Tuesday, September 26, 2023

TANZANIA KUSHIRIKIANA NA MAREKANI KUBORESHA MIFUMO YA USIMAMIZI MASUALA YA AFYA

 


Na. WAF - Washington USA.

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeingia makubaliano na Serikali ya Marekani juu ya uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa masuala ya Afya kwa kwa kuanzisha Maabara za Taifa za Afya ya Jamii za kisasa.

 

Makubaliano hayo yamefikiwa mara baada ya Waziri wa Afya Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui kufanya kikao na Mkuu wa Masuala ya Kimaita Idara ya Afya na Huduma za Kibinadamu nchini Marekani Bi Susan Kim, kwa kujadiliana kuhusu uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa masuala ya Afya.

 

“Tumekuja hapa kujifunza jinsi idara hiyo inavyosimamia na kuratibu huduma za maabara za Kitaifa za Afya ya Jamii ambapo tumekubaliana kuanzisha Maabara za Taifa za Afya ya Jamii ambazo zitakuwa na jukumu la ufuatiliaji wa magonjwa hususani yanayoathiri afya ya jamii na vihatarishi vyake, uchunguzi wa magonjwa na tafiti za masuala ya afya ya jamii” amesema Waziri Ummy Mwalimu

 

Amesema, uanzishwaji wa maabara hizo utaimarisha uwezo wa Tanzania katika kujikinga, kujiandaa na kukabiliana na majanga ya afya kama vile UVIKO 19, Marburg na Ebola.

 




THAMANI YA UWEKEZAJI NSSF YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 111.


Na Mwandishi Wetu


THAMANI ya uwekezaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), imeongezeka kwa asilimia 111 kutoka Sh trilioni 3.4 Machi 2021 hadi kufikia Sh trilioni 7.15 Juni 30 mwaka 2023.


Kwa mujibu wa mfuko huo ongezeko la thamani hiyo ya uwekezaji imechangiwa na kukua kwa thamani ya vitegauchumi, michango ya wanachama na mapato ya uwekezaji.


Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Masha Mshomba, katika kikao cha wahariri wa vyombo vya habari na mfuko huo kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Dar es salaam jana.


Alisema lengo la mfuko huo ni kuhakikisha thamani ya uwekezaji inaongezeka na kufikia Sh trilioni 11.6 ifikapo mwaka 2025/26.


Alisema pia thamani ya vitegauchumi vya mfuko imekua kwa asilimia 55 hadi kufikia Sh trilioni 7.15 Juni 30, 2023 kutoka Sh trilioni 4.62 zilizofikiwa Juni 30 mwaka 2021.


"Wastani wa mapato ya uwekezaji kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023, yalifika Sh bilioni 72.06 ikiwa ni ongezeko la asilimia 92 ukilinganisha na Sh bilioni 37.35 zilizokusanywa mwezi Machi 2021," alisema Mshomba.


Aidha, alisema mapato halisi ya Mfuko yameongezeka kutoka wastani wa asilimia 3.31 Machi 2021, hadi kufikia asilimia 5.32 kwa kipindi kilichoishia Juni 30, mwaka 2023.


Alisema mapato ya uwekezaji kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 93 na kufikia Sh bilioni 864.76 katika mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni 2023 ukilinganisha na Sh bilioni 448.17 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha Juni 30, mwaka 2021.


 


Pia, alisema katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023,


Mfuko ulilipa Sh bilioni 61.93 kwa mwezi kama mafao kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko la asilimia


22 ukilinganisha na Sh bilioni 50.58 zilizolipwa kwa mwezi kipindi kilichoishia Machi Mosi, mwaka 2021.


"Ongezeko hili lilichangiwa na kuongezeka kwa madai ya fao la upotevu wa ajira na mkupuo maalum," alisisitiza.


Aidha, Mshomba alisema malipo ya mwaka ya mafao kwa wanufaika mbalimbali wa Mfuko yaliongezeka kwa asilimia 25 na kufikia Sh bilioni 743.17 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023 ukilinganisha na Sh bilioni 594.33 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, mwaka 2021.


Kuhusu idadi ya wanachama alisema kati ya Machi Mosi, mwaka 2021 na Juni 30 mwaka 2023, Mfuko uliandikisha wanachama 547,882 na idadi ya


wanachama wachangiaji iliongezeka kwa asilimia 36 kutoka 874,082 Machi Mosi 2021 hadi kufikia wanachama 1,189,222 Juni 30, mwaka 2023.


Alisema ongezeko hilo limechangiwa na mkakati wa serikali wa kuvutia wawekezaji, pamoja na utekelezaji wa mpango wa Mfuko katika uandikishaji wanachama.


Aidha, alisema wanachama wachangiaji katika Mfuko wameongezeka kwa asilimia 26 hadi kufikia wanachama wachangiaji 1,189,222 Juni 30, mwaka 2023 ikilinganishwa na wanachama wachangiaji 945,029 waliofikiwa Juni 30, mwaka 2021.


Alisema katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023, makusanyo ya michango kwa mwezi uliongezeka kutoka Sh bilioni 97.67 iliyofikiwa Machi Mosi mwaka 2021 hadi kufikia Sh bilioni 143.05 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023.


 


"Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa waajiri wanaoleta michango kwa wakati na mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa sekta binafsi," alisema.


Mkurugenzi huyo alieleza kuwa makusanyo ya michango kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 43 hadi kufikia Sh trilioni 1.7 katika mwaka ulioishia Juni 30, mwaka 2023 ukilinganisha na Sh trilioni 1.2 zilizokusanywa katika mwaka ulioishia Juni 30, mwaka 2021.


Mkurugenzi huyo alisema katika kipindi husika, Mfuko umeweza kupunguza siku za ulipaji wa mafao ya wanachama wake kutoka wastani wa siku 68 zilizokuwa Machi Mosi, mwaka 2021 hadi wastani wa siku Juni 30, mwaka huu 2023 kwa mwanachama aliyekamilisha taarifa zake kwa usahihi.


“Kupitia maboresho haya, asilimia 75 ya madai ya mafao yanalipwa ndani ya siku 30, moja kwa moja kupitia akaunti ya mwanachama, mstaafu ama mtegemezi,” alieleza.


Akizungumzia miradi ya uwekezaji ya Mfuko, Mshomba alisema NSSF inaatekeleza miradi mitano ambayo ni miradi ya nyumba za makazi za Dungu, Toangoma, Mtoni Kijichi, jengo la kibiashara na makazi la Mzizima Towers na Hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano, Mwanza.


Alisema changamoto na kasoro za kizabuni na kimikataba zilizokuwepo zilisababisha miradi hiyo kusimama mwaka 2016.


"Miradi hii imepitia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanyiwa mapitio na kufanyiwa kaguzi maalum ikiwepo ile ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) iliyokamilika mwishoni mwa mwaka 2020.


Alisema katika kipindi kilichoanzia Machi Mosi, 2021, Mfuko ulitatua changamoto zilizokuwepo na kwa sasa utekelezaji wa miradi yote unaendelea na miradi hiyo inatarajia kukamilika kati ya Juni na Septemba mwakani.


Kuhusu mradi wa Dege Eco Village alisema katika mwaka wa fedha 2023/24, Mfuko unatarajia kuuza mradi huo wenye eneo la ekari 302, Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa thamani yad ola za Marekani milioni 220 sawa na Sh bilioni 450 hadi 500. Mradi huo una nyumba 3,750 zilizokuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.


Alisema mradi huo umeuzwa kama ulivyo, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Bodi ya Mfuko na serikali ili kurudisha fedha za wanachama zilizowekezwa awali katika mradi huo.


Akizungumzia mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi alisema unamilikiwa kwa ubia kati ya NSSF kwa asilimia 96 na Jeshi la Magereza asilimia nne na unatarajiwa kushirikisha wakulima 845. Kiwanda kinatarajiwa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka.



















MAGAZETI YA LEO TAREHE 26 SEPTEMBA 2023.






















Monday, September 25, 2023

DHAHABU YA GGR YAIFUNGUA TANZANIA KIMATAIFA USAFISHAJI MADINI

GGR kuleta mabadiliko katika uongezaji thamani madini

Geita

Imeelezwa kuwa Kiwanda cha Kusafisha dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) kinachomilikiwa na Mwekezaji Mtanzania Sarah Masasi kimeiweka Tanzania katika Soko la Kimataifa katika usafishaji wa dhahabu duniani.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde Septemba 25, 2023 Mkoani Geita baada ya kutembelea na kuzungumza na mwekezaji na wafanyakazi wa kiwanda cha kisasa cha kusafisha madini ya dhahabu cha GGR.

Waziri Mavunde amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kiwanda hicho kupata Ithibati ( ISO Certification) za aina tano ikilinganishwa na kiwanda kikubwa cha kusafisha madini ambacho hakina ISO zote hizo.

Pia, Waziri Mavunde ameiagiza timu ya wataalam iliyoundwa ikihusisha wataalam kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Madini, wawakilishi wa wachimbaji wadogo na wamiliki wa viwanda vya usafishaji wa madini kuandaa taarifa itakayoelezea namna bora ya upatikanaji wa malighafi na ushiriki wa BoT kwenye kuwasaidia wachimbaji wadogo kuzalisha dhahabu itakayopelekwa kwenye viwanda hivyo.

" Dhahabu itakayosafishwa kwenye viwanda hivi sehemu ya uzalishaji huo itanunuliwa na Benki Kuu ya Tanzania," amesema Mavunde.

Aidha, amesema kuwa ili kuwezesha kiwanda hicho kupata malighafi ya kutosha amemuagiza Katibu Mkuu, Wizara ya Madini kuitisha kikao na wadau wote wanaomiliki leseni za madini ili kuzungumza kwa pamoja na hatimaye viwanda vya usafishaji madini ya dhahabu vya ndani ya nchini vipate malighafi ya kutosha.

Kwa upande wake, Mmiliki wa Kiwanda hicho cha Geita Gold Refinery (GGR) Mama Masasi ameishukuru Serikali kwa kumpatia ushirikiano katika kipindi chote kuanzia ujenzi hadi kukamilika na kuanza usafishaji wa dhahabu katika ubora wa 999.9.

"GGR tupo tayari kufanya kazi na Wachimbaji wote wa madini ili kusafisha dhahabu yao katika kiwanda hiki kwa kuwa kimekidhi vigezo muhimu vya kimataifa," amesema Mama Masasi

Naye, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Mheshimiwa Costantine Kanyasu amesema kuwa anatamani kumuona mwekezaji huyo anafanikiwa katika kiwanda hicho na kusisitiza Serikali iendelee kumpa ushirikiano katika shughuli zake.

Aidha, ameomba tafiti zifanyike zaidi ili wachimbaji wapate maeneo mengi ya kuchimba madini na hatimaye kiwanda hicho kiweze kupata mzigo kutoka kwa wachimbaji wa madini ili kuongezwa thamani.

Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula na watendaji wengine wa Wizara ya Madini na Taasisi zake. 








WAANDISHI WA HABARI WAPATA ELIMU YA MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA 2022.

 

Kamisaa wa sensa ya watu na makazi 2022 Anna Makinda akizungumza na waandishi wa habari katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara katika mafunzo ya matokeo ya sensa ya mwaka 2022 yaliyofanyika jijini Mwanza ukumbi wa mamlaka ya chakula na dawa TMDA
...............................
Alodia Dominick, Mwanza.

Waandishi wa habari katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara wameanza mafunzo ya siku mbili yatakayowajengea uwezo wa kuandika habari kuhusu usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Septemba 25, 2023 katika ukumbi wa mamlaka ya chakula na dawa (TMDA) jiji Mwanza na yatahitimishwa Septemba 26,2023.

Kamisaa wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Anna Makinda akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa, wametoa mafunzo hayo ili kuwawezesha kupata uelewa jinsi ya kuandika habari za matokeo ya sensa ya 2022 ambayo ilikuwa na mazoezi mengine mawili ya kuhesabu majengo na anuani za makazi.


"Niombe muwe watulivu na wasikivu katika mafunzo haya ili mada zitakazofundishwa mzielewe na mnaporudi kwenye mikoa yenu muweze kuandika habari za takwimu kwa usahihi" amesema Makinda

Makinda amevipongeza vyombo vya habari hususani redio za kijamii kwa kufanikisha sensa ya watu na makazi ya 2022 kwani watumia redio hizo kuliendesha vipindi vya kuelimisha jamii na watu walikuwa wakiwauliza maswali ya uelewa katika vipindi hivyo.

Amesema, kuwa baada ya kupata takwimu na kujua idadi ya watu wote nchini sasa wanaenda kurudisha fadhira kwa wananchi kwani kipindi cha uhamasishaji waliomba wananchi wajiandikishe na sasa wanaenda kuwaletea maendeleo kwa kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa maisha yao.

Akifungua mafunzo hayo mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Mwakilagi kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Amos Makala ametaja lengo la mafunzo kuwa ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari jinsi ya kuandika habari za matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022.

Amesema mkoa Mwanza kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 ina watu 3.7 milioni huku 2012 ilikuwa na watu 2.7 milioni na kuwa ni miongoni mwa mikoa yenye watu wengi ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora na Geita.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kagera press club Mbeki Mbeki amesema waandishi wayachukue yatakayofundishwa katika mafunzo ili yawawezeshe kuwaelimisha wananchi. 

Mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Mwakilagi katika mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari juu ya matokeo ya sensa ya mwaka 2022