Monday, August 12, 2019

NDOA ZA KIISLAMU, KIKRISTO, BOMANI SASA KUSAJILIWA OFISI YA MKOA


Mkuu wa mkoa wa Daresalaam, Paul Makonda amesema yuko kwenye mpango wa kutaka kusajili ndoa zote zinazofungwa katika mkoa wa Daresalaam, dhamira ikiwa ni kuwasaidia wanawake ambao wanalaghaiwa na wanaume wapate nusra.

Makonda ametangaza nia hiyo mapema hii leo wakati akizungumza na waandishi wa habari.


Amesema watasajili ndoa zote kuanzia zile za Kiislamu ambazo dini yake inaruhusu kuoa wanawake wanne, lakini pia ndoa ya kikristo ambayo inaruhusu mwanamke mmoja na ile ya bomani.

Amesema baada ya ya kukamilika kwa ugeni wa SADC, wataanza mchakato wa majadiliano ili kuangalia njia nzuri ya kuondoa udanganyifu wa wanaume.

"Hili sio suala la Makonda peke yake, tutajadiliana na wadau ili kuona namna tutakavyoliweka, lakini natamani kuleta furaha miongoni mwa wanawake, huwezi ongoza watu ambao hawana furaha, lazima tuangalie namna ya kuwasaidia," alisema Makonda

Amesema Serikali ya Mkoa imejipanga kukutana na wadada wote wa mkoa huo, walioumizwa baada ya kuahidiwa kuolewa na kisha mwanaume kuingia mitini na kuangalia ni njia gani nzuri zaidi ya kuwaokoa na janga hilo.

Makonda  amedai ya kwamba amekuwa akikutana na malalamiko mengi sana kutoka kwa wadada wa mkoa huo kwamba wamechoka kutapeliwa.

''Tunaompango mzuri tu wa kukutana na wadada walioumizwa,  huwezi kuwa kiongozi afu unaongoza watu walioumizwa na kutapeliwa na vijana ambao wanaona raha tu, tunataka tufikie hatua mtu akioa anaandika kwenye database ya mkoa,  ili mwanamke akitaka kuolewa anaangalia huyu jamaa kaoa au hajaoa'' amesema Makonda.

Makonda ameongeza kuwa,  wanaoumizwa wengi ni kina dada kwa sababu wanawake wakipenda huwa wanapenda kweli na wao kuwa wahanga wakubwa wa matapeli.

Amesema mkutano wa SADC wanataka kuutumia kujifunza mambo mbalimbali,  ikiwemo suala la wadada kutapeliwa juu ya masuala ya ndoa, kwa kuangalia nchi zingine zinashughulika vipi na masuala hayo

Viwanda vya sayona, Elven agri wajipanga kutumia fursa za soko la SADC



Na Selemani Magali, Daresalaam.

Kiwanda cha Sayona pamoja na kiwanda cha Elven Agri cha mapinga Bagamoyo wazalishaji wa chakula asilia cha matunda vimeelezea mikakati yao ya kulitumia soko la umoja wa Nchi za SADC.

Akizungumza na ujumbe wa SADC uliotembelea viwanda hivyo hivi karibuni, meneja mauzo na masoko wa Kampuni ya Elven Agri, Bw Brij Bhayare amesema sasa wataanza kuangalia soko la nchi hizo ili kukuza biashara yao.

Amesema toka kuzinduliwa kwa Kampuni hiyo na Rais wa awamu ya Tano, Mh John Pombe Magaufuli mwaka 2017, kampuni hiyo imekuwa ikiuza bidhaa zake nje ya Mipaka ya Tanzania pamoja na soko la ndani ya Nchi.

“Tumekuwa tunauza bidhaa zetu katika masoko ya Marekani, Ulaya na Japani, lakini pia tunauza sana katika supermarkets za hapa Tanzania, tutaangalia pia soko hilo la SADC,” Alisema Brij

Kampuni hiyo kwa sasa inazalisha bidhaa za kusindikwa za matunda ya maembe, mananasi, na Ndizi mbivu na kwa siku wanapokea tani laki tatu za matunda.

Amesema wametoa ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi kwa wakazi wa Mapinga Bagamoyo Tanzania lakini pia kupokea matunda mengi kutoka kwa wakulima.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa Kampuni ya mitisum group watengenezaji wa vifaa vya ujenzi na vinywaji aina ya sayona amesema mkutano wa 39 wa wakuu wa Nchi za Jumuiya ya maendeleo kusini mwa africa (SADC) utatoa fursa ya kuongeza masoko katika nchi hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ,Lugoba Chalinze Mkoani wa Pwani mara baada ya ziara fupi iliyofanywa  na baadhi ya wajumve wa SADC katika kiwanda hicho, Mlawa alisema kauli ya aerikali ya awamu ya tano ya kujenga viwanda nchini itakamilika kutokana na mkutano huo utakaofanyika nchini.

Mlawa alisema ili kusambaza bidhaa zao katika nchi za SADC ,hivi sasa wanejipanga kujenga soko lingine mkoani Mbeya ili iwe rahisi kwa usambazaji.

Alisema hivi sasa wanasambaza bidhaa zao katika nchi ya Msumbiiji na Malawi na wanampango wa kupeleka nchini Ghana.

""Ndio maana tunasema kuwa mkutano huu utakuwa na fursa kubwa kwa sisi wenyeviwanda kuweza kusambaza bidhaa zetu kwa urahisi katika nchi za SADC"alisema Mlawa.

Naye Mkurugenzi Mratibu wa Kiwanda hicho,Laurance Manyama alisema ,asilimia 95 ya wafanyakazi ni wazawa na asilimia iliyobaki ni wataalamu kutoka nje ambao wanawafundisha wazawa.

Manyama alisema kiwanda chao kinachukua matunda kutoka kwa wakulima nchini zaidi ya tani laki tatu kwa siku.

Wakati huohuo,Wakili wa Serikali Godfrey Nyamsanda ,aliueleza uongozi wa kiwanda hicho kutengeneza bidhaa zilizo na ushindani katika soko la SADC.

"Hii ni fursa kubwa kwa viwanda vya Tanzania kupata masoko katika nchi za SADC tumieni fursa hiyo kwa kuzalisha bidhaa zilizo bora"alisema Nyamsanda



Sunday, August 11, 2019

SAFARI YA MWISHO YA WALOTEKETEA KWA MOTO mOROGORO

Huzuni, Simanzi, Majonzi Na Vilio Vyatawala Mjini Morogorogo 

HUZUNI, simanzi, majonzi na vilio vimetawala mjini Morogoro leo wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwaakiongoza umati wa wananchi wa Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia kutokana na ajali ya moto wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 71 huku wengine 59 wakijeruhiwa.

Mazishi hayo yameanza kufanyika leo (Jumapili, Agosti 11, 2019) katika eneo la makaburi la Kola Hill mjini Morogoro ambapo Waziri Mkuu amemwakilisha Rais, Dkt. John Magufuli. Ametoa pole kwa wafiwa wote na amewaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki cha maombolezo.

Akizungumza na wananchi katika ibada ya kuwaombea marehemu waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Msamvu mjini Morogoro iliyofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano waliouonesha wakati huu wa amajonzi.

Kufuatia ajali hiyo iliyotokea jana saa 2 asubuhi baada ya lori lenye shehena ya mafuta ya petrol kupinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu mjini Morogoro wakati dereva alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki. Rais Dkt, Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo ya Kitaifa kuanzia jana Jumamosi Agosti 10,2019 na bendera zote zipeperushwe nusu mlingoti.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isac Kamwelwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, viongozi wa dini na wananchi wa mkoa wa Morogoro.

MBUZI 10,000 WACHINJWA KWA AJILI YA SIKUKUU YA EID MKOANI SINGIDA

 Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata ) Mkoa wa Singida, Sheikh, Burhan Mlau akiwa Machinjio ya Ng’ombe ya mkoa huo akiwa amesimama jirani na nyama ambazo zitatolewa sadaka katika kusheherekea Sikukuu ya Eid inayofanyika duniani kote kesho. 
 Mratibu wa utoaji wa sadaka hiyo kutoka Taasisi ya Noor al-yaqeen Foundation ya Zanzibar, Abdul-hamid Khamis (kushoto), akizungumzia utoaji wa sadaka hiyo. Kulia ni Mratibu wa utoaji wa sadaka hiyo mkoa wa Singida, Hassan Hamad.
 Pilika pilika machinjioni.
Ng’ombe  wa sadaka wa Eid wakiwa machinjioni mkoani Singida wakisubiri kuchinjwa.

Na Dotto Mwaibale, Singida
 
MBUZI na kondoo 10,000 wamechinjwa kwa ajili ya kitoweo cha Sikukuu ya Eid mkoani Singida.
 
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata ) Mkoa wa Singida, Sheikh, Burhan Mlau alisema kiloweo hicho ni sadaka inayotolewa kwa ajili ya sikukuu hiyo.
 
” Ni kawaida kila mwaka katika sikukuu ya Eid kuchinja wanyama kama sadaka na kuwa wanyama hao hutolewa na taasisi mbalinbali za kiislam kutoka uturuki, na Misri ambao hufanya kazi ya kuchinja” alisema Mlau.
 
Alisema mwaka huu wamechinjwa kondoo na mbuzi 10,000 huku  ng’ombe wakiwa 1300 na kuwa kitoweo hicho kinatolewa kwa jumuiya mbalimbali za kiislam mkoani humo.
 
Alisema sherehe za baraza la Eid mwaka huu zitafanyika katika wilaya zote za mkoa wa Singida ambazo amezitaja kuwa ni Mkalama, Manyoni, Itigi, Singida Mjini, Singida Vijijini, Iramba na Ikungi.
 
Sheikh Mlau alitumia fursa hiyo ya Sikukuu ya Eid kuwaomba waislam mkoani humo kuwa na mshikamano na kupendana.
 
Mratibu wa utoaji wa sadaka hiyo kutoka Taasisi ya Noor al-yaqeen Foundation ya Zanzibar, Abdul-hamid Khamis amezishukuru taasisi za dini za mkoa wa Singida kwa ushirikiano mkubwa walioutoa na kufanikisha zoezi zima la kuchinja na kutoa sadaka hiyo.

SADC kuanzisha mfuko wa kilimo wa kanda



Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imesema ipo kwenye mkakati wa kuanzisha mfuko wa kilimo wa kanda kwa ajili ya kusaidia nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Hayo yamesemwa leo Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kilimo, Chakula na Maliasili wa jumuiya hiyo Domingos Gove wakati anazungumza na waandishi wa habari za mikutano ya SADC inayoendelea jijini.

“Kwa sasa tupo katika mkakati wa kuanzisha mfuko wa kilimo wa pamoja wa kikanda ambao lengo ni kuhakikisha tunasaidiana katika chakula kwa nchi za SADC,” amesema Gove.

Amefafanua katika mkakati huo pia watahakikisha kunakuwa na miundombinu itakayofanikisha nchi wanachama zinajikita kwenye kilimo kwa ajili ya kupata chakula cha kutosha kwa nchi zao.

Mkurugenzi huyo wa Kilimo, Chakula na Maliasili ameongeza kuwa kwenye mfuko huo ambao utaanzishwa kwa nchi za SADC utahakikisha kunakuwa na usambazaji wa mbegu bora zisizo na magonjwa, upatikanaji wa soko kwa malighafi zinazohusika kwenye suala la kilimo.

Pia amesema mikakati mingine ni kuongeza ushindani na uzalishaji wa nafaka pamoja na kuhakikisha kunakuwa na sera ya kulinda usalama wa chakula.

Rais Magufuli atoa Tsh. 500,000 kwa kila Majeruhi wa ajali ya Moto Morogoro


Rais Magufuli ametoa Tsh. 500,000 kwa kila majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea Morogoro jana alipowatembelea na kuwafariji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ameeleza hayo leo akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokwenda kuwatembelea majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea jana Msamvu Morogoro.

Pia Rais Magufuli pia ametoa motisha ya fedha kwa wauguzi na madaktari wanaotoa huduma kwa majeruhi hao.

“Serikali itagharamia gharama zote za matibabu kwa majeruhi, ninyi (madaktari) endeleeni kutoa huduma, na gharama zote mzilete serikalini, hawa wote ni Watanzania, tutawahudumia,” amesema.

Ameendelea kwa kusema, "Nasisitiza, tusiwe majaji, tusiwe wepesi kutoa hukumu, si kila aliyehusika katika ajali hii alikwenda kuchota mafuta, wengine walikuwa wanapita tu, wengine walikwenda kuokoa, wengine walikuwa na shughuli zao,”.

Saturday, August 10, 2019

RAIS DKT. MAGUFULI ATUMA SALAMU AJALI YA MOROGORO

Image may contain: text

IDADI YA WALIOKUFA NA MAJERUHI AJALI YA MOROGORO

Taarifa kutoka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kuhusu ajali ya kuungua moto kutokana na kulipuka kwa gari la mafuta mkoani humo.


Mpaka sasa watu 62 wameripotiwa kufariki dunia na wengine 70 kujeruhiwa.


Aidha, taarifa hiyo imesema majeruhi 39  kati yao hali zao ni mbaya hivyo wanakimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwaajili ya matibabu zaidi.


Maiti zote 62 zimehidhiwa hospitali ya mkoa wa Morogoro kwaajili ua utambuzi na ndugu zao huku nyingine kati ya hizo hali zao ni mbaya sana kiasi ambacho haziwezi kutambulika.

GARI LA TIF LAPATA AJALI IRINGA.

Gari la Taasisi ya The Islamic Foundation yenye makao yake makuu mkoani Morogoro limepata ajali mkoani iringa na kujeruhi.


Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sheikh Ibrahim Twaha, ilisema gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser  T.198 AHE lilikuwa na watu watatu na kwamba hakuna aliyepoteza masiha.


Alisema ajali hiyo imetokea mkoani Iringa ambapo walikuwa wakienda kununua Ng'ombe sehemu kilomita 50 kutoka Iringa mjini, kwaajili ya kuchinja siku ya sikukuu ya Iddi.