Thursday, July 25, 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI MKUTANO WA KIMATAIFA WA BARABARA.

 

Na Mwandishi Wetu


TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la tisa la Kimataifa la Usafiri Endelevu na Ubunifu Bora ambao umeandaliwa na Chama cha Wataalamu wa Barabara (TARA).


Mkutano huo utakaofanyika jijini Arusha wiki ijayo utafunguliwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 wa ndani na  nje ya nchi.


Mkurugenzi Mkuu wa TARA, Eliamlisi Joseph, alisema jana kuwa mada kuu ya kongamano hilo itakuwa  Usalama, Umakini na Uendelevu wa Mifumo ya Usafiri kwa Ukuaji wa Uchumi Duniani.


Alisema madhumuni ya mkutano  huo wa Kimataifa wa usafiri endelevu na ubunifu bora ni kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya usafiri kuhusu usafiri salama, mahiri na endelevu na mifumo ya ukuaji wa uchumi ulimwenguni kupitia kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu bora.


Alisema lengo ni kuwawezesha wadau katika sekta ya uchukuzi, kuchangia ipasavyo katika maendeleo, utekelezaji na usimamizi wa mifumo endelevu na bora ya usafiri na kutoa jukwaa la kina kwa wadau ili  kuelewa changamoto na fursa za sasa.


Alisema washiriki watapata  maarifa kuhusu mitindo, changamoto na fursa za hivi punde katika sekta ya usafiri, ikijumuisha maendeleo ya teknolojia, mabadiliko ya udhibiti na masuala ya mazingira.


Joseph alisema  washiriki watapewa zana muhimu, mbinu, na mbinu bora za kuboresha uwezo wao wa kitaaluma na michakato ya kufanya maamuzi katika mipango ya usafiri, uendeshaji na usimamizi.


“Hili ni tukio kubwa na la kimataifa ambalo litafunguliwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa na wadau mbalimbali wa nje na ndani  ya nchi watashiriki na wakuu wa taasisi mbalimbali kama Wakala wa Barabara TANROADS, Wakala wa Barabara Vijijini  TARURA na Mfuko wa Barabara,” alisema


Afisa Tawala wa TARA, Anne Nkoma alisema watu watakaoshiriki mkutano huo watapaswa kulipia kiingilio cha 750,000 kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo na wale wenye kampuni watakaokwenda kuonyesha bidhaa zao watalipia sh miliombi mbili.


“Mtu akitaka kudhamini mkutano huu kwa kuleta vifaa mbalimbali kwenye mkutano wetu atapata unafuu wa gharama za kushiriki mkutano,” alisema


Wednesday, July 24, 2024

WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA

 



Na Alodia Dominick  Bukoba,

Wadau mbalimbali  wa uchaguzi hapa nchini wameombwa kuhamasisha jamii kujitokeza wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura. 

Wito huo umetolewa Julai 24, 2024 na mwenyekiti wa tume huru ya taifa ya  uchaguzi Jaji Mbarouk S Mbarouk katika mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi mkoani Kagera ambao ulilenga kutoa taarifa  mbalimbali za maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Amesema kuwa, uzinduzi la daftari la kudumu ulifanyika mkoani Kigoma na Waziri  mkuu wa Tanzania Kasimu Majaliwa na kuwa uzinduzi awamu ya pili utafanyika kuanzia Agosti  05, mwaka huu hadi Agosti 11, mwaka huu katika mikoa ya Kagera na Geita.

Amewaomba viongozi wa dini, makundi mbalimbali ya wenye ulemavu na wanawake kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura na akasema mama  wajawazito, wenye watoto wachanga, wazee na wenye ulemavu watapewa kipaumbele wakati wa kupiga kura. 

Wakati huo huo, Kaimu mkurugenzi wa tume huru ya Taifa ya uchaguzi Giveness Aswile amesema kuwa, tume ya taifa ya uchaguzi inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya mkoani Kagera katika daftari la kudumu wapatao 219,321.

Ameeleza kuwa, kuandikishwa kwa wapiga kura wapya  zaidi ya laki 200 mkoani Kagera ni ongezeko la asilimia 15.5 ya wapiga kura milioni 1.4 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura hivyo tume  baada ya uandikishaji inatarajia mkoa wa Kagera utakuwa na wapiga kura milioni 1.6.

Aidha amevitaja vituo vya kuandikisha wapiga kura kuwa idadi yake ni zaidi ya vituo elfu 40 ambavyo vitatumika katika uboreshaji wa daftari mwaka 2024, vituo elfu 39 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Zanzibar, hili ni ongezeko la vituo zaidi ya 2,000 ikilinganishwa na vituo zaidi ya elfu 37 vilivyotumika mwaka 2019/2020.

Ameongeza kuwa, Kagera vituo vya uandikishaji vitakuwa 1,778 vilivyoongezeka ni vituo  101.

Aidha, ameongeza kwamba zoezi la uboreshaji daftari la kudumu litakuwa la siku saba, kwa Tanzania waligawa zoezi  hilo katika mizunguko13 na sasa wako mzunguko wa pili Kagera na Geita na shughuli za uandikishaji zitakuwa zinaanza saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni wahusika ni kuanzia miaka 18 na kuendelea. 

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, katibu wa chama cha watu wenye ulemavu mkoa wa Kagera (CHAWATA) Sweatbert Bishanga ameiomba tume huru ya taifa ya uchaguzi  kuandaa vitabu maalum vya kupigia kura kwa ajili ya wasioona katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.

Amesema katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais mwaka 2020 wasioona walipewa vitabu ambavyo viliwawezesha kupiga kura wenyewe bila kupigiwa na mtu ili kukwepa kupigiwa kura kwa kiongozi wasiyemuhitaji.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wameomba tume huru ya taifa ya uchaguzi kutumia vyombo vya habari kuelimisha jamii faida za kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

MAONYESHO YA VYUO VIKUU 15 NJE YA NCHI KUFANYIKA ARUSHA

 





Na Mwandishi Wetu

 

VYUO 15 kutoka nje ya nchi vinatarajiwa kushiriki maonyesho yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi jijini Arusha.


Maonyesho hayo ya siku moja yatafanyika siku ya Jumamosi tarehe 27 mwezi huu, kwenye hoteli ya Four point by Sheraton Hoteli, zamani ikijulikana kama New Arusha.


Mkurugenzi wa Global Education Link (GEL), Abdulmalik Mollel, alisema walianza kufanya maonyesho Zanzibar kuanzia tarehe 15 hadi 21 mwezi huu na mahitaji yamekuwa makubwa kwa wanafunzi.


Alisema baada ya kumaliza maonyesho ya Zanzibar GEL ilifanya maonyesho mengine jijini Dar es Salaam lakini kutokana na mahitaji kuwa makubwa kwenye mikoa mingine wameandaa mengine jijini Arusha.


“Maonyesho ya Zanzibar yalifana sana na wanafunzi wamekuwa wengi kwa hiyo tulipoona mahitaji yamekuwa makubwa tumeona tufanye na Arusha siku ya Jumamosi ili wanafunzi wengi  wapate fursa ya masomo,” alisema.


Alisema mwanafunzi atakayeshiriki kwenye maonyesho hayo atapata taarifa zote kuhusu vyuo vikuu nje ya nchi na atakaye taka kudahiliwa atapata udahili hapo hapo.


“ Wanafunzi, wazazi na walezi watumie fursa hii kukutana na wawakilishi wa vyuo vikuu vya nje ya nchi kutoka nchi za Uingereza,  Canada, India, Cyprus, China Iran na vingine vingi vitashiriki kwa hiyo wanafunzi waje kwa wingi tutafungua maonyesho saa tatu na tutayafunga jioni kwa hiyo tukutane Arusha,” alisema.


Meneja wa (GEL)Regina Lema  alisema wamekuwa na kampeni ya muda mrefu ya maonyesho ya vyuo vikuuu nje ya nchi ambapo walianzia visiwani Zanzibar.

 

“Napenda kuwakaribisha wakazi wa kanda ya kaskazini kuja kwenye maonyesho ya vyuo vikuu vya nje ya nchi ili waone fursa mbalimbali zinazopatikana na kutakuwa na udahili wa hapo hapo kwa watakaohitaji kusoma nje ya nchi,” alisema Lema

 

“Kutakuwa  na vyuo vikuu 15 vya nje ya nchi na kutakuwa na fursa ya ufadhili wa asilimia 100 kwa vyuo vikuu vya Irani kwa hiyo sisi GEL tunaona hii ni fursa adimu ambayo wanafunzi wote wanapaswa kuitumia,” alisema

 

 Aidha, alisema walianza maonyesho hayo Zanzibar kuanzia tarehe 15 mpaka 21 mwezi huu na tarehe 23 na 24 maonyesho kama hayo yalifanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.

 

 “Huu ni mwendelezo wa maonyesho ya vyuo vikuu nje ya nchi, tulianza Zanzibar, tukaja Dar es Salaam na sasa tunaelekea Arusha siku ya Jumamosi pale Four point by Sheraton hii ni fursa kubwa siyo ya kukosa,” alisema

Tuesday, July 23, 2024

CTI WADAU WA VIWANDA WATETA KUHUSU DIRA YA TAIFA 2050.

 


Na Mwandishi Wetu


SHIRIKISHO la Wenye Viwanda (CTI), limependekeza maendeleo ya viwanda yapewe kipaumbele kwenye Dira ya Taifa ya 2050.


 


Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa CTI, Leodegar Tenga wakati wa mjadala wa wadau wa viwanda wakijadili Dira ya 2050 na kuzungumzia maendeleo ya viwanda kwa ujumla.


 


Mkutano huo ulioandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), pia ulizindua tuzo za Rais za Mzalishaji Bora Viwandani PMAYA ambazo hufanyika kila mwaka kwa wenye viwanda.


 


Tenga alisema hakuna  nchi duniani hata moja ambayo iliwahi kupiga hatua kubwa kiuchumi bila kuwekeza kwenye viwanda kwa hiyo lazima kuwe na mikakati madhubutu ya kukuza viwanda.


 


“Kuna msemo wa Kiswahili kwamba kupanga ni kuchagua kwa hiyo tuchague kuwekeza kwenye viwanda ili tusonge mbele na ili viwanda vifanye kazi vizuri lazima tuwe na watalamu wetu kwa hiyo tena lazima tuwekeze kwenye elimu bora,” alisema Tenga


 


Alisema ili viwanda viweze kufanya kazi vizuri, lazima serikali iwekeze pia kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli na kuwekeza kwenye rasilimali watu.


 


“Maono ya nchi ni kujipanga ili tutimize tulichopanga kwa hiyo sisi CTI tunaamini viwanda ni muhimu na ili kupata rasilimali lazima tuwe na kilimo kwa hiyo lazima tuwekeze pia kwenye kilimo,” alisema


 


“Tumefungua masoko mengi upande wa Afrika Mashariki (EAC),  kusini mwa jangwa la sahara (SADC) sasa tujipange kuuza bidhaa zetu za viwandda nje ya nchi badala ya sisi kuwa soko la bidhaa za wenzetu,” alisema Tenga


 


 Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo alisema katika maandalizi ya Dira ya Taifa  2050 imeweka kipaumbele kikubwa kwenye maendeleo ya ya viwanda nia ikiwa ni  kuondoa utegemezi wa kununua bidhaa nyingi nje ya nchi.


 


Profesa Mkumbo alisema wasomi mbalimbali wamesema kwenye maandiko yao kuwa tofauti kubwa baina ya nchi tajiri na zile maskini ni kwamba nchi tajiri zina viwanda vingi wakati nchi maskini hazina viwanda na zinategemea kununua bidhaa nje ya nchi.


 


“Itakuwa vigumu sana kutengeneza Dira ya Taifa bila kuweka viwanda katikati ya dira hiyo kwasababu hilo ni la msingi na tafiti nyingi zinaonyesha kuwa hatuwezi kuendelea kwa kuendelea kununua bidhaa nje ya nchi, lazima tuwe na viwanda vingi tuuje  nje,” alisema


 


Alisema katika utafiti ambao umefanywa na serikali katika maandalizi ya dira hiyo uliohusisha watu 7,668 nchi nzima waliochaguliwa kisayansi walitaka vipaumbele vitano viwepo kwenye dira hiyo.


 


Alitaja moja ya kipaumbele kilichotajwa na wananchi hao kuwa ni suala la viwanda na kwamba asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani zinatokana na kilimo  hivyo kilimo nacho kitaendelea kuwa kipaumbele kwenye dira hiyo.


 


Alisema kipaumbele kingine kilichotajwa kwenye utafiti huo ni uwekezaji mkubwa kwenye rasilimali watu kwani uchumi wa viwanda unahitaji watu waliosoma vizuri.


 


“Lazima dira yetu ituelekeze kuwekeza kwenye elimu na siyo elimu tu bali elimu iliyobora,” alisema Profesa Mkumbo.


 


Monday, July 22, 2024

RAIS DKT. SAMIA AFANYA UTEUZI NA KUHAMISHA NA KUTENGUA BAADHI YA VIONGOZI.

 





DC OKASH AWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM BAGAMOYO.

 

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash tarehe 20 Julai, 2024 amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM mbele ya Halmashauri Kuu  ya CCM Wilaya ya Bagamoyo kuanzia Januari hadi Juni 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.


 Akiwasilisha taarifa hiyo mkuu huyo wa wulaya, alisema kuwa, kwa ujumla Halmashauri zote mbili  zimeendelea kufanya vizuri katika nyanja zote hasa upande wa ukusanyaji wa mapato, miundombinu ya Elimu na Afya.


 "Waheshimiwa wajumbe kwa upande wa ukusanyaji mapato mfano Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo kwa Mwaka wa fedha 2023/24 ilipanga kukusanya bilion 5.8 lakini kwa ujumla imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 6.3 sawa na aslimia 106 haya ni mafanikio  makubwa.Alisema Mhe. Okash.


 Hata hivyo,Mhe Okash alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa wa Tanzania Dkt. Samia  Suluhu Hassan kuwapatia Fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo pamoja na uboreshaji wa huduma za afya, maji na umeme.


 Halmashaurji Kuu ya CCM Wilaya ya Bagamoyo iliridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha kuanzia January hadi June 2024.











Thursday, July 18, 2024

GLOBAL EDUCATION LINK YADAHILI WANAFUNZI MAONYESHO YA VYUO VIKUU ZANZIBAR.

 






Na Mwandishi Wetu


WAKALA wa Elimu ya Vyuo Vikuu nje ya Nchi Global Education Link (GEL), imeanza kudahili wanafunzi papo hapo kwenye maonyesho yanayoendelea kwenye viwanja vya Maisala visiwani Zanzibar.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa GEL, Abdulimalick Mollel, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonyesho hayo yanayoendelea visiwani humo.


Alisema kwenye maonyesho hayo kuna vyuo vya nje ya nchi ambavyo vimetoa udhamini wa asilimia 50 kwa wanafunzi wanaotaka kwenda kusoma kwenye vyuo hivyo na vingine vimetoa ufadhili wa asilimia 100.


“Tumeleta wawakilishi wa vyuo 20 kutoka Irani kuna ufadhili wa asilimia 100 analipiwa kila kitu na kuna vyuo ambavyo mwanafunzi atalipiwa asilimia 50 ya ada kwa hiyo mwanafunzi akija kwenye maonyesho haya akichagua kozi GEL tunamdahili hapahapa,” alisema


Alisema lingine la manufaa kwenye maonyesho hayo ni uhusiano wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi kwani uzoefu unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya wahitimu wa vyuo vya nje ya nchi wanaajiriwa mara tu wanapomaliza vyuo.


Alisema mara nyingi wanafunzi wanaohitimu vyuo vya hapa nchini huanza kuhangaika kutafuta ajira kwenye maeneo mbalimbali na kulalamikia ugumu wa ajira wakati vyuo vya nje hali ni tofauti kwa wahitimu wao.


“Vyuo vya nje vinafanikiwa kutoa wahitimu ambao wanaajiriwa mara tu wanapohitimu ndiyo maana tumewakutanisha na vyuo vya ndani ili waweze kubadilishana maarifa, wao wanafanyaje kuwaaandaa wanafunzi tunaangalia je ni suala la mitaala au ushirikiano mwema na taasisi za ajira,” alisema


“Kwa hiyo tulicholeta hapa ni ushirikiano baina ya vyuo hivi kama kuna chuo kikuu cha hapa ndani kilichoko tayari kushirikiana na chuo chochote cha nje watakutana na kubadilishana ujuzi na maarifa mbalimbali ili waweze kutoa wahitimu bora,” alisema


Alisema lingine ni fursa ya kupata udahili kwani baadhi yao wamekuwa wakikosa nafasi za kujiunga na vyuo vikuu kutokana na ufinyu wa nafasi kwenye baadhi ya kozi wanazoomba hasa zile za afya na uhandisi.


Mollel alisema idadi ya wanafunzi wanaoomba nafasi za kozi za afya na uhandisi ni wengi kuliko nafasi zilizopo hivyo kuna umuhimu wa kuwatafutia nafasi kwenye vyuo mbalimbali nje ya nchi.


“Tumekuja na vyuo hapa ambavyo vinaruhusu wanafunzi kudahiliwa hapa nchini akasoma kwenye chuo cha nje kwa miaka kadhaa kisha akarudi kumalizia elimu yake hapa Tanzania kwa hiyo sisi tunaona hii ni fursa kwa vijana wetu,” alisema.


Aidha, alitoa wito kwa wanafunzi wa Zanzibar na wadau wa elimu kuwa dunia imekuwa kama kijiji hivyo wanatakiwa kutumia fursa za nje kwani hata gharama za masomo kwenye vyuo vya nje zinalingana na za masomo ya hapa nchini.


“Watanzania wachangamkie fursa za ufadhili wa vyuo vikuu wasidharau kwasababu tuna mtindo wa wa kudharau kwasababu ya kuogopa kujaza fomu zenye maelezo mengi lakini sisi tuna ofisi hapa Zanzibar waje tutawatafsiria maelezo hayo,”


“Unaweza kukuta fomu moja ya scholarship inakaratasi hadi 13 sasa kwa mwanafunzi ni mara yake ya kwanza kuomba ufadhili anakata tama lakini kwa kuwa tuko hapa waje tuwaelekeze na tuko hapa kufungua fursa zilizoko duniani ili wanafunzi waweze kusoma nje,” alisema


Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Hussein Mwinyi kwa kuonyesha utayari wa kushirikiana na Global Education Link kuendelea kuwatafutia fursa za elimu ya juu nje ya nchi.


Tuesday, July 16, 2024

MABASI 100 MWENDOKASI YANAKUJA

 

Na Mwandishi wetu 



SERIKALI iko mbioni kuleta mabasi 100 ya mwendokasi nia ikiwa ni kuongeza nguvu kwenye eneo la huduma ya usafiri kwa Jiji la Dar es Salaam 


Msajili wa Hazina Nehemiah Kyando Mchechu amesema hayo jana kwenye kikao maalum na Wahariri kuwa mabasi 100 yatanunuliwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya NMB.

 


Mchechu amesema kwa kipindi cha miezi miwili amekuwa akifanya vikao na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Kampuni ya Mabasi Yendayo Haraka (UDART), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na sasa wamefikia ukingoni.


"Nimekuwa na vikao nao vya mara kwa mara na wadau hawa ili kuokoa hii hali  maana tumeona inaenda kuleta crisis (maafa) na kuathiri taswira nzuri ya Serikali kwenye mradi huu” amesema Mchechu.


Kwa mujibu wa Mchechu mabasi hayo yatakuwa yamewasili nchini ndani ya miezi sita ijayo ili kusaidia kutatua changamoto ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi kwa mkoa wa Dar es Salaam.


Kauli ya Mchechu imekuja wakati kukiwa na malalamiko kwa wadau na wananchi juu ya ubora wa mabasi hayo kutokana na mrundikano wa watumiaji pamoja na uchache wa usafiri huo kulinganisha na mahitaji yaliyopo.


Mbali na changamoto hizo baadhi ya mabasi hayo pia ni machakavu na pia yapo katika mfumo wa kizamani kwa  kutokidhi mahitaji ya watumiaji ikiwemo wenye ulemavu na wazee.


Pia msajili wa hazina amesema ni muhimu sana kwa mji kama Dar es Salaam kuwa na kampuni za usafiri zaidi ya moja zitakazosaidiana kutoa huduma hiyo kwa wananchi.


Mwaka jana Oktoba 24, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed  Mchengerwa aliuelekeza uongozi wa Dart kuongeza watoa huduma ili kuboresha huduma ya usafiri huo.


Aidha, Mchechu ameitaka Dart ifikapo Agosti mwaka huu kuhakikisha wametengeneza mifumo ya ukusanyaji fedha ili kudhibiti mapato na kupunguza wizi. 


“Kuna wizi mwingi unafanyika kwenye cash, mimi huwa nasema ni ‘headache’ kusimamia huu mradi kwenye suala la malipo. Tumekubaliana na Dart kuwa hadi Agosti 2024 wawe wamekamilisha mfumo wa nauli kwa njia ya mtandao.” amesema Mchechu


WAZIRI MKUU AZINDUA MITAMBO YA KISASA YA KURUSHIA MATANGAZO.

 





Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Julai 15, 2024 amekagua na kuzindua mitambo na vifaa vipya vya kurushia matangazo vya kampuni ya Azam Media Limited.


Vifaa hivyo ni pamoja na Magari ya kisasa ya kurushia matangazo (OB Van), kamera za kisasa pamoja na mfumo wa kusaidia maamuzi viwanjani (VAR).


Vifaa hivyo vilivyogharimu shilingi bilioni tano vitatumika katika kurushia matangazo ya mpira wa miguu wa ligi Kuu Tanzania bara na Zanzibar pamoja na michezo mingine.


Akizungumza na wafanyakazi wa Azam Media pamoja na wadau wa michezo Mheshimiwa majaliwa amesema manunuzi ya vifaa hivyo ni mapinduzi makubwa katika tasnia ya habari kwani kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya kipekee kuwa na vifaa vya kisasa vya aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Mheshimiwa Majaliwa pia ameshuhudia uzinduzi wa chaneli mpya ya Azam 4 HD ambayo itatumika kurusha ligi kuu ya Ufaransa (Legue 1) na ligi kuu ya Ujerumani (Bundesliga)