Thursday, August 15, 2024

OMBI LA WAKILI WA UTETEZI KESI YA WANANDOA KUJERUHI LAGONGA MWAMBA MAHAKAMANI

 

Bharat Nathwani mbele  na mke wake Sangita Nathwani  nyuma kabisa wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam kusikiliza kesi inayowakabili ya kumjeruhi jirani yao inayowakabili.

................................................

Na Mwandishi Wetu


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imekataa ombi la wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) la kutaka shahidi Kiran Ratilal awasilishe kipande kifupi cha video (clip) kinachoonesha alivyotumbukizwa kwenye ndoo ya mchanganyiko wa saruji.


Nathwan na Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.


 


Ombi hilo liliwasilishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Aaron Lyamuya na Wakili wa Utetezi Edward Chuwa kwa niaba ya wateja wake, wakati Kiran Lalit Ratilal alipokuwa akiulizwa maswali ya dodoso kutokana na ushahidi wake aliyoutoa dhidi ya washtakiwa hao.


 


Wakili Chuwa alimuuliza Kiran Lalit Ratilal ambae ni shahidi wa nne katika kesi hiyo, kama ni kweli kwenye ushahidi wake alidai kuwa anayo clip inayoonesha alivyotumbukizwa kwenye ndoo hiyo na upo tayari kuitoa,  alidai ni kweli anayo, lakini kwa wakati huo hana.


 


"Kwa hiyo umeomba kuitoa mahakamani kama kielelezo kutokana na maelezo yako uliyoyatoa,"alidai Wakili Chuwa


 


Baada ya Chuwa kudai hivyo, Hakimu Lyamuya alimueleza kuwa shahidi hakuomba kutoa kipande hicho, lakini Wakili Chuwa aliendelea kudai kuwa wanataka itolewe kama ushahidi.


 


Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraji Nguka alidai kuwa wao hawako tayari kutoa kielelezo hicho, lakini kama Chuwa anataka kufanya hivyo wanaweza kukitoa wao katika utetezi wao kwa kufuata utaratibu.


 


Wakili Chuwa alidai kuwa kama kuna hatua za kufuata yeye hazikumbuki, ndipo Hakimu Lyamuya aliwaeleza kuwa kuna taratibu za kisheria shahidi kutoa kielelezo wakati wa kipindi cha maswali ya dodoso zinatakiwa zifuatwe.


 


"Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wake katika shauri la Lilian na Jesus ya mwaka 2018 ilitoa utaratibu, kwa hiyo Chuwa kama ulitaka kufanya hivyo ulitakiwa kufuata taratibu kwenye hiyo rufaa imeonesha hatua kwa hatua,"


 


"Ombi hili linakuja randomly, ombi hili limekataliwa,"alisema Hakimu Lyamuya


Baada ya Hakimu Lyamuya kusema hivyo, Wakili Chuwa alidai kuwa wamemaliza maswali ya dodoso kwa shahidi.


 


Wakili Nguka alimuuliza shahidi baadhi ya maswali ( Re-examination) kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kwa mahakama, alidai upande wa utetezi ulimuuliza sana uhusiano wa mume wake na Hospitali ya Regency, akadai kuwa mume wake sio daktari ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo.


 


Wakili huyo, aliiomba mahakama iwapangie tarehe ya karibu ili walete mashahidi wengine katika kesi hiyo na kudai kuwa wapo tayari kuendelea hata leo.


 


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 30, 2024 saa tatu asubuhi kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.


Wednesday, August 14, 2024

MKUTANO WA MICO HALAL WAIBUA MAMBO KUHUSU UMUHIMU WA BIDHAA ZA HALAL

 


Na Mwandishi Wetu

 

UKUBWA wa soko la bidhaa za Halal duniani umeendelea kuongezeka kutoka Dola trilioni 1.2 miaka 10 iliyopita hadi kufikia dola trilioni 2.29 mwaka jana.

Hayo yamesemwa leo  tarehe 14 Agosti 2024 na mtoa mada Salum Awadh wakati akizungumza kwenye kongamano la pili kuhusu mwenendo, fursa na maendeleo ya soko la bidhaa za Halal duniani wakati wa kongamano hilo ambalo limeandaliwa na MICO Halal International Bureau.

Alisema ongezeko hilo ni kubwa na linaonyesha mwamko mkubwa kwa watu kutumia bidhaa za Halal kwenye maeneo mbalimbali duniani kuanzia kwenye bidhaa na utoaji wa huduma.

Alisema soko la Halal liko kwenye maeneo  kuanzia ya chakula, fedha, dawa, mavazi, vyombo vya habari na  usafiri.

“Fursa la bidhaa za Halal ni kubwa sana hasa ukiangalia waislamu wanawajibika kutumia bidhaa za Halal na hata wasio waislamu wanaweza kutumia bidhaa za Halal,” alisema

Alisema watanzania wanapaswa kutumia ongezeko la matumizi ya bidhaa za Halal kama fursa ya kutengeneza fedha kwani soko lake limeendelea kuongezeka siku hadi siku.

“Kwenye soko la OIC pekee kuna soko kubwa sana kwasababu watumiaji wa bidhaa za Halal ni wengi sana. Soko liko kubwa hapa nchini, liko Afrika na dunia nzima soko lipo ni wananchi wenyewe kuchangamkia fursa,” alisema

Alisema serikali imekuwa ikihamasisha watu kupeleka nyama kwenye masoko ya mataifa ya uarabuni kama United Arab Emirates (UAE) na Saudi Arabia ambazo zimekuwa zikizingatia matumizi ya bidhaa za Halal.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam, Shamim Khan, alipongeza MICO Halal kwa kuandaa kongamano hilo ambalo litawasaidia wafanyabaiashara kujua namna ya kuzingatia misingi ya Halal kwenye bidhaa zao.

“Nawapongeza sana MICO Halal kwa kuleta hili kongamano kwasababu tulikuwa tunajua maana ya Halal lakini hatuishi kwa kufuata misingi ya Halal kwa hiyo elimu hii itawezesha sisi tuishi kwa kufuata Halal,” alisema

“Lazima tujue unapokwenda supamaketi unanunua kitu kilichofuata Halal kinakuwa kwenye mwonekano gani na kama kimezingatia hasa misingi ya bidhaa za Halal, lazima tujue kitu gani ni halali na kitu gani ni haramu” alisema

Friday, August 9, 2024

MADAKTARI BINGWA KUTOKA INDIA KUFANYA UPASUAJI WA MAGOTI NA NYONGA DAR ES SALAAM.

 


Ni matunda ya ziara ya Rais Samia India

·      Wagonjwa nje ya nchi sasa kumiminika kutibiwa hospitali za Tanzania

Na  Mwandishi Wetu

DAKTARI  bingwa wa upasuaji wa magoti na nyonga kutoka  hospitali maarufu duniani YASHODA iliyoko mji wa Hyderabad nchini India, Dk. Ram Mohan Reddy na wenzake, wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi huu kwaajili ya kutoa matibabu ya upasuaji wa kibingwa wa magoti na nyonga.


 

Madaktari hao watafanya upasuaji huo  kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa upasuaji wa magoti na nyonga  wazawa katika Hospitali ya Taifa  Muhimbili- tawi la Mloganzila ambapo matibabu hayo ya kibigwa yatafanyika.


 

Mkurugenzi mtendaji wa Global Medicare, ambao ni  mawakala wa tiba utalii nchini, Abdulmalik Mollel, alisema madaktari hao watafanya upasuaji wakibingwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la  Mloganzila kuanzia tarehe 26 hadi 28 mwezi huu Agosti 2024.

 
 

Mollel alisema madaktari hao  bobezi  watashirikiana na madaktari bingwa wazawa kwenye kambi hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo madakitari wa ndani kwa kubadilisha uzoefu ambao utawapa ujunzi  zaidi madaktari wenyeji ambao utawawezesha kufanya upasuaji kama huo hata baada ya kuondoka kwa daktari huyo mgeni.


 

“Mwaka jana tulifanya kambi kama hii ya upasuaji na ilikuwa na mafanikio makubwa sana kwasababu kulikuwa na watu zaidi ya 2,300 waliokuwa wanahitaji huduma hiyo  na madaktari wetu walifanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na wale wa nje na tunatarajia daktarin huyu bingwa na bobezi na wenzake katika matibabu ya upasuaji wa nyonga na magoti watawafanyia watu wengi watakao jitokeza mapema nakufanyiwa uchunguzi wa awali,” alisema

 
 

Alisema baada ya uchunguzi wale watakao ngundulika wanahitaji matibabu hayo ya kibingwa ya upasuwaji watafanyiwa.

 
 

Aliongeza kwa kusema, kwa muda mrefu watanzania wenye matatizo ya afya walikuwa wakienda nje ya nchi kwa matibabu lakini baada ya serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya watanzania wengi sasa wamekuwa wakitibiwa  hapa nchini.

 
 

Mollel alisema serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye vifaa tiba kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa kama iliyoko kwenye mataifa makubwa duniani na imesomesha wataalamu bobezi ( super specialist)  wa fani mbalimbali kwenye tiba.



 

“Tanzania kwa sasa inavifaa vya kisasa vya kutosha na wataalamu bobezi kama walioko nchini India na kwingineko kwa hiyo sasa ni muda muwafaka madaktaari bobezi wa nje waje hapa nchini kujengeana uwezo (Capacity building)  na wenzao wa ndani ambao wamekuwa wakifanyakazi kubwa sana kwaajili ya Taifa,” alisema  Mollel ambaye pia ni Mkurugenzi wa Global Education Link (GEL).

 

Alisema huduma za madaktari wabobezi zinazopatikana hapa nchini zimewavutia watu wengi wa nchi jirani kuja kutibiwa hapa nchini badala ya kwenda nchi za nje kufuata tiba kama hiyo ambapo hutumia muda mwingi na gharama kubwa ukilinganisha na kuja hapa nchini.

 


“Kuja kwa madakatri hawa wabobezi ni jambo jema sana kwasababu madaktari wetu watachukua zile teknolojia ambazo zitakuwa hazijafika hapa nchini nasisi kama tuna ujuzi ambao tumewazidi wanachukua  na kwa uwekezaji uliofanywa na serikali katika sekta ya afya Tanzania sasa ni kitovu cha utalii tiba kwa nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa jangwa la sahara,” alisema Mollel.

 

“YASHODA ni miongoni mwa hospitali kubwa duniani inayopatikana nchini India yenye vitanda 4,000 kwa hiyo inafanya vizuri sana na mwaka jana mwezi wa tano ujumbe wa madaktari bingwa wa Tanzania walienda kujifunza, hivyo basi, wao wana kitu gani tofauti na hivi tulivyonavyo, tulijifunza wana mazingira gani yanayosababisha watu duniani kupendelea kwenda kutibiwa kwao,” alisema
 

 

Aidha, alisema  lengo lilikuwa ni kujifunza yale ambayo yamewafanya wawe bingwa kwenye utalii tiba duniani na kuja kutekeleza nchini yale ambayo wameyafanya yakawapa sifa ya kuwa kitovu cha utalii tiba na kupata wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

 

“Moja ya mafanikio ya ziara tuliyofanya India mwaka jana ni ujio wa madaktari kutoka YASHODA ambayo ni moja ya hospitali tulizotembelea zenye ubora na viwango vya daraja la kwanza duniani na ina madaktari mahiri na wenye mtandao mkubwa duniani kutokana na ubobezi wao,” alisema

 


GLOBAL EDUCATION LINK YATOA VISA 100 KWA WANAOKWENDA KUSOMA NJE YA NCHI

 

Na Mwandishi Wetu


 WAKALA wa Elimu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL), imetoa Visa 100 kwa kundi la kwanza la wanafunzi wanaotarajia kuanza kwenda kwenye vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi kuanza masomo hayo kuanzia wiki ijayo.


Hiyo inakuja ikiwa zimepita wiki mbili tu tangu matokeo ya kidato cha sita kutoka ambapo mamia ya wanafunzi wa Tanzania wenye kuhitaji kusoma nje ya nchi kupitia GEL wameshaanza kufanya maandalizi ya kuondoka kuanzia wiki ijayo.


Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Global Education Link Abdulmalik Mollel, wakati akigawa Visa 100 kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuondoka wiki ijayo na amezungumza na wazazi na wanafunzi wanaotarajiwa kwenda nchini humo.


 Mollel alisema lengo la mkutano huo ni kukabidhi Visa, kujadili na wazazi na  wanafunzi kuhusu mambo mengi ya kuzingatia katika maandalizi ya safari yao, kuwakutanisha wazazi na wanafunzi na wawakilishi wa vyuo vikuu ambavyo wanafunzi hao wanatarajia kwenda kusoma pamoja na wanafunzi kujaza nyaraka mbalimbali.


 “Leo tumekutana na wanafunzi hawa kuwapa viza zao ambazo zimekamilika kuwapa bima za afya kuwaeleza tarehe za kusafiri ndege watakazotumia kusafiria, kujua sehemu watakazokaa, watasafiri na nani na watapokelewa na nani,” alisema Mollel


“Wataanza kuondoka kwenda kwenye vyuo vikuu mbalimbali duniani kuanzia wiki ijayo na baada ya hapo kila wiki kundi la wanafunzi kuanzia 50 mpaka 70 watakuwa wanaondoka kwenda mataifa mbalimbali,” alisema Mollel.


Mollel aliwataka wanafunzi kuzingatia walichofuata nje ya nchi na kuachana na starehe na badala yake wazingatie masomo na kuhakikisha wanahitimu wakiwa na alama nzuri ili kuwapa moyo wazazi ambao wamejinyima kwaajili yao kuwalipia ada.


Alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa na kawaida ya kufanya mambo ambayo yanasababisha washindwe kumalizia masomo yao hali ambayo inawakatisha tamaa wazazi wao.


“Msiende kunywa pombe wala kwenda klabu za usiku kwasababu kule mnakwenda kufuata elimu. Malizeni masomo mpate kilichowapeleka starehe hata Tanzania zipo,” alisema Mollel


Aiman Mohamed kutoka Mwanza ambaye anatarajia kwenda masomoni nchini India wiki ijayo, alisema anashukuru uratibu uliofanywa na Global Education Link na kumwezesha kupata chuo cha Sharda cha nchini India.


“Kwa dhati kabisa niwapongeza waratibu wa safari yetu Mollel na wenzake kwa namna walivyokuwa karibu nasisi wakati wote wa kuratibu safari na hatimaye mambo yamekuwa mazuri na wiki ijayo tunasafiri kwenda masomoni kutimiza ndoto zetu,” alisema


Rita Nichalaus naye kutoka Mwanza ambaye anatarajia kujiunga na chuo kikuu cha Sharda kilichoko New Delhi India alisema amefurahi kupata elimu ya mambo ambayo wanatakiwa kufanya na ambayo hawatakiwi kuyafanya wanapokuwa masomoni.


“Mwongozo tuliopewa ni muhimu sana kwasababu mwanafunzi anapofika ugenini asipofahamu tabia na tamaduni za wenyeji anaweza kujikuta yuko matatizoni lakini tumeelezwa namna ya kuishi tukiwa huko ni jambo jema na la msingi sana kwetu,” alisema







Tuesday, August 6, 2024

KESI YA WANANDOA KUJERUHI, WAKILI WA SERIKALI AKATAA KESI KUAHIRISHWA.

 

Bharat Nathwani mbele  na mke wake Sangita Nathwani  nyuma kabisa wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam jana kusikiliza kesi inayowakabili ya kumjeruhi jirani yao inayowakabili.

....................................

Na Mwandishi Wetu


UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kujeruhi inayowakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) wamekataa kuahirishwa kesi kwa madai kuwa wakili wa utetezi anataka kuchelewesha kesi hiyo kwa kudai kuwa anashida ya kiafya.


 


Aidha, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam iliomba pande zote mbili katika kesi hiyo kutumia lugha za kuheshimiana ndani ya chumba cha mahakama kwa sababu kuna watu wanajifunza kutoka kwao.


 


Ombi hilo la kukataa, liliwasilishwa jana Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo, wakati shahidi Kiran Ratilal akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Utetezi, Edward Chuwa.


 


Mwanga alifikia hatua hiyo, baada ya Wakili Chuwa kuomba ahirisho la maswali ya dodoso kwa shahidi Ratilal, kwa madai kuwa hawezi kuendelea kwa sababu ya afya yake na pia kuna dawa za kutumia.


 


Baada ya Chuwa kudai hayo, Mwanga alidai kuwa hawawezi kukubali ahirisho kwa sababu, wakili huyo alitakiwa kulisema hilo mapema kabla kesi haijaanza kusikilizwa kuwa ikifika muda fulani waahirishe.


 


"Jamhuri hatuwezi kukubali, wakili alitakiwa kulisema hili mapema anachokifanya ni kutaka kuchelewesha kesi hatuwezi kukubali kuahirisha tunaomba amalize maswali ya dodoso kwa shahidi,"


 


" Mara ya mwisho alisema anaenda Mahakama Kuu, lakini alivyotoka nje alikuwa anazungumza na vyombo vya habari na pia hakusema anaenda kwenye kesi gani,"alidai Wakili Mwanga


 


Hata hivyo, Chuwa alidai kuwa siku hiyo hakusema anakwenda Mahakama Kuu, alidai kuna kazi anakwenda kuifanya na pia alikuwa akizungumza na media saa ngapi?


 


"Naenda kuonana na daktari katika Hospitali Hindul Mandal na siku ya kesi ninaweza kuja na ushahidi hapa mimi nina umri wa miaka 60, nimeomba ahirisho kwa sababu ya ugonjwa,"alidai Wakili Chuwa


 


Hakimu Lyamuya alisema yeye hayuko kwenye nafasi ya kusema kama Wakili ni mgonjwa au sio mgonjwa kwani hali hiyo ni  vile ambavyo mtu mwenyewe anajisikia.


 


"Kwa sababu umesisitiza kwa umri wako wa miaka 60, mahakama inaahirisha kesi hii kwa nafasi ya mwisho ya kufanya maswali ya dodoso ni haki yako, lakini siku ya kesi itakayotajwa inatakiwa ifike mwisho tusiipeleke hii kesi mbali sana,"alisema Hakimu Lyamuya


 


Pia, Hakimu Lyamuya aliwataka watumie lugha ya kuheshimiana pale wanapouliza maswali kwa sababu ni watu wengi wanasikiliza, lakini pia kuna wanafunzi washeria ambao wanajifunza kila kitu kutoka kwao.


 


Hakimu Lyamuya alifikia hatua hiyo, baada ya Wakili Chuwa kumtuhumu Wakili Mwanga kuwa anamsaidia shahidi, baada ya kupinga shahidi wake kuulizwa swali ambalo tayari alishalijibu.


 


"Mheshimiwa mimi sijamsaidia shahidi kujibu swali bali ninepinga shahidi kuulizwa swali hilohilo ambalo tayari alishalijibu,"alidai Mwanga


 


Kesi imeahirishwa hadi Agosti 15,2024 kwa ajili ya upande wa utetezi kuendelea kumuuliza masawali ya dodoso shahidi.


 


Nathwan pamoja na mke wake Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam


wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.


RAIS SAMIA AACHA ALAMA YA KIPEKEE MOROGORO.

 

Maelfu wanufaika na msaada wa kisheria


Wamshukuru na kutaka huduma ziwe endelevu


 


Na Mwandishi Wetu


RAIS Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Morogoro huku akiacha alama kubwa kwa uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na timu ya wanasheria waliosaidia kutoa msaada wa sheria bure kwa maelfu ya wananchi.


Wananchi  wengi walifurahia msaada wa kisheria walioupata kutoka kwa wanasheria wa mpango wa mnsaada wa sheria wa Mama Samia Legal Aid ambao bado wanaendelea kutoa msaada kwenye viwanja vya nane nane mkoani hapa.


Kulikuwa na timu ya wanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria waliokuwa wakisikiliza kero za kisheria kwenye ziara hiyo na kuzitatua na kulikuwa na timu ingine ya Rais Samia ambayo inaendelea kutoa huduma hiyo katika maonyesho ya nane nane yanayoendelea mkoani Morogoro.


Baadhi ya wananchi wametoa ushuhuda wa namna walivyonufaika na ziara ya Rais Samia kwa huduma za msaada wa kisheria walizopata kwenye ziara hiyo.


Mmoja wa wananchi waliopata msaada wa kisheria kutoka kwa Mama Samia Legal Aid anasema amefurahia mpango huo kwani umekuw mkombozi kwa watu ambao hawana uwezo wa kuweka mawakili.


“Mpango wa Mama Samia imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi napendekeza kama itampendeza Rais Samia hii isiwe tu kampeni maana kampeni inaisha muda ila ikiwa Taasisi ya kudumu itawasaidia sana wananchi wanyonge ambao wanapambana sana kusaka haki zao kisheria.”


Mkazi mmoja wa mkoani Morogoro  Juma Hamadi ambaye akipata msaada wa kisheria nane nane  alisema alisema  amepata huduma kwa ukarimu wa hali ya juu kwa watumishi wa mpango wa mama Samia na anatarajia matatizo yake ya mgogoro wa shamba yatamalizika.


Anasema wananchi wengi hawana uwezo wa kuweka mawakili kusimamia kesi zao hivyo aliomba serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kuufanya mpango huo wa msaada wa sheriaa kuwa endelevu.


Mwanaidi Selamani alisema  alitembelea banda hilo la sheria la Mama Samia na amekutana na amepata ufumbuzi wa matatizo yake ya mgogoro wa nyumba ambao ulikuwepo kwa muda mrefu Kibaigwa.


“Hapa kwa msaada wa Rais Samia tunapata msaada wa kisheria bure tunamshukuru Rais Samia huyu mama anawapenda wananchi wake kwa kweli apewe maua yake hii huduma ni mkombozi kwetu,”anasema.


Mkazi wa Morogoro Mjini, Antony Gervas, yeye anasema huduma za msaada wa sheria ziwe endelevu kwani wengi hawana uwezo na kuongeza kuwa katika maonesho ya nanenane amejifunza kupitia kampeni hiyo itasaidia wananchi wengi wasiokuwa na uelewa wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali.


 


“Kwa mpango huu Rais Samia anastahili kupongezwa sana na namshukuru  kwa kampeni hii ambayo imepiga kambi hapa nanenane Morogoro kwasababu itawasaidia wananchi na watanzania kwa ujumla kupata haki zao,”anasema.


 


Naye, Ibrahim Waso mkazi wa Arusha ambaye alihudhuria maonyesho hayo Nane Nane Morogoro  anasema amepata huduma nzuri kwenye banda la kampeni hiyo na amejifunza mambo ya kisheria ya kufuata na kutoa elimu kwa wananchi wenzao wa vijijini.


“Tumepewa namba za kupiga kwa ajili ya msaada wa kisheria tutawapa watendaji wasambaze kwa wananchi ili wanufaike na huduma hii ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, tunamshukuru sana Rais hakika mama anaupiga mwingi kwa wananchi wake,”anasema.


Mkazi wa  Kihonda Morogoro ,  Jamila Abdalah anasema amefarijika kupata huduma nzuri ambayo hakutegemea kuipa ya elimu ya masuala ya sheria.


“Nampongeza sana Rais kwa kuona umuhimu wa kampeni hii, kweli watu wengi hapa nchini hawana uwezo wa kuweka mawakili  na tunajua mawakili ni ghali lakini ameliona hilo na kuleta kampeni hii ambayo itawasaidia sana watanzania tunashukuru sana,”anasema.  


Kampeni hiyo hadi sasa imewafikia wananchi zaidi ya 490,000 wa mikoa saba na kutatua migogoro iliyokuwa ikiwakabili.


Kampeni hiyo inafanyika kwa miaka mitatu na ilianza mwezi Machi, 2023 hadi mwezi Februari, 2026 kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ikilenga kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza.


WATANZANIA WAHIMIZWA KULA NA KUNYWA BIDHAA ZA KOROSHO

 

NA HADIJA OMARY , LINDI.


Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Ikulu (kazi maalum)  George Mkuchika Amewahimiza watanzania kupenda Kula na kunywa bidhaa za korosho kwani zinavirutubisho vingi vya kupambana na magonjwa pamoja na kufanya uhamasishaji wa  uongezaji wa thamani ya zao hilo.



Mkuchika ametoa Rai hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi, Wadau na wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakati wa maadhimisho ya siku ya Kula na Kula korosho ambayo ni mahusisi kwa ajili ya uhamasishaji wa ulaji na unywaji korosho.


Katika maadhimisho hayo Wananchi Wadau na wakulima wa korosho walijionea bidhaa mbalimbali zitokanazo na korosho kama vile chapati, maandazi, kashata , maziwa ya korosho pamoja na mvinyo.


Amesema ulaji wa  korosho licha ya kumlinda Mlaji na magonjwa lakini pia ni husaidia kukuza uchumi kwa mtu mmoja Mmoja na Soko la ndani .


" Kwa upande wa afya ya Binadamu ukila korosho zilizobanguliwa unakuwa na faida ya kuzuia ugonjwa wa moyo kwa kuzuia shindikizo la damu, ukila korosho unaongeza viini lishe vinavyozuia hatari ya kupata ugonjwa wa kansa pamoja na kuzuia Hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari"




Kaimu mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI Naliendele, Dr. Rashid Kidunda  amesema licha ya Mikoa hiyo ya Lindi na Mtwara kuwa  ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho lakini ni asilimia 10 pekee ya kile kinachozalishwa ndicho kinachotumika kama chakula kwa wakazi wa mikoa hiyo


"Unaweza kuona ni kwa namna gani tupo chini Katika ulaji na unywaji wa korosho kwa hivyo ili kukuza Soko la ndani tuliamua  kuzifanya siku ya tarehe 5 August kila mwaka tuadhimishe siku hii" Amesema Kidunda 


Amesema Nchini Tanzania korosho imeendelea kuwa zao kubwa la kibiashara  Katika kuchangia kipato cha wakulima hasa Katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma 


" Kwa sasa tumeona Mikoa mingine 17 ikiingia Katika kilimo cha zao hilo na sisi kama TARI Naliendele tumepewa jukumu la  kufanya utafiti na kutatua changamoto za wakulima wa zao Hilo" alifafanua 


Kaimu mkurugenzi wa Bodi ya korosho Reveliani  Ngaiza amesema zao la korosho ni zao la kipekee tofauti na mazao mengine kwa kuwa Lina matumizi mengi kuanzia kwenye Majani, Mbegu,  Tawi , shina na hata mzizi wake


" Ukiacha ulaji wa korosho zao la korosho kwa upande wa Majani yanatumika kama Dawa kutibu minyoo tumboni, kuzuwia kuhara , kutoa Gesi tumboni pamoja na kutibu vidonda vya tumbo"


"Lakini ukichukia Jana ukachanganya na gome la mkorosho unapata Dawa ya kutibu ugonjwa wa meno, maganda ya korosho baada ya kubangua yakikamuliwa upatikana kimiminika chakutengeneza wino wa kuandikia kupitia kalamu"







Sunday, August 4, 2024

KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID KUNUFAISHA MAELFU NANENANE.

 

Na Mwandishi Wetu, Morogoro


WANANCHI wanaopata msaada wa kisheria za mama Samia Legal Aid zinazoendelea kutolewa kwenye maonyesho ya Nane nane mkoani Morogoro wameelezea namna walivyonufaika na huduma hizo.


Wakizungumza mkoani hapa jana, wananchi hao walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka huduma hizo kwenye maonyesho hayo ambapo wamesema zimekuwa mkombozi kwao.


Renatha Manda alimshukuru Rais Samia kwa msaada wa kisheria baada ya kusaidiwa na huduma hizo alipokwenda kwenye maonyesho hayo.


“Nilikuwa na tatizo la mirathi nikaenda wakanipa ushauri wa kisheria na kwa kweli nimeridhika na najua suala langu litafika mwisho hivi karibuni,” alisema


Luciani Mwanitu kutoka Nzuguni Dodoma alisema alifika kwenye banda la Mama Samia Legal Aid ambapo amepata elimu kuhusu namna wanavyotoa huduma hizo na alishauri huduma hizo zipanuliwe ili wananchi wengi hasa wa vijijini waweze kufikiwa.


“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuanzisha huduma hii ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi wengi sana. Nawaomba waisogeze zaidi vijijini ili wananchi wengi zaidi waendelee kunufaika nayo,” alisema


Uwezo Maulid mkazi wa Shinyanga aliyefika kwenye banda hilo alisema amesaidiwa kwenye kesi ya mirathi ya mume wake ambaye alikuwa mtumishi wa umma kwenye manispaa ya Shinyanga Mjini.


“Nimefika hapa wamenipokea vizuri wamenipa mwanasheria wa huko Shinyanga ili aweze kunisimamia kupata haki zangu za msingi mimi mke wa merehemu Seif,” alisema na kuongeza


“Naomba mheshimiwa Rais aweze kunisaidia kwasababu kila ninapokwenda mahakamani naambiwa nirudi nyumbani mtandao umegoma kwasababu siku hizi kesi zinaendeshwa kwa mtandao. Huu ni mwaka wanne tangu mwaka 2021  nilipokonywa hadi nyumba na ndugu wa marehemu,” alisema


Alisema lakini baada ya kufika kwenye banda la mama Samia Legal Aid na kupewa mwanasheria anaamini suala lake litashughulikiwa na kufika mwisho ili aweze kupata haki zake kama mjane wa marehemu mume wake.






Wananchi wakipata huduma za msaada wa sheria bure banda la Mama Samia Legal Aid mkoani Morogoro kwenye maonyesho ya Nane Nane

WMA WATAKA WAKULIMA KUZINGATIA VIPIMO KWENYE UJAZO WA MAZAO.

 

Wakala wa Vipimo (WMA) umewataka wakulima kuzingatie sheria ya vipimo inayotaka ujazo wa mazao yao kwenye gunia yasizidi kilo 100.


Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa WMA, Albogast Kajungu amefafanua sheria hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika manda la WMA kwenye maonesho la wakulima nane nane.


Amesema moja ya mambo wanayowaeleza wakulima ni namna ya kuweka ujazo wa mazao yao na kuzingatia vipimo vilivyowekwa na Serikali.


Amesema katika kutafsiri neno lumbesa kwenye ujazo wa gunia sheria inasema lumbesa ni kile kilichozidi juu ya ujazo wa kilo 100.


Ameongeza kwa kusema kuwa wakulima wanapaswa kuzingatia sheria ya ujazo wa mazao kwenye gunia nayo ni kuhakikisha ujazo huo usizidi kilo 100.


Amesema sheria inataka mazao yote yanapaswa yafungashwe kwenye ujazo wa kilo 100 na si vinginevyo.


Katika kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa ili kulinda haki ya mkulima na mnunuzi, inashauriwa kuwe na vituo vya kuuzia mazao ambapo mizani itawekwa hapo ili kuhakiki ujazo mazao husika


Saturday, August 3, 2024

WANASHERIA WATATUA MIGOGORO ZIARA YA RAIS SAMIA MOROGORO

 


Na Mwandishi Wetu

TIMU ya wanasheria wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid imeambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake ya mkoani Morogoro kwaajili ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Rais Samia yuko katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro iliyoanza tarehe mbili na inayotarajiwa kukamilika tarehe saba siku ya Jumatano mwezi huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo alisema wameambatana na Rais Samia ili kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria.

“Tutakuwa na Rais muda wote wa ziara hapa Morogoro na tupo na Waziri wetu mheshimiwa Pindi Chana na wasaidizi wa kisheria ngazi ya wilaya na mkoa, kila anapofika mheshimiwa Rais kama kuna mtu anachangamoto ya kisheria tunaichukua na kuifanyia kazi,” alisema

“Kupitia ziara hii tumeshatoa msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali na hata jamii ya wamasai tumekutana nao kwenye maeneo mbalimbali na tumewapa elimu ya sheria kuhusu migogoro yao ya mara kwa mara ya ardhi,” alisema Beatrice.

Alisema wakati wanasheria wengine wakiwa kwenye ziara  hiyo, Rais Samia ametuma wanasheria wengine kupitia Kampeni ya Mama Samia Legail Aid kutoa huduma za msaada wa kisheria kwenye maonyesho ya nane nane mkoani humo.

Beatrice alisema timu ya wanasheria hao iliwasili mkoani Morogoro juzi na inaendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi mbalimbali ambao wanamatatizo ya kisheia kwa kuwapa msaada wa kisheria.

Tangu wanasheria hao wawasili kwenye viwanja vya nane nane mkoani Korogoro wananchi wengi wamekuwa wakifika kwenye banda la mama samia Legal Aid  katika  maonyesho hayoambapo wamekuwa wakipewa msaada wa kisheria.

Mama Samia yuko mkoani hapwa kwa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya za Mkoa wa Morogoro na mpaka sasa ameshatembelea Wilaya ya  Gairo, Kilosa, Mvomero,  na kesho Jumapili anatarajaiwa kuwasili wilaya ya Kilombero.

Mmoja wa wananchi aliyepata huduma ya msaada wa kisheria Jerome Kiangi,  alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kutatua matatizo yao ya kisheria.

“Kwa kweli nampongeza Rais Samia kwa upendo wake kwa watanzania amegundua kwamba wengi wetu tunahitaji msaada wa kisheria nimekuja hapa nimesikilizwa na wanasheria na wamesema tatizo langu la mgogoro wa nyumba litapatiwa ufumbuzi namshukuru sana,” alisema mwananchi huyo.

Mwananchi mwingine, John Lubeja alipongeza hatua ya rais Samia kutuma wanasheria kwenye maonyesho hayo kwani wamekuwa mkombozi kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kupata huduma za kisheria.

“Kupata wakili ni gharama sana kwa hiyo huduma kama hizi zinaposogezwa karibu na wananchi kama hapa kwenye maonyesho tena bure ni jambo la faraja sana na la kupongeza mno,” alisema Lubeja.