Tuesday, August 16, 2016

TRA YAZINDUA KAMPENI YA KUHAKIKI NAMBA YA UTAMBULISHO WA MLIPA KODI (TIN)

 Kamishna wa TRA Bw. Alphayo Kidata akipata maelezo kutoka kwa Rehema Shayo Meneja wa Usajili TRA wakati akikagua utekelezaji wa uhakiki huo.
...........................................................................................................
 

Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) imezindua zoezi maalumu kwa ajili ya kuhakiki na kuboresha taarifa za usajili wa namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN).

Uzinduzi huo umefanywa na Kamishna Mkuu wa Ofisi hiyo Bw, Alphayo Kidata kwa kushirikiana na wafanyakazi wa ofisi hiyo mapema hii leo jijini Dar es salaam, ambapo kuanzia sasa zoezi hilo litakuwa endelevu katika mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani .

Kidata alisema kuwa lengo kubwa la uzinduzi wa zoezi hilo ni kubadili mfumo wa sasa wa kuhifadhi kumbukumbu za walipa kodi kwa kuweka mfumo mpya unaoendana na ukuaji wa teknolojia ambao utakuwa na walipa kodi wake wanaostahili kuwepo kwenye wigo.

Aidha aliongeza kuwa mfumo huo utasaidia kuwaondoa walipa kodi hewa ,kuongeza ufanisi katika suala zima la usimamizi wa ukusanyaji kodi kwa kiwango cha juu na kuwezesha ulipaji kodi kuwa nafuu kwa mlipaji.

Hata hivyo katika hatua nyingine Kidata ametoa wito kwa yeyote mwenye namba ya utambulisho wa mlipa kodi kufika katika ofisi za mamlaka hiyo ili kuweza kupata utaratibu wa zoezi zima jinsi linavyokwenda
.

USIKOSE, KIPINDI CHA "SAFARI YA DODOMA" TBC TAREHE 17.08.2016.

Katika kufanikisha agizo la mhe. Rais John Magufuli, na kutekeleza maamuzi ya kuhamishia makao makuu ya serikali Dodoma, TBC imeamua kuandaa kipindi maalum ili kuwafahamisha wananchi juu ya uamuzi huo, faida zake na pia nini kifanyike au nini kimefanyika mpaka sasa.
Kipindi hiki kinaitwa “SAFARI YA DODOMA” ambacho kinarushwa kila siku ya jumatano saa 3:00 usiku, TBC1.

Kipindi hiki cha muda wa saa moja, kinawakaribisha wadau mbalimbali toka serikalini, mashirika na jamii kupata fursa kuja kuelezea umuhimu na jinsi ambavyo wamejiandaa kuhamia Dodoma, pia ni fursa gani zilizopo Dodoma, zikiwemo jitihada za wafanyabiashara na wawekezaji kutumia nafasi hii kuelezea namna ambavyo wanaweza kustawisha makao makuu ya nchi, Dodoma.
 
Kipindi cha kwanza kilichorushwa jumatano iliyopita ya tarehe 10 agosti 2016, tulikuwa na mhe. Cleopa Msuya, waziri mkuu mstaafu. Ambaye alitueleza hali ilivyokuwa wakati huo ameteuliwa kuwa waziri mkuu, na jinsi ambavyo maamuzi ya kuhamia Dodoma yalitekelezwa.

Katika kipindi cha jumatano tarehe 17 Agosti 2016, saa 3:00 usiku, kwenye studio za TBC1 tutakuwa na mgeni, mhe. Jenister Mhagama, waziri wa nchi, ofisi ya waziri mkuu, sera, bunge, kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu.

Pia tutakuwa na nafasi ya kuwasikiliza wadau mbalimbali wakitoa maoni yao kuhusiana na maamuzi haya, pia tutakaribisha simu ili kujibu maswali mbalimbali yatakayotolewa kwenye kipindi, ambapo mshindi atajipatia zawadi toka chuo kikuu cha Dodoma (udom).
 
Nakukaribisha kutazama kipindi hiki, jumatano saa 3 usiku, TBC1

Kwa maoni tutumie barua pepe: maonidodoma@tbc.go.tz

Pia jiunge nasi katika mitandao ya kijamii:
SMS: Andika dodoma, acha nafasi, Ujumbe wako, tuma kwenda 15559
WhatsApp: 0678 279 107
Facebook: tbconetanzania
Twitter: tbconetanzania
Instagram: tbconetanzania
Youtube: TBC1.

KATIBU MKUU MALI ASILI AKEMEA UINGIZWAJI WA MIFUGO KWENYE MAENEO YA HIFADHI

MIL
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ametoa wito kwa wadau wauhifadhi nchini kukemea kwa nguvu zote tabia ya uingizaji wa mifugo ndani ya hifadhi za Misitu na Wanyamapori nchini kwakuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi na kunahatarisha ustawi wa hifadhi hizo ambazo ni muhimu kiikolojia na uchumi na wa taifa.

Milanzi ametoa wito huo juzi wakati akifunga mafunzo maalum ya kijeshi katika kituo cha Mlele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi, Mkoani Katavi kwa Mameneja wa Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro na Askari wa TANAPA kwa ajili kubadilisha mfumo wa utendaji katika taasisi hizo kutoka wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu (paramilitary) kuboresha utendaji wao wa kazi.

“Mifugo katika hifadhi zetu sio sahihi ni kinyume kabisa chasheria za nchi, endeleeni kulikemea hili, tusipige siasa kufurahishana kwakua madhara yake ni mengi ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji, muingiliano wa magonjwa baina ya mifugo na wanyamapori na kuharibu ubora wa vivutio vyetu” Alisema Milanzi.

Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 Ibara ya 18 (2) inakataza kabisa kuingiza mifugo ndani ya hifadhi, Sheria hiyo inasema “Si ruhusa mtu yeyote kuingia na kulisha mifugo ndani ya Mapori ya  Akiba, Mapori Tengefu na Ardhioevu”.

Milanzi alisema kuwa hifadhi za taifa nchini zina umuhifu mkubwa kwa uchumi wa taifa kwakuwa kupitia utalii zinachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za nje (foreign currency). Aidha sekta hiyo inatoa ajira zaidi ya milioni moja na nusu kupitia huduma za kitalii nchini. 

Mbali na faida za kiuchumi hifadhi hizo pia zina faida nyingi za kiikolojia ambazo ni uhifadhi wa vyanzo vya maji, kusaidia upatikanaji wa mvua na hewa safi kwa viumbe hai ikiwemo binaadamu. Alisema kuharibu hifadhi hizo kwa kulisha mifugo ndani yake ni jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa ni kuhatarisha pia maisha ya binaadamu ambayo yanategemea hifadhi hizo.

Alieleza kuwa Serikali inaenda kulifanyia kazi tatizo hilo pamoja na migogoro mingine ya ardhi kwa ajili ya kuyatafutia suluhu kwa kushirikisha Wizara zinazohusika ambazo ni Ardhi, Kilimo na Mifugo, Sheria na Katiba, Tamisemi, Maliasili na Utalii na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.

Akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo, Milanzi alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uadilifu, nidhamu, ujasiri, uaminifu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa muda mfupi na hivyo kuwataka kuyatumia kuongeza ufanisi katika kulinda maliasili zilizopo kwenye maeneo yao.

Aliwataka pia wahitimu hao kutafsiri mafunzo hayo na maendeleo ya sekta ya uhifadhi nchini na kuliongezea taifa mapato kwa kuboresha huduma za utalii, kubuni bidhaa mpya za utalii na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Alan Kijazi aliwataka wahitimu hao kutumia mafunzo waliyoyapata kuziba mianya yote ya ujangili na kwamba jamii inategemea kuona kazi hiyo kwa vitendo.

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na UNDP kupitia mradi wa “Spanest” yalifanyika kuanzia tarehe 15 Julai hadi tarehe 13 Agosti, 2016 kwa kuwahusisha washiriki 69 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Tanapa. Mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwa awamu yanatemewa
kuhusisha taasisi zote za uhifadhi wa wanyamapori nchini kuelekea kwenye mabadiliko ya muundo wa utendaji kazi kutoka mfumo wa Kiraia  kwenda mfumo wa Jeshi Usu (Paramilitary).

MBUNGE WA RUFIJI AIOMBA SERIKALI KUISADIA WILAYA YA RUFIJI KUPATA MAENDELEO.



 
MBUNGE wa Rufiji Mohamed Mchengerwa ameiomba serikali kuiangalia kwa jicho la pekee wilaya ya Rufiji kwani katika mkoa wa Pwani ndiyo ambayo haina kiwanda chochote hivyo kuna umasikini mkubwa.

 Pia ameiomba kufufua kiwanda cha pamba na kusukuma Wakala wa Bonde la Mto Rufuji (Rubada) kutekeleza majukumu yake ili kuondokana na umaskini uliopo kwenye wilaya hiyo. Alisema ni zaidi ya miaka 41 sasa Rubada imekuwa haifanyi kazi yake ipasavyo na kwamba wakati wakala huo unaanzishwa kulikuwa na kiwanda cha pamba ambacho sasa kimekufa.

Kauli hiyo aliitoa  jana katika kijiji cha mkongo wakati wa uzinduzi wa Programu ya mafunzo ya kilimo na ujasiriamali kwa vijana ambayo yamefadhiliwa na Shirika la Chakula duniani(FAO) na kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo.

 "Wilaya hii ina umasikini mkubwa tunaomba serikali ituangalie jitihada hizi za rubada leo ndizo zilitakiwa kufanyika miaka 41 iliyopita,malalamiko mengi ya wananchi yalikuwa juu yarubada itusaidie kupima ardhi.

 Tupate viwanda wilaya zote za mkoa huu hatuna kiwanda hata kimoja lakini wakati wanapewa miaka ya 70 kulikuwa na kiwanda cha pamba ila kilikuwa kimekufa na hadi sasa hakuna kiwanda chochote hapa mkoani,"alisema Mchangelwa.

 Alisema kukosekana kwa rubada hiyo kumesababisha wananchi kukosa imani na serikali yao na kwamba hiyo inatokana na kuwa nyuma kimaendeleo hivyo inabidi suala hilo lifanyiwe kazi lengo likiwa ni kurudisha imani hiyo kwa serikali yao. Aidha, aliiomba serikali kuwapa vijana wa mkoa huo elimu ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.

 Akizindua mafunzo hayo,RC Ndikilo alisema uzinduzi wa mafunzo ya kilimo katika kambi ya mkongo ya namna ya kuongeza tija ya uzalishaji chakula na biashara ya awamu ya kwanza wataanza vijana 62 kutoka rufiji na nje ya mkoa wa pwani na badae watarudi katika mashamba yao kuelimisha wengine. Alisema vijana hao watapata mafunzo kwa kipindi maalum kwa hiyo na kwamba watayatumia katika maeneo mbalimbali nchini.

 "Vijana wasiendelee kuwa wahuni changamoto za ajira zinaanza kutaftiwa ufumbuzi,wasikae tu,nimefarijika kuona changamoto zinatatuliwa,vijana wapatiwe mbegu bora baada ya mafunzo na kutafutiwa masoko,"alisema.

 Alitoa Rai kwa wakuu wote wa mikoa hiyo kuunda vikundi vya vijana na kuendelezwa katika shughuli mbalimbali na kwamba Kambi hiyo iwe endelevu kwani rais mstaafu aliweka jiwe na msingi lakini hakuna kilichoendelea.

 "Tunaomba mambo haya yawe endelevu,kambi iwe mfano wa kuigwa katika mkoa wa pwani kuna zaidi ya ekari 200 ziko hapa kwa hiyo ardhi si tatizo hivyo tukiwatoa vijana vijiweni na wakija hapa msiseme hakuna ardhi maana kambi hii ni yao hivyo iwe endelevu kwa kuwapa mafunzo vijana,"alisema.

MZEE AKILI MALI, ASIMAMISHWA UANACHAMA YANGA, LICHA YA KUOMBA RADHI.



Hatimaye mzee mkongwe katika baraza la wanayanga Yahya Akilimali amesimamishwa rasmi uanachama licha ya kujitetea na kujisafisha.Katika mkutano wa dharura uliofanyika Jangwani leo asubuhi mzee Akilimali alikiri kauli zake na kuwasilisha utetezi.

“Katika watu tunaompenda Manji, mimi namba moja lakini ikumbukwe Mwana umleavyo ndivyo akuavyo, Manji alikuwa anatuita akitaka kufanya jambo. Ila siku hizi hatuiti hatuambii lolote anafanya tu, nimemwambia Manji, mimi ndio nimempa ukuu wa Yanga. Sisi tunampenda kweli Yusuf na nimemtaka radhi jana”.

“Labda niseme hivi Kama kukurupuka ni Tusi kama nilivyomwambia Yusuf, basi naomba radhi kwake Manji na wanayanga wote”. Licha ya kuwasilisha utetezi huo kikao Cha viongozi wa Matawi ya klabu ya Yanga imemsimamisha Katibu wa baraza la Wazee, Yahya Akilimali kwa kile kinachoitwa kumkashifu Mwenyekiti wa klabu hiyo kongwe nchini Yusuph Mehboob Manji.Mzee Akilimali amesimamishwa kwa muda usiojulikana.

Kwa ufupi tuuu wanachama wa Yanga wameomba mzee Akilimali asimamishwe japo kuwa ameomba radhi.