Wednesday, May 8, 2024

WAHITIMU MAFUNZO YA AWALI YA KIJESHI KWA KUJITOLEA WAASWA KUWA WAZALENDO. 

 

Na Mwandishi wetu,
Lindi.

 Brigedia Jenerali Charles Peter Feruzi amewataka vijana waliohitmimu  mafunzo ya awali ya kijeshi ya jeshi la kujenga Taifa (JKT)  kuwa wazalendo waaminifu  katika kusimamia na kuijenga  nchi yao.

Brigedia Jenerali Charles Feruzi ametoa rai hiyo wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa kujitolea  oparesheni ya miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha 843 huko Wilayani Nachingwea 

Amewataka wahitimu hao kutumia Mafunzo waliyoyapata katika kuijenga na kuilinda Nchi  kwa kuzingatia kiapo chao.

Pia amewataka kujiepusha na matumizi yasiyofaa katika mitandao ya kijamii na  badala yake waitumie mitandao katika kujifunza na kwa manufaa bila kuvunja sheria na Taratibu za Nchi yao.

Luteni Kanali Nyagalu  Malecela ni mkuu wa kikosi cha 843 Nachingwea amesema vijana hao wakiwa kambini hapo kwa majuma 16  wameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya awali ya kijeshi na kuwajenga vijana hao kuwa wakakamavu pamoja na wazalendo

Awali akitoa salamu za Wilaya katibu tawala wa wilaya ya Nachingwea Haji Mabruck Balozi, aliwasihi wahitimu hao  kuendelea kujiendeleza kimasomo.

" ni kwa kupitia Elimu kijana unaweza kuwa Meneja wa Benk, Mkuu wa kikosi, Mbunge , Waziri na Hata Rais hivyo niwasihi vijana kujiendeleza kimasomo ili mfikie malengo yenu" alisema Balozi.

Nao baadhi ya wahitimu  wakaeleza umuhimu wa mafunzo hayo sambamba na kuwasihi vijana wengine kujiunga na jeshi hilo








Thursday, May 2, 2024

MAHAKAMA YAELEZWA NATHWANI ALIVYOMJERUHI JIRANI YAKE.

 

Bharat Nathwani katikati na mke wake Sangita Bharat anayeshuka ngazi wakishuka kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana kusikiliza kesi yao ya kumjeruhi jirani yao.

.....................

Na Mwandishi Wetu

MSIMAMIZI wa Msikiti wa Wahindi Lohana aitwae, Ankit Dawda (32) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jinsi wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) walivyomshambulia jirani yao Lalit Ratilal na kutoa matusi ya nguoni kwa lugha ya kihindi.


Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.


Dawda alidai hayo jana mbele Hakimu ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.


Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisiadiana na Frank Rimoy, Dawda alidai kuwa kazi yake anasafisha mazingira ya msikiti, kupamba na kutoa mapambo pia kukusanya vitu vya msikiti huo, na kusimamia usafi na ukarabati jengo nzima yenye nyumba za makaazi ambapo msikiti huo upo katika na jengo hilo.


Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa ofisini kwake akiendelea na majukumu yake ya kazi, ghafla alifuatwa na watu ambao hakuwafahamu wakimueleza kwamba aende akaangalie  juu ya ghorofa kuna makelele.


Alidai kuwa alivyofika juu alikuta Sangita Bharat akilalamika na kuwafokea mafundi waliokuwa wakifanya ujenzi katika eneo hilo watoe viroba vya vigae vilivyokuwa katika kibaraza wakati vitu vyote vilikuwa katika eneo la Lalit Ratilal na hakuna kitu kilichopo katika eneo la Sangita Bharat.


Dawda alidai kuwa kwa wakati huo kulikuwa na kelele nyingi zinaendelea, ndipo Sangita Bharat akaendelea kupaza sauti yake kwamba uchafu uliyokuwa katika kibaraza chao utoke.


"Kwa sababu hao mafundi hawakutoa hivyo vigae, Sangita Bharat akaanza kurusha matusi kwa lugha ya kihindi, na hapo hapo waume zao wakawasili na Sangita akawa anaendelea kutoa matusi ambapo Kiran Lalit akapigwa na Bharat Nathwani - mume wa Sangita, hadi kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo  ya saruji akatumbukia huko na mume wake naye akapigwa kifuani, kichwani na mguuni akadondoka chini akazimia".


"Waliita ambulance wakamshusha chini wakapelekwa hospitali lakini sikujua ni hospitali gani wamepelekwa,"alidai Dawda


Kesi imeahirishwa hadi Juni 3,2024 kwa ajili ya kuendelea kwa mashahidi wa upande wa mashitaka.


Awali, Fundi Seremala, Dominic Mpakani (43) aliileza mahakama jinsi mshitakiwa Bharat Nathwan allivyomshambulia jirani wake, Lalit Ratilal kwa kumpiga kichwa kifuani kisha akadondoka chini na nakupoteza fahamu kwa muda.


Aidha, alidai kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya mke wa Bharat (Sangita Bharat) na mke wa Lalit, (Kiran) ambao walikuwa wakirushiana maneno kwa ukali kwa lugha ya kihindi huku, baada ya muda kidogo waume zao walifika kwa pamoja na kuingilia ugomvi huo.


Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa nyumbani kwa Lalit Ratilal maeneo ya mtaa wa Mrima katika jingo la Lohana, alimuita kwa ajili ya kuifanyia kazi zinazohusiana na mbao na kazi zingine ndogo ndogo.


Alidai kuwa alifika katika jengo hilo saa tatu asubuhi ambapo bosi wake huyo anakaa floor ya tatu, wakati anaendelea na kazi alidai kuwa Sangita alikuwa amesimama kwenye dirisha lake na Kiran alikuwa amesimama kwenye mlango wake, kila mmoja alianza kuzungumza kwa ukali na kwa jaziba wakitumia lugha ya kihindi.


"Lakini nilimsikia mke wa Bharat, Sangita akimwambia mke wa Lalit kwamba uchafu wake apeleke huko ambapo vitu vyote vilikuwa vimewekwa katika eneo la Lalit na hakuna kitu chochote kilichokuwa katika eneo la Sangita. Baada ya dakika kadhaa sijui walipiga simu au vipi waume zao walikuja kwa wakati mmoja na malumbano yakaendelea kwa wote wanne," alidai Fundi Mpakani


Shahidi huyo alidai kuwa, wakati malumbano hayo yanaendelea wote walikuwa wamesimama kwenye mlango wa Lalit, baada ya muda Bharat akampiga kichwa Lalit na Lalit akadondoka chini na kupoteza fahamu.


Shahidi mwingine ambae ni Dk Lucia Augustino (52) wa Hospitali ya Mnanzi Mmoja alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa Idara ya Dharura chumba namba  20 muda wa mchana alipokea wateja wawili wenye asili ya kiashia walikuwa wamechafuka kuanzia kichwani hadi miguuni , mama alichafuka sana kuliko baba.


Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ambao ni raia wa Tanzania jinsia ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jingo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023.


Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.


Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara Lalit Ratilal katika mwili wake kwa kumpiga kichwa, ngumi na mateke kichwani.


Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya Lalit na Kiran kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.



Wednesday, May 1, 2024

NEMC YAPIGA KAMBI KANDA YA ZIWA KUELIMISHA MATUMIZI YA ZEBAKI.

 





Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wameanza kampeni ya kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya zebaki kwa migodi ya dhahabu kanda ya ziwa.


Akitoa elimu hiyo kwa wachimbaji wa migodi ya Wilaya ya Misungwi Mwanza, Meneja wa usajili wa kemikali na maabara za kemia, kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Musa Kazumila, alisema elimu hiyo inatokana na matakwa ya mkataba wa Minamata (Minamata convention).


Alisema mkataba huo unataka kutekeleza matakwa yake ambapo moja likiwa la kudhibiti matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo na kuongeza kuwa wameanza na wachimbaji wa migodi ya Chata, Shokeraera, Shilalo na luhala zilizopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.


Alisema katika mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya  Dunia na  kuratibiwa na (NEMC), Mkemia Mkuu amepewa jukumu la kutoa elimu ya usimamizi salama pamoja na matumizi salama ya zebaki kwani ndiye anayesimamia utekelezaji wa Sheria Na.3 ya mwaka 2003 inayohusu usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani ikiwemo zebaki.


Aidha, alisema  lengo la utoaji wa elimu hiyo pia ni kuwajengea uwezo wachimbaji na watumiaji wa zebaki ili waweze kutambua jinsi zebaki inavyoingia mwilini, madhara yake namna ya kujikinga.


Naye Dereki Masako kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dodoma, aliainisha maeneo ambapo madhara ya zebaki yanatokea kuwa ni wakati wa usagaji wa mawe na kudondosha matope ili zebaki ikamate na wakati wa uchukuaji wa kusanyiko anapokamua na kitambaa kwani matone hudondoka chini na kusambaa ardhini na hewani na kuleta madhara.


Alisema ni vyema wachimbaji wakatumia vifaa Kinga ili kujilinda dhidi ya athari za zebaki na kubainisha madhara yake kuwa ni kuharibu mfumo wa fahamu na kuleta athari ya kushindwa kuhisi, kukakamaa kwa mwili, macho na kuharibika kwa Figo.


Alisema zebaki huathiri ukuaji wa mtoto kwa mama mjamzito kupita kwenye kondo la mama, kupoteza nguvu za kiume kwa wanaume, msongo wa mawazo na mwili kuwasha na kupungua.


Mmoja wa wachimbaji, Haji Nasri, alikiri kutokuwa na uelewa wa madhara ya zebaki na kwamba wamefurahishwa  na elimu hiyo kwani wengi wao wamekuwa wakijishughulisha na uchimbaji wa dhahabu bila kuzingatia madhara ya kiafya yanayoweza kutokea.


Saturday, April 27, 2024

ULEGA ZIARANI KUKAGUA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA MAFURIKO MKURANGA

 

Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega  leo Aprili 27, 2024 ametembelea maeneo yalioathiriwa na mafuriko ya maji ya mvua katika jimbo la Mkuranga, mkoani Pwani na kufanya tathimini ni kiasi gani maeneo hayo yameathirika na kuona hatua za kuchukua ili kutatua changamoto hizo.


Katika ziara yake hiyo Mhe. Ulega ameanza kukagua maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo ikiwemo barabara na madaraja katika kata ya Mwandege, Tambani, Vikindu, Mkuranga, Kiparang’anda, Mkamba, Kimanzichana, Nyamato na Lukanga.


Aidha, ametoa rai kwa wananchi wanaokaa katika maeneo hayo yalioathiriwa na mafuriko kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kushughulikia changamoto hizo.













MAGAZETI YA LEO TAREHE 27 APRIL 2024.

 























Friday, April 26, 2024

TRA KAGERA YAVUKA LENGO LA UKUSANYAJI KODI.

 

Meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Kagera Castro John

Afisa elimu kwa umma TRA Kagera Ruekaza Rwegoshola akitoa elimu ya kodi kwa waandishi wa habari

..............................

Na Alodia Babara,

Bukoba.


Mamlaka ya mapato nchini TRA mkoa wa Kagera imevuka lengo la ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha Januari hadi Machi 2024 na kufikia asilimia 107.


Meneja wa mamlaka hayo mkoa wa Kagera Castro John akizumgumza na waandishi wa habari  Aprili 25, 2024 katika kikao kilicholenga kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari pamoja na kueleza mafanikio ya ukusanyaji wa kodi kipindi cha Januari hadi Machi, 2024.


"Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Kagera tulipanga kukusanya shilingi bilioni 28.24 lakini tulikusanya shilingi bilioni 30.2 na hivyo kuvuka lengo na kufikia  asilimia 107" amesema John.


John ametolea ufafanuzi wa kodi mpya ya bodaboda ambayo inapaswa kulipwa kwa mwaka elfu 65,000 ambapo kila robo mwaka zinapaswa kilipwa shilingi 16,200 na zinalipwa kwa awamu nne hivyo akawaomba wamiliki wa pikipiki za biashara kulipa kodi hiyo.


Aidha katika mkutano huo amewaomba waandishi wa habari kuendelea kuhamasisha walipakodi kulipa kwa wakati ili kuongeza mapato ya nchi.


Afisa elimu kwa umma  Ruekaza Rwegoshola ameeleza kuwa, kupitia ulipaji kodi serikali imekuwa ikitoa huduma mbalimbali kwa wananchi wake zikiwemo huduma za Afya, maji, ujenzi wa miundombinu ya barabara na vyumba vya madarasa.


Amesema, asilimia 70 ya mapato ya serikali yanatokana na ukusanyaji kodi na kwa mwaka 2023/2024 serikali ilipitisha bajeti ya trioni 44.39 na TRA ilipewa lengo la kukusanya trioni 26.75 hivyo TRA inayo kazi kubwa kuhakikisha  inakusanya kodi.


TaSUBa YAANDAA KONGAMANO LA MUUNGANO.

 

Makamo wa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Mwikwabe Msafiri (katikati) akizungumza na washiriki katika kongamano hilo, kulia ni Katibu wa Makamo wa Rais, Cinthia Vincent Lwanda na kushoto ni Waziri Mkuu wa Serikali ya wanafunzi, Raban Erasto Mbiti.

.....................................

Na Athumani Shomari 

Bagamoyo.


Katika Maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya Muungano, Serikali ya wanafunzi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imeandaa kongamano la Muungano ambalo limewashirikisha wanafunzi wa chuo hicho na wageni kutoka nje ya chuo.


Katika kongamano hilo lililofanyika tarehe 25 April 2024, mada za muungano ziliwasilishwa na kisha kutoa nafasi kwa washiriki kutoa maoni mbalimbali kuhusu Muungano.


Washiriki hao walisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao leo unaadhimishwa kwa kutimiza miaka 60 una faida nyingi kwa watanzania wote.


Wamezitaja baadhi ya faida hizo ni pamoja ushirikiano wa wananchi wa bara na visiwani katika mambo mbalimbali.


Wamezungumzia changamoto kadhaa ambazo zinazoukabili muungano ambazo miongoni mwa hizo ni zile zinazohitaji kufanyiwa kazi na Serikali na nyingine ni zinazohitaji uzalendo wa wananchi wa kuyatambua mazuri ya muungano na kutoa maoni kurekebisha kasoro kwa kuzingatia ushirikiano, umoja na dhamira yenyewe ya muungano.


Wamesema wapo watu wanazungumzia kasoro za muungano tu bila ya kutaja faida zilizopo hali ya kuwa faida zake nyingi na kwamba kasoro zinatakiwa kutajwa kwa lengo la kurekebisha na sio kuubeza muungano wenyewe.


Aidha wamesema licha ya faida zilizopo yapo mambo kadhaa ambayo yanahitaji kufanyiwa mapitio kurekebisha kasoro zilizopo ili kila mwananchi afurahie matunda ya muungano.


Wamesema miongoni mwa maeneo yanayohitaji marekebisho ni pamoja na maswala ya kodi kwa pande zote mbili ili kuleta uwiano utakaoleta furaha kwa wananchi wote.


Makamo wa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Mwikwabe Msafiri amesema lengo la kongamano hilo ni kuleta uelewa wa pamoja kwa wanachuo ambao wanaonekana umri wao ni mdogo ukilinganisha na umri wa muungano.


(Nikiangalia naona wote tuliopo hapa umri wetu ni mdogo na umri wa muungano ni mkubwa hivyo ipo haja ya kujadili maswala ya muungano ili tuweke kumbukumbu zetu sawa, Alisema Mwikwabe.


Maadhimisho ya sherehe za muungano huadhimishwa kila mwaka ambapo waka huu muungano wa Tanganyika na Zanziba umetimiza miaka 60.




Washiriki wa kongamano hilo wakifuatilia mada zilizowasilishwa na watoa mada.