Alodia Babara
Ngara.
Watu wanne katika kata ya Rusumo wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamepoteza maisha na wengine saba kunusurika kwenye nyumba baada ya chumba walichokuwa wamelala kuwaka moto kutokana na jiko la mkaa ambalo limesababisha madumu ya petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa katika chumba hicho kushika moto na kulipuka.
Kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera Zabron Muhumha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Aprili 25, 2024 saa 04:00 alfajiri na kusababisha vifo vya vijana wanne waliokuwa wamelala kwenye chumba kimoja.
Amesema jeshi la zimamoto na uokoaji kituo cha Rusumo kilipata taarifa ya tukio la moto wa kuunguza nyumba inayomilikiwa na Didas Dominick Kalido yenye vyumba vinne ambapo watu waliolala katika nyumba hiyo walikuwa 11 na miongoni mwa chumba kimoja cha nyumba hiyo walikuwa wamelala vijana wanne na wote walipoteza maisha na saba walitoka wakiwa na majeraha madogomadogo.
“Waliofariki ni Rajabu Paul (16) mnyambo mkazi wa Kahaza Rusumo, George Josephat (18) mkazi wa Mwibumba Rusumo, Eustace amejulikana kwa jina moja ni mkazi wa Muleba na Revocatus Jacob (16) mkazi wa Mwibumba Rusumo alikuwa anauza mayai ya kuchemsha” Amesema Kamanda Muhumha.
Aidha amewataja wengine saba ambao walikuwa kwenye nyumba na walitoka na majeraha madogo kuwa ni Deokres Medard (31) mhaya, Pelis Theofil (20) mkazi wa Rusumo, Elizaberth John (24) Mhaya, Rashid Peter (29) mhangaza, Safina Theophil (12), Evelin Rashid miaka miwili, Bismas Theores miezi kumi.
Amesema kuwa, baada ya jeshi hilo kufanya uchunguzi wa awali umebaini kuwa chumba walichokuwa wamelala marehemu kilikuwa kinahifadhi madumu ya petrol na aliyekuwa anauza mayai alichemsha mayai kwa kutumia jiko la mkaa na hivyo wakavuta hewa chafu wakawa wamezidiwa na madumu ya petrol yakashika moto na kulipuka na kusababisha vifo vyao.
Amesema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospital ya wilaya ya ngara, Nyamihaga na taratibu nyingine za mazishi zinaendelea kufanyika.
Ametoa wito kwa jamii kuwa makini katika kuhifadhi vitu vya milipuko kama petrol nadisel, kwenye nyumba ambayo wanalala kwani ni hatari sana na kuwa wameishapigia kelele wananchi kuacha tabia hiyo na pamoja na kutoa elimu mara kwa mara bado wananchi wameendelea kuhifadhi petrol kwenye nyumba wanazolala.
Amewataka wauza patrol na disel kutouza katika madumu kwani ni hatari na badala yake wawawekee moja kwa moja kwenye vyombo vyao vya moto na akatolea mfano wale wanaoishi visiwani kuwa na vibari maalum vya kusafirisha petrol na disel, na kuhusu majiko ya mkaa watu waache tabia ya kulala nayo ndani yakiwa yanawaka au watumie nishati mbadala.
No comments:
Post a Comment