Sunday, August 25, 2019

NAIBU WAZIRI NISHATI ASEMA WATAKALIPISHWA NGUZO ZA UMEME WAMBIP ATAWAPIGIA.

Image may contain: 3 people, including Subira Mgalu, people on stage and indoor
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza katika Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) lililofanyika Agosti 24, 2019 mkoani Kilimanjaro kumpongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya.
...................................

Na Veronica Simba – Kilimanjaro.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa namba yake ya simu ya mkononi kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na kuwaelekeza ‘wambipu’ ili awapigie na kutatua kero husika, endapo wataambiwa kulipia nguzo, nyaya au mita wakati wakipeleka maombi ya kuunganishiwa umeme maeneo ya vijijini.


Ametoa onyo kali kwa mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ngazi ya Wilaya na Mkoa ambao watakaidi agizo la serikali linaloelekeza kuwa wananchi wote wa vijijini waunganishiwe umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 tu pasipo kulipia kifaa chochote ikiwemo nguzo, nyaya au mita.


Alikuwa akizungumzia yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya nishati, kwenye Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 24, 2019, ambalo lililenga kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya.


“Rais Magufuli alisema tupunguze gharama za kuunganishia wananchi umeme vijijini kutoka shilingi 177,000 hadi 27,000 tu na atakayekwenda TANESCO akashindwa kuunganishwa kwa bei hiyo au akaambiwa lipia nguzo, lipia waya, lipia mita; Namba yangu ni 0652558010. Nibipu, nitakupigia,” alisema huku akishangiliwa na umati wa wananchi.


Akitoa takwimu za waliounganishiwa umeme vijijini, mkoani Kilimanjaro kwa gharama hiyo ya shilingi 27,000 tangu agizo hilo lilipoanza kutekelezwa mwezi Mei mwaka huu, amesema mpaka sasa idadi imefikia 5,000 huku waliounganishwa kwa mwezi Julai pekee ni zaidi ya watu 2,000.


Amesema Mkoa wa Kilimanjaro unaongoza Tanzania kwa kuwa na umeme katika maeneo mengi ambayo ni asilimia 87.


“Mkoa una Kata 148 ambazo zote zina umeme. Una vijiji 519 ambavyo kati yake, 453 vina umeme. Bado vijiji 66 tu ambavyo vipo wilaya ya Hai (5), Siha (7), Rombo (8), Mwanga (4), Moshi (22) na Same (20).


Amesema, kati ya vijiji 66 vya Mkoa wa Kilimanjaro ambavyo bado havijaunganishiwa umeme, vitabaki 35 kufikia Desemba mwaka huu na kati ya hivyo, serikali imeiagiza TANESCO kuchukua vijiji 18 ili iviunganishe hivyo Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III – 2), utaunganisha vijiji 17 tu vitakavyokuwa vimesalia.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, pamoja na mambo mengine, amempongeza Rais Magufuli kwa kuwapa nafasi za uongozi wanawake ambao wameonesha kuwa wanaweza, akitolea mfano wa Makamu wa Rais, Mama Samia Hassan na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu.
Image may contain: 6 people, including Subira Mgalu, people sitting
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati), akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Chama Tawala na Serikali, wakishiriki katika Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) lililofanyika Agosti 24, 2019 mkoani Kilimanjaro kumpongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya.
Image may contain: 7 people, people sitting and outdoor

Sehemu ya umati wa wananchi wakiwa katika Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) lililofanyika Agosti 24, 2019 mkoani Kilimanjaro kumpongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya.

Tuesday, August 20, 2019

BILIONI 1.3 ZAHITAJIKA KIBAHA KUJENGA MADARASA 65.

Na Omary Mngindo, Kibaha.
KIASI cha shilingi bill. 1.3 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 65 vya madarasa katika shule ya sekondari wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya Assumpter Mshama alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa, ambapo alisema mpango huo unalenga kuunga mkono juhudi za serikali ya kuboresha elimu, chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

Alieleza kuwa kampeni hiyo iliyopewa jina la Elimisha Kibaha, ilianzishwa Aprili 25 mwaka huu na tayari imeshawafikia wadau mbalimbali wakiwemo wananchi mmoja mmoja ambao wamejitolea pesa taslimu kuanzia shilingi elfu moja na kuendelea.

"Nimewaita hapa kwa lengo la kuwaambia wa-Tanzania kuwa kampeni yetu ya Elimisha Kibaha inaendelea, tunahitaji kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 65 kwenye shule zetu za sekondari," alisema Mshama.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imetokana na upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari, za Kibaha Mji na halmashauri ya wilaya kufuatia ongezeko la wanafunzi kutokana na agizo la elimu bure lililotolewa na Rais Magufuli.

"Kufuatia ongezeko la wanafunzi kwa mwaka wa 2017, jumla ya wanafunzi 3,560 walifaulu, mwaka 2018 wanafunzi 3,938 na mwaka 2019 wanafunzi 4,930 ongezeko hili limechangiwa pa na wakiwemo waliohamia kutoka maeneo mbalimbali" alisema Mshama.

Alisema kuwa vinahitajika vyumba vya madarasa 65, viti 3,250 na meza 3,250 na kuwa chumba kimoja cha darasa, viti na meza kinagharimu shilingi milioni 16.5 na kwamba vyumba, meza pamoja na viti vinagharimu shilingi bilioni 1.3.

"Uzinduzi wa kampeni yetu utafanyika Agost 30, mgeni rasmi tunataraji atakuwa Humphrey Polepole Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kauli mbiu yetu Kibaha 1, Mtu 1, Tofali 1, Elfu 1 kwa Roho 1," alisema Mshama.

Alimalizia kwa kutaja namba za simu na akaunti ambapo 0657,790 327, 0763961173 akaunti ya NMB 21210032409.

DKT. KALEMANI ATOA UFAFANUZI KWA KAMATI YA BUNGE KUHUSU UUNGANISHWAJI UMEME KWA WATEJA WA VIJIJINI.

Image may contain: 1 person, on stage and indoor
Na Veronica Simba – Dodoma.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa idadi ya wanaounganishiwa umeme vijijini kupitia miradi mbalimbali inayoendelea ni ya awali na itakuwa ikiongezeka kadri wananchi husika watakavyokuwa wakilipia gharama yake ambayo ni shilingi 27,000 tu.


Alieleza hayo leo, Agosti 20, 2019 jijini Dodoma, wakati akijibu hoja iliyoibuliwa na wajumbe kadhaa wa Kamati hiyo walioonesha wasiwasi wao kuwa idadi ya wananchi wanaounganishiwa umeme vijijini ni ndogo.


“Kinachofanyika hivi sasa ni kupeleka miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali vijijini na kuunganisha wateja wa awali, Wengine wataendelea kuunganishwa kwa wakati wao kadri wanavyolipia,” alifafanua Waziri.


Aidha, kuhusu agizo la serikali kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kutumia vifaa vya ndani ya nchi, Waziri ameieleza Kamati husika kuwa msimamo huo unatokana na matumizi ya vifaa vya ndani kuwa na tija zaidi kuliko vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi.


Akifafanua, alieleza kuwa kuagiza vifaa nje ya nchi ni gharama kubwa ukilinganisha na kutumia vifaa vya ndani.


Pia, alisema, ni rahisi zaidi kwa serikali kusimamia na kudhibiti ubora wa vifaa vya ndani kuliko vinavyotengenezwa nje ya nchi.


Aidha, aliongeza kuwa muda unaotumika kupata vifaa vinavyotengenezwa ndani ya nchi tangu siku vinapoagizwa ni mdogo kulinganisha na ule unaotumika kuagiza na kuletewa vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.


Waziri pia alizungumzia katazo lililotolewa na serikali kuhusu wananchi vijijini kulipia nguzo ambapo alisema uamuzi huo ulifikiwa ili kuwapunguzia gharama wananchi hao ambao wengi kipato chao ni kidogo.


“Kwa uhalisia, umeme vijijini unatolewa bure kwa wananchi na gharama zake kuchukuliwa na serikali.


Hata hiyo 27,000 wanayolipa ni gharama za ushuru wa thamani tu ambayo ni asilimia 18 ya gharama husika.


Sasa ukimlipisha mwananchi huyo nguzo itarudisha tatizo palepale, hivyo nasisitiza tena kwamba wananchi wa vijijini hawatakiwi kulipia nguzo.”


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, ameieleza Kamati hiyo kuwa, tangu kuanzishwa kwake, REA imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Miradi ya Awali, Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Kwanza (REA I), Awamu ya Pili (REA II) na Awamu ya Tatu (REA III).


Alisema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo mwaka 2021, kutawezesha vijiji vyote 12,268 vya Tanzania Bara kufikiwa na miundombinu ya umeme.


Katika kikao hicho, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilikuwa ikipokea taarifa ya maendeleo na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya REA pamoja na changamoto inazokabiliana nazo.


Wengine walioshiriki kikao hicho ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Haji Janabi pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.