Monday, September 11, 2023
Sunday, September 10, 2023
Saturday, September 9, 2023
RC AYOUB APOKEA KERO ZA WAKULIMA WA MWANI PWANIMCHANGANI, AAHIDI HATUA ZA HARAKA
NA ANDREW CHALE, ZANZIBAR.
MKUU wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe Ayoub Mohammed Mahmoud amewaomba wananchi wa Shehia za Pwanimchangani na Kandwi wanaojihusisha na kilimo cha Mwani kuendelea kuwa na imani na Serikali yao kwani inalifanyia kazi suala lao la mwani kuungua na kukosa soko la uhakika.
RC Ayoub amesema hayo, katika mwendelezo wa ziara yake ya Shehia kwa Shehia inayoendelea ndani ya Mkoa huo, ambapo akiwa Shehia ya Pwanimchangani, amepokea kero mbalimbali ikiwemo kero kubwa ya wakulima wa zao la mwani ambao wamelalamikia kwa mahoteli kutiririsha maji machafu hali inayopelekea mwani wao kuungua huku pia wakikosa soko la uhakika.
Ambapo akijibu kero ya
Bi.Mwatima Musa Silima wa mkulima wa Mwani la bei za mwani na umwagaji maji machafu kwenye mwani wao, RC Ayoub amesema kuwa umwagaji wa maji unatokana na mahoteli kudhibitiwa na watu wa mazingira wa kutomwaga maji baharini.
"Hoteli zinadhibitiwa umwagaji maji mengi baharini, kuna utafiti uliofanyika umetazama haya yote ya maji na bei ya mwani.
Kwa hiyo tunataraji kuja na utaratibu mkakati wa namna gani bei ya mwani itaongezeka, Serikali upande wake imeunda kamapuni maalum ya kushughulikia mwani ili upande bei hivyo hili linafanyiwa kazi." Amesema RC Ayoub.
Pia suala la mwani kutoota vizuri baharini linatokana na suala la mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa kikwazo cha wakulima kutopata mwani wa kutosha.
"Tunalo tatizo jingine la Mabadiliko ya tabia nchi, yamekuwa ni kikwazo kwa wakulima kutokupata mwani wa kutosha.
Nini kifanyike, mapendekezo mbalimbali yametolewa ikiwemo baadala ya kuwa maji madogo pekee, wakulima wasogee kwenye maji mengi kidogo ili yasiunguze sana ule mwani, ili mfike huko mnahitaji vifaa ikiwemo mahitaji ya boti ya kufikia huko, Serikali haya yote inafanyia kazi." amesema RC Ayoub.
Aidha, amemwagiza Sheha wa Pwanimchangani kuitisha kikao cha Wananchi kutatua kero zilizopo chini yake ikiwemo ujenzi holela wa mahoteli kwa kufunga njia pamoja na masuala mengine ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana katika miradi ya maeneo yao ikiwemo hoteli na shughuli za Kitalii.
TANZANIA KUVUNA DOLA MILIONI 2.1 KUPITIA UVUVI WA BAHARI KUU
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa bahari kuu (DFSA) Dkt. Emmanuel Sweke (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Albacora Bw. Imanol Loinaz wakibadilishana nyaraka za mikataba itakayoiwezesha kampuni hiyo kuendelea kuvua ukanda wa bahari kuu muda mfupi baada ya kuisaini Septemba 08, 2023 jijini Dar-es-salaam, Anayeshuhudia tukio hilo katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdallah Ulega na Viongozi na watendaji kutoka Wizarani hapo na ile ya Uchumi wa bluu na Uvuvi kutoka Zanzibar.
...........................
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu (DSFA) zinatarajia kuvuna takribani Dola Milioni 2.1 kupitia mauzo ya leseni 45 za uvuvi wa bahari kuu zilizonunuliwa na wawekezaji kutoka nchi za China na Hispania.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba ya mauzo ya leseni hizo iliyofanyika septemba 08, 2023 jijini Dar-es-Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa eneo la bahari kuu kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar lina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 220,000 ambazo kwa muda mrefu zimekuwa hazitumiki ipasavyo.
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa sana kwetu hivyo ni lazima tuwe wabunifu katika utekelezaji wa maelekezo yake ambayo amekuwa akitutaka tuhakikishe rasilimali hii ya maji ya bahari inatumika kikamilifu kuwanufaisha Watanzania wote” Amesema Mhe. Ulega.
Aidha, Mhe. Ulega amebainisha kuwa eneo la bahari linalomilikiwa na Tanzania bara na Zanzibar lina uwezo wa kuhimili mpaka meli 100 hivyo ametoa rai kwa wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza kwenye Uvuvi wa bahari kuu kufanya hivyo ambapo amewahakikishia hali ya usalama na mazingira rafiki ya kufanya shughuli zao wakati wote.
Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi kutoka Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Wizara yake kupitia mamlaka ya usimamizi wa Uvuvi wa bahari kuu (DSFA) itasimamia na kutekeleza vipengele vyote vilivyopo kwenye leseni hizo.
Hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha eneo la bahari kuu linatumika vizuri ili kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini.
TANZANIA TAYARI TUNAENDELEA KUWEKEZA KATIKA KILIMO KINACHOENDANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI-DKT JAFO
NA MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali imewekeza katika teknolojia ya kilimo kinachomili mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi ya mazingira inayotekelezwa nchini.
Dkt. Jafo amesema hayo alipochangia mjadala wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Septemba 08, 2023.
Ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kufadhili miradi ya kilimo inayotekelezwa nchini ili pawepo na tija na uhakika wa chakula.
Kutokana na Makubaliano ya Paris kuhusu nchi zilizoendelea kuchangia fedha kwa mataifa yanayoendelelea katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Waziri Jafo alipendekeza kupitia fedha hizo pia pawe na mafungu maalumu ya kuwezesha kilimo cha kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Waziri Jafo alisema ili kukabiliana na changamoto ya ukame unaosababishwa na uhaba wa mvua katika baadhi ya maeneo Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya uchimbaji wa malambo 114 ya umwagiliaji.
“Tunafahamu sekta ya kilimo inaathirika sana kwa maana mvua hazitoshi hivyo miradi ya adaptation ni muhimu sana kama nchi hizo zikiwekeza katika teknolojia ya kilimo. Tuipongeze Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuja na Mradi wa BBT kwa vijana na tunaona umeanza kutimiza ndoto za vijana,” alisema.
Aidha, katika kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija pamoja na kuwepo kwa changamoto za kimazingira, Dkt. Jafo alisema Serikali inaimarisha uzalishaji wa nishati ikiwemo mradi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere na kusambaza umeme vijijini.
Alifanua kuwa hatua ya usambazaji nishati vijiji itasaidia kuwavutia wawezekaji kufungua viwanda vya uchakati wa mazao na hivyo kukuza uchumi kwa kuuza bidhaa zilizochakatwa badala ya mazao ghafi.
“Katika mkutano huu tumewataka wenzetu watimize wajibu wao kuchangia fedha za kusaidia nchi zinazoendelea katika miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi hasa kwenye smart agriculture kwani mvua hazitoshi kilimo,” alisisitiza Waziri Jafo.
Friday, September 8, 2023
DOLA MILIONI 50 KUWANUFAISHA WAVUVI
........................................
Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula barani Afrika (AGRF) umekuwa na matokeo chanya kwa upande wa program ya “Jenga kesho iliyo njema” (BBT) mara baada ya benki ya CRDB kwa kushirikiana na Mfuko wa kimataifa wa kuhifadhi mazingira (GCF) kutoa kiasi cha Dola milioni 50 zitakazotumika katika utekelezaji wa program hiyo.
Hayo yamebainika wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango wa kuwezesha wavuvi nchini unayoratibiwa na benki ya CRDB.
Tukio lililofanyika Septemba 08, 2023 ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha vijana hao wanapata mtaji mara baada ya kumaliza mafunzo yao kwa vitendo.
“Hii inamaanisha kuwa hawa wajasiriamali tunaowatengeneza kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi sasa wamepata uhakika kabisa wa kupata mikopo yao na kwa kuwa tayari wana maandiko mazuri ya biashara wataingia moja kwa moja kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hizo mbili” Amesema Mhe. Ulega.
Aidha Mhe. Ulega ametoa wito kwa benki hiyo kugeukia upande wa tasnia ya ufugaji wa samaki ambako ameweka wazi kuwa anaamini kuna faida kubwa sana endapo wafugaji hao watawezeshwa rasilimali fedha na zana mbalimbali za kisasa za kufanyia shughuli hiyo.
“Wavuvi ni jamii iliyoonekana kuwa masikini kuliko jamii yoyote na kwa muda mrefu wamekuwa na kipato cha chini sana lakini walichokuwa wanakosa ni namna ya kupata tija katika mnyororo wa thamani wa shughuli zao za uvuvi na mimi wakati wote nimekuwa nikiamini mnayo suluhu ya kuwaondoa wavuvi na wafugaji hawa kwenye hali hiyo kwa sababu ninaamini kabisa Mifugo na Uvuvi ni Utajiri” Ameongeza Mhe. Ulega.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Bw. AbdulMajid Nsekela amesema kuwa mikopo yenye masharti nafuu itawapa fursa vijana hao kujipanga kwani ina muda mrefu zaidi wa matazamio kuliko aina nyingine zote za mikopo inayotolewa na benki hiyo.
“Vijana watapata muda usiopungua miaka 3 ya matazamio mara baada ya kuchukua mikopo hii hivyo tunaamini kipindi hicho kinatosha kwa wao kufanya shughuli zao na kuanza kupata faida itakayowawezesha kuanza kuirejesha” Amebainisha Bw. Nsekela.
Mpango wa mikopo kwa wavuvi uliozinduliwa leo utawanufaisha wavuvi waliopo kwenye vyanzo vyote vya maji ya asili kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar ambapo vikundi vya vijana na wanawake watapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kuainisha aina ya zana wanazotaka kukopeshwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Bw. AbdulMajid Nsekela (kushoto) akielezea namna benki hiyo itakavyotekeleza mpango wa kuwawezesha wavuvi nchini muda mfupi kabla ya uzinduzi wa mpango huo uliofanyika Septemba 08, 2023 jijini Dar-es-Salaam. Katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na kulia ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akizindua mpango wa kuwawezesha wavuvi nchini tukio lililofanyika Septemba 08, 2023 jijini Dar-es-Salaam ikiwa ni moja ya matokeo ya Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya Chakula (AGRF), Kushoto kwake ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Suleiman Makame na kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Bw. AbdulMajid Nsekela.
BIMA YA AFYA KWA WOTE SULUHU YA KUDUMU YA MATIBABU KWA RIKA ZOTE
Na WAF, Bungeni Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema, Bima ya afya kwa wote itakuwa suluhu ya kudumu kwa wananchi wote ikiwemo watoto wasio na wazazi na wasiojiweza ambao awali walikuwa wakilipiwa na wahisani kupitia "Toto Afya Kadi".
Dkt. Molel amebainisha hayo leo Septemba 8, 2023 wakati akijibu swali la Mhe. Abdul-Haffar Idrissa Juma Mbunge wa Mtoni katika Bunge la 12, kikao cha tisa, Jijini Dodoma
Dkt Mollel amesema ni kweli kuwa, mfumo wa kulipia watoto kupitia "Toto Afya Kadi" umebadilika na kwa sasa unafanyika kupitia utaratibu wa shule na vifurushi vya bima ya afya vya najali, wekeza na Timiza na kueleza suluhu ya kudumu ni kuingia kwenye Bima ya afya kwa wote itayotoa fursa kwa wananchi wote kupata matibabu bora katika vituo vyote.
"Suluhisho la kudumu ni kukamilika kwa Muswada wa sheria wa Bima ya Afya kwa wote ambao tunaamini utawezesha watoto wengi zaidi wasio na walio na changamoto za kiafya kulipiwa Toto Afya Kadi". Amesema
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali imeendelea kutoa elimu mashuleni ili kutambua uwepo wa Bima ya afya kwa watoto, huku akitoa wito kwa waheshimiwa Wabunge kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika ngazi zote ikiwemo wazazi juu ya vifurushi vyenye matibabu kwa watoto na umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote.
Pia Dkt. Mollel amesema, Serikali ina utaratibu wa kutoa matibabu bure kwa watu wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu kupitia barua ya kiongozi katika eneo lake analoishi inayothibitisha hali yake ili apewe matibabu.
WABUNGE WALIA NA UADILIFU KATIKA MANUNUZI YA BIDHAA ZA UMMA.
Mdee amtaka Mwigulu ajitafute ili kudhibiti mianya ya upigaji.
Na Albert Kawogo Dodoma.
Bungeni.
WAKATI muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya 23, ikisubiri kupitishwa bungeni jijini Dodoma, baadhi ya wabunge wamedai bila Serikali kuweka mikakati ya ufuatiliaji na usimamizi watekelezaji wake, haitsaidia katika kutokomeza vitendo vya ubadhilifu wa fedha za umma.
Maoni hayo yametolewa bungeni jijini Dodoma wakati wakichangia mjadala wa muswada huo unaolenga kufuta Sheria ya Ununuzi ya Umma Na. 7 ya 2011.
Mbunge Viti Maalum, Halima Mdee amesema changamoto ya ubadhirifu wa fedha za umma unaotokea katika manunuzi na ugavi mbalimbali, inatokana na baadhi ya watumishi wa Serikali kutokuwa na weledi, hivyo mabadiliko ya sheria hiyo yanapaswa kwenda sambamba na mikakati ya usimamizi na ufautiliaji wa suala hilo.
“Changamoto kubwa tuliyonayo ni kuwa na watu wenye uweledi, watu wenye uzalendo wanaopenda taifa lao na kutekeleza wajibu waliopewa kuutekeleza kisheria,” amesema Mdee.
Katika hatua nyingine, Mdee alishauri mamlaka ya waziri wa fedha kutunga kanuni za manunuzi ya umma yapunguzwe, badala yake kanuni hizo zitungwe au ziidhinishwe na mhimili huo kabla hazijatumiwa.
“Haiwezekani Bunge likaruhusu waziri apewe mamlaka makubwa namna hiyo, kwa mujibu wa kanuni ya 128, maeneo 28 muhimu amepewa waziri akatunge kanuni. Hii haiwezekani vinginevyo tukubali akitunga sheria kanuni alete kwenye kamati ya Bunge ya bajeti na sheria ndogo, kabla hazijafanya kazi,” amesema Mdee.
Mbunge wa Handeni Mjini, Kwagilwa Nhamanilo, alishauri Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), iimarishwe ili iweze kusimamia mikataba ya manunuzi ambayo taasisi za umma zinaingia na sekta binafsi, kwa lengo kulinda maslahi ya nchi.
“Tukiangalia wajibu, usimamizi na utekelezaji wa mikataba ni vyema kuiwezesha ofisi ya AG sababu sheria ya manunuzi haikamiliki bila kuwa na mikataba. Lazima tuiwezeshe kibajeti, kusomesha watalaamu wetu na kusimamia kwa ukaribu sisi kama Bunge,” amesema Nhamanilo.
Naye Mbunge wa kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha amesema “nchi yetu inatumia zaidi ya asilimia 70 ya fedha za bajeti katika masuala ya manunuzi na ugavi, hiki ni kiwango kikubwa sana kwa mantiki hiyo tuna wajibu wa kutunga sheria madhubuti ili tuweze kudhibiti vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili.”
“Lakini suala la kuwa na sheria nzuri ni jambo moja na suala la kuwa na sheria inayotekelezeka ni jambo jingine. Ili tuweze kusimamia sheria hii ipasavyo ninapendekeza Serikali kuweka watendaji walio makini,” amesema Nahodha.
Awali akisoma kwa mara ya pili muswada huo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema unalenga kuweka masharti bora ya usimamizi wa manunuzi ya umma na ugavi na uondoshaji mali kwa njia ya zabuni.
Pia, sheria hiyo pendekezwa inalenda kutatua changamoto zilizobainika katika utekelezaji wa mashari na utaratibu wa maunusiz, ikiwemo kutokutofautisha masharti ya ununuzi kati ya taasisi za umma, kutojumisha masuala ya ugavi, kutokuwa na sehemu mahususi inayoanisha masuala ya usimamizi wa mikataba ya manunuzi kwa njia ya kielktroni na ukomo wa thamani ya mradi.
































































