Thursday, October 20, 2016

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI MGENI RASMI MAHAFALI YA BWAWANI SEKONDARI

indexcapturejj
Tarehe 21 Oktoba, 2016 saa 3:00 asubuhi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Mhe. Balozi Hassan Simba Yahya anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za mahafali ya 13 ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Bwawani iliyopo Mkoa wa Pwani.

Shule ya Sekondari Bwawani inamilikiwa na Jeshi la Magereza, ilianzishwa mwaka 1978 kwa lengo la kutoa elimu ya Sekondari kwa Watumishi wa Magereza ambapo hivi sasa Shule hiyo inatoa elimu ya Sekondari kwa vijana wa kike na kiume kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.

Shule hiyo pia inatoa elimu ya Kidato cha Tano na Sita, katika muunganiko wa masomo ya Historia, Jiografia na Kiswahili (HGK), Historia, Jiographia na Kiingereza(HGL). 

Aidha, mwaka huu inatarajia kuanzisha mkondo wa masomo ya sayansi(CBG) yaani masomo ya Kemia, Baiologia na Jiografia.

Jumla ya Wanafunzi 94 wa shule hiyo wanatarajia kuhitimu elimu yao ya kidato cha nne  mwezi Novemba mwaka huu.

Sherehe hizo zitajumuisha mambo yafuatayo:-
  • Mgeni rasmi kutembelea maeneo ya shule na kuweka mawe ya ufunguzi katika majengo ya shule;
  • Mgeni rasmi kuangalia Maonesho ya Taaluma kwa Wanafunzi Washiriki;
  • Mgeni rasmi kutoa vyeti na zawadi mbalimbali kwa Wanafunzi wahitimu na;
  • Mgeni rasmi kutoa hotuba
Sherehe za mahafali hayo zinatarajia kukamilika saa 8:00 mchana. Vyombo vya Habari vinakaribishwa kwenye sherehe hizo tarehe 21 Oktoba, 2016 kuanzia saa 3:00 asubuhi.

Imetolewa na: Lucas Mboje,
Mrakibu Msaidizi wa Magereza,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
DAR ES SALAAM

20 Oktoba, 2016.

VICHWA VYA HABARI MAGAZETINI LEO OKTOBA 20, 2016,

TANGAZO KWA WAJASILIAMALI BAGAMOYO.

Wajasiliamali wote wilayani Bagamoyo mnatangaziwa maonyesho ya wajasiliamali yatakayofanyika  Tarehe 26-30 mwezi huu wa 10 katika viwanja vya  Mwanakalenge Bagamoyo mjini.

Maonyesho hayo yanasimamiwa na shirika  la maendeleo ya viwanda vidogovidogo (SIDO).

Mjasiliamli anaetaka kushiriki kwa kupeleka bidhaa zake awasliane na Afisa biashara wilaya ya Bagamoyo kwamaelezo zaidi.

Atakaepata taarifa hii amjulishe na mwenzie.

Tangazo hili limetolewa na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bagamoyo.

Wednesday, October 19, 2016

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI MHANDISI WA MAJI LINDI

ale1
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi  wa mamlaka ya maji Lindi  Mhandisi  Adam Alexanda aliyeshikilia makabrasha  kutokana na kushindwa kusimamimia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika manispaa ya Lindi pamoja na matumizi mabaya ya ofisi,  Waziri mkuu amemuelekeza Mkuu wa Kupambana na rushwa TAKUKURU mkoani Lindi  kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za  Mhandisi huyo.
 ale2

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam Alexander akisikiliza maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
.......................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam Alexander kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi pamoja na kushindwa kusimamia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa ya Lindi.

Waziri Mkuu amemkabidhi Mhandisi huyo kwa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Bw. Stephen Chami na kumuelekeza afanye uchunguzi zaidi juu ya suala hilo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 19, 2016) wakati alipotembelea mradi wa maji wa Ng’apa ambapo ameagiza nafasi hiyo ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa Sengulo.

“Kamanda wa TAKUKURU fanya mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema analipwa Wizarani, mimi najua analipwa na LUWASA. Angalia kazi aliyokwenda kuifanya Dar es Salaam kama inalingana na siku alizokaa,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Mhandisi hiyo anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za ofisi pamoja na kupokea mshahara bila la kulipa kodi ya mapato ya mshahara (PAYE), kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri kwa muda mrefu.

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanapata shida huku watendaji waliopewa dhamana ya kuwatumikia hawaonekani kwenye vituo vyao vya kazi. “Huyu nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es Salaam.”

Alipoulizwa sababu za kutokuwepo ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi huyo alisema kwamba alikuwa Dar es Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili ya kutatulia changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.

“Unatumia siku ngapi kuandika proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika proposal na unakaa Dar es Salaam hata Katibu Mkuu wako hajui na huko unajilipa posho tu! Tena baada ya kulipwa sh.120,000 kwa siku wewe unajilipa sh.150,000. Hatuwezi kuvumilia hali hii,” amesema.