Thursday, December 8, 2016

MAITI SITA ZAOKOTWA MTO RUVU BAGAMOYO.

rcpppppp
Kamanda wa  Polisi mkoa wa Pwani,  kamishna Msaidizi wa  Polisi, ACP-  Boniveture Mushongi, akizungumza na waandishi wa Habari.

Miili ya watu sita  wakiwa wamekufa  imeokotwa katika mto Ruvu kata ya  Makurunge  wilayani Bagamoyo mkoa wa  Pwani.
Akitoa Taarifa kwa waandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa  wa  Pwani,  Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP- Boniventure Mushongi,  Alisema  tukio hilo  limebainika Tarehe  06 mwezi  Desemba  2016, Saa 11 alfajiri baada ya  raia wema  waliokuwa wakifanya  shughuli za uvuvi  katika mto huo kutoa Tarifa Polisi.
Alisema kufuatia hali hiyo Polisi walifika katika eneo hilo na  kukuta  mwili wa mtu  mmoja ukiwa unaelea  ambapo katika kufuatilia imebainika miili ya watu wengine  wanne wote wakiwa wameshafariki ambao wanakadiriwa kuwa na umri  wa kati ya miaka 25-35.
Aidha, aliongeza  kuwa, siku ya Tarehe  06 Desemba 2016 ulipatikana mwili wa mtu mwingine  akiwa amekufa anakadiriwa kuwa umri  wa miaka  kati ya 25- 30 na kufanya  idadi ya miili iliyookotwa katika eneo hilo kufikia sita.
Kamanda  Mushongi alisema kuwa miili hiyo yote  ilizikwa na kwamba imekuwa vigumu kuwatambua kutokana na kuharibika vibaya huku kukiwa hakuna kitambulisho  chochote  kinachoashiria watu hao  ni  watu  wa  wapi  na  wametoka wapi.
Alisema hali ya  miili hiyo inaonyesha  ilitupwa  katika mto Ruvu na kusafirishwa na  maji  kwa umbali mrefu hivyo kushindwa kubaini kwa haraka mahali haswa mauaji hayo  yalipotekelezwa.
Jeshi  la   mkoa wa  Pwani  linaendelea na  upelelezi  ili  kubaini waliohusika kutekeleza mauaji   hayo  na  kwamba  atakaebainika sheria itachukua  mkondo wake.
Kamanda Mushon gi  amewaomba  wananchi  mkoani  Pwani,  kutoa  ushirikiano  kwa jeshi  la  polisi  ili kubaini  watu wote  wanaotekeleza uhalifu  kwa namna  yoyote  ile. 
Katika tukio lingine,  Kamanda Mushongi alisema  Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyang'hundu wilayani Kibiti, Mohamedi Aliy Thabiti mwenye umri wa miaka  45, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na  mapanga kichwani.
Alisema tukio hilo  limetokea Tarehe m05 Desemba  2016 majira ya Saa 2 :30 usiku wakati Mwenyekiti alipokuwa anarejea nyumbani kwake  akiwa na mpenzi wake Sophia  Maulidi katika Kitongoji  cha Besabu kijiji cha Nyambunda kata ya  Bungu  wilaya ya  Kibiti.
Alisema  wakiwa njiani katika eneo hilo  walitokea watu  watatu  wakiwa  wamepakiza  kwenye  Pikipiki  aina Boxer isiyokuwa na namba ambapo waliwaamuru  kusimama na kumpiga risasi na mapanga kichwani.
Kamanda Mushongi  alisema mwenyekiti huyo  alifariki  wakati  anapatiwa matibabu  katika Hospitali ya Mision ya Mchukwi kufuatia kujeruhiwa vibayasana.
Jeshi  la  Polisi  mkoani  pwani  linaendelea na  msako  wa ili kuwakamata waliohusika katika  tukio hilo.                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                          

Tuesday, December 6, 2016

UFAFANUZI KUHUSU MIZIGO YA WAMA BANDARINI.

index 
 
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapenda kuutaarifu umma kuwa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) iliingiza nchini maboksi kumi na moja (11) ya vitabu/kamusi kutoka nchini Japani kwa ajili ya matumizi ya elimu.

Kwa mujibu wa sheria ya forodha ya Afrika Mashariki (The East African Community Customs Management Act, 2004), pamoja na Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT Act, 2015), vitabu hivi havitozwi kodi ya forodha wala ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Vitabu hivi vililipishwa tozo ya uondoshaji mizigo bandarini (Customs Processing fees) shilingi 42,483 na tozo ya Maendeleo ya Reli (Railway Development Levy) shilingi 106,438 ikiwa ni jumla ya shilingi 148,921. Baada ya malipo hayo kufanyika, vitabu hivyo vilichukuliwa na WAMA tangu tarehe 10 , 2016.

Tunapenda kutoa ufafanuzi kwamba taarifa zilizoandikwa na baadhi ya magazeti hivi karibuni juu ya vitabu hivyo kuwamo katika orodha ya bidhaa zinazopaswa kupigwa mnada kwa sababu ya kutolipiwa kodi siyo sahihi.

Kwa kuwa vitabu hivyo havikupaswa kulipiwa kodi ya Forodha wala VAT kwa mujibu wa sheria, ni wazi kuwa WAMA hawakupaswa kuomba msamaha wa kodi kwenye Mamlaka yoyote ile.  

Orodha iliyowahi kuchapishwa na baadhi ya magazeti hapa nchini na ambayo ilijumuisha jina la WAMA haikuwa sahihi.
Pamoja Tunajenga Taifa Letu
1.   J. Kidata
KAMISHNA MKUU

MIKOA NA HALMASHAURI ZATAKIWA KUWEKA TAHADHARI JUU YA KIPINDUPINDU.


ummi1
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kushoto akipokea vifaa mbalimbali vya matibabu ya mabadiliko ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi vyenye thamani takribani milioni 100 za kitanzania kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Pink Ribbon Red Ribbon  Bi. Celina Schocken jijini Dar es salaam.
..........................
 
MIKOA na halmashauri nchini zimetakiwa kuweka tahadhari juu ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia usafi binafsi na usafi wa mazingira hasa wakati wa mvua za vuli na msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ili kuweza kuepuka ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu kwa mwezi Novemba 2016 uliofanyika jijini Dar es salaam.

“Mikoa na Halmashauri zote nchini ziwe katika hali ya tahadhari juu ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia usafi binafsi na usafi wa mazingira hasa wakati wa mvua za vuli na msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ili kuweza kuepuka ugonjwa huo” alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Mikakati ya kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu ishirikishe sekta mbalimbali za afya nchini bila kusahau jamii husika na kuhakikisha kila Halmashauri inaunda na kuimarisha Kamati ya Afya ya Kata.

Aidha Waziri Ummy ameiagiza Mikoa na Halmashauri zote nchini kutoa taarifa ya wagonjwa wapya wa Kipindupindu ili jitihada za makusudi za kupambana na ugonjwa huo zifanyike mapema ili kujenga taifa lisilo na magonjwa ya mlipuko.

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa takwimu zinaonesha katika mwezi Novemba 2016 jumla ya mikoa sita ikiwemo Morogoro yenye wagonjwa 282, Dodoma 96 na vifo 2, Mara 31, Kigoma 30 na vifo 4, Arusha 11 na Dar Es Salaam 8 kutoka wagonjwa  250 na vifo 4 kwa mwezi Oktoba mwaka huu.

Kwa wakati huohuo Waziri Ummy amepokea vifaa vya matibabu ya mabadiliko ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi vyenye thamani takribani milioni 100 za kitanzania kutoka Shirika la Kimataifa la Pink Ribbon Red Ribbon ili kupambana na ugonjwa huo nchini.

Akikabidhi msaada huo Mtendaji Mkuu wa Shirikahilo Bi. Celina Schocken amesema kuwa wametoa vifaa hivyo ili kuisaidia nchi kwa juhudi za kimakusudi katika kupambana na ugonjwa wa saratani ili kuokoa maisha ya wanawake wa Tanzania.

“Tumeamua kutoa vifaa hivi ili kuisaidia nchi kwa juhudi za kimakusudi katika kupambana na ugonjwa wa saratani ili kuokoa maisha ya wanawake wa Tanzania ”alisema Bi. Schocken.