Monday, March 9, 2020

WAWANAWAKE TUGHE PWANI WACHANGIA MSAADA WA CHAKULA KWA WALIOPATWA NA MAFURIKO RUFIJI

Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wanawake  wa serikali kuu na afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani Catherine Katele kulia akimkabidhi msaada wa magunia ya mahindi Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji Maria Katemana kwa ajili ya kuwapatia wananchi waliopata maafa ya mafuriko kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni. (PICHA NA VICTOR MASANGU).
.......................................


VICTOR MASANGU, RUFIJI

Baadhi ya wananchi Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani wamekosa makazi ya kuishi kutokana na nyumba zao pamoja na maduka  kuzingirwa na maji  ikiwemo wengine kukumbwa na changamoto ya mazao yao mbali mbali  zaidi ya hekta 4,000 kusombwa na maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha maafa ambayo yamepelekea wananchi kuishi katika mazingira magumu  hivyo kupelekea kuishi katika mazingira magumu.


Hayo yalibainishwa  na wananchi hao wakati wa ziara ambayo imefanywa na Wanawake wa  chama cha wafanyakazi wa serikali kuu na afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani  yenye lengo la kutembelea  baadhi ya maeneo ambayo yamekumbwa na maafa ya mafuriko  kwa ajili ya  kutoa msaada wa vyakula kwa walengwa.


Wananchi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti akiwemo Shamte Ally na Said Salumu walisema walidai kwamba  mvua  ambazo zinaendelea kunyesha kwa kipindi hiki zimewaletea hasara kubwa ya mazao yao, mifugo, pamoja na makazi kuzingirwa na maji hivyo wameiomba serikali ya awamu ya tano kuwasaidia  msaada wa kupata chakula  pamoja na sehemu  kwa ajili ya  kuishi.


Aidha waliongeza kuwa kwa sasa kutokana na kuwepo kwa hali hiyo baadhi ya bidhaa ya vyakula katika maeneo mengine zimepanda bei hivyo wengine kutokana na kipato chao kuwa cha chini wanashindwa kumudu gharama kwa ajili ya kununua vyakula hivyo wameomba wadau mbali mbali kwa kushirikiana na serikali kuliangalia suala hilo kwa jicho  la tatu katika kuwasaidia kuondokana na hali hiyo.


Kwa kweli ndugu waandishi kwanza tunashukuru sana hawa wakinamama wa Tughe Mkoa wa Pwani kwa kuweza kuja mpaka huku katika maeneo ya Rufiji, kwani kwa sasa tupo katika hali ngumu sana kutokana na mazao mbali mbali ya chakula ambayo ndio tulikuwa tunayategemea sisi pamoja na watoto wetu yote wamesombwa na maji, lakini pia tunashukuru kupatiwa msaada huu lakini bado tunahitaji zaidi ili tuweze kujikimu,” walisema wananchi hao.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji Maria Katemana alikiri  kuwepo kwa maafa hayo na kubainishwa kwamba  hadi sasa zaidi ya hekta 4000 za mazao ya aina mbali mbali ikiwemo mahindi mpunga,  yamesombwa na maji ambapo  pia kuna baadhi ya shule nne  za msingi zimefungwa kwa muda kutokana na  kuwepo kwa hali hiyo ya mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.


“Kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu kwa niaba ya serikali ya Wilaya ya Rufiji kwa msaada huu wa chakula cha mahindi ambao umetolewa na Wanawake wa TUGHE Mkoa wa Pwani kwa lengo la kuwasaidia baaadhi ya wananachi amabao wamekumbwa na mafuriko hayo ambayo kwa kweli yamesabisha hekta  zaidi ya 4000 za mazao kusombwa na maji na kuna maeneo mengine ya shule bado maji yapo, hivyo tunaendelea kujitahidi kwa hali na mali ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao, alisema Maria.


Kufuatia kutokea kwa  maafa hayo ya mafuriko Wanawake kutoka chama cha wafanyakazi wa serikali kuu na afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani  wameguswa na tukio hilo na kuamua kwenda kutoa msaada wa vyakula mbali mbali ikiwemo mahindi kwa wananchi ambao wamekumbwa na maafa ya  mafuriko hayo kwa lengo la kuwasaidia kuweza kupata chakula ikiwemo kupata mbegu kwa ajili ya kupanda tena kutokana na mazao yao yaliyosombwa na maji.


Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wanawake  wa serikali kuu na afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani Catherine Katele alisema kwamba waliamua kwenda kutembelea baadhi ya maeneo ambayo yamekumbwa na mafuriko  na kutoa msaada wa vyakula kama mahindi ambayo yatawasaidia wananchi kuweza kupata chakula na mengine kuyatumia kwa ajili ya  kupanda mazao mengine ambayo yamekwenda na maji.


“Sisi kama wanawake wa TUGHE Katika Mkoa wa Pwani kwa kweli tumeguswa sana na jambo hili la wenzetu wa Rufiji kupata maafa ya mafurikio, hivyo tukaona ni vyema tufunge safari ya kuja mpaka huku na kweli tumejionea jinsi ya nyumba mbali mbali ambazo zimezingirwa na maji na mazao ambayo yamesombwa na maji kwa hiyo kwa hiki kidogo tulichokitoa cha msaada wa mahindi kitaweza kuwasaidia kwa namna moja ama nyingine na pia tutazidi kuendelea kutoa misaada mbali mbali kwa watu wenye mahitaji, “alisema Katele.


Wilaya ya Rufiji iliyopo Mkoa wa Pwani ambayo ina jumla ya kata zipatazo 13 imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya maafa ya mafuriko hasa katika kipindi cha mvua zinaponyesha kutokana na baaadhi ya maeneo kuwepo pembezoni mwa mto Rufiji hivyo kupelekea baadhi ya mazao kusombwa na maji na nyumba nyingine kuzingirwa na maji na kusababisha wananchi kuishi katika mazingira magumu.

Baadhi ya wanawake wa Chama cha Tughe Mkoa wa Pwani wakiwa wanatoa msaada wa mahindi kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji akiwa ameongozana na viongozi mbali mbali wa serikali kwa ajili ya kuwapatia wananchi ambao mazao yao yamesombwa na maji na wengine nyumba zao kuzingirwa kutoka na mafuriko yaliyotokea. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

Wanawake wa chama cha Tughe Mkoa wa Pwani wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbali mbali wa serikali wakiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji mara baada ya halfa fupi ya kukabidhi magunia ya mahindi lengo ikiwa ni kuwapatia wananchi ambao wamekumbwa na maafa ya mafuriko na kusababisha mazao yao kusombwa na maji. (PICHA NA VICTOR MASANGU).

Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji Maria Katemana akizungumza jambo na baadhi ya viongozi wa wanawake wa Tughe Mkoa wa Pwani walipofika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha na kutoa msaada wa magunia ya mahindi pamoja na vyakula mbali mbali wa wananchi ambao wanamahitaji kutokana na kupata mafuriko. (PICHA NA VICTOR MASANGU.)

Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wanawake wa serikali na afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani Catheline Katele akifafanua jambo kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji hayupo pichani kuhusiana na ujio wao wa kufanya ziara maalumu yenye lengo la kutoa msaada wa vyakula mbali mbali ikiwemo magunia ya mahindi kwa ajili ya wahanga wa mafuriko. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji Maria Katemana akiwa na wanawake wa Tughe Mkoa wa Pwani wakiwa wanatembea kwa furaha mara baada ya kumalika kwa sherehe ya kutoa msaada wa vyakula mbali mbali ikiwemo magunia ya mahindi ambayo yametolewa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na mafuriko (PICHA NA VICTOR MASANGU)

Baadhi ya viongozi wa Tughe Mkoa wa Pwani wakiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Rufiji wa kati kati wakipiga makofi ikiwa ni ishara ya kufurahi mara baada ya kumaliza kutoa msaada wa magunia ya mahinda kwa waananchi waliokubwa na maafa ya mafuriko. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

Baadhi ya wanawake wa Tughe Mkoa wa Pwani wakiwa wanaimba nyimbo maalumu mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kwa ajili ya halfa ya kukabidhi mahitaji mbali mbali kwa wananchi ambao walipatwa na mafuriko na mazao yao kusombwa na maji na wengine nyumba zao kuzingirwa na maji. (PICHA NA VICTOR MASANGU)


MBOLEA ZA VIWANDANI ZINAHARIBU MASHAMBA.

Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika Maandalizi ya eneo la kutengenezea mbolea ya asili inayotokana na kuoza kwa mimea (MBOJI).
.............................................


NA HADIJA HASSAN LINDI.

Matumizi makubwa ya kemikali na mbolea za viwandani ni moja ya sababu inayowafanya wakulima katika maeneo mengi hapa nchini kufanya kilimo cha kuhama hama kutokana na mashamba yao ya awali kupoteza rutuba ya udongo.

Hayo yameelezwa na Ofisa Mradi wa Shirika la kilimo endelevu Tanzania (SAT) Stanslaus Kisatu, katika mafunzo ya maofisa ugani jamii 37 wa vijiji vinne vya Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi yaliyofanyika katika ofisi ya kijiji cha Kinyope.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyotolewa na Shirika la kilimo endelevu Tanzania (SAT) kwa kushirikiana na SWISS AID TANZANIA yana lengo la kuwafundisha wakulima mbinu mbali mbali za kilimo hai ikiwa pamoja na urutubishaji Aridhi, matengenezo na matumizi ya mbolea ya asili inayotokana na kuoza kwa mchanganyiko wa mimea (MBOJI) ambayo itatumika katika upandaji wa mazao katika mashamba yao.

Kisatu alisema kuwa kilimo cha kuhama hama ni moja ya madhara yanayotokana na wakulima kutofuata kanuni za kilimo hai na badala yake kutumia kemikali na viuwatilifu vingine hali inayopelekea Aridhi kuchoka na kushindwa kutengeneza virutubisho kwa mimea inayopandwa.

“Aridhi ikichoka inamfanya mkulima kushawishika kufanya kilimo katika eneo lingine kutokana na kupata mazao machache kwa sababu anapopata mazao kidogo hulazimika kutafuta Aridhi mpya , hivyo kitendo hicho kinachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa misitu ya hifadhi” alisema kisatu.

“sasa hivi wakulima wamekuwa wakilalamika sana kuwa mashamba yao yanaingiliwa na nyani lakini kumbe wao wamejikuta wameanzisha mashamba katika makazi ya wanyama poli hivyo moja kwa moja wanawapelekea chakula wanyama poli bila wao kujua, lakini wakifuata mbinu za kilimo hai kulikuwa hakuna sababu ya kutoka eneo moja kwenda sehemu nyingine kwa kuwa Aridhi ambayo wanaitumia itakuwa inaboreshwa siku hadi siku” alifafanua kisatu.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema kuwa kwa kutumia kanuni hiyo ya kilimo hai licha ya kuwa ni rafiki wa mazingira lakini pia ni gharama yake ni nafuu ukilinganisha na matumizi ya kemikali na viuwatilifu vya viwandani Kwa upande wake mariamu Bwanaly Mgani jamii kutoka kijiji cha Ruhoma alisema kuwa matumizi ya mbolea ya asili inayotokana na kuoza kwa mchanganyiko wa mimea (MBOJI) ni nafuu na inaweza kutumika kwa wakulima hata wa hali ya chini kwa kuwa inatumia malighafi yanayowazunguka katika mazingira yao.

Nae Mgani jamii kutoka katika kijiji cha Kinyope alisema kuwa kutokana na mafunzo hayo amejifunza kuwa endapo wakulima wote hapa nchini wataamua kutumia mbolea ya asili (MBOJI) kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza uwezekano wa magonjwa mengi yanayotokana na matumizi ya kemikali.

Mchanganyiko wa nyasi mbichi, nyasi kavu, samadi pamoja na maji vikiwa pamoja tayari kwa kutengeneza mbolea ya asili inayotokana na kuoza kwa mimea (MBOJI) iliyotengenezwa na washiriki hao wa mafunzo



Saturday, March 7, 2020

Katibu Mkuu CCM: Tutatumia Dola Kubaki Madarakani



Katibu  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ali, amekiri chama chake kuitumia dola kuhakikisha kinabaki madarakani.

Amesema kama chama chochote kinachoongoza serikali kitashindwa kutumia dola kubaki madarakani, utakuwa uzembe wa chama chenyewe.

Kwa kulitambua hilo, Dk. Bashiru amesema CCM imekuwa ikitumia dola kujihakikishia ushindi wakati wa uchaguzi na mwaka huu wamepanga "kuitumia dola kweli kweli".

Lakini, kiongozi huyo wa CCM akaonya kuwa chama kinachoongoza serikali, hakipaswi kuitumia dola kunyanyasa wapinzani wake.

Dk. Bashiru aliyasema hayo katika mahojiano maalum na vyombo vya habari vya IPP alivyovitembelea jijini Dar es Salaam jana.

"Ukishakuwa chama tawala, kuna dhana inaitwa nafuu ya mwenye madaraka. Ukishindwa kutumia nafuu hiyo, utakuwa kama KANU (chama tawala cha zamani cha Kenya), iliposhindwa kutumia nafuu hiyo, haikuwahi kurudi madarakani au UNIP ya Zambia.

"Unashika dola halafu unatumia dola kubaki madarakani. Akitokea mtu mwenye busara zaidi, akakwambia usitumie dola, ukamsikiliza, siku ukishatoka hurudi!

"Hata kwenye kazi, kazi inatafuta kazi. Kwa hiyo, aliye na dola anatumia dola hiyo kubaki madarakani. Ukweli hata Chadema ikiingia madarakani, kuiondoa kwenye dola itakuwa ni uzembe wake, kwa sababu ana nafuu na faida ya kuwa na dola.

"Kinachotakiwa usitumie dola vibaya kunyanyasa wapinzani wako. Wanaosubiri sisi (CCM) tulegelege kutotumia dola kubaki kwenye dola, watasubiri sana. Huo ndio ukweli, si wa Tanzania, si wa CCM, hata (Donald) Trump (Rais wa Marekani) kumwondoa leo ni ngumu," alisema.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kauli yake hiyo, Dk. Bashiru alisema: “Watu wakisema unatumia dola, wanadhani unakwenda kuiba, dola ni chombo cha wananchi, kutumia dola ni kutumia wananchi waliokukabidhi dola ili wakubakize kwenye dola, hii ndiyo maana yake tu.

“Hawa wananchi ambao tumeshirikiana wote kutafuta maji, kujenga miundombinu ya barabara kwa kodi zao, hakuna chombo kinachoweza kukusanya kodi ambacho si dola, ndiyo moja ya sifa, sifa kubwa ya dola ni kukusanya kodi, tutatumia kodi za wananchi.

“Ndiyo matumizi ya dola, tutatumia vyombo vya ulinzi na usalama kuwahakikishia wananchi wako salama, ndiyo matumizi ya dola.

“Sasa, wewe ukiwa na dola halafu wahuni wanakwenda Rufiji na Kibiti, si unakumbuka kulikuwa hakupitiki? Tulitumia dola kulinda usalama wa watu. Nimepita mara nyingi wakati mwingine ninashuka kula kuku wa kuchemsha, hayo ndiyo matumizi ya dola ninayosema.”

Dk. Bashiru alisema wanatumia dola kwa sababu wamekabidhiwa dhamana kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha usalama upo.

“Kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na rushwa, tumevitumia kuwatisha wala rushwa, sasa hayo matumizi mabaya? Tutaitumia kweli kweli.

“Matumizi ya dola ni kuwatumia wananchi wenye dola kwa kuwa dola ni mali ya wananchi, sisi tumekabidhiwa dhamana ya kuiendesha, tukiiendesha vizuri wananchi watatuamini zaidi, tukiiendesha vibaya, wanatuadhibu, wanampa mtu mwingine. Hata hao wengine wanatafuta dola.

“Faida tuliyo nayo tuna dola, wengine wanatafuta, mwenye dola akiishika vizuri, akaitumia vizuri na kufanya yale iliyoahidi, akatumia vizuri kujengea imani wapigakura, hawabadilishi ile dola kumpa mtu mwingine, hii ndiyo faida ya kuwa na dola.

“Mwaka huu kuna uchaguzi, tunakwenda kuomba, yaani tutapiga magoti tukiwa na maelezo mnajua tuliahidi hiki, tumefanya hivi, mmetupa kodi zenu tumefanya haya. Kwa hiyo watu wasitafsiri vibaya, lakini huwezi kuzuia tafsiri kwa kuwa hii ni dhana ya kifalsafa kidogo.

“Mtu anaweza kutumia maneno haya niliyoyasema akatafsiri vingine, maana yake ni hiyo, tutatumia dola kodi, taasisi za serikali kutekeleza ilani, tutatekeleza ahadi na kufika Oktoba, tutakuwa kwenye nafuu zaidi na faida zaidi kubaki madarakani," alifafanua.

KIFO CHA UPINZANI
Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwapo mkakati wa chama chake kuhakikisha kinaua upinzani nchini, Dk. Bashiru alisema hakuna dhamira hiyo, lakini kama kuna vyama vitakufa, CCM haiwezi kuzuia.

“Hatuna mpango wa kuzuia kifo, siyo kazi yetu kuzuia kifo cha chama, ni jukumu la chama kutokufa, mtu atakayekaa barabarani kusababisha chama kife kwa kushindwa ni halali yangu, na hili ni jukumu la vyama vyote vilivyosajiliwa kubaki hai, siyo jukumu la CCM kuvilea vyama visife, kifo kibaya cha chama huanza mapema.

“Ni kama ugonjwa wa kichwa, huanza taratibu, maumivu ya kichwa huanza polepole, na kifo cha chama huanza polepole kwa kushindwa, kifo cha kisiasa siyo kifo cha watu na katika siasa kuna kufa na kuzaliwa, vipo vilivyokufa, vipo vinachechemea, vingine haviwezi kufa, navijua," alisema.

Dk. Bashiru pia alitolea ufafanuzi madai ya CCM kununua wanachama kutoka vyama vya upinzani, akisema hakuna anayenunuliwa na kwamba wanaotoka upinzani ni 'watamu kweli' na matarajio yao ni kupokea wengine wengi zaidi kipindi hiki.

“Sijawahi kuona mavuno mazuri kama ya mwaka huu na mwaka jana na shughuli inaendelea, kama huo ndiyo mwelekeo wa vyama vya upinzani kufa, vijifunze namna ya kutunza wanachama wao," alitamba.

MCHUJO MKALI CCM
Katika mahojiano hayo, Dk. Bashiru pia alidokeza kuwapo mchujo mkali ndani ya chama kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuweka wazi kuwa mgombea wao wa urais mwaka huu ni Dk. John Magufuli.

Alisema kuna vigezo kadhaa vitakavyozingatiwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia nyendo za wanachama wao ambao tayari wameshaanza kupitapita na kupenyeza fedha kwa miamala ya simu ili kupita kwenye kura za maoni.

“Ninawatahadharisha, uteuzi siyo kura za maoni peke yake, ni kura za maoni na mjadala wa jina kwa jina kuhusu sifa za aliyeshinda na kukubalika kwa wananchi, hatutafuti wagombea wa CCM, tunatafuta wagombea wa CCM watakaopigiwa kura na wana CCM na wasiyo wana CCM na mwisho vikao ndivyo vinateua,” alisema.

Dk. Bashiru alisema kila mwana CCM ana haki ya kugombea uongozi, lakini hana haki ya kuteuliwa kwa sababu uamuzi wa kuteua ni wa vikao na hakuna atakayeteuliwa kuwania ubunge na udiwani bila kuangalia rekodi yake ya utendaji na mahudhurio yake kwenye vikao vya Bunge na mabaraza.

“Hakuna uteuzi wa bure, wapo wanaojihangaisha kuzungumza na wapigakura wakidhani wakimalizana nao kwenye kura za maoni, wamepata uteuzi, tutazingatia kura za maoni, na kwenda kwenye kumbukumbu zako ulisema nini, uliahidi nini na umetekeleza nini," alionya.

Dk. Bashiru pia alizungumzia maandalizi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka huu, akisema imejikita katika vipaumbele vitatu ambavyo ni kilimo, maji pamoja na ulinzi na usalama.

UKAWA TISHIO
Mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pia alikiri kuwa kuungana kwa baadhi ya vyama vya siasa katika kile kilichoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kulikuwa tishio kwa CCM katika uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema hilo lilijidhihirisha kwenye idadi ya kura ambazo CCM ilizipata kwa nafasi ya urais, akibainisha kuwa ilikuwa mara ya kwanza mgombea wao kushinda kwa kura chache.

Mtaalamu huyo wa sayansi ya siasa alisema Ukawa pia ulisababisha CCM kupoteza majimbo mengi zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

“Rais John Magufuli alipata kura ambazo mgombea wa CCM hajawahi kuzipata katika mfumo wa vyama vingi -- asilimia 58 na mgombea wetu (alikuwa) hajawahi kutofikia asilimia 60, Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakati anaingia alifikia asilimia 80,” alifafanua.

Dk. Bashiru pia alitoa ufafanuzi kuhusu kauli yake kwamba mchakato wa Katiba Mpya ni kiporo kilichochacha, akisema Ukawa ulioaminiwa na wananchi umesambaratika.

“Ndiyo maana nakiita kiporo kilichochacha, Ukawa iko wapi? Wanaweza kuingia na ajenda hiyo mwaka huu? Wanaweza kuaminika mwaka huu? Walikuwa wanatafuta Katiba Mpya kweli? Haijapatikana wamesambaratika…

"Kumbe ilikuwa ni geresha, ilikuwa ni kuteka mchakato wa Katiba Mpya kutafuta Ikulu, Ikulu haikupatikana, Ukawa imesambaratika. Kuwa na wanasiasa wa namna hiyo wa kuwavuta wananchi kutafuta jambo jema na kuwaacha solemba, nacho ni kiporo kilichochacha.

"Sasa, unataka kuumwa matumbo kula kiporo cha namna hiyo? Hatujamaliza matatizo ya Corona, tuingie kwenye kuumwa matumbo? Rais Magufuli akasema 'hatuwezi kuwa na siasa za kinafiki, watu wanatafuta Ikulu kwa kisingizio cha Katiba Mpya'", alisema.

UPINZANI KUITWA IKULU
Dk. Bashiru pia alimpongeza Rais Magufuli kwa kuendelea kukutana na Watanzania wa makundi mbalimbali Ikulu, akikumbusha kuwa amefanya hivyo kwa wafanyabiashara, wenye ulemavu na makundi mengi ambayo hukutana na wasaidizi wake.

"Ameshatuelekeza tukutane na makundi ya wawakilishi wote, anakutana na mabalozi, hata viongozi wa upinzani wana haki ya kukutana naye Ikulu, ndiye pekee ameifanya Ikulu ionekane ni ya Watanzania.

“Kama hiyo ndiyo inatajwa ni kujenga maridhiano, ni mkakati mzuri lakini siyo ile ya mtazamo wa kisiasa, bali kwa mtazamo wa kitaifa, Ikulu ni ya Watanzania wote na kila mmoja anaweza kukutana na Rais Ikulu,” alisema.

Chanzo: Nipashe