Wednesday, February 26, 2020

DC BAGAMOYO KUFUATILIA FEDHA ZA TASAF KWA KAYA MASIKINI.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa (kati kati) akizungumza na wananchi wa kata ya Nianjema hawapo pichani katika mkutano wa hadhara ambao aliuandaa kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto za wananchi hao.
 ...............................................


NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO.

BAADHI ya wazee wanaoishi katika kaya masikini na mazingira magumu  Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani wameiomba serikali ya awamu ya tano kuingilia kati sakata la kero yao kubwa ya kuonewa kwa  kipindi kirefu kutokana na  kutopatiwa fedha ambazo zinatolewa na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa ajili ya kujikimu kimaisha pamoja na kuanzisha miradi midogo midogo.


Hayo yalibainisha wakati wa mkutano wa hadhara ambao umeandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Kawawa kwa wananachi wa Kata ya Nianjema kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto mbali mbali zinazowakabili ili kuzitafuatia ufumbuzi pamoja na kuweka mikakati ya kuleta maendeleo kwa wananchi kwa ushirikiano wa serikali na jamii kwa ujumla.


Aidha mmoja wa wazee hao akizungumza kwa  niaba ya wezake wanaoishi katika kaya masikini Ole Shamba alisema kwamba wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa katika suala zima la upatikanaji wa fedha kutoka TASAF hivyo wanajikuta maisha yao yanakuwa ni magumu kutokana na kukosa mahitaji muhimu wao na familia zao.


“Kwa kweli huu mpango kiukweli unatusumbua sana na leo hii kwa kuwa amekuja Mkuu wetu wa Wilaya Zainabu Kawawa tumeona ni bora tuseme kilio chetu ambacho kimekuwa ni kero kubwa ya siku nyingi maana hata sasa nimesahau kutokana na kipindi kimekuwa ni kirefu sana na ukizingatia taratibu zote tumeshazikamilisha sasa nashindwa kuelewa kwa hiyo tunaomba sana serikali yetu itusaidia katika suala hili,”aslisema Shamba.


Aidha katika hatua nyingine wazee hao walimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa kuwa na utaratibu wa  kufanya mikutano na wananchi wake kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili na kumuomba alichukue suala hilo kwa uzito mkubwa ili fedha zote ambazo zinatolewa ziweze kuwafikia walengwa na sio vinginevyo.


Kwa upande wake MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa baada ya kusikiliza kilio hicho ameahidi kulivalia njuga suala hilo na kuwaagiza watendaji wa TASAF kuhakikisha fedha zote zinazotolewa zinawafikia walengwa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa bila ya ubaguzi na upendeleo  na kuachana kabisa na vitendo vya  kufanya ubadhilifu kwa maslahi yao binafsi kwani atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.


Pia ,Mkuu huyo alibainisha kwamba lengo kubwa la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inawaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbali mbali na mifuko ambayo imeanzishwa hivyo atahakikisha kwamba wale walengwa wote ambao wanaishi katika mazingira magumu pamoja na kaya ambazo ni masikini wanawekwa katika utaratibu wa kusaidiwa fedha  kwa kuzingatai vigezo mbali mbali ambavyo vimetolewa na TASAF.


“Kwa kweli katika hili jambo mimi nitalisimamia kweli kweli kwa kushirikiana na viongozi wangu wengine pamoja na watendaji wa mamlaka husika lakini kikubwa fedha hizi ni lazima ziwafikie watu ambao ni walengwa na wanaoishi katika kaya masikini, na kitu kingine watendaji inabidi kuchunguza uhalisia wa kaya husika kama ni masikini au la na wananchi msiwe wadanganyifu ili wananchi wa maeneo husika waweze kupata haki zao, awe bibi au babu sio anakaa Mkuranga unamwandikisha Bagamoyo hii hapana,”alisema Zainabu.


Kwa  upande wake Mratibu wa ….TASAF Wilaya ya Bagamoyo Dionise Mahilane amesema kwamba kwa sasa wamejipanga kuondokana na changamato ya kuwepo kwa baadhi ya wananchi kuwa wadanganyifu katika utoaji wa taarifa zao ili kuhakikisha inawasaidia wale ambao ni walengwa na wanaishi katika kaya masikini kwa kuzingatia vigezo vilivyoweka sambamba na kutoa elimu jumuishi kwa jamii.
    

Naye Diwani wa Kata ya Nianjema Abdul Pyalla alisema kuwa kwa sasa kutokana na kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya kaya masikini kutokupata fedha hizo watafanya zoezi la kupita katika mitaa ili kutoa elimu ya watu ambao wanastahili kusaidiwa sambamba na kuhakiki orodha ya kaya  ambazo zinatakiwa kupatiwa msaada lengo ikiwa ni kuondokana na kero hiyo ambayo imekuwa ni usumbufu mkubwa.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Kulia Zainabu Kawawa akiwa anasikiliza moja na hoja ambazo zilikuwa zinatolewa na wananchi wa kata ya Nia njewa wakati wa mkutano huo amabao ulifanyika katika viwanja vya shule ya msingi nia njema.

 Mkuu wa kituo cha Polisi Bagamoyo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, (ASP) Michael Kakoshi licha ya kulinda hali ya usalama katika eneo hilo la mkutano wa hadhara akiwa anasikiliza changamoto mbali mbali ambazo zilikuwa zikitolewa na wananchi wa kata hiyo ya Nianjema.

Baadhi ya wazee wa Kata ya Nianjema Wilayani Bagamoyo wakiwa wanamsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo katika mkutano huo wa hadhara ambao ulihudhuriwa na wadau mbali mbali wa maendeleo pamoja na viongozi wa serikalia na wakuu wa Idara.

Diwani wa Kata ya Nianjema Abdul Pyalla akizungumza jambo na wananchi katika Mkutano wa hadhara ambao uliandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa lengo la kuwasikiliza wananchi kero zao ili kuweza kuzitafutia ufumbufu. (PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU)


Monday, February 24, 2020

WANACHAMA WA CHADEMA MTAMA WAJIUNGA CCM

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Ngome ya Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kata ya Majengo Halmashauri Mtama yateketezwa kwa kuzinduliwa shina la Wakereketwa wa chama cha Mapinduzi CCM Kambalage katika Kata hiyo.

Uzinduzi huo umefanyika februaari 22 na katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa Dkt, Bashiru Ally ulioambatana na kupokea kadi ya muasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Majengo Halmashauri ya Mtama Namkuva Lihengelebwede pamoja na ugawaji wa kadi za mabalozi wa chama hicho zaidi ya 1800.

Inaelezwa kuwa awali mwaka 2015 kata ya majengo na Mtama katika halmashauri hiyo ni miongoni mwa ngome kongwe za chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokuwa ikitumika na chama hicho kupanga mikakati mbali mbali wakati wa uchaguzi mkuu.

Akizungumza mara baada ya kuzindua Shina hilo Katibu mkuu wa chama cha Mapinduzi CCM Taifa Dkt, Bashiru amewataka wanachama wa chama hicho kutumia mashina ya wakereketwa kuwa vijiwe vya kazi ya kuwashawishi wapinzani kujiunga na chama cha Mapinduzi (CCM).

“hawa watu huwa hawaji peke yao wanakuja na watu nyuma yao, wanakuja na kadi zao na wanakuja na siri zao, wanakuja na mikakati yao pia, kwa hivyo tumieni vijiwe hivi kuwaita na leo nimefurahi kumpata muasisi wa Chadema hapa nakupongeza sana” alisema Dkt, Bashiru. “

Chama cha Mapinduzi CCM ni Chama cha Kitaifa na ni chama cha wananchi wote hivyo tunavyompata mwananchama mmoja mpya ndio tunaongeza nguvu katika chama chetu hivyo ni wajibu wetu kama wana CCM kuwapa heshima watu hawa wanaokuja kwetu” alieleza Dkt Bashiru.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mtama Nape Nnauye alisema kuwa kitendo cha Rais Magufuli kuchagua Eneo la Mtama kuwa Halmashauri kimekuwa mwarobaini wa kufuta upinzani katika kata za mtama na majengo katika Halmashauri hiyo.

Alisema tangu kata hiyo ya Mtama kuwa Makao Makuu ya Halmashauri pamoja na mambo mengine yanayofanywa ya utekelezwaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM wananchi wa maeneo hayo wameendelea kuwa na imani na Rais wao.

Kwa upande wake Namkuva Lihengelebwede Muasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Majengo na Mtama Halmashauri ya Mtama alisema kuwa miongoni mwa vitu vilivyomshawishi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM ni baada ya Rais Magufuli kuifanya Mtama kuwa Makao Makuu ya Halmashauri.

“Kitendo cha Mheshimiwa Rais kuifanya mtama kuwa Halmashauri mimi na wenzangu tukaona ni vyema tukajiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM ili kumuunga Mkono Rais wetu kwa ajili ya Maendeleo ya Mji wetu” alieleza Lihengelebwede.

MAGAZETI YA LEO TAREHE 24 FEB. 2020