Thursday, September 21, 2023

USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI NI MUHIMU KATIKA KUKABILIANA NA UPUNGUFU FEDHA ZA MAENDELEO.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kukabiliana na upungufu wa fedha za maendeleo ili kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) duniani.

 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akichangia katika mjadala wa viongozi wa ngazi ya juu kuhusu ufadhili wa maendeleo uliyokuwa na dhima ya kutafuta suluhisho la kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs). Mkutano huo umefanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.

 

Makamu wa Rais amesema ili kushawishi sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ni vema mataifa yakajielekeza katika kuweka sera rafiki kwa sekta binafsi. Ameongeza kwamba kupitia ripoti ya hivi karibuni ya Mtazamo wa Kiuchumi wa Afrika (AEO 2023) kuhusu ufadhili mbadala, inabainisha wazi kuwa sekta ya binafsi ni miongoni mwa wadau muhimu katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

 

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kwa kupitia ushirikiano wa kikanda na kimataifa, Tanzania imefanikiwa kuwa na njia mbalimbali za ufadhili ambazo ni rafiki kwa sekta binafsi ikiwemo kutengeneza ramani ya wawekezaji ya malengo ya maendeleo endelevu.

 

Ameongeza kwamba katika uboreshaji wa miundombinu, Tanzania imetumia mbinu ya Ufadhili wa Mikataba ya Ujenzi na Ununuzi wa Kihandisi (EPC+F) ili kuongeza ufadhili wa sekta binafsi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri.

Makamu wa Rais ametaja mifano mingine kuwa ni pamoja na utoaji wa hati fungani ya kwanza nchini yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 300 iliotolewa na Benki ya CRDB kwa lengo la kufadhili miradi rafiki ya mazingira ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta za miundombinu, nishati mbadala , viwanda, ujenzi na usambazaji maji.

Vilevile Makamu wa Rais amesema kwamba ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi nchini Tanzania katika kuongeza kasi ya kufufua uchumi na kuinua kipato cha watu, Benki Kuu ya Tanzania imeanzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa benki za biashara kwa ajili ya kukopesha wakulima kwa riba isiyozidi 9%. Amesema matokeo ya mpango huo wa ushirikiano yameleta tija ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kwenye sekta ya kilimo kuongezeka kutoka asilimia 7.3 katika mwaka ulioshia Julai 2021 hadi asilimia 46.4% Julai mwaka 2023.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

21 Septemba 2023

New York - Marekani. 





MAGAZETI YA LEO TAREHE 21 SEPTEMBA 2023.

 






















TUWALINDE WATOTO DUNIA IMEBADILIKA, WAZIRI MHAGAMA


Na Mwandishi wetu- RUVUMA
Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya vitendo vya kikatili kwa kuhakikisha wanatoa taarifa ili hatua za kisheria zichukuliwe badala ya kuwa sehemu ya kuwaficha watu wanaofanya vitendo hivyo vinavyosababisha madhara makubwa kwa watoto.
 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kilagano, Kijiji cha Muungano Zomba , Wilaya ya Songea Vijijini katika ziara yake Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma ambapo amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwa mfano bora kwa watoto wao.

Mhe. Jenista amesema vitendo vya ukatili vimekuwa vikikithiri kila kukicha maeneo mbalimbali huku baadhi ya vitendo hvyo vikifanywa na wazazi wenyewe, walezi na hata watu wa karibu ambao wanategemewa na jamii kuwa sehemu ya kuwajenga watoto katika malezi bora.

“Dunia imeharibika na wala siyo siri na lazima tuelezane walindeni hao watoto tutadaiwa na Mwenyezi Mungu, lazima tuwe waangalifu jengeni tabia ya kuwafuatilia watoto kila wanapotoka shule mtoto anafananaje, anaonesha na tatizo? msikilize na kina mama wenzangu mjenge urafiki na watoto siyo mtoto anakusogelea unakuwa mkali hutaki kumsikiliza,”Amesisitiza Mhe. Jenista.

Sambamba na hayo amewahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia, Polisi, Walimu na Wadau wengine wote kuendelea kutoa huduma ya elimu ya malezi na makuzi ya watoto kwa wazazi na walezi ili waelewe wajibu wao wa kulea watoto katika msingi wa haki na usawa wa kijinsia.

“Ndugu zangu watoto wanapitia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, vipigo kutoka kwa wazazi, walezi na walimu, kubakwa, kulawitiwa, mimba na ndoa za utotoni pia wanatumikishwa katika kazi zisizoendana na umri wao na hata kukosa haki zao za elimu kwahiyo ni wajibu wa kila mmoja kupaza sauti ”, Alieleza. 

Katika hatua nyingine Mhe. Jenista amewaahidi wakazi wa Kijiji cha Maduwalo, Kata ya Maposeni akisema Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili zikiwemo maji na barabara akisema yote yatafanyiwa kazi pamoja na kushirikiana na Mawaziri wenye dhamana ili wananchi wapate huduma hizo muhimu kama lilivyo lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha katika ziara hiyo Mhe. Jenista aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari ya Daraja Mbili iliyopo Kata ya Maposeni, Kijiji cha Maposeni, kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya Sekondari katika Kijiji cha Lugagara , Kata ya Kilagano, kukabidhi vifaa kwa watu wenye ulemavu, vifaa vya michezo pamoja na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa nyumba ya Mganga wa Zahanati ya Mdunduwalo kijijini hapo iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari ya Daraja mbili Makamu Mkuu wa Shule Bw. Damson Wenela ameeleza kuwa ujenzi huo umefikia hatua ya lenta na mpaka sasa umegharimu zaidi ya shilingi milioni 48.

“Mradi wa ujenzi wa bweni unaendelea na mpaka sasa upo hatua ya lenta jumuiya ya shule ya sekondari Daraja mbili inatoa shukrani wa Serikali, Mbunge wetu wa Peramiho Mhe. Jenista Mhagama, viongozi wa Kata na Vijiji na kwa ushirikiano wanaotupa kufanikisha mradi huu muhimu kwa watoto wetu,”Ameeleza Bw. Wenela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mdunduwalo kilichopo katika Kata ya Maposeni Bw. Longnus Haule amesema kuwa kuletwa kwa miradi katika kijiji chake imekuwa faraja kwa wakazi wao akisema imekuja kwa wakati muafaka kwani imekuwa kiu yao ya muda mrefu.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Ndg. Thomas Msolwa amebainisha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza miradi mingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

“Niwaombe ndugu zangu sisi ndiyo wa kuyasema haya kwa vitendo CCM inatekeleza ahadi zake kwa vitendo kwa sababu ndiyo kiu yake kubwa kuwaletea wananchi wake maendeleo. Mbunge wetu anatimiza kwa vitendo madarasa, barabara, umeme, maji yote hayo anafanya tunayomtuma,”Amebainisha Mwenyekiti Huyo.







Wednesday, September 20, 2023

MAJALIWA: TANZANIA KUWA WAZALISHAJI WAKUBWA WA NISHATI

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Septemba 20, 2023 amefungua Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania na amesema kwamba Serikali imedhamiria kuwa mzalishaji mkubwa na nishati.


“Tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe wazalishaji wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada tutauza nje ya nchi.“


Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo baada ya kufungua kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.


Amesema kuwa Tanzania haitegemei kuzalisha umeme kwa kutumia maji pekee bali inaendelea kuweka mkazo katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati nyingine kama gesi na jua.


Waziri Mkuu amesema katika kongamano hilo la kimataifa la nishati ambalo limehusisha viongozi na wadau kutoka katika mataifa mbalimbali Duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati.


Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa kuzisisitiza nchi zote wanachama kuhakikisha taasisi za mafunzo zinatoa programu maalum za mafunzo katika sekta za nishati ili kuongeza idadi ya watu walio na ujuzi na maarifa kwenye sekta hiyo.


Amesema kuwa nishati ni sekta muhimu katika kufikia lengo la uanzishwaji wa viwanda na katika kuimarisha na kuwezesha uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi. “Lazima tufanye kazi kwa ushirikiano na wadau wote ili kufungua fursa kwa Watanzania wote.”


Amesema ili kuwaendeleza wafanyabiaahara wa ndani na Watanzania kushiriki katika sekta ya nishati, Serikali itaendelea kuhakikisha kanuni na taratibu zinazofaa zinawekwa ili kuwezesha ushirikishwaji katika mnyororo wa thamani wa maendeleo kwenye sekta ya nishati


Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema wameendelea kutekeleza mipango mbalimbali waliojiwekea katika kuhakikisha umeme unapatikana wakati wote nchini.


Dkt. Biteko amesema zaidi ya kampuni 100 za nishati kutoka katika maeneo mbalimbali duniani zinashiriki katika kongamano hilo ambalo lilitanguliwa na mkutano wa viongozi wa nishati. 






Tuesday, September 19, 2023

KAMATI YA SIASA BAGAMOYO YARIDHIISHWA NA UJENZI WA MIRADI MBALIMBALI YA MAENDELEO INAYOENDELEA KATIKA HALMASHAURI YA WILAYA YA BAGAMOYO.


Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Bagamoyo  tarehe 18 September 2023 imetembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo ili kuona namna inavyoendelea.


Miradi iliyotembelewa ni pomoja na Mradi wa ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa Dharura (EMD) katika Hospitali ya Wilaya Bagamoyo, mradi wa Ujenzi wa Shule ya Msingi mpya Kiharaka, Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Chasimba na Mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari Makurunge.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Sharifu Zahoro ameridhishwa na kasi ya ujenzi ya miradi hiyo kwa hatua iliyofikiwa.


Mwenyekiti huyo amewaomba wataalamu wanaohusika katika kusimamia Miradi hiyo,  kuhakikisha wanaendelea na kasi hiyo ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati kama ilivyopangwa. 


"Niwapongeze sana wataaamu mnaosimamia mradi hii kwa kazi nzuri mnayoifanya miradi inaenda vizuri sana ninachowaambia muendelee na kasi hii mpaka kukamilika kwake huku mkizingatia thamani ya fedha inayotumika ilingane na ubora wa Miradi husika" amesema Mhe. Zahoro 


Aidha Mwenyekiti huyo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zinazojenga miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamlyo, pia ametoa pongezi kwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo pamoja na MKurugenzi wa Halmashauri kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea Bagamoyo.


Nae Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bi..Halima Okashi amesema wataendelea kushirikiana bega kwa bega na watumishi wa Halmashauri kuhakikisha miradi hiyo na itakayokuja inafanyika kwa weledi na kukamilika ikiwa na ubora uliokusudiwa.


Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Bw. Shauri Selenda, Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Hassan kwa kutoa fedha zinazosaidia kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri ya Bagamoyo, 


"Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kutupatia fedha nyingi zinazosaidia kujenga hii miradi ambayo leo tumetembelea na kuikagua, Serikali imetupatia takribani Bilioni 1.3 iliyowekezwa katika miradi hii.