Wednesday, August 17, 2016

TCRA YAZINDUA KAMPENI YA KUONGEZA UFAHAMU KUHUSU MATUMIZI SAHIHI NA SALAMA YA MITANDAO.

index
Kitengo cha dharura cha kuitikia matukio ya usalama kwenye mitandao nchini (Tanzania Computer Emergency Response Team- TZ-CERT) kimepewa jukumu la kitaifa la kuratibu matukio ya usalama katika mitandao kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kikanda na kimataifa katika kusimamia matukio ya usalama mitandaoni.

TZ-CERT ilianzishwa kwa sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010, kifungu namba 124. Kifungu namba 5(1) cha kanuni za Mawasiliano ya kielektroniki na Posta zilizotolewa Desemba 2011, kilielekeza uanzishwaji wa TZ-CERT ndani ya mfumo wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Huduma za TZ-CERT zilizinduliwa rasmi tarehe 17 mwezi May mwaka 2015.

Majukumu makuu ya TZ-CERT kisheria ni kuwa kiungo cha kitaifa nchini na kwa nchi za nje kwa masuala yote yanaohusiana na usalama mtandaoni. Katika kutimiza wajibu wake TZ-CERT:

1.   Inatoa ushauri wa kitaalamu wa kukabiliana na matukio ya kiusalama yanayotokea na kuzuia madhara zaidi.

2.   Inafanya uchambuzi wa taarifa za matukio ya usalama wa mtandao kutoka vyanzo mbalimbali, kimataifa na kitaifa.

3.   Kutoa mwongozo wa kitaalamu “Security Advisory” kwa umma na wadau katika maeneo ambayo yameonekana kuwa na madhaifu.

4.   Uhamasishaji, kuelimisha na kujenga uwezo (Awareness & Capacity Building) wa masuala ya usalama wa mitandao kwa serikali na wadau kutoka sekta mbalimbali.

5.   Tathimini ya udhaifu wa mifumo ya kompyuta (Vulnerability assessment) katika mitandao ya wadau wa TZ-CERT.

Ikumbukwe kwa sasa Tanzania kuna watumiaji wa mtandao wanaokadiriwa kufikia milioni Kumi na Saba (17 milioni) kutokea milioni Tano (5 milioni) katika mwaka 2011.

Kutokana na uzoefu uliopatikana kwa muda wa mwaka mmoja toka ianze rasmi kutoa huduma, TCRA imebaini pamoja na mambo mengine ukosefu wa taarifa muhimu za usalama wa mitandaoni kumechangia kuwepo kwa matukio ambayo yangeweza kuepukika.

2.   Kwa nini kampeni ya kuongeza ufahamu?
Kampeni hii ya kuongeza ufahamu imekuja wakati muafaka baada ya timu ya TZ-CERT kubaini changamoto nyingi na aina mbalimbali za matatizo ya kwenye mtandao ambayo wanakutana nayo watanzania wengi kutokana na ufahamu mdogo wa jinsi ya kujilinda mitandaoni, kulinda taarifa zao mtandaoni pamoja na matumizi sahihi ya mtandao kwa ujumla wake.

3.   Kampeni itawalenga watu gani?
Kampeni hii inawalenga watumiaji wa huduma za Intaneti wa rika zote kuanzia watoto mpaka watu wazima.

4.   Kampeni itahusisha nini?
Kampeni hii inazinduliwa rasmi leo tarehe 17 mwezi 8 mwaka 2016 na itaendelea kwa miezi mitatu. Hata hivyo kampeni za kuelekea uzinduzi wa leo zilianza tarehe 01 Agosti, 2016. Kwa kuwa kampeni hii ni ya matumizi ya mitandao itaendeshwa zaidi kwenye mitandao ambapo watumiaji wa mitandao mbali mbali Tanzania watatumia muda wao kujifunza njia bora na salama za matumizi ya mtandao.

Katika kipindi hiki cha kampeni wananchi watajifunza mada mbali mbali ikiwa ni pamoja na matunzo sahihi ya kompyuta na programu zake, taratibu za kutumia mitandao kwa usalama, matumizi sahihi ya namba au neno la siri, sheria ya makosa ya mitandao, uwekaji wa taarifa kwenye mitandao ya kijamii na matumizi sahihi ya mitandao kwa watoto.

Kampeni hii itatolewa katika akaunti za TZ-CERT za mtandao wa facebook (https://www.facebook.com/Tz-Cert), twitter (https://twitter.com/tz_cert) na instagram (https://www.instagram.com/), pamoja na vyombo vya redio na TV kufikisha jumbe mbalimbali za kuelimisha watumiaji wa mitandao na umma matumizi sahihi ya mitandao.

5.   MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA UTUMIAPO HUDUMA ZA INTANETI/MITANDAO

1.   Kuwa makini na taarifa za binafsi  unazoziweka kwenye mitandao wa jamii.

1.   Ukisaidiwa kuanzisha akaunti za mtandao wa kijamii, hakikisha unabadilisha neno la siri lilotumika mara moja na neno hilo la siri usimshirikishe mtu yeyote.

  • Usijibu jumbe unazopokea kwenye akaunti yako ya barua pepe unaokutaka kuhakiki taarifa zako.
1.   Usijibu ujumbe wowote wa barua pepe unaokueleza kuwa umeshinda bahati nasibu.

1.   Usifungue kiambatisho au kubofya kiungo (link) unayotumiwa na mtu usie mjua kabla ya kuhakikisha uhalali wa barua pepe husika.

Ili kujiepusha na kukiuka sheria mbalimbali za mawasiliano ya mtandao umma wote unashauriwa kuzingatia yafuatayo:

1.   Usitunge na kusambaza ujumbe wa maudhi, uzushi au uchochezi.

1.   Usiendelee kusambaza ujumbe wa chuki, maudhi au uchochezi unaopokea kutoka kwa mtu mwingine. Badala yake ufute mara uupokeapo au toa taarifa.
  • Usitembelee tovuti na blogu za ponografia/ngono,
1.   Usitengeneze akaunti za mitandao ama kwa lengo la kufanya utapeli, ulaghai au kwa kutumia taarifa zisizo zako.

1.   Tunza vifaa unavyohifadhia kumbukumbu zako.
  • Uzinduzi wa tovuti mpya ya TZ-CERT
Pamoja na uzinduzi wa kampeni hii, pia tovuti mpya ya TZ-CERT itazinduliwa rasmi leo. Tovuti hii yenye lugha ya kingereza na Kiswahili itaanza kutumika rasmi kutoa taarifa muhimu za kuwasaidia wananchi kujilinda na matukio ya kwenye mitandao. Tovuti hii pia hutumika kutuma na kutoa taarifa ya matukio mbali mbali kwa TZ-CERT kwa msaada wa kitaalamu. Anwani ya tovuti hizi ni www.tzcert.go.tz
    Imetolewa na:

Kaimu Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
Mawasiliano Towers
20 Bara Bara ya Sam Nujoma
S.L.P. 474
14414 DAR ES SALAAM
17 Agosti 2016

ALIYEKUWA MKURUGENZI WA MAMLAKA YA VITAMBULISHO (NIDA) DICKSON MAIMU, AFIKISHWA MAHAKAMANI LEO TAREHE 17-08-2016

[​IMG]
Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa-NIDA- Dickson Maimu (wa tatu kushoto) na viongozi wengine  nane wa taasisi hiyo wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu mapema hii leo.
..................................................................................

Mnamo mwezi January 2016, Rais Dkt. Magufuli aliamua kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) Bwana Dickson Maimu na kumsimamisha kazi yeye na wafanyakazi wengine ili kupisha uchunguzi wa namna ilivyotumika kiasi cha shilingi bilioni 179.6

Katika zoezi la upatikanaji wa vitambulisho vya taifa malamiko  mengi yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuchelewa kupatikana vitambulisho hivyo huku maeneo mengi yakiwa wananchi hawajapata  mpaka sasa.

 Katika kutengua uteuzi wa Mkurugenzi huyo wa NIDA Dickson Maimu, Rais Dkt. Magufuli aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ifanye  uchunguzi wa namna fedha hizo zilivyotumika na ikiwa kunavitendo vya rushwa hatua za kisheria zilchukuliwe dhidi ya wahusika.

Aidha, alizitaka  pia Taasisi za Ofisi ya  mkaguzi  mkuu wa hesabu  za serikali (CAG) na ile ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA)  ilitakiwa kufanya  uchunguzi wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA.

Katika uchunguzi huo Ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG, ilitakiwa kufanya uchunguzi na kuangali vitambulisho vya taifa kama vinaendana na kiasi cha fedha zilizotumika na NIDA ambazo ni bilioni 179.6

RC PWANI, AWATAKA VIJANA KUJITUMA KWA KUFANYA KAZI.

SENSA 13
 Mkuu wa mkoa wa Pwani injinia, Everist Ndikilko.
....................................................................................
Vijana wametakiwa kuacha tabia ya kukaa vijiweni na badala yake wajitume katika kuifanya kazi ilikujipatiamaendeleo binafsi na taifa  kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikiro wakati wa sherehe za ufunguzi rasmi wa programu  ya kambi ya vijana ya kuwafundisha masuala ya  kilimo na  maarifa ambayo ipo chini ya mamlaka ya uendelezaji wa bonde la mto rufiji (RUBADA) iliyofanyika  katika kijiji cha Mkongo.

Ndikilo amebainisha kwamb serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli isingependa kuona vijana wa kitanzania  hawataki kutumia fursa zilizopo na kuamua kujiingiza katika vitendo ambavyo vipo kinyume na taratibu na sheria za nchi.

Naye mwakilishi wa shirika la chakula  duniani (FAO) nchini Tanzania Fred Kafeero  amesema kwamba kulingana na ripoti zinaonyesha asilimia 70 ya vijana katika  africa hawana ajira hivyo kunahitajika juhudi za makusudi za kuweza kuwasaidia katika kilimo cha mboga mboga,huku Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Juma Chwayo akiwaomba vijana hao kutumia fursa ya kilimo kupitia mafunzo watakayoyapata.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa ameutaka uongozi wa RUDABA kuhakikisha kwamba wanaepukana na malalamiko ambayo yalikuwa yanatolewa dhidi yao na badala yake waweke mikakati endelevu ya kuwasaidia vijana kujiendeleza zaidi  pamoja na kuongeza  juhudi za ujenzi wa viwanda kwa lengo la kuweza kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza uchumi.

Kwa upande wao baadhi ya vijana ambao watanufaika na profamu hiyo akiwemo Saimoni Nyimmba pamoja na Joseph Bada wamesema kwamba  mafunzo hayo ya kilimo na maarifa  pindi watakapomaliza yataweza kuwasaidia  kuwapatia  kipato pamoja na kuachana na suala la kuwa tegemezi  sambamba na  kuondokana na kile kilimo cha kizamani.

MAFUNZO hayo ya kilimo na maarifa yataweza kuwanufaisha vijana wapatao 200 kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania ambapo kwa sasa yataanza kuwanufaisha vijana 62 kutoka katika Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani ambapo ujuzi watakaupata wataweza kupata fursa ya kujiajiri wao wenyewe na kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kupitia sekta ya kilimo.