Monday, August 21, 2023

WATANZANIA TUJENGE UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA ZETU: MHE. UMMY MWALIMU

 

Na Englibert Kayombo – WAF Tanga

 

Wito umetolewa kwa watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kutambua hali zao kiafya mapema na kuepukana na maradhi ambayo yanaweza kugharimu fedha nyingi za matibabu na hata kusababisha ulemavu hadi vifo.

 

Wito huo umetolewa leo na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya nchini Tanzania alipokuwa akifungua kambi ya upimaji afya ya Afya Cheki iliyoandaliwa na Uongozi wa Afya Cheki kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

 

“Watanzania wengi tunakwenda Hospitali tayari ugonjwa umeshakuwa mkubwa sana, wagonjwa wa Saratani wanakwenda Hospitali, Saratani ikiwa hatua ya nne, hatuna mazoea ya kupima afya mapema kujua hali zetu” ameeleza Mhe. Ummy mwalimu kwa kutolea mfano wa hali ya ugonjwa wa Saratani.

 

Amesema kuwa maradhi yakigundulika mapema huwa ni rahisi kuyatibu lakini pia kupunguza madhara, hivyo kupitia kambi hiyo ya Afya Cheki anawahimiza, kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi wa Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla umuhimu wa kupima afya.  katika Taasisi ya Saratani ya Ocean ameshuhudia akiona wagonjwa wanafika wakiwa wanaugua Saratani ya tezi dume, Saratani ya Mlango wa Kizazi, ugonjwa umeshasambaa mwili mzima.

 

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya nchini. “Huduma za matibabu ni gharama, wananchi wengi bado hawamudu gharama za matibabu, suluhisho pekee ni kujiunga na bima ya afya ili tuwe na uhakika wa matibabu pale tutakapokuwa tumeugua” aemesema Mhe. Ummy Mwalimu.

 

Kwa upande wake Mratibu wa AfyaCheki Dkt. Isack Maro amesema kuwa kazi hiyo wanaifanay kwa ari bila kushurutishwa kuwaelimisha na kuwahamasisha watanzania umuhimu wa kupima afya zao na kuweza kupata huduma za matibabu mapema.

 

“Kuna ongezeko kubwa sana la magonjwa hasa ya kuambukiza, magonjwa haya yanaanza taratibu bila dalili zozote na huonekana baadae yakiwa tayari yameshaathiri kwa kiwango kikubwa, hivyo tunawakumbusha wananchi kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao hata mara moja kwa mwaka na kutambua namna ya kuzuia magonjwa haya ya kuambukiza” amesema Dkt. Isack Maro.

 

Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Riziki Kisonga ambaye pia ni Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini amesema kuwa kupitia Kambi hii ya Afya Cheki Wizara ya Afya itashiriki katika kutoa huduma ili wananchi wa Mkoa huo na maeneo Jirani waweze kupata huduma za upimaji afya Jirani na maeneo yao.


“Wizara ya Afya kwenye kambi hii tumejipanga kutoa huduma ya upimaji wa ugonjwa wa kifua kikuu, maambukizi ya Viruisi vya Ukimwi, huduma za upimaji na utoaji wa dawa za Malaria pamoja na upimaji wa magonjwa yote yasiyokuwa ya kuambukiza” amesema Dkt. Riziki.

 

Kambi ya upimaji Afya kupitia kampeni ya Afya Cheki imeanza leo Agosti 21 na itakuwepo mpaka Agosti 25, 2023 ambapo wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo Jirani wanakaribishwa kuja kupata huduma za upimaji afya bure bila gharama yeyote katika Viwanja vya Usagara. 




RIDHIWANI KIKWETE: MSHIKAMANO HULETA MAFANIKIO.

 

Na Mwandishi wetu- Chalinze.

Upendo, Amani na Mshikamano ndio siri pekee ya mafanikio katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii.


Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala bora Ndg.Ridhiwani Kikwete wakati akiongea na wananchi wa maeneo mbalimbali katika kata ya Talawanda alipofanya ziara ya kuhamasisha na kukagua shughuli za maendeleo katika Halmashauri ya Chalinze.


Ridhiwani Kikwete alisema yeye Mbunge ametoa ahadi nyingi katika jimbo lake na utekelezaji wa ahadi hizo unahitaji mshikamano baina yake, wananchi na watendaji wa serikali ili kufikia malengo ya utekelezaji wa ahadi.


Alisema haiwezekani Mradi wowote utekelezwe bila ya mshikamano kwani hata kupata sehemu ya kuweka Mradi husika inahitaji, utayari, na mshikamano wa wananchi wa eneo hilo.


Aliendelea kwa kusema kuwa yeye Mbunge yupo tayari kushirikiana na wananchi wa jimbo lake ili kutekeleza ahadi zake kwao.


Katika ziara hiyo ya Mbunge ambayo ilimfiksha katika vijiji vya Msigi, Magulumatari na Mindukene imelenga zaidi kutoa mrejesho wa kazi kwa wananchi wa maeneo hayo pamoja  na kutekeleza ahadi waliyo ahidiwa wananchi katika mikutano na maombi mbalimbali waliyowasilisha kwa mbunge huyo.


Mbunge huyo wa jimbo la Chalinze alitekeleza ahadi yake ya kuchangia mabati kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Chama katika kata hiyo. 










MEYA WA IRINGA: ATOA MATUMAINI YA KUINUNUA RUVU SHOOTING.

 


Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amewaomba wadau na mashabiki wa soka ndani na nje ya mkoa wa Iringa kuwa wavumilivu wakati mipango ikiendelea juu ya manunuzi ya timu ya Ruvu Shooting ya Championship. 


Katika taarifa yake iliyosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, ilisema Manispaa hiyo ipo mbioni kukamilisha taratibu zote za manunuzi ya timu hiyo ya Maafande yenye makazi yake mkoani Pwani na kuelezwa kuwa itahamishiwa rasmi Iringa. 



Ruvu Shooting ilishuka msimu uliopita na msimu ujao itashiriki Championship inayotarajia kuanza Septemba 2 mwaka huu, huku mapema ikielezwa kuwepo sokoni rasmi kupigwa bei. 


Ngwada alisema kuwa bado taarifa hazijawa rasmi licha ya mazungumzo kuendelea akisema kuwa baada ya kukamilisha taratibu zote wataweka wazi.


 "Niwaombe wadau na mashabiki kuwa na uvumilivu kwenye hili wakati taratibu zikiendelea, tukikamilisha tutaweka wazi na nchi itafahamu" alisema Ngwada. 



Iringa haijawa na timu Ligi Kuu kwa misimu minne sasa tangu waliposhuka daraja Lipuli na msimu ujao haijawa na uhakika wa kushuhudia michuano hiyo pamoja na championship.


CHANZO 

https://www.mwanaspoti.co.tz/ms/soka/meya-ngwada-kuhusu-ruvu-shooting-tuwe-wavumilivu-4341308



MAGAZETI YA LEO JUMATATU TAREHE 21 AGOSTI 2023.

 























Sunday, August 20, 2023

KIKWETE: TUSICHANGANYE DINI NA SIASA.

 

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuacha kuchanganya dini na siasa.


Mh. Kikwete ameyasema hayo leo Tarehe 20 Agosti 2023 wakati akizindua kanisa la SDA Rorya mkoani Mara, na kuongeza kwa kusema kuwa, heshima ya viongozi wa dini itabaki kwenye uongozi wa dini na kwamba wakichanganya dini na siasa heshima yao itashuka.


Aidha alifafanua kuwa nchi hii ambayo serikali yake haifungamani na dini ila wananchi wake ni waumini wa dini tofaiti wanapaswa kuheshimiana na kuepuka kila kinacholeta viashiria vya udini.


Alisema kama ni mwanasiasa anapaswa kubaki kwenye siasa na kama ni mwana dini anapaswa kubaki kwenye dini kwa kufanya hivyo ndio kutaleta ndhamu, kuheshimiana na kutunza amani iliyopo hapa nchini.


Alionya kuwa mgawanyo utakaosababishwa  na dini ni mbaya na unaweza kuleta mpasuko ambao hatutoweza kuuba.


Alisema kuyatazama maswala kiutawala, maswala ya kisiasa kwa mtazamo wa kidini ni hatari kwa amani ya nchi 


Alisisitiza kuwa, viongozi wa dini watakaokuwa na mtazamo wa kisiasa tunatakiwa tuwanyanyapae.


BILIONI 30 KUTATUA CHANGAMOTO YA UMEME URAMBO, KIGOMA.

 

Na Mwandishi wetu -Urambo.


Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweza kutatua changamoto ya umeme katika Wilaya ya Urambo na Mkoa wa Kigoma ambapo zaidi ya Bilion 30 zimepelekwa katika kuhakikisha zinajenga Kituo Cha Kupoza Umeme katika Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora.


Akizungumza a katika Ziara ya Wilaya hiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania UWT Mary Chatanda amewapongeza Kampuni ya TBEA_ CHINA na uwongozi wa Tanesco na Serikali kwa ujumla kwa kusimamia kikamilifu mradi huo ambao utakuwa chachu ya kuondoa Changamoto za umeme katika baadhi ya Vitongoji.


Mwenyekiti Chatanda alisema Serikali ya awamu ya sita inalengo la kuondoa adha ya umeme kwa wananchi wake katika kuhakikisha wanapata umeme kila sehemu na kwasasa amewaomba wananchi kuhakikisha wanalinda Miundombinu ya umeme katika maeneo yao.


" Nimeona maeneo mengi huwa wanachoma moto nguzo hivyo niwaombe wananchi wangu kuwa makini na kulinda Miundombinu ya Tanesco katika maeneo yenu ili Serikali izidi kuleta fedha nyingi na kuepusha umeme kuzimika mara kwa mara"


Hata hivyo Mwenyekiti Chatanda amefurahishwa na ajira ya vijana ambao wanaofanya katika Ujenzi huo wanatoka katika Wilaya ya Urambo na Wilaya jirani za Mkoa wa Tabora kwa kuwa wao Viongozi wanahimiza kuwajali na kuthamini wazawa ambao wapo katika eneo la mradi ili wawe chachu ya kuwa walezi wa Mradi husika.


"Mwenyekiti Chatanda amewasii vijana ambao wamepewa ajira hapo kuwa waaminifu na waadilifu katika kulinda vifaa na Miundombinu iliyopo katika mradi huo ili mradi umalizike kwa wakati na uwe bora zaidi ."






RAIS DKT. SAMIA AMTEMBELEA MKUU WA MAJESHI MSTAAFU JENERALI SARAKIKYA

 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na kuzungumza na Mkuu wa Majeshi wa kwanza Mstaafu Jenerali Mrisho S. Sarakikya wakati alipomtembelea kumjulia hali nyumbani kwake Mkoaranga Wilaya ya Arumeru Arusha leo tarehe 20 Agosti, 2023.



TANZANIA, INDIA ZAIMARISHA USHIRIKIANO KIUCHUMI.

 

Arusha


Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Serikali ya Tanzania na nchi ya India umeimarika na umeendelea kuzinufaisha nchi hizo kiuchumi.


Dkt. Biteko amesema hayo katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 77 ya Uhuru wa India zilizoandaliwa na watanzania wenye asili ya nchi hiyo yaliyofanyika Agosti 19 jijini Arusha.


"Kama mnavyofahamu nchi ya India na Tanzania zimekuwa na mahusiano ya muda mrefu ya kidiplomasia kiuchumi na jamii ya wahindi katika nchi yetu inajishughulisha na uwekezaji mwingi katika biashara na viwanda," amesema Dkt. Biteko.


Aidha, Dkt. Biteko amesema nchi ya India imefanya biashara nyingi kwenye Sekta ya Madini ikiwa pamoja na uuzaji na ukataji wa madini na mnyororo mzima wa shughuli uongezaji thamani madini.


Amesema hapa nchini wapo watu wenye asili ya India wapatao elfu 50 na kati ya hao wageni wenye pasipoti ya India wapo kati ya elfu 15 na elfu 20 na Arusha pekee ina zaidi ya watu 2000 wenye asili ya India na wamewekeza kwenye maeneo mengi na kufanya biashara mbalimbali.


Dkt. Biteko ameongeza kuwa, wageni wanaofika nchini kutoka India wamekuwa mstari wa mbele katika kuwekeza na kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara kwenye Sekta ya Madini, viwanda na maeneo mengine.


"Tumeungana nao kusheherekea uhuru wao na kuwatia moyo, kuwatakia kila la heri kama Serikali tunawaunga mkono kwenye kila juhudi wanazozifanya na tunaliombea mema Taifa la India liendelee kuimarika ni Taifa kubwa lenye watu wengi na mchanganyiko mkubwa wa utamaduni," amesema Dkt. Biteko.


Kwa upande wake, Balozi wa India nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema Tanzania imekua sehemu salama pa kuishi na kufanya biashara na kuendeleza shughuli za utamaduni za nchi yao. Ameongeza kuendelea kuimarisha ushirikiano huo katika nyanja zote.


Naye, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mrisho Gambo amesema anajivunia umoja, upendo na mshikamano uliopo kati ya Watanzania wenye asili ya India wanaoishi hapa nchini hususan wanavyochangia katika masuala mbalimbali ya maendeleo.


"Ukiangalia kwenye ajira wametoa ajira nyingi kwenye viwanda, lakini pia wanalipa kodi kwa Serikali. Nawaahidi kuwapa ushirikiano jamii ya Wahindi ili shughuli zao ziweze kuwa salama zaidi," amesema Gambo.



Nchi ya India huadhimisha sherehe za Uhuru kila ifikapo tarehe 15 Agosti ya kila mwaka ambapo jamii ya wahindi nchini pia imeadhimisha sherehe hizo mkoani Arusha.





TWIGA MINERALS YASHINDA KIPENGELE CHA KAMPUNI ZA UBIA NA SERIKALI

 


Yatoa Gawio la Shilingi Bilioni 84 Serikalini


Arusha


Kampuni ya Twiga Minerals Cooperation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Cooperation imeongoza katika kipengele cha Kampuni zenye ubia na Serikali katika utoaji Gawio kwa Serikali.


Tuzo ya ushindi kwa kampuni hiyo ilitolewa Agosti 19, 2023 jijini Arusha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu na Taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma.


Akizitaja kampuni zilizofanya vizuri katika kipengele hicho, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema kuwa kampuni ya Twiga imefanya vizuri katika kipengele hicho kwa kutoa gawio kwa Serikali ya kiasi cha shilingi bilioni 84 Mwaka wa Fedha 2022/23.


Kampuni ya Barrick ndiyo kampuni ya kwanza kuingia ubia na Serikali miongoni mwa kampuni za madini hali ambayo ilihamasisha na kampuni nyingine kutoka nje kusaini mikataba yenye thamani kubwa na Serikali katika shughuli za uchimbaji wa madini ya aina mbaimbali yakiwemo madini muhimu na ya mkakati.


Aidha, ubia na kampuni hiyo umetajwa mara kadhaa kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mbalimbali huku kampuni hiyo ikitaja kuutumia ubia wa Tanzania kuutekeleza katika nchi nyingine ilikowekeza.


Migodi iliyo chini ya kampuni ya Twiga Minerals ni pamoja na North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi. 


Mwezi Januari, 2023 wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Meneja Mkazi wa kampuni ya Twiga Melkiory Ngido alisema mwaka 2020 kampuni hiyo ilitoa gawio kwa Serikali kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 huku kipindi cha mwaka 2017 hadi 2022 kiasi cha shilingi bilioni 24.3 kilitolewa kwa halmashauri kama tozo mbalimbali zinazotozwa katika maeneo yenye shughuli za migodi yake.


" Kampuni ya Twiga imepanga kuendeleza shughuli za utafiti ili kuongeza uhai wa migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu na ni matazamio ya uhai wa mgodi wa Bulyanhulu ni kufika mwaka 2040 na North Mara kufika mwaka 2039," alisema Ngido katika kikao hicho. 





BUSH LAWYER AFICHUA SIRI YA BARAZA LA MAASKOFU WA KANISA KATOLIKI KUPINGA MKATABA WA BANDARI.

 

Na Mwandishi Wetu.


IKIWA ni siku moja tu tangu Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) wakutame jijini Dar es Salaam na kutoa tamko lao kupinga mkataba wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Mussa Chengula maarufu ‘Bush Lawyer’ ameibuka na kufichua siri ya kupinga mkataba huo.



Akizungumza na waandishi wa habari jana Agost 19/2023 jijini Dar es Salaam, Chengula amewataka wakosoaji wa mkataba wa Bandari kuacha kujificha kwenye kichaka cha mkataba ilihali wana jambo jingine lililojificha dhidi ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.



Chengula maarufu kwa jina la ‘Bush Lawyer’ amedai viongozi wa dini wamekuwa ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa ubadhirifu unaoikosesha serikali mapato yanayotokana na bandari yetu hiyo.


 “Baadhi ya viongozi maarufu na makundi ya kijamii wakiwemo wanasiasa, wafanya biashara na wakubwa na baadhi ya viongozi wa Dini walijituma kwa maslahi yao binafsi na kutumika kwa maslahi ya washirika wao binafsi na kugeuza Bandari yetu kuwa shamba la bibi kwa kuagiza vitu mbalimbali kwa njia ya msamaha wa kodi huku wakifanya biashara ya vitu hivyo kinyume na makusudio ya msamaha waliomba na kupewana serikali”, alisema na kuongeza.



“Jambo hili lilishawahi kuthibitishwa na serikali ya awamu ya nne kupitia Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda alipobaini uwepo wa magali yaliyoingia kwa njia ya msamaha wa kodi na kukutwa yadi yakiuzwa kama mali ya kibiashara ya mtu binafsi mpaka serikali ya awamu ya nne ikafikiria namna ya kuondoa swala la msamaha wa kodi kwa taasisi za Dini ili kulinusuru Taifa na ufisadi wa kimazingira kupitia baadhi ya taasisi za Dini”.



Aidha ‘Bush Lawyer’ amesema TEC ni vema ikajipambanua kuwa wanapinga mkataba wa bandari kutokana na maslahi yao binafsi badala ya kujiegemeza na kudai ni sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, ilihali hawakutuambia utafiti wa kujua watu wengi hawakubaliani na mkataba huo waliufanya kwa kutumia sampo gani.



Kuhusu haki ya kutoa maoni na kujieleza, Bush lawyer alisema kuwa, kila Mtanzania yuko huru kutoa maoni yake juu ya suala lolote lile kwa lengo la kujenga na kustawisha maendeleo ya Taifa letu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 18. kifungu kidogo cha kwanza na cha pili (1-2).



Hata hivyo amesema kwa kuzingatia ibara ya 26 kifungu kidogo cha kwanza na chapili (1-2) maoni sio kejeri, dharau, uwongo, uzushi, kashfa, matusi au kupinga uwamuzi wowote wa kisheria bila kufuata taratibu za kisheria zinazotajwa ibara ya 30 kipengele kidogo cha (3) na cha (5). Hayo sio maoni yanayotakiwa na ibara hizo tajwa hapo juu na vipengele vyake ispokuwa ni uwasi na uvunjifu wa katiba ya nchi katika kuathiri utekelezaji wa mamlaka za nchi na sheria zake.



Katika hatua nyingine ‘Bush lawyer ameishauri serikali kuangalia upya juu ya uwezekano wa kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa yenye dhamira ovu ya kuvunja umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.



“Kutokana na sababu za kiusalama tunaishauri serikali isitishe kwa dharura mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ambavyo vinaonekana vikitumia mikutano hiyo kukejeri, kudharau, kukashifu, kutukana viongozi wa serikali na mamlaka zake pamoja na kuchochea wananchi kutokuwa na Imani na mahusiano mazuri na Serikali yao.



‘Bush Lawyer’ amesema ushauri huu ni umuhimu ukazingatiwa kwa dharura na kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi kwa sababu katika utendaji wa shughuli za kisiasa uko muda wa kufungua kampeni na upo mwisho wa muda wakufunga kampeni hivyo hakukuwa na sababu yoyote ya kimaendeleo na uchumi wa Taifa kuruhusu harakati ya kufanya mikutano ya kisiasa kwa vyama ambavyo vimeshindwa kupata ridhaa ya wananchi.