Monday, September 25, 2023
Sunday, September 24, 2023
UWEKEZAJI KATIKA ELIMU NA AFYA NDIYO UKOMBOZI WA WATANZANIA-KIKWETE JR.
NA MWANDISHI WETU- KIWANGWA, CHALINZE
Mbunge wa Chalinze na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Ndg. Ridhiwani Kikwete amefanya ziara fupi katika kata ya Kiwangwa kuongea na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Kijiji kuhusu shughuli za maendeleo katika eneo hilo.
Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine, Mbunge wa Chalinze Ndg. Kikwete alitumia fursa hiyo kukabidhi mifuko 200 kwa serikali ya kijiji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne katika shule ya Sekondari ya Ridhiwani Kikwete inayojengwa katika Kijiji cha Kiwangwa, Kata ya Kiwangwa, Halmashauri ya Chalinze.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge huyo aliwashukuru wadau mbalimbali wanaochangia maendeleo katika halmashauri hiyo na kuwahimiza wadau wengine wanaoguswa kuchangia shughuli mbalimbali na si kusubiri serikali.
Alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba viongozi kuhakikisha wanasimamia ujenzi na thamani ya michango hiyo ionekane kwa faida ya jamii tunayoiongoza.
Akizungumza baada ya kupokea mifuko hiyo ya Theruji, Diwani wa kata hiyo Ndg. Malota Kwaga amemshukuru Mbunge na kuwaomba viongozi wenzake kuendelea kumuunga mkono Mbunge kwa kazi nzuri anazozifanya akishirikiana na uongozi mzuri wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza Ndg. Diwani aliwakumbusha juhudi mbalimbali anazofanya Mh. Rais kwa ajili ya watu wa Kiwangwa na Chalinze ni za kipekee huku akishukuru serikali kwa fedha zaidi ya shilingi Bilioni 2 zilizopelekwa katika kata hiyo kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo zahanati, shule ya sekondari , umeme, maji n.k.
Baada ya kumaliza ziara ya Shuleni hapo, Ndg. Kikwete alikwenda kutazama zahanati ya Kiwangwa ambayo inapangwa kupanuliwa kuwa kituo cha Afya ili kuhudumia wananchi wa kata hiyo. Akizungumza Mbele ya Mbunge , Diwani Malota alimueleza Ndg. Mbunge kuwa, zahanati hiyo inapokea wagonjwa zaidi ya 3000 kwa wiki hivyo kuwa moja ya zahanati zinazohudumia watu wengi ukizingatia kuwa shughuli za kilimo zinafanyika sana katika eneo hilo.
Saturday, September 23, 2023
WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO 11 KAGERA
Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Kasimu Majaliwa ametoa maagizo 11 kwa viongozi wa Kagera ikiwemo kuonyesha kwa vitendo kaulimbiu inayosema ni wakati wa vitendo timiza wajibu wako huku akiagiza wakuu wa mikoa wote nchini kuendesha mafunzo ya uongozi kwa watumishi wa Serikali nchi nzima.
Ametoa maagizo hayo Septemba 22, mwaka huu wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya uongozi kwa viongozi wa kada mbalimbali za Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo yaliyoandaliwa na mkuu wa mkoa huo Hajati Fatma Mwassa.
"Kaulimbiu hii imekuja wakati muafaka ambapo mkoa unahitaji mabadiliko katika kila eneo la ustawi wa jamii ya wana Kagera, kaulimbiu hii ni wito kwa kila kiongozi aliyepo hapa kutafakari nini ameufanyia mkoa huu katika kuleta maendeleo ya haraka, aidha inamtaka kila kiongozi atimize wajibu wake katika dhamana aliyopewa na kuleta tija inayotarajiwa, kaulimbiu hii ni kichocheo cha kuamsha kila kiongozi aliyepo kuchukua hatua za makusudi kuunusuru Mkoa wa Kagera"amesema Majaliwa.
Amesema hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, Kagera imekuwa inasuasua na upande wa ukuaji uchumi kwa takribani miaka kumi mfululizo imekuwa haifanyi vizuri licha ya uwezo wa mazingira mazuri ya kiuchumi.
Aidha ametoa maagizo kumi na moja kwa viongozi hao ambapo amesema kuwa anatambua kupitia mafunzo hayo wamejiwekea maazimio ambayo yanahitaji mkakati wa utekelezaji hivyo, basi kila mmoja atoe taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo"Wekeni utaratibu wa kufanya tathmini ili kubaini mafanikio ya mafunzo haya ambayo yamegharimu fedha nyingi za Serikali, Kila robo mwaka hakikisheni mnafanya kikao cha kupeana mrejesho kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo" aliagiza
Amemtaka mkuu wa Mkoa huyo kuweka mikataba ya utendaji kazi na wakuu wote wa idara na vitengo katika halmashauri zote,pia amewataka viongozi na watendaji wote kukumbuka wajibu wao kuwatumikia zaidi wananchi na kutatua kero zao kwa kuweka utaratibu wa kuwafuata, kuwasikiliza na kupata ufumbuzi wa kero zao hususani kero za masuala ya migogoro ya ardhi na makundi mbalimbali katika jamii kama wakulima na wafugaji.
"Kumbukeni kwamba ninyi mnawajibika moja kwa moja kwa wananchi, wasikilizeni na kutatua kero kwa wakati ili waendelee kuiamini Serikali iliyopo madarakani kwani dhamira ya Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwatumikia wananchi, nasi tuliopewa dhamana ya kumsaidia kila mmoja atimize wajibu wake ili wote tuwe tunaongea lugha moja ambayo ni kuwatumikia wananchi na kwa kuwatatulia kero zao"ameagiza Majaliwa
Pia amewataka watumishi hao kukunbuka kuwa mwaka kesho kutakuwepo na uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo ni tathimini ya utumishi wao kwa wananchi na ni kipimo cha imani ya wananchi kwa Serikali iliyopo madarakani hivyo akawataka kuweka mikakati mahsusi ya kutatua kero za wananchi zinazoweza kuwa kikwazo katika uchaguzi ujao na si kuongeza kero kwa wananchi,ikiwemo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa,urasimu usio na tija katika kuwahudumia wananchi.
"Hakikisheni uwepo wa usimamizi wa Fedha zinazoletwa na Serikali pamoja na mapato ya ndani ili zitumike ipasavyo katika maeneo yenu, miradi itekelezwe kwa ubora, ufanisi na ilingane na thamani ya fedha inayoletwa ili wananchi wanufaike na kuendelea kuiamini Serikali yao,vongozi wote wafuatilieni kwa karibu wakandarasi wanaopewa kazi, iwapo mtabaini mapungufu chukueni hatua za haraka msisubiri mpaka Viongozi wakuu waje kwenye maeneo yenu na kubaini mapungufu kwenye miradi wakati ninyi mpo, wakandarasi wanapojenga miradi chini ya viwango na kusababisha upotevu wa fedha za kodi za Watanzania pia kuwashirikisha watumishi waliopo katika idara na ofisi zetu"amesema
Naye mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa katika taarifa yake kwa waziri mkuu amesema mkoa huo unakabiliwa na utapiamlo mkubwa udumavu mkali kwa watu wake ambapo ni asilimia 34.6,pia hari ya uchumi mkoa huo ni mkoa wa 25 kati ya 26 ambapo wamevuka nafasi moja kwa sababu miaka kumi iliyopita Kagera imekuwa ikishika nafasi ya 26 ambayo kwa sasa imechukuliwa na mkoa wa Simiyu.
"Tunao mdondoko mkubwa kwa wanafunzi ambapo tumebaini wanafunzi 16,000 wa shule za msingi na 6,700 wa sekondari hawakumaliza masomo yao kwa kipindi kilichopita,namba ya utapiamlo ni kali sana na hatuwezi kuendelea kubaki nyuma namna hii tumeamua kuleta mafunzo haya ya uongozi ili yatusaidie kujipanga upya kimkakati kuhakikisha hari hii inatoweka"amesema Mwassa.
Naye Emmanuel Alfred kutoka Taasisi ya uongozi aliyekuwa mkufunzi mkuu wa mafunzo hayo amesema matarajio yao ni kwamba watumishi hao wataenda kwa chachu ya maendeleo katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ipasavyo
Friday, September 22, 2023
TANZANIA KUFIKIA LENGO LA AFYA KWA WOTE MWAKA 2030.
Serikali yaTanzania imejidhatiti kutekeleza malengo ya kufikisha huduma za afya kwa wote hadi ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu jana akiwa kwenye kikao cha Huduma za Afya kwa wote kilichofanyika kwenye Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa Jijini Newyork.
"Tanzania inaungana na wajumbe wengine wa kikao hiki katika kutekeleza azimio hili la kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa huduma bora za afya popote alipo". Amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema kuwa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi nchini Tanzania zimeendelea kuimarika kutoka asilimia 38 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 43 mwaka 2022 huku bajeti ya afya ikiendelea kuboreshwa maradufu kutoka Dola Milioni 529 mwaka 2019 hadi kufikia Dola Milioni 950 mwaka 2022.
Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania imeendelea kutekeleza azimio la Afya kwa wote waliloweka Viongozi wakuu wa nchi kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2019 kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kuhamasisha wananchi kujiunga na skimu mbalimbali za Bima ya Afya.
"Serikali ya Tanzania inaendelea kutenga fedha kuhakikisha inafikia lengo la afya kwa wote ikiwemo kuwasilisha muswada wa bima ya afya kwa wote katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania". Amesema Waziri Ummy.
Amesisitiza ili kufikia lengo la afya kwa wote ni lazima huduma za afya ngazi ya msingi ziboreshwe ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya wakiwa karibu zaidi na maeneo yao, kuimarisha utoaji wa elimu ya afya pamoja na kuongeza nguvu za mapambano dhidi ya magonjwa na utoaji tiba.
"Tunahimiza ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na wadau wa sekta ya afya kuungana pamoja katika kufikia malengo tuliyoweka ya afya kwa wote hadi ifikapo mwaka 2030 kwa kuwekeza kwenye Ubunifu wa Teknolojia mpya, Rasilimali, mbinu bora za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na Huduma za chanjo na dawa". Amesisitiza Waziri Ummy.
MAKAMU WA RAIS DKT PHILIP MPANGO AHUTUBIA MKUTANO WA 78 WA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kwa sasa dunia inashuhudia kufifia kwa mshikamano thabiti wa kihistoria, udugu na kujitolea, kutoingiliana, usawa baina ya mataifa na kunufaishana uliowekwa na waanzilishi wa Umoja wa Mataifa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani. Amesema ili kurejesha imani na mshikamano baina ya mataifa ni vema mataifa yaliyoendelea kuhakikisha yanatimiza ahadi zake na sauti za mataifa yanayoendelea zinasikilizwa.
Amesema kumekuwepo na kutoaminiana baina ya mataifa na hivyo kupelekea mmomonyoko wa utawala wa sheria, mataifa kuunda miunganiko tofauti na ile ya asili pamoja na kurejea kwa maamuzi ya upande mmoja. Ameongeza kwamba kwa sasa kumekuwa na maswali zaidi juu ya ufanisi wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa pamoja na Taasisi za Fedha za kimataifa zikihitajika kufanyiwa maboresho ya haraka.
Makamu wa Rais amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuwakemea kwa uwazi wale wote wanaoshiriki katika kuchochea migogoro barani Afrika kwa lengo la kuuza silaha au kupata utajiri wa rasilimali zilizopo. Ameongeza kwamba dunia inahitaji kuwekeza zaidi katika mazungumzo na diplomasia katika kutatua migogoro ya kivita ili kuifanya kuwa sehemu salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Tanzania itaendelea kuchangia katika juhudi za kuleta na kudumisha amani barani Afrika na kwingineko duniani na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza uungaji mkono katika mipango ya kikanda ya kuleta amani katika maeneo yenye vita barani Afrika. Amesema hadi kufikia mwezi machi 2023 Tanzania imekua ndio mchangiaji mkubwa wa 12 kati ya nchi 125 katika shughuli za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.
Makamu wa Rais amesema utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu umekuwa wa kukatisha tamaa hasa kutokana na kutotekelezwa kwa ahadi za kifedha na teknolojia kutoka kwa nchi zilizoendelea duniani na upungufu wa fedha katika nchi nyingi za Afrika.
Amesema Tanzania imedhamiria kutekeleza kikamilifu malengo ya maendeleo enedelevu kama inavyotarajiwa ambapo Julai mwaka huu iliwasilisha Ripoti ya pili ya Hiari ya Taifa (VNR) ambayo inaonyesha kwa ujumla kumekuwa na mafanikio makubwa kwa lengo namba 2 – 7 kwa ongezeko la uwiano wa kutosha wa chakula, upatikanaji wa dawa muhimu, kupungua vifo vya chini ya miaka 5,hatua muhimu katika kuhamasisha usawa wa kijinsia, uboreshaji wa upatikanaji wa maji mijini na vijijini pamoja na utoaji wa huduma ya nishati ya umeme. Ameongeza kwamba pamoja na kuwepo kwa utendaji wa wastani katika lengo namba 1,8 na 10, Tanzania imedhamiria kuchukua hatua kuboresha zaidi juhudi za mapato ya ndani huku ikitumia mfumo wa ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi pamoja na kuweka kipaumbele kwenye uwekezaji katika sekta za huduma za jamii, kilimo na biashara ya kilimo, uongezaji thamani na miundombinu, pamoja na kuinua ujuzi wa vijana.
Kuhusu mazingira, Makamu wa Rais amesema Tanzania inasisitiza wito wake wa kuchukua hatua za haraka na za pamoja za kupunguza uzalishaji wa gesijoto pamoja na kuimarisha hatua za kukabiliana na hali hiyo. Amesema ni lazima kuweka mazingira wezeshi na kuwezesha uwekezaji unaohitajika ili kutumia rasilimali kwa ajili ya kuongeza utekelezaji wa ahadi zinazohusu mabadiliko ya tabianchi na uondoaji wa kaboni katika uchumi wa dunia. Aidha amesema Tanzania inasisitiza wito wake wa mabadiliko ya haki katika kufikia nishati safi kwa nchi za Afrika.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuwa imara katika kupinga dhuluma popote inapotendeka na kwa yeyote yule. Ametoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi visivyo vya haki kwa mataifa kwani vimekua vikidhoofisha uhuru na ustawi kwa wote.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
22 Septemba 2023
New York – Marekani.
MUFTI ZUBEIR, AFANYA ZIARA UNIVERSITY OF OXFORD UK.
Mheshimiwa Mufti wa Tanzania tarehe 21.09.2023 siku ya Alhamis alikuwa na ziara ya kutembelea chuo kikuu maarufu Duniani cha Oxford, katika ziara yake ya kikazi nchini Uingereza.
Aidha Mufti Sheikh Abubakar Zubeir alikuwa na mazungumzo maalum na Professor Farhanĺ Ahmad Nizami, ambaye ni Mkurugenzi wa Oxford Centre for Islamic studies kuona jinsi gani Tanzania inaweza kunufaika na Fursa za Masomo za chuo kikuu cha Oxford kilichopo nchini Uingereza.
Katika mazungumzo hayo Mkurugenzi wa Oxford Centre for Islamic Studies alimwambia Mufti Sheikh Zubeir awaombe Waislam na watanzania kwa ujumla kuchangamkia na kuomba nafasi za masomo maarufu kama Chevering scholarship kabla ya mwisho wa maombi (deadline) mwezi November 2023.
Mufti alimalizia ziara yake kwa kushukuru kwa kupata fursa ya kukutana na Mkurugenzi na kusisitiza kuwa atawahamasisha Waislaam Tanzania waone umuhimu wa kupata elimu bora toka kwenye vyuo vikuu vya hadhi ya juu Duniani kama Oxford.
.jpeg)







.jpeg)










































