Sunday, February 9, 2020

PINK HIJAB YAKUTANISHA WANAWAKE WA KIISLAMU KUJIKOMBOA KIUCHUMI

Mwanzilishi wa Pink Hijab Initiatives Trust in Tanzania, Khadija Omar akitoa hotuba katika Kongamano hilo lililowakutanisha Wanawake wa Kiislamu lengo ikiwa ni kuwapa elimu kuhusu biashara ili kuwapa nafasi kujikomboa kiuchumi.

 ...........................................

Taasisi ya Pink Hijab Initiatives Trust imefanya Kongamano maalum kuwakutanisha Wanawake wa Kiislamu kuwapa elimu kuhusu biashara ili kuwapa nafasi kujikomboa kiuchumi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mwanzilishi wa Taasisi hiyo, Khadija Omar amesema wamefanya Kongamano hili ili kutoa nafasi zaidi kwa Wanawake hao waweze kujiinua kibiashara na nakujiinua kiuchumi.

"Kongamano hili la leo unaona tumewaalika Wataalamu kina Prof. Mussa Assad, CAG Mstaafu, Mwanahiba Mzee kutoka Ecobank na Zuhura Muro yeye mtoa mada, Wafadhili kutoka KCB Bank wanaosema Boresha Bidhaa ya Mwanamke kwenye Biashara", amaesema Khadija.

Khadija amesema wamefanya Kongamano lakutoa elimu hiyo baada yakuona Wanawake hao wako nyuma kibiashara kipindi cha miaka mitano ya nyuma, amesema Serikali imekuja na sera ya uchumi wa Viwanda ameeleza wao kama Pink Hijab wamekuja na ukombozi wa Uchumi kwa Wanawake.

Kwa upande wake, Mtoa Mada katika Kongamano hilo, Mjasiriamali Zuhura Muro amezungumzia kikwazo cha uwepo wa mfumo dume kwa Wanawake hao, amewaasa kuchukua hali hiyo nakujitambua kama Wanawake ili kuendelea na kuhakikisha wanajikomboa kiuchumi katika jamii inayowazunguka.

"Kwa Wanawake wanachotakiwa kufanya ni Kujitambua, Kujiamini na kujitawala akiweza hayo Mwanamke huyo ameshinda sioni kama kuna kitu kitamzuia kujikomboa na kujiinua kiuchumi", amesema Mama Zuhura Muro

Naye, CAG Mstaafu, Prof. Mussa Assad amesema Wanawake wana uwezo mkubwa kufanya mambo makubwa mazuri kama wataziona nafasi zao katika jamii, Prof. Assad amesema Wanawake hao wanatakiwa kufanya mambo bila kukata tamaa sambamba na Wanaume kufanya hivyo.

"Kama mimi miezi mitatu iliyopita, nimejaribu kuingia huko kwenye Biashara na sina ujuzi mkubwa katika Biashara na kikubwa naamini unajiamini na hukati tamaa", amesema Prof. Assad.

CAG Mstaafu, Prof. Mussa Assad akitoa hoja katika Kongamano maalum lililoandaliwa na Pink Hijab Initiatives Trust Tanzania mahsusi kuwapa nafasi Wanawake na kujikomboa kiuchumi katika jamii inayowazunguka.

Sehemu ya Wanawake waliohudhuria Kongamano hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Mjasiriamali na Mtoa mada katika Kongamano hilo, Bi. Zuhura Muro akitoa somo kwa Wanawake hao wa Kiislamu kuhusu Kujitambua, Kujiamini na kujitawala.



Wednesday, February 5, 2020

WAWILI wakamatwa ubungo Kibo kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya





Na Isack Thadeo
  
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawashikiria watu wawili kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 508.163.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya James Kaji amesema watuhumiwa hao walikamatwa maeneo ya Kibo Ubungo January 27 mwaka huu wakiwa na gari aina ya Sienta rangi ya Silva yenye namba za usajili T 776 DSE. 

"Maafisa  wa mamlka walifanya upekuzi kwenye gari hilo na kukamata unga ambao baada ya uchunguzi kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa serikali, ilithibitisha kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin" alisema James

Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Sultan Ngowi mwenye umri (24) Mchaga mkazi wa Tabata segerea na Jimmy Mlaki miaka (24) Mchaga mkazi wa Kinondoni Dar es salaam ambapo walikamatwa na mzani pamoja na nyaraka mbalimbali wanatarajiwa kupelekwa mahakamani muda wowote.

 Aidha Mmlaka inawakumbusha Vijana kutojihusisha na biashara haramu Wala matumizi ya dawa za Kulevya atakayeshiriki atachukuliwa hatua stahiki za kisheria ikiwemo kifungo Cha maisha.

Tuesday, February 4, 2020

WANAFUNZI WATUMIKA KUUZA BIASHARA NDOGONDOGO KILWA BADALA YA KWENDA SHULE.

 
Kijana mmoja (jina linahifadhiwa)  (10) ambae ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi hotel tatu wilayani Kilwa akiwa amebeba beseni la majani ya kunde na kunde kwa ajili ya kupeleka sokoni tayari kwa kuuza.
 
Kijana mmoja (jina linahifadhiwa)  (10) ambae ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi hotel tatu wilayani Kilwa akihojiwa na mwandishi wa BAGAMOYO KWANZA BLOG kijijini hapo huku akiwa ameandaa beseni la majani ya kunde na kunde kwa ajili ya kupeleka sokoni tayari kwa kuuza, Picha zote Na Hadija Hassan.
 ........................................................

NA HADIJA HASSAN, LINDI

BAADHI ya watoto waliochini ya miaka 18 wanaoishi katika kata ya hotel tatu wilayani kilwa Mkoani Lindi hutumika kufanya biashara ndogo ndogo za ujasiriamali ili kuongeza pato la familia.

Hayo yamebainika baada ya BAGAMOYO KWANZA BLOG kufika kijijini hapo na kukuta baadhi ya watoto wenye umri wa kwenda shule wakijihusisha na biashara hizo ambapo wamedai kuwa wamelazimika kufanya hivyo ili kuweza kupata fedha ya kupata chakula BAGAMOYO KWANZA BLOG ilimshuhudia kijana mmoja (jina linahifadhiwa)  (10) ambae ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi hotel tatu wilayani Kilwa akiwa amebeba beseni la majani ya kunde na kunde kwa ajili ya kupeleka sokoni tayari kwa kuuza.

Mtoto huyo alisema kuwa hiyo ni kawaida kwa mama yake kumpatia biashara ndogo ndogo kwa wakati tofauti kwenda kutembeza mitaani ama kuuza sokoni kwa ajili ya kujipatia pesa ya kuendeshea maisha yao.

“hizi kunde kanipatia mama nikauze kwa kutembeza mtaani lakini siki nyingine mama huwa anapika keki au maandazi ambayo naendaga kuuza sokoni , pale tunakuwaga watoto wengine kila mtu akiwa na biashara yake ambao tunakujaga kuuza vitu mbali mbali” alieleza mtoto huyo.

Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto huyo alikiri kumtumia mtoto wake katika biashara ndogo ndogo huku akieleza kuwa analazimika kufanya hivyo kutokana na hali ngumu ya maisha

“huyu ana wiki sasa hajaenda shuleni anahali ya homa na yupo kwenye dozi, hata hizo kunde mlizomkuta nazo kwa leo sikumtuma kwenda kuuza ila kwa sababu njaa inawauma na hapa ndani hakuna chakula baada ya mimi kufika na hizi kunde kutoka shambani yeye akaona bora akaziuze ili tupate angalau pesa ya kununua anga”

Nae mtendaji wa kijiji cha hotel tatu Abdalah Shante amekiri kuwepo kwa baadhi ya watoto katika kata hiyo kutumikishwa na wazazi ama walezi wao katika kufanya biashara ndogo ndogo ambapo alisema kuwa hali hiyo inatokana na hali ngumu ya kipato walionao wazazi hao.

“Wakazi wa kata hii vipato vyao ni vidogo hivyo wanategemea biashara ndogondogo kama vile maandazi, vitumbua, kashata na vitu vingine vidogo vidogo kama hivyo, kwa hivyo baada ya muda wa masomo wazazi huwapatia watoto wao biashara hizo wenyewe wakiwa shambani ili watakaporudi kutoka huko waweze kununua unga ua mboga wanakula” alieleza Shante.

Licha ya kukiri kufahamu kuwa sheria hairuhusu kuwatumikisha watoto Shante alisema kwamba kutokana na hali halisi ya maisha wao kama serikali ya kijiji jitihada walizozichukuwa za haraka ni kuzungumza na wazazi wa watoto ambao wanajihusisha katika biashara kuwaeleza licha ya kuwatumia watoto hao kwenye biashara zao lakini wahakikishe watoto hao wanahudhuria shuleni bila kukosa

“kutokana na hali ya maisha ilivyo tumeona hata tukiwakataza wasiwatumie kabisa watoto hao kama vile tutawaonea tu bure kwa maana biashara hizo ndizo zinazowapatia chakula baada muda wa shamba ila tulichowaambia wahakikishe hao watoto wao wanafanya hizo biashara baada ya muda wa shule kupita ili watoto hao wasikose masomo kutokana na biashara hizo” aliongeza.

HALMASHAURI YA CHALINZE YATOA PIKIPIKI KUMI KWA MAOFISA UGANI

NA MWAMVUA MWINYI, CHALINZE

HALMASHAURI Ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani inakabiliwa na changamoto katika shughuli za ugani ikiwemo usafiri wa uhakika kuwafikia wakulima ambao wapo vijijini na vitongoji.


Aidha kuna vijiji 31 ambavyo havina maofisa, hivyo kutokana na changamoto hizo wakulima wamekuwa hawapati huduma yenye tija kwa kushindwa kufikiwa na maafisa ugani mara kwa mara.


Changamoto hizo zimewekwa bayana na mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze, Bi Amina Kiwanuka katika makabidhiano ya pikipiki kumi zenye thamani ya mil.25 kwa maofisa ugani wa vijijini na magari ya halmashauri mapya mawili yenye thamani ya zaidi ya milioni 290.

Alieleza, kutokana na changamoto hiyo kupitia idara ya kilimo halmashauri ya Chalinze imejiwekea malengo hadi kufikia 2021/2022 iweze kununua pikipiki 50 kutoka kwenye bajeti za mapato ya ndani kwa ajili ya maofisa ugani wa vijiji na kata.


“Pikipiki hizi zitawasaidia maofisa ugani hawa kuwatembelea wakulima kwa wakati na kuwapa huduma ambazo zitawawezesha kuongeza tija katika sekta ya kilimo”alifafanua Amina.


Hata hivyo Amina alielezea, maofisa hao wataweza kutumia pikipiki hizo kwenda kuhudumia katika vijiji ambavyo havina maofisa ugani.


Nae mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze ,Saidi Zikatimu alieleza, halmashauri hiyo ilianza kutenga bajeti ya pikipiki mwaka wa fedha 2018/2019 na kununua pikipiki 15 zenye thamani ya milioni 37.5 na kupewa maofisa ugani wa kata.


“2019/2020 zimenunuliwa pikipiki hizi kumi za milioni .25 na kupewa maofisa ugani wa vijiji vya pembezoni pia tumetenga milioni 32.4 kwa ajili ya pikipiki 12 kwa mwaka 2020/2021″


Zikatimu alisema ,kutokana na umuhimu wa usafiri  ili kurahisisha utendaji kazi magari yaliyonunuliwa nayo yanakwenda kusaidia kusukuma kazi za idara mbalimbali ambazo zinahitaji matokeo kupitia usafiri.


Kwa upande wake ofisa ugani wa kijiji cha Kimange, Aloyse Jumanne aliishukuru halmashauri kwa kuiona changamoto ya ukosefu wa usafiri na kuifanyia kazi.


Alibainisha kuwa, usafiri huo unakwenda kujibu kero za wakulima ambao walikuwa hawafikiwi kwa wakati na kujikuta wakishindwa kunufaika na kilimo cha kisasa.