Makamo wa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Mwikwabe Msafiri (katikati) akizungumza na washiriki katika kongamano hilo, kulia ni Katibu wa Makamo wa Rais, Cinthia Vincent Lwanda na kushoto ni Waziri Mkuu wa Serikali ya wanafunzi, Raban Erasto Mbiti.
.....................................
Na Athumani Shomari
Bagamoyo.
Katika Maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya Muungano, Serikali ya wanafunzi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imeandaa kongamano la Muungano ambalo limewashirikisha wanafunzi wa chuo hicho na wageni kutoka nje ya chuo.
Katika kongamano hilo lililofanyika tarehe 25 April 2024, mada za muungano ziliwasilishwa na kisha kutoa nafasi kwa washiriki kutoa maoni mbalimbali kuhusu Muungano.
Washiriki hao walisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao leo unaadhimishwa kwa kutimiza miaka 60 una faida nyingi kwa watanzania wote.
Wamezitaja baadhi ya faida hizo ni pamoja ushirikiano wa wananchi wa bara na visiwani katika mambo mbalimbali.
Wamezungumzia changamoto kadhaa ambazo zinazoukabili muungano ambazo miongoni mwa hizo ni zile zinazohitaji kufanyiwa kazi na Serikali na nyingine ni zinazohitaji uzalendo wa wananchi wa kuyatambua mazuri ya muungano na kutoa maoni kurekebisha kasoro kwa kuzingatia ushirikiano, umoja na dhamira yenyewe ya muungano.
Wamesema wapo watu wanazungumzia kasoro za muungano tu bila ya kutaja faida zilizopo hali ya kuwa faida zake nyingi na kwamba kasoro zinatakiwa kutajwa kwa lengo la kurekebisha na sio kuubeza muungano wenyewe.
Aidha wamesema licha ya faida zilizopo yapo mambo kadhaa ambayo yanahitaji kufanyiwa mapitio kurekebisha kasoro zilizopo ili kila mwananchi afurahie matunda ya muungano.
Wamesema miongoni mwa maeneo yanayohitaji marekebisho ni pamoja na maswala ya kodi kwa pande zote mbili ili kuleta uwiano utakaoleta furaha kwa wananchi wote.
Makamo wa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Mwikwabe Msafiri amesema lengo la kongamano hilo ni kuleta uelewa wa pamoja kwa wanachuo ambao wanaonekana umri wao ni mdogo ukilinganisha na umri wa muungano.
(Nikiangalia naona wote tuliopo hapa umri wetu ni mdogo na umri wa muungano ni mkubwa hivyo ipo haja ya kujadili maswala ya muungano ili tuweke kumbukumbu zetu sawa, Alisema Mwikwabe.
Maadhimisho ya sherehe za muungano huadhimishwa kila mwaka ambapo waka huu muungano wa Tanganyika na Zanziba umetimiza miaka 60.
Washiriki wa kongamano hilo wakifuatilia mada zilizowasilishwa na watoa mada.
No comments:
Post a Comment