Friday, April 26, 2024

TRA KAGERA YAVUKA LENGO LA UKUSANYAJI KODI.

 

Meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Kagera Castro John

Afisa elimu kwa umma TRA Kagera Ruekaza Rwegoshola akitoa elimu ya kodi kwa waandishi wa habari

..............................

Na Alodia Babara,

Bukoba.


Mamlaka ya mapato nchini TRA mkoa wa Kagera imevuka lengo la ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha Januari hadi Machi 2024 na kufikia asilimia 107.


Meneja wa mamlaka hayo mkoa wa Kagera Castro John akizumgumza na waandishi wa habari  Aprili 25, 2024 katika kikao kilicholenga kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari pamoja na kueleza mafanikio ya ukusanyaji wa kodi kipindi cha Januari hadi Machi, 2024.


"Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Kagera tulipanga kukusanya shilingi bilioni 28.24 lakini tulikusanya shilingi bilioni 30.2 na hivyo kuvuka lengo na kufikia  asilimia 107" amesema John.


John ametolea ufafanuzi wa kodi mpya ya bodaboda ambayo inapaswa kulipwa kwa mwaka elfu 65,000 ambapo kila robo mwaka zinapaswa kilipwa shilingi 16,200 na zinalipwa kwa awamu nne hivyo akawaomba wamiliki wa pikipiki za biashara kulipa kodi hiyo.


Aidha katika mkutano huo amewaomba waandishi wa habari kuendelea kuhamasisha walipakodi kulipa kwa wakati ili kuongeza mapato ya nchi.


Afisa elimu kwa umma  Ruekaza Rwegoshola ameeleza kuwa, kupitia ulipaji kodi serikali imekuwa ikitoa huduma mbalimbali kwa wananchi wake zikiwemo huduma za Afya, maji, ujenzi wa miundombinu ya barabara na vyumba vya madarasa.


Amesema, asilimia 70 ya mapato ya serikali yanatokana na ukusanyaji kodi na kwa mwaka 2023/2024 serikali ilipitisha bajeti ya trioni 44.39 na TRA ilipewa lengo la kukusanya trioni 26.75 hivyo TRA inayo kazi kubwa kuhakikisha  inakusanya kodi.


TaSUBa YAANDAA KONGAMANO LA MUUNGANO.

 

Makamo wa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Mwikwabe Msafiri (katikati) akizungumza na washiriki katika kongamano hilo, kulia ni Katibu wa Makamo wa Rais, Cinthia Vincent Lwanda na kushoto ni Waziri Mkuu wa Serikali ya wanafunzi, Raban Erasto Mbiti.

.....................................

Na Athumani Shomari 

Bagamoyo.


Katika Maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya Muungano, Serikali ya wanafunzi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imeandaa kongamano la Muungano ambalo limewashirikisha wanafunzi wa chuo hicho na wageni kutoka nje ya chuo.


Katika kongamano hilo lililofanyika tarehe 25 April 2024, mada za muungano ziliwasilishwa na kisha kutoa nafasi kwa washiriki kutoa maoni mbalimbali kuhusu Muungano.


Washiriki hao walisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao leo unaadhimishwa kwa kutimiza miaka 60 una faida nyingi kwa watanzania wote.


Wamezitaja baadhi ya faida hizo ni pamoja ushirikiano wa wananchi wa bara na visiwani katika mambo mbalimbali.


Wamezungumzia changamoto kadhaa ambazo zinazoukabili muungano ambazo miongoni mwa hizo ni zile zinazohitaji kufanyiwa kazi na Serikali na nyingine ni zinazohitaji uzalendo wa wananchi wa kuyatambua mazuri ya muungano na kutoa maoni kurekebisha kasoro kwa kuzingatia ushirikiano, umoja na dhamira yenyewe ya muungano.


Wamesema wapo watu wanazungumzia kasoro za muungano tu bila ya kutaja faida zilizopo hali ya kuwa faida zake nyingi na kwamba kasoro zinatakiwa kutajwa kwa lengo la kurekebisha na sio kuubeza muungano wenyewe.


Aidha wamesema licha ya faida zilizopo yapo mambo kadhaa ambayo yanahitaji kufanyiwa mapitio kurekebisha kasoro zilizopo ili kila mwananchi afurahie matunda ya muungano.


Wamesema miongoni mwa maeneo yanayohitaji marekebisho ni pamoja na maswala ya kodi kwa pande zote mbili ili kuleta uwiano utakaoleta furaha kwa wananchi wote.


Makamo wa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Mwikwabe Msafiri amesema lengo la kongamano hilo ni kuleta uelewa wa pamoja kwa wanachuo ambao wanaonekana umri wao ni mdogo ukilinganisha na umri wa muungano.


(Nikiangalia naona wote tuliopo hapa umri wetu ni mdogo na umri wa muungano ni mkubwa hivyo ipo haja ya kujadili maswala ya muungano ili tuweke kumbukumbu zetu sawa, Alisema Mwikwabe.


Maadhimisho ya sherehe za muungano huadhimishwa kila mwaka ambapo waka huu muungano wa Tanganyika na Zanziba umetimiza miaka 60.




Washiriki wa kongamano hilo wakifuatilia mada zilizowasilishwa na watoa mada.


MAGAZETI YA LEO TAREHE 26 APRIL 2024.

 




















Thursday, April 25, 2024

AJALI YA MOTO YAUA WANNE NGARA.

 

Alodia Babara

Ngara.

Watu wanne katika kata ya Rusumo wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamepoteza maisha na wengine saba kunusurika kwenye nyumba baada ya chumba walichokuwa wamelala kuwaka moto kutokana na jiko la mkaa ambalo limesababisha madumu ya petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa katika chumba hicho kushika moto na kulipuka.


Kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera Zabron Muhumha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Aprili 25, 2024 saa 04:00 alfajiri na kusababisha vifo vya vijana wanne waliokuwa wamelala kwenye chumba kimoja.


Amesema jeshi la zimamoto na uokoaji kituo cha Rusumo kilipata taarifa ya tukio la moto wa kuunguza nyumba inayomilikiwa na Didas Dominick Kalido yenye vyumba vinne ambapo watu waliolala katika nyumba hiyo walikuwa 11 na miongoni mwa chumba kimoja cha nyumba hiyo walikuwa wamelala vijana wanne na wote walipoteza maisha na saba walitoka wakiwa na majeraha madogomadogo.


“Waliofariki ni Rajabu Paul (16) mnyambo mkazi wa Kahaza Rusumo, George Josephat (18) mkazi wa Mwibumba Rusumo, Eustace amejulikana kwa jina moja ni mkazi wa Muleba na Revocatus Jacob (16) mkazi wa Mwibumba Rusumo alikuwa anauza mayai ya kuchemsha” Amesema Kamanda Muhumha.


Aidha amewataja wengine saba ambao walikuwa kwenye nyumba na walitoka na majeraha madogo kuwa ni Deokres Medard (31) mhaya, Pelis Theofil (20) mkazi wa Rusumo, Elizaberth John (24) Mhaya, Rashid Peter (29) mhangaza,  Safina Theophil (12), Evelin Rashid miaka miwili, Bismas Theores miezi kumi.


Amesema kuwa, baada ya jeshi hilo kufanya uchunguzi wa awali umebaini kuwa chumba walichokuwa wamelala marehemu kilikuwa kinahifadhi madumu ya petrol na aliyekuwa anauza mayai alichemsha mayai kwa kutumia jiko la mkaa na hivyo wakavuta hewa chafu wakawa wamezidiwa na madumu ya petrol yakashika moto na kulipuka na kusababisha vifo vyao.


Amesema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospital ya wilaya ya ngara, Nyamihaga na taratibu nyingine za mazishi zinaendelea kufanyika.


Ametoa wito kwa jamii kuwa makini katika kuhifadhi vitu vya milipuko kama petrol nadisel, kwenye nyumba ambayo wanalala kwani ni hatari sana na kuwa wameishapigia kelele wananchi kuacha tabia hiyo na pamoja na kutoa elimu mara kwa mara bado wananchi wameendelea kuhifadhi petrol kwenye nyumba wanazolala.


Amewataka wauza patrol na disel kutouza katika madumu kwani ni hatari na badala yake wawawekee moja kwa moja kwenye vyombo vyao vya moto na akatolea mfano wale wanaoishi visiwani kuwa na vibari maalum vya kusafirisha petrol na disel, na kuhusu majiko ya mkaa watu waache tabia ya kulala nayo ndani yakiwa yanawaka au watumie nishati mbadala.


CCM MKOA WA PWANI YAWANOA VIONGOZI WAKE.

 







Na Omary Mngindo, Mlandizi.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kupitia Katibu wake wa Siasa na Uenezi,  DAVID MRAMBA kimeanza ziara ya Tarafa kwa Tarafa kikiwapiga msasa viongozi wake wa ngazi za Kata.


Katika ziara hiyo iliyoanzia Tarafa ya Mlandizi Jimbo la Kibaha Vijijini ilihudhuriwa na viongozi wanaotokea Kata sita zinazounda Tarafa hiyo, na kupewa jina la Step by Step inayolenga kuwaweka pamoja viongozi hao.


Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Kibaha JOEL KITUU amezungumzia semina nzuri ya Makatibu, Uenezi pamoja na Katibu Uhamasishaji wa Vijana.


PENDO ERNEST Katibu wa Siasa na Uenezi Kata ya Janga amegusia shilingi milioni NANE kutoka mfuko wa Jimbo, zilizolenga kumwaga kifusi eneo la Zahanati ya Fiona, ambapo zimemwagwa trip mbili tu.


HADIJA MAGUTO Katibu CCM Tawi la Mkwajuni Kata ya Mtambani amezungumzia fidia kupisha barabara ya Mzenga mpaka Makofia Bagamoyo, ambapo amesema wanapata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.


DKT. ROSE KUTOA MABATI 100 UJENZI WA OFISI YA CCM KILOMBERO.

 

Na Mwandishi Wetu, Kilombero

MWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk. Rose Rwakatare, ameahidi kutoa mabati 100 kwaajili ya ujenzi wa ofisi ya chama hicho Wilaya ya Kilombero inayoendelea kujengwa ambayo itagharimu milioni 250 hadi kukamilika.


Alitoa ahadi hiyo jana April 24, 2024 mara baada ya kutembelea ofisi hiyo kuangalia maendeleo ya ujenzi wake alipokuwa kwenye ziara yake ya kukagua athari za mafuriko katika Wilaya hiyo.


Kwenye ziara yake hiyo juzi, Dk. Rose alitoa msaada wa tani tano za mchele kwa waathirika wa mafuriko wa Jimbo la Mlimba mkoani humo.


Akizungumza kwenye eneo la ujenzi wa jengo hilo juzi, Dk. Rose aliwapongeza viongozi wa chama hicho mkoa wa Morogoro kutokana na kasi kubwa ya ujenzi huo.


“Mara ya mwisho kufika hapa ujenzi ulikuwa haujaanza na mimi kama mwenyekiti wa wazazi wa Mkoa nitatoa mabati 100 kwaajili ya kupaua nawaomba wanachama wengine wajitokeze kuchangia jengo hili kwasababu hiki ni chama chetu wote,” alisema Dk. Rose.


Alisema jengo hilo litakuwa na manufaa makubwa kwa chama hicho na kwamba iwapo wanachama wengine watajitokeza kwa wingi kutoa michango yao linaweza kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.


Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Kilombero, Joseph Mwambeleko, alimshukuru Dk. Rose kwa kutembelea maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya chama na msaada wa mabati 100 ambao ameahidi kuutoa.


Aliwaomba wanachama wa chama hicho na wadau wa maendeleo nchini kuchangia ujenzi huo na kwamba misaada hiyo haiku kwaajili ya mtu binafsi bali kwaajili ya chama chao.


“Chama chetu kitajengwa na nguvu ya wanachama kwa hiyo nawaomba wenye nia ya kutaka kusaidia wasiogope kitu chochote kwasababu hawamchangii mtu wanakichangia chama chao,” alisema.


Alisema jengo hilo linajengwa kwa nguvu za wanachama na marafiki wa chama hicho ambao chama kimewaandikia barua ya shukrani kutambua mchango wao.


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya, aliwaomba wadau wa maendeleo Wilaya ya Kilombero kuendelea kuchangia ujenzi wa ofisi za chama hicho.


“Wakati wa uchaguzi mwaka juzi niliahidi kwamba kipaumbele changu ni kujenga ofisi za chama na leo nafurahi sana kuona jengo limesimama na bado asilimia ndogo tu likamilike kwa hiyo wanachama waje watusaidia kumalizia ujenzi,” alisema.


“Huu si wakati wa uchaguzi, uchaguzi ni 2025 kwa hiyo watu wasiogope kuja kuchangia ujenzi wa jengo la chama chao, nawahakikishia kuwa wote watakaokuja tutawalinda,” alisema Msuya.