Saturday, March 21, 2020

KAWAMBWA AKABIDHI VITI MWENDO KWA WATOTO WENYE ULEMAVU.

 
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, akiwa katika picha ya pamoja na watoto wenye ulemavu pamoja na wazazi na walezi mara baada ya kukabidhi vitu hivyo vya magurudumu katika ofisi yake mjini Bagamoyo leo Tarehe 21 Machi 2020.
..............................................


Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa amekabidhi viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu wa miguu katika jimbo lake.


Akizungumza wakati wa kukabidhi viti mwendo hivyo, Dkt. Kawambwa alisema kuwa, viti mwendo hivyo ni msaada kutoka kwa mama Janeth Magufuli hivyo anakabidhi kwa walengwa ili kutimiza wajibu wake kama alivyooagizwa na mama Janeth Magufuli.


Alisema Viti mwendo hivyo vitawasaidia watoto hao kutembea sehemu mbali mbali kwa kuendesha wenyewe au kuendeshwa na kuondoa usumbufu wa kuwabeba hata pale wanapokuwa na safari za lazima kama vile Hospitali Nk.


Aidha, amewataka wazazi na walezi kuvitunza vifaa hivyo ili viendelee kuwahudumia watoto hao kwa muda mrefu zaidi jambo ambalo litampa moyo yule aliyetoa na kufikiria kutoa msaada mwingine.


Katika hatua nyingine Mbunge huyo wa Jimbo la Bagamoyo aliwashauri kina mama wenye watoto walemavu kuunda kikundi na kukisajili ili waweze kupatiwa mikopo ya serikali inayotolewa kwa vikundi.


Alisema serikali haiwezi kusaidia wananchi mmoja mmoja hivyo ni vyema wakiwa kwenye kikundi ili waweze kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri ambayo haina riba na kwamba itawasaidia kujiendeleza kulingana malengo watakayojiwekea.


Dkt. Kawambwa alitoa rai hiyo baada ya kina mama wenye watoto walemavu kumuomba awasaidie wapate mitaji kwaajili ya biashara ili kukabiliana na malezi ya watoto hapo.


Kwa upande wao wazazi na walezi wa watoto hao wamemshukuru Mbunge huyo kwa kufikisha viti hivyo kama alivyokabidhiwa na mama Janeth Magufuli.


Aidha wamesema shukrani zimfikie mama Janeth Magufuli mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa moyo wa huruma na kuweza kufikiria kuwa kuna watu wenye uhitaji wa vitu hivyo.
 
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, akiwa katika picha ya pamoja na watoto wenye ulemavu pamoja na wazazi na walezi mara baada ya kukabidhi vitu hivyo vya magurudumu katika ofisi yake mjini Bagamoyo leo Tarehe 21 Machi 2020.
 
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, akizungumza na wazazi na walezi kabla ya kukabidhi viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu ofisini kwake Bagamoyo mjini  leo Tarehe 21 Machi 2020.

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, akizungumza na wazazi na walezi kabla ya kukabidhi viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu ofisini kwake Bagamoyo mjini  leo Tarehe 21 Machi 2020.
 
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, akikabidhi mfuko wa wenye spana zinazotumika kufungulia viti mwendo hivyo ikiwa vitaharibika ofisini kwake Bagamoyo mjini  leo Tarehe 21 Machi 2020.

Muonekano wa viti mwendo vilivyokabidhiwa kwa watoto wenye ulemavu na Mbunge wa Jimbo Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa leo Tarehe 21 Machi 2020.

Kutoka kulia ni Katibu wa Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Margret  Joseph , Diwani wa kata ya Magomeni, Mwanaharusi Jarufu, na Diwani wa viti maalum tarafa ya Mwambao, Shumina Rashidi, wakati wa kukabidhi viti mwendo katika ofisi ya Mbunge wa Bagamoyo dkt. Shukuru Kawambwa. 


BAGAMOYO: MUME AMUUA MKEWE BAADA YA KUMFUMANIA NA MWANAUME MWINGINE.

Watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani, kwa tuhuma za kumuua mwanamke na kumfukia katika shamba la mahindi.


Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wankyo Nyigesa alisema tukio hilo limetokea tarehe 10 mwezi wa tatu mwaka huu 2020 Kata ya Kibindu Tarafa ya Chalinze wilaya ya kipolisi Chalinze Mkoani humo.

Alisema tukio hilo limetokea baada ya Chacha Chacha Machangu mwenye umri wa miaka 27 Mkuliya mkazi wa Kibindu kumfumania mkewe (jina linahifadhiwa) akiwa na mwanaume mwingine.

Alisema mara baada ya Chacha kumfumania mkewe na mwaume mwingine alimshambulia kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo cha mwanamke huyo usiku wa kuamkia tarehe 10 Machi 2020.

Kamanda Nyigesa alisema mara baada ya tukio hilo, Chacha Machangu kwa kushirikiana na ndugu zake ambao ni Emanuel Chacha Machangu mwenye umri wa miaka 19 Mkuriya na Hamisi Chacha Machangu mwenye umri wa miaka 22 Mkuriya wote wakazi wa Kibindu walichimba shimo katika shamba la mahindi na kuufukia mwili wa marehemu huyo.

Aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi lilipata taarifa tarehe 19/03/2020 na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote watatu waliojihusisha na tukio hilo na wao wenyewe kwa ridhaa yao walionesha mahali shimo lilipo.


Kamanda Nyigesa alisema Baada ya Jeshi la Polisi kufukua ulipatikana mwili wa marehemu ambao ulifanyiwa uchunguzi na daktari kisha kufanyiwa mazishi kwa heshima zote.
 

Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika uhalifu huu. 


Friday, March 20, 2020

DC LINDI ATAKA WATOTO WASITEMBEE HOVYO KUEPUKA CORONA


NA HADIJA OMARY, LINDI.

MKUU wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga amewataka Wazazi na Walezi Wilayani humo, kuhakikisha Watoto hawatoki Majumbani mwao baada ya Shule kufungwa ili kuendelea kuchukuwa taadhari dhidi ya ugonjwa wa corona.

Ndemanga ameyasema hayo jana alipokuwa anazungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG baada ya kubaini uwepo wa mikusanyiko ya watoto katika Mitaa mbali mbali ya Manispaa ya Lindi wakiwa katika michezo yao.

Aidha, alisema kuwa lengo la Serikali kufunga Shule hizo ni moja ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa hatari wa corona kwa kupunguza misongamano ya watu katika maeneo mbali mbali.

“lengo la Serikali kufunga Shule lilikuwa kuwanusuru watoto hao pamoja na familia zao na ugonjwa huo kwa kupunguza misongamano na mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima sasa kama watoto hao wataendelea kufanya mikusanyiko mingine wakiwa nje ya shule basi haitakuwa na maana kwa shule kufungwa” alisema Ndemanga.

Ndemanga alisema kuwa ni wajibu wa mzazi au mlezi kuhakikisha kuwa mtoto haendi kwenye mikusanyiko ya michezo yoyote ikiwa ni pamoja na mchezo wa mpira, kuogelea bichi na kadhalika.

“Endapo mtoto ataachwa akienda mtaani na mzazi pasipokujua yupo wapi ikitokea kwa bahati mbaya tatizo amepata huko la ugonjwa wa corona sasa atakuwa analeta ugonjwa ndani jambo ambalo Serikali haikupenda litokee” alieleza Ndemanga.

Ndemanga alisema ili kuendelea kuwalinda watoto hao ni wajibu wa wazazi kwa kushirikiana na Serikali kuendelea kutoa elimu kwa watoto wao juu ya ugonjwa huu hatari wa Corona.

Nae Mganga Mkuu wa Manispaa ya Lindi Libamba Sobo alisema kuwa katika mikusanyiko ya michezo ya watoto sio tu hatari kwa watoto wale waliofunga Shule bali hata watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano nao ni hatari zaidi kwa kufikwa haraka na magonjwa kutokana na kinga zao.

Pamoja na mambo mengine alisema kuwa taadhari ya kunawa mikono kila baada ya muda inaweza kuwa msaada mkubwa wa kutopata maabukizi ya virusi hiyo vya corona hivyo ni wajibu wa wazazi na walezi kuwakumbusha watoto wao kunawa mikono mara kwa mara wanapotoka kucheza hata kama wakiwa maeneo ya nyumbani Kwa upande wake yusuph khatibu (8) mwanafunzi wa Darasa la pili katika shule ya Msingi Stadium iliyopo katika Manispaa hiyo ya Lindi aliwahasa watoto wenzao kuacha kukusanyika katika michezo mbali mbali mpaka pale ugonjwa huo utakapoisha au utakapopatikana tiba yake