Sunday, October 13, 2019

BAGAMOYO YAFIKIA ASILIMIA 55.12 UANDIKISHAJI WAPIGA KURA.

 
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard Kapinga (kulia) akielezea hali ya uandikishaji wapiga kura unavyoendelea wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipotembelea Kata za Halmashauri hiyo kuangalia zoezi hilo linavyoendelea, wa pili kulia ni
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi Fatuma latu.
........................................

Jumla ya wananchi 37,994 wamejiandikisha kwenye daftari la wapiga kura katika Halmashauri ya Bagamoyo mpaka kufikia tarehe 12 Oktoba 2019.


Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard Kapinga, alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) ya Wialaya ya Bagamoyo wakati wa ukaguzi wa vituo vya kujiandikisha wapiga kura uliofanyika Halmashauri ya Bagamoyo.


Kapinga alisema jumla ya wananchi waliotarajiwa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kwenye Halmashauri ya Bagamoyo ni 68,929 ambapo idadi hiyo ya waliojiandikisha kwa kipindi cha siku tano ni sawa na asilimia 55.12.


Alisema kutokana na hali hiyo, Halmashauri hiyo mpaka siku ya mwisho inaweza kufikia lengo la asilimia 100 katika kuandikisha wapiga kura.


Kamati ya Ulinizi na Usalama (KUU) ya Wilaya ya Bagamoyo imeongozwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Bi Kasilda Mgeni katika kukagua vituo vya uandikishaji wapiga kura katika kata mbalimbali za Halmashauri hiyo.


Akizungumza na wananchi katika vituo vilivyotembelewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la wapiga kura ili kila mwananchi apate haki yake ya kupiga kura siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mita, Vitongoji na Vijiji ambayo inatarajiwa kuwa ni Novemba 24, 2019.


Alisema kuchagua viongozi ni haki kila mwananchi aliyefikisha umri wa kupiga kura hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuitumia haki hiyo ili kuchagua viongozi watakaofaa kuongoza na kuleta maendeleo.


Alisema katika kipindi hiki wapo baadhi ya watu ambao wanapita kuwadanganya wananchi kuwa hakuna umuhimu wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ambapo amewataka wananchi hao kuacha kudanganywa na kwamba kila mwananchi atumie nafasi hiyo vizuri kwa maslahi yake, familia yake, eneo lake analoiishi na Taifa kwa ujumla.


Katibu Tawala huyo wa wilaya alisema Serikali ya wilaya ya Bagamoyo haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakaebainika kuhujumu uchaguzi huo kwa maslahi yake binafsi.


Alisema maendeleo katika ngazi mbalimbali yanaletwa kwa kusimamiwa vizuri na viongozi, hivyo ili kupata viongozi hao ni lazima wananchi wafuate taratibu za kupiga kura ikiwemo kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.


Aliongeza kwa kusema kuwa, katika kipindi hiki wananchi wasikubali kudanganywa na kuchagua watu ambao hawana uchungu wa maendeleo na badala yake wachague viongozi waadilifu, wenye maono ya maendeleo, na watakaofanya kazi kwa kujituma ili kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.


Aidha, alimalizia kwa kufafanua kuwa, ili mtu apate haki ya kupiga kura siku ya uchaguzi, njia pekee ni kujiandikisha kwenye daftari na si vinginevyo.


Alisema kitambulisho cha mpiga kura, kitambulisho cha uraia havitamuwezesha kupiga kura hivyo waisiache kujiandikisha kwa kudhani wanaweza kupiga kura kwa kutumia kitambulisho cha uraia au cha mpiga kura.


Kwa upande wake Kamanda wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Bagamoyo, Raymond  Katima, amewataka wananchi wilayani hapa kujiepusha na vitendo vya rushwa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na Vijiji.


Katima alisema kila mwananchi anayo haki ya kumchagua kiongozi amtakae na kwamba asikubali kupewa kitu cha aina yoyote kutoka kwa mgombea ili amchague kwani kufanya hivyo atakuwa amepokea rushwa na kuuza uhuru wake wa kumchagua kiongozi.


Alisema katika kipindi hiki wapo baadhi ya wagombea wanatamuia mbinu mbalimbali ili kupata madaraka ikiwemo kutoa rushwa, na kuonya kuwa, atakaebainika kutoa au kupokea rushwa ya aina yoyoyte hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


Alisema wananchi wasikubali urafiki wa muda mfupi wenye lengo la kubadilisha mawazo yao katika kuchagua viongozi.


Halmashauri ya Bagamoyo ina jumla ya kata 11 ambazo ni Yombo, Fukayosi, Zinga, Kerege, Mapinga, Kiromo, Dunda, Magomeni, Nianjema, Kisutu na Makurunge.
  Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni (kulia) akichukua taarifa za uandikishaji wapiga kura kwenye kituo cha uandikishaji wapiga kura Mwavi kata ya Fukayosi Halamshauri ya Bagamoyo, katikati ni
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard Kapinga.
 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni akichukua taarifa za uandikishaji wapiga kura kwenye kituo cha uandikishaji wapiga kura, Kitongoji cha Kibaoni kata ya Makurunge katika Halmashauri ya Bagamoyo.
 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni akionyesha kitambulisho cha mpiga kura na kuwafahamisha wananchi kwamba kuwa nacho hicho hakumfanyi mtu kupiga kura bila ya kujiandikisha kwenye Daftari la wapiga kura, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bi Fatuma Latu.
 
Wananchi wakimsikiliza Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, katika kituo cha Mwavi kata ya Fukayosi Halmashauri ya Bagamoyo.

 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, katika kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Halmashauri ya Bagamoyo wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) ilipotembelea vituo vya kujiandikisha wapiga kura.
Wananchi wakimsikiliza Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, katika Kitongoji cha kifude kata ya Makurunge, halmashauri ya Bagamoyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bi Fatuma Latu, (kushoto) akisalimia wananchi wa Kitongoji cha Geza ulole kata ya Makurunge pamoja na kumkaribisha Katibu Tawala (DAS) wilaya ya Bagamoyo ili azungumze nao. waliokaa wa pili kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, anaefuata ni Afisa, Tarafa Tarafa ya Mwambao Dorisi Mwakatobe na wa kwanza kulia ni Afisa Tarafa, Tarafa ya Yombo, Gladness Shafii.
Wananchi wakimsikiliza Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, katika Kitongoji cha Geza ulole, kata ya Makurunge, halmashauri ya Bagamoyo. 
Kamanda wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Bagamoyo, Raymond  Katima, ambae ni Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, (KUU) akizungumza na wananchi kuhusu madhara ya rushwa wakati wa kukagua vituo vya kuandikisha wapiga kura.   
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bi Fatuma Latu, wakimsikiliza Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Bagamoyo alipokuwa akitoa elimu ya rushwa kwa wananchi.

ZAIDI YA WANANCHI LAKI TANO KAGERA WAMEJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA KUPIGA KURA.

Na Alodia Dominick, Bukoba.

Wananchi wapatao 577, 330 Mkoani Kagera wameishajiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa huku halmashauri ya wilaya ya Bukoba ikiongoza kwa uandikishaji huo kwa asilimia 82.4 ikilinganishwa na wilaya nyingine za mkoa huo.

Takwimu hizo zimetolewa jana Oktoba 12, 2019. na mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti baada ya kufanya ukaguzi kwa baadhi ya vituo katika kata ya Kemondo na Maruku halmashauri ya wilaya ya Bukoba.

Brigedia Gaguti amesema, halmashauri ya wilaya ya Bukoba inaongoza kwa mkoa wa Kagera katika uandikishaji kwa ajili ya kupiga kura za serikali za mitaa kwa asilimia 82.4 ikilinganishwa na wilaya nyingine ambazo ziko chini ya asilimia 60 na kuwa wananchi waliokadiliwa kujiandikisha katika mkoa wa Kagera ni 1.2 milioni na ambao wameisha jiandikisha ni 577, 330.

Aidha amesema, watendaji wa kata na vijiji waendelee kutoa hamasa kwa wananchi ili siku  zilizobaki wananchi waweze kujitokeza kujiandikisha katika vitongoji na mitaa yao wapate haki ya kuwachagua viongozi wao.

Ameongeza kila mwananchi ahakikishe rafiki, jirani yake ndugu na jamaa wamejiandikisha katika maeneo yao na kuwa kwa kufanya hivyo watawapigia kura viongozi ambao ni waadilifu kutokana na siku za nyuma kuchaguliwa viongozi wasio na maadili ambao walishiriki kuuza ardhi za vijiji na hivyo kuwaletea hasara wananchi.

kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi mkoa wa Kagera, Mapinduzi Severian amesema kwamba, uandikishaji kwa ajili ya kupiga kura za serikali umeanza octoba 08 mwaka huu na utamalizika octoba 14 mwaka huu.

Naye Mtendaji wa kata ya Kemondo Syliacus Sostenes amesema kwamba, zoezi la uandikishaji katika kata yake halikwenda vizuri kutokana na zoezi hilo kuchanganywa na zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho vya mpiga kura.

Friday, October 11, 2019

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AKABIDHI HUNDI YA MILIONI 127 KWA VIKUNDI LIWALE

Na Hadija Hassan, Lindi.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally amekabidhi hundi ya shilingi milioni 127,044,255 kwa vikundi 29 vya Wanawake, vijana na Watu wenye ulemavu Wilayani Liwale Mkoani Lindi.


Mkongea amekabidhi hundi hiyo katika kijiji cha Lindota Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mara baada ya kutembelea na kukagua shughuli mbali mbali zinazofanywa na makundi hayo ikiwemo vikundi vya ubanguaji wa Korosho, uchomeleaji vyuma, ukamuaji mafuta ya alizeti, ushonaji , Ufundi seremala pamoja na madereva Bodaboda .


Akizungumza na Wananchi pamoja na wajasiriamali hao Mkongea aliishauri Halmashauri hiyo kuangalia namna bora ya kuwasaidia wajasiriamali kuwakopesha mashine za kisasa ikiwa ni pamoja na zile za kubangulia korosho ili kufikia azma ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati na viwanda.


Hata hivyo Mkongea alisema kuwa ili vikundi hivyo viweze kuwa endelevu ni vyema kwa wajasiriamali hao wakaweka nguvu ya kuunganisha vikundi vyao ili Serikali iweze kuwakopesha vitendea kazi vitakavyoweza kuwarahisishia kazi zao.


Awali akitoa taarifa kwa kiongozi huyo wa Mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Afisa Maendeleo ya jamii Wilaya ya Liwale Mosesi Mkovele alisema fedha hizo za mikopo zimetokana na asilimia 10% ya makusanyo yao ya ndani ambayo ni ya awamu ya pili ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha wa 2018/19 na awamu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2019/20.


Aidha Mkovele alibainisha kwamba shilingi milioni 58,488,219 zinazotolewa Zinakamilisha malipo kwa vikundi kutoka katika asilimia 10% ya mwaka wa fedha wa 2018/19 ambapo kwa awamu ya kwanza zilikuwa zimetolewa shilingi milioni 67,000,000 kati ya shilingi milioni 125,488,219 zilizopaswa kutolewa kama asilimia 10%.


Aliongeza kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2019/20 Halmashauri hiyo imetenga kiasi cha shilingi milioni 202,180,860 ambapo kwa awamu ya kwanza jumla ya shilingi milioni 68,556,036 zinatolewa kwa vikundi husika. 

Kwa upande wake katibu wa mtandao wa vikundi vya wajasiriamali Wilaya ya Liwale, Mariamu Zuberi alisema kuwa Mikopo hiyo inayotolewa na Halmashauri itasaidia kwa kiwango kikubwa kukuza kipato , kuongeza fursa za ajira, pamoja na kukuza mitaji kwa vikundi vinavyonufaika.

MBUNGE JUMAA KUJENGA UWANJA WA MPIRA MLANDIZI.

Na Omary Mngindo, Mlandizi

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijiji Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, amesema kuwa atajenga uwanja wa Mpira wa Miguu wa kisasa mjini Mlandizi.

Jumaa ametoa kauli hiyo akiwa anazungumza na wakazi wa Kata ya Mtongani mjini hapa ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake jimboni hapa, ambapo alisema hatua hiyo inalenga kuendelea kuupandisha hadhi mji wa Mlandizi.

Kauli ya Jumaa imefuatia swali la mmoja wa wakazi kuhoji mipango ya Halmashauri ya kutenga maeneo kwa ajili ya kuzikia, ambapo ofisa Ardhi Msaidizi Franck Mwalembe alimweleza Jumaa kuwa halmashauri tayari imeshatenga viwanja katika eneo la Kiwalani.

"Halmashauri imetenga eneo ya kuzikia, viwanja vya michezo na huduma mbalimbali za kijamii, niwatoe wasiwasi wananchi kuhusiana na maeneo muhimu, halmashauri yenu imejiandaa vizuri katika masuala ya kijamii," alisema Mwalembe.

Akizungumza na wananchi hao katika eneo la stendi ya Mtongani, Jumaa alisema kuwa pamoja naa kuwepo kwa uwanja wa Mpira wa Miguu wa JKT Ruvu uliopo maeneo ya Mlandizi Bondeni, nae atajenga mwingine ikiwa ni alama ya uongozi wake.


"Nimeamua kuweka alama kwa wananchi wangu wa Mlandizi, pamoja na kuwepo kwa uwanja wa JKT Ruvu nawahakikishia nitajenga uwanja wa Mpira wa Miguu, ili iwe kumbukumbu yangu kwa wana Mlandizi mlionichagua kuwaongoza kwa vipindi viwili vya ubunge wangu," alisema Jumaa.

Sanjali na hilo mbunge huyo amewataka wananchi jimboni humo kutokubali kuuza hovyo ardhi, kwani kwa sasa mji huo unakuwa kwa kasi kubwa, huku wawekezaji wakijitokeza kwa wingi kutaka ardhi kwa ajili ya kujenga viwanda vikubwa na vidogo.

MKONGEA AZINDUA UJENZI WA RADIO NACHINGWEA, AWAASA WANAHABARI.

 
Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally,(katikati) akizungumza na wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa kituo cha Radio cha Mashujaa fm. wilayani Nachingwea jana Oktoba 10, 2019, kulia ni Mkuu wa wilaya ya hiyo, Rukia Muango, na kushoto ni Meneja wa Mashujaa fm, Zakia Gaspa.
 
Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally, akifungua kitambaa kwenye jiwe la msingi ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi ujenzi wa kituo cha Radio cha Mashujaa fm. wilayani Nachingwea jana Oktoba 10, 2019, anaeonekana kwa mbele akiwa na furaha ni Meneja wa Mashujaa fm, Zakia Gaspa.
PICHA ZOTE NA HADIJA HASSAN. 
..........................................

Na Hadija Hassan, Lindi.


Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally, amewataka wanahabari Nchini kuandika habari kwa Kuzingatia weledi pamoja na maadali ya habari.


Mkongea ametoa wito huo jana Oktoba 10, 2019 wakati wa kuzindua mradi wa ujenzi wa kituo cha Radio ya Mashujaa Fm, wilayani Nachingwea Mkoani Lindi uliofanywa na mbio hizo za mwenge.


Alisema vyombo vya Habari na wanahabari kwa jumla wamekuwa na nafasi kubwa katika jamii kwa masuala ya kuelimisha, kuburudisha na hata kuhabarisha hivyo ni vyema kwa wanahabari kuhakikisha habari wanazozitoa ziwa ni zenye uhakika na zisizokuwa na uchochezi.


"Hii ni kwa sababu ulimi wa mwanahabari ukikosea kidogo urekebishaji wake unakuwa na kazi kubwa, hivyo hakikisheni mnafanya kazi kwa uangalifu ili kile ambacho kinafanyika ndicho kinachomfikia mwananchi au mwanajamii" alisisitiza Mkongea.


Awali Meneja wa mashujaa FM, Zakia Gaspa akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa kituo hicho cha Radio alisema kuwa kituo hicho hadi kukamilika kwake kimeghalimu kiasi cha shilingi milioni 15 Gaspa alisema katika kuhakikisha inasaidiana na Serikali katika mambo mbalimbali ya maendeleo radio yao imekuwa Ikijikita katika shughuli mbali mbali za kijamii ili kuhakikisha wananchi wanashiriki katika shughuli za kimaendeleo.