuwa katika hatua mbalimbali za kuwaondoa wananchi wetu katika umaskini katika hatua zinazofanana,na huu ni wakati muafaka katika kuimarisha ushirikiano wetu kwa faida ya watu wetu kwa ujumla”Alisisitiza Mhe.Desalegn.

Aidha amesema  kuwa  mabadiliko  ya  kilimo  katika  nchi  zetu ndio  msingi  wa  maendeleo  pamoja  na  utumiaji  wa  teknolojia  bora utasaidia katika maendeleo ya viwanda vidogo vidogo.

Viongozi hawa wamekubaliana kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu juu ya namna sekta mbalimbali zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za benki, madini na gesi, elimu na  mawasiliano.

Ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Haile Mariam Dessalegn imekuwa ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza kuwa wakati umefika wa kukuza biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa thamani ya biashara kati yake ni Dola za Marekani milioni 2.24 tu.

MAJALIWA AWAASA WATANZANIA WAISHIO NJE YA NCHI KUTOJIHUSISHA NA DAWA ZA KULEVYA

MAJALIWA+PICHA
DAWA za kulevya ni moja kati ya vitu vyenye madhara makubwa ambavyo vinachangia kuporomosha uchumi wa Taifa kwa sababu yanaathiri vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi.

Hata hivyo dawa za kulevya zimekua zikiigharimu Serikali kwa kutumia fedha nyingi katika kupambana na athari zitokanazo na matumizi dawa hizo, hivyo imewataka wananchi na jamii kiujumla kutojihusisha na biashara hiyo haramu.

Mbali na dawa hizo kulisababishia Taifa madhara ya kiuchumi na kiafya, pia biashara hiyo ya dawa za kulevya inachafua na kushusha hadhi ya Tanzania kimataifa.

Madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu kwa mtumiaji ikiwa ni pamoja na  kuchanganyikiwa, kuwa na ulevi uliopindukia na hatimaye kusababisha kifo kama mtumiaji atazidisha matumizi.

Katika kuhakikisha biashara hiyo inakomeshwa Serikali imeunda Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini ambayo ndiyo inayoongoza mapambano hayo.

Jumatano ya Machi 22, mwaka huu akiwa nchini Mauritius, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizungumza na Watanzania waishio nchini huko katika mkutano alioutisha kwenye hoteli ya Meridien mjini Port Louis.

Akizungumza na Watanzania hao aliwataka wajiepushe na masuala yahusuyo dawa za kulevya. Aliwataka Watanzania wote wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa husika na kamwe wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya.

“Vita ya dawa za kulevya ni kubwa, hata hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi ilikuwa inapoteza vijana ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya. Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” alisema.

Alisema katika kudhibiti biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua kuunda Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya kazi vizuri. “Na tutakamata kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila kujali cheo, uwezo na mamlaka aliyonayo,”.

Aliongeza kuwa mamlaka hiyo inafanya kazi ya kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara, lengo likiwa ni kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na madhara waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.

Waziri Mkuu alisema kuna Watanzania wengi wamefungwa katika magereza mbalimbali duniani na wengine wamehukumiwa kunyongwa baada ya kuthibitika  kuwa wanajihusisha na matumizi, usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya, hivyo aliwataka wawe mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kujiepusha na dawa za kulevya.

Akizungumzia idadi ya watu ambao hadi sasa wamekwishakamatwa katika nchi mbalimbali, Waziri Mkuu alisema takwimu za jumla zinaonyesha kuwa Watanzania 515 wamekamatwa na kufungwa gerezani kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa ya kulevya.

“Nchini China Watanzania walioko magerezani ni zaidi ya 200; Brazili kuna Watanzania 12; Iran wako Watanzania 63; Ethiopia Watanzania saba na Afrika Kusini wako Watanzania 296,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kwamba “Dawa za kulevya ni hatari sana kwa usalama na ustawi wa Taifa letu. Vita hii inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa. Sote kwa pamoja tunapaswa kuunga mkono jitihada hizo,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa taarifa zililizopatikana ndani ya Jeshi la Magereza Tanzania hadi Machi 26, mwaka huu kulikuwa na wafungwa 512 wanaotumikia vifungo vyao katika magereza mbalimbali kutokana na makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, ambapo kati yake wanaume ni 491 na wanawake 21.

Mbali na wafungwa pia kuna mahabusu 1,284 wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na utumiaji, usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya, ambapo kati yao wanaume ni1,166 na wanawake ni 118.

Katika hatua nyinngine, Waziri Mkuu aliwataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga mshikamano wa pamoja na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya Taifa.

Alisema ni vema wakatumia fursa walizonazo katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati na utalii.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed aliwaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa kuwa umoja wao ndiyo nguzo yao.

“Mko hapa kwa ajili ya kutafuta elimu na wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo  zitawasaidia kuboresha maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie kilichowaleta,” amesema.

Dkt. Khalid aliwahakikishia Wanzania hao walioko nje ya nchi kuwa Tanzania  iko salama na wanaendelea kudumisha amani na utulivu kama walivyoiacha wakati walipondoka.

Naye Mwenyekiti wa muda wa Umoja wa Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald Kongwa ambaye ni Ofisa wa benki ya Standard Chartered nchini Mauritius alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kipato wanachokipata watakitumia kwa kuwekeza Tanzania kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa.

Alisema wanaunga mkono na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika  kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi wa miundombinu ya kisasa, ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.

Bw. Kongwa alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya kujifunza mambo mbalimbali nchini Mauritius kama namna bora ya kuendesha kilimo cha miwa kwa sababu nchi hiyo inazalisha zaidi ya tani 600,000 za sukari kwa mwaka na tani 530,000 inauzwa nje ya nchi.”Tutumie fursa hii kujifunza zaidi ili tuweze kukuza uchumi wetu,”.

Aliongeza kuwa mbali na kujifunza kilimo cha miwa pia Tanzania inaweza kutangaza vivutio vyake vya utalii nchini Mauritius ili kuwawezesha watalii wengi wanaoingia nchini humo kuweza kuvifahamu na hatimaye kuwa nchini. Kwa mwaka Mauritius inapata watalii zaidi ya milioni moja.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA
IJUMAA, MACHI 31, 2017.