Friday, February 28, 2020

MGUMBA ATAKA HALMASHAURI ZITENGE ARDHI KWAAJILI YA KILIMO KWA VIJANA

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la vijana katika kilimo lililofanyika Njombe na kukutanisha vijana 200 toka mikoa ya Njimbe ,Iringa na Ruvuma jana.
.......................................


Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba ameziagiza halmashauri zote nchini kutenga ardhi ya kutosha kwa ajili ya vijana kuzalisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi .

Ametoa agizo hilo mjini Njombe wakati alipofungua kongamano la vijana wa mikoa ya Njombe,Ruvuma na Iringa kujadili fursa zilizopo katika sekta ya kilimo nchini.

Mgumba amesema kumekupo na malalamiko ya vijana kukosa ardhi kutokana na halmashauri kuwa na mashamba pori mengi yasiyopimwa na kulimwa.

“Halmasahauri zote zihakiki mashamba pori yote au yaliyochukuliwa mikopo na hayalimwi yapimwe na kugawiwa kwa vijana walio tayari kufanya kazi za kilimo nchini”.alisema Naibu Waziri Mgumba.

Ili kufanikisha hilo Mgumba mewataka vijana kujisajili kwenye daftari la wakulima linaroratibiwa na wizara yake ili serikali iwatambue na kujua changamoto zao na kisha kuwaonyesha fursa za ajira kwenye kilimo.

Naibu Waziri Mgumba amesisitiza halmashauri nchini kutoa fedha za mikopo kwa vijana bila urasimu ili vijana wanufaike na kuanzisha kazi za uzalishaji mazao ya kilimo na mifugo.

Mgumba aliwafahamisha kuwa serikali imeelekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuendelea kutoa mikopo kwa vijana ili wapate mitaji.

“Wapo vijana wengi wasomi wameamua kujiajili katika kilimo ili kufikia malengo ya kuongeza ajira ikiwa ni malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano kukuza sekta ya kilimo” alisema Mgumba.

Tanzania ina eneo la hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo hivyo vijana wajitokeze kutumia fursa hiyo kuanzisha kazi za kuzalisha mazao ya kilimo .

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe aliziagiza halmashauri zote za mkoa wa Njombe kuandaa katiba kwa

ajili vijana kushiriki shughuli za kilimo.

Aliongeza kusema watendaji wote wa halmashauri wapunguze urasimu kwa kukaa muda mrefu bila kupitisha maombi ya vijana wanaostahili mikopo ya fedha za mapato

ya ndani.

“Halmashauri punguzeni urasimu msikae zaidi ya robo mwaka bila kutoa mikopo kwa vijana,akina mama na walemavu” alisema Mkuu huyo wa wilaya ya Njombe.

Naye Mkurugezi wa Shirika la SUGECO Revocatus Kimario linaloratibu mafunzo maalum kwa vijana kwenda Israel na Marekani kujifunza fursa za kilimo kwa vitendo kwa mwaka mmoja amesema wengi wamenufaika.

Kimario amesema hadi sasa zaidi ya vijana 1000 wamepatiwa mafunzo ya kilimo,mifugo na uvuvi nchini Israel na wengine 90 nchini Marekani wamerudi nyumbani

wamefanikiwa kuzalisha ajira nyingi kwa wenzao .

Kimario ameishauri jamii kutotumia kilimo kama adhabu bali kitumike kama fursa ya kukuza ajira na kipato cha kaya na taifa.

Kongamano hilo la siku mbili linawakutanisha vijana wapatao mia mbili toka mikoa ya Njombe,Ruvuma na Iringa chini ya uratibu wa Wizara ya Kilimo na wadau toka wizara za kisekta na taasisi binafsi.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la vijana katika kilimo linalofanyika Njombe na kukutanisha vijana 200 toka mikoa ya Njimbe ,Iringa na Ruvuma jana.

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akisikiliza maelezo ya jinsi ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo toka kwa kijana mjasiliamali Fatuma  Mbaga (kushoto) toka Shirika la SUGECO la Morogoro.

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la vijana katika kilimo linalofanyika Njombe na kukutanisha vijana 200 toka mikoa ya Njimbe ,Iringa na Ruvuma jana.

Thursday, February 27, 2020

DC BAGAMOYO APIGA MARUFUKU NGOMA ZA VIGODORO

Image may contain: 1 person

NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa ambaye pi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) amepiga marufuku ngoma  na miziki ambayo inafanyika nyakati za usiku bila utaratibu  maarufu kama ‘Vigodoro’ kwani zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili kwa wananchi.


Agizo hilo amelitoa  wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nianjema, wadau wa maendeleo pamoja na wakuu mbali mbali wa idara wakati wa mkutano wake wa kikazi kwa ajili ya kusikiliza kero na changamoto mbali mbali za wananchi kwa lengo la kuweza kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuweka mipango  madhubuti kwa ajili ya kuleta chachu ya maendeleo.


Zainabu alisema kwamba  katika baadhi ya maeneo ya Wilaya yake kumekuwepo  wimbi la ngoma ambazo zinachezwa nyakati za usiku na kupelekea kero na usumbufu mkubwa kwa watu wengine hivyo ameamua kuchukua hatua ya  kupiga marufuku hali hiyo kwa lengo la kuondokana na mambo mbali mbali ambayo yamekuwa yakijitokeza hasa katika wakati wa usiku.


“Kuanzia leo katika mkutano huu napenda kusema napiga marufuku kabisa mambo ya vigodoro vya usiku kwani vimekuwa ni kero sana na vinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuvunja maadili ya Mtanzania na kwamba katika hili nitahakikisha ninalisimamia kwa ukaribu mno ili kukomesha kabisa kuwepo kwa hali hii katika Wilaya ya Bagamoyo,”alifafanua Zainabu.


Aidha Mkuu huyo alibainisha kwamba wananchi wa Bagamoyo kwa sasa wanatakiwa kubadilika na kuwa na mtazamo chanya kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbali mbali za miradi ya maendeleo kuliko kutumia muda wao mwingi katika kukesha nyakati za usiku wakicheza ngoma ambazo hazina faida yoyote katika Taifa la Tanzania.


“Mimi kikubwa ninachotaka kuwaambia hasa wananchi wa Wilaya ya Bgamoyo tuachane kabisa na kujikita zaidi katika kukesha kwenye vigodoro,  ni vyema zaidi mkatumia fursa mbali mali zilizopo mkajishughulisha katika shughuli za kujipatia kipato ili kuweza kuondokana na  wimbi la umasikini hivyo ni rai yangu wote tukashirikiana katika kuleta maendeleo na sio kukesha kwenye vigodoro ambavyo ni havina faida yoyote ile,”alisema Zainabu.


Pia Mkuu huyo wa Wilaya alifafanua kwamba mtu yoyote ambaye anahitaji kufanya shughuli yake ya usiku ni lazima apatiwe kibali maalumu kutoka katika Ofisi yake kwa kuzingatia sheria na utaratibu ambao utakuwa umewekwa,ili kuhakikisha mambo yote ambayo yanakuwa yanajitokeza nyakati za usiku ikiwemo masuala ya  uhalifu  na wizi yanakomeshwa kwa kiasi kikubwa.


Katika  hatua nyingine ametoa onyo kali kwa wale wote ambao watabainika kukiuka agizo lake ambalo amelitoa na kwamba atahakikisha anawachukulia hatua kali za kisheria wale wote ambao watabainika bado wanaendeleo kinyemela  kujihusisha na masuala ya kupiga ngoma za usiku na vigodoro bila ya kuwa na kibali maalumu.


Nao baaadhi ya wananchi ambao hawakuta kutaja majina yao walimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa hatua ambayo ameifanya ya kupiga marufuku kabisa mambo ya vigodoro hasa katika nyakati za usiku kwani yamekuwa ni tatizo kubwa kutokana na kuwepo kwa matukio mbali mbali ambayo yanasabisha momonyoko wa maadili hasa kwa vijana.


“Kwa kweli sisi kama wananchi wa Wilaya ya Bgamoyo hili agizo la Mkuu wetu kupiga marufuku ngoma za usiku maarufu vigodoro sisi tunamuunga mkono kwa asilimia mia moja kwani imekuwa ni kero sugu ya siku nyingi na wakati mwingine yani watu hatulali kabisa na kingine kuna baadhi ya matukio ambayo yanafanyika hivyo kwa hatua hii itaweza kusaidia kuondoa na kupunguza kabisa changamoto amabzo zimekuwa zikijitokeza katika maeneo ambayo tunaishi,”walisema.


Kwa upande wake mmoja wa wadau wa maendeleo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nianjema Abdul Pyalla, alisema kwamba suala hilo la vigodoro  ni kweli limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi hivyo atahakikisha anashirikiana bega kwa bega na Mkuu wa Wilaya  pamoja na wananchi husika katika mitaa mbali mabli kwa lengo la kuwaelimisha zaidi kuhusu umuhimu wa kutumia muda wao katika shughuli za maendeleo kuliko kukesha kwenye ngoma.


Baadhi ya Wananchi wa Wilayani Bagamoyo wakiwa wametulia kwa makini kumsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ambaye aliitisha Mkutano maalumu kwa ajili ya kuzungumzia mambo mbali mbali ya maendeleo kwa wakazi wa kata ya Njia njema pamoja na kuwasikiliza changamoto zao. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

Wednesday, February 26, 2020

MGALU ATAKA UMEME VIJIJINI UONGEZE UFAULU KWA WANAFUNZI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

NAIBU Waziri wa Nishati Subira Mgalu ametoa Rai kwa vijiji vyote ambavyo tayari vimeunganishwa na huduma ya Umeme, kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) kuitumia fursa hiyo kuboresha ufaulu pamoja na kuinua kiwango cha elimu katika Maeneo yao.

Mgalu aliyasema hayo alipofanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi kwa lengo la kukagua maendeleo ya Mradi huo wa Umeme vijijini (REA) pamoja na kuwasha umeme katika vijiji vya Naluleo, Makata na Mengele Wilayani humo.

Akizungumza na wananchi, Walimu pamoja na Wanafunzi baada ya kuwasha umeme katika Shule ya Msingi Naluleo, Mgalu alisema ni mategemeo ya Serikali kuwa baada ya umeme kufika katika maeneo yao utaboresha na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kutokana na mazingira wezeshi ya kusoma na kujifunzia muda wote.

Aidha, Mgalu pia aliwaasa wanafunzi wa kike hapa Nchini kuepuka vishawishi kwa vijana wakiume pamoja na kuwataka walimu pamoja na Wazazi kuwa walinzi namba moja wa wanafunzi hao wakike kuhakikisha hawakatishi masomo yao kwa kupata ujauzito.

“Niwaombe sana hii sio kazi ya mzazi au mwalimu peke yake, nikazi yetu sote tunapomuona mtoto wa kike anafanya vitendo hivyo tumkemee, sisi walimu tuwe chachu hasa walimu wa kiume inatia uchungu kuona mwanafunzi wa kike anapata ujauzito kisha mwalimu ndio anahusishwa iwe ni ya kweli au kwa kusingiziwa hiyo sio sawa” alisema Mgalu.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Liwale Sara chiwamba alisema kuwa Swala la kutokomeza mimba kwa wanafunzi ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika Mkoa huo wa Lindi hasa kupitia kampeni ya “tumsaidie akue asome mimba baadae” yenye lengo la kumfanya mtoto wa kike atimize ndoto zake.

Kwa upande wake Abdull Mohamdi mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Naluleo alisema kuwa upatikanaji wa umeme huo utakuwa mkombozi kwa walimu na wanafunzi hasa wakati wa kujiandaa na mitihani kuweza kujisomea nyakati za usiku.

“Baada ya umeme huu sasa wanafunzi tutakuwa na muda wa kutosha wa kuweza kujisomea kwa sababu hatutakuwa na shida tena ya kutafuta nishati ya umeme kama zamani “ alieleza.