Saturday, August 10, 2019

BILIONI 4.6 KUJENGA NA KUKARABATI CHUO CHA UFUNDI KARAGWE.

Image may contain: 5 people, people standing and outdoor
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4.6 kutekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.


Hayo yamesemwa Wilayani Karagwe na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu katika wilaya hiyo, ambapo amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni kuongeza udahili wa wanafunzi wanaochukua masomo ya ufundi.


Ole Nasha amesema serikali imeweka mkakati wa kukarabati na kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya, kwani ili kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kama nchi kuwa na vijana wenye maarifa na stadi mbalimbali za ufundi zitakazowawezesha kuajiriwa, kujiajiri na kushiriki katika uchumi wa viwanda.


“Rais ameweka nguvu nyingi katika kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja, hospitali zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna mambo mengi yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji ufundi, hivyo mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” ameongeza Ole Nasha.


Wakati huo huo, Naibu Waziri ametoa miezi mitatu kwa wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha wanamaliza ujenzi na ukarabati wa chuo hicho, ambapo amesema hajaridhishwa na sababu zilizotolewa na mhandisi msanifu kutoka TBA zilizopelekea kutokamilika kwa mradi kwa wakati.


Ole Nasha anesisitiza kuwa hakuna wakati wowote ambao fedha iliyopaswa kutolewa imeshindwa kutolewa na VETA kwani mpaka sasa TBA imeshalipwa zaidi ya shilingi bilioni moja ambayo ni asilimia 25 ya fedha yote iliyopaswa kulipwa wakati ujenzi umefikia asilimia 44 tu.


Awali Mhandisi Msanifu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Kelvin Joas alimweleza Naibu Waziri kuwa kutokukamilika kwa mradi huo kwa wakati nikutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo za kimkataba na kuwapelekea kuomba kuongezewa muda wa miezi sita baada ya muda wa mkataba kuisha Julai 26,2019.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Godwin Kitonka amesema Halmashauri yake inaishukuru serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutenga fedha zaidi ya bilioni 4.6 kwa ajili ya kujenga majengo mapya ambayo ni pamoja na jengo la utawala, ukumbi mdogo, vyoo vya nje, bweni la wasichana na kukarabati karakana ya ushonaji na uchomeleaji chuma.


Mwanafunzi Masau Josephat, ameishukuru serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuongeza majengo ambayo awali hayakuwepo kwani mwanzoni hayakuwa yakiidhisha, huku wakiiomba serikali kuongeza baadhi ya kozi ambazo hazipatikani chuoni hapo ili kupanua wigo wa upatikanaji wa maarifa na stadi kwa vijana wa Karagwe na maeneo ya jirani.

MTU MOJA AFARIKI BAGAMOYO BAADA YA KUGONGWA NA GARI.

Mtu mmoja ambae hakufahamika jina lake amegongwa alfajiri ya leo Agosti 10, 2019, katika Daraja la Kioga jirani na mashamba ya Mpunga ya kilimo cha umwagiliaji (JICA) barabara ya Bagamoyo/ Msata.


Mtu huyo (kutokana na kusagika sana) inaaminika kuwa ni mwanamke huenda alikuwa akienda kwenye mashamba ya mpunga kwaajili ya shughuli za kilimo.


Taarifa kutoka watu waliobaini mwili huo, walisema mtu huyo aligongwa kabla ya jua kutoka na kwamba mara baada ya kugongwa na gari moja (ambalo halikufahamika)  magari mengine yaliendelea kumkanyaga na kusababisha kusagika kiasi cha kushindwa kumtambua.


Walisema wapita njia walibaini kuwa huyo ni mtu aliyegongwa, hivyo wakuchukua hatua ya kuwapigia simu polisi wa usalama barabarani ili wafike eneo la tukio.


Aidha, walisema kuwa mara baada ya taarifa hiyo, polis kikosi cha usalama barabarani Bagamoyo, walifika eneo la tukio na kuanza kukusanya mabaki ya mwili huo na kutia ndani ya kiroba kwaajili ya hatua zaidi za uchunguzi.


BAGAMOYO KWANZA BLOG ilibahatika kupata picha zinazoonyesha asikari wa usalama barabarani wakipakia mabaki ya mwili huo kwenye viroba mithili ya nyama na kwamba kutoka na maadili ya kazi hatutoweza kuziweka picha hizo.

UBALOZI WA MAREKANI NA UINGEREZA WATOA TAMKO KUHUSU HAKI ZA RAIA.

WATU ZAIDI YA 54 WAFARIKI MOROGORO BAADA YA GARI LA MAFUTA KUWAKA MOTO.

Image may contain: motorcycle and outdoor
Ajali mbaya imetokea leo Agosti 10, 2019 eneo la Msamu mkoani  morogoro  baada ya gari la kubeba mafuta kuungua.


Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema kuwa, gari hilo la mafuta lilikuwa likitokea Dar es salaam na kwamba baada ya kufika Msamvu mwendesha bodaboda alikatisha barabara bila ya kuangalia.


Waliendelea kusema kuwa, mara baada ya mwendesha bodaboda huyo kukatisha barabara ghafla lori hilo la mafuta lilimgonga na kupoteza muelekeo hali iliyosababisha kupinduka.


Aidha, baada ya kupinduka kwa lori hilo watu mbalimbali wakiwemo waendesha bodaboda walikimbilia kuiba mafuta na ndipo moto ulipowaka na kuwaunguza watu wengi zadi pamoja na pikipiki.


Taarifa zaidi zinasema wakati watu mbalimbali wanaendelea kuiba mafuta kwenye gari hilo huku mwingine alienda kufungua betri ya gari hilo na ndipo aliposababibsha shoti na kupelekea kulipuka kwa moto.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe amefika katika eneo la tukio na kuthibitisha kuwa miili ya watu iliyohesabiwa mpaka sasa ni 54.
Image may contain: one or more people, fire and outdoor

Thursday, August 8, 2019

WATAFITI WA TARI- NALIENDELE WAGUNDUA JANI LA MKOROSHO KUTOA MICHE.

Kitalu cha miche bora ya Mikorosho kilichoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) Naliendele.

Kitalu cha miche bora ya Mikorosho kilichoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) Naliendele.
......................................

Na hadija Omary, Lindi.

Taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) Naliendele, Kilichopo Mjini Mtwara imegundua Njia ya uzalishaji wa Miche ya mikorosho kwa kutumia jani la mti huo.


Hayo yameelezwa na kaimu Mkumkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Fortunatus Kapinga, jana katika ufunguzi wa Maonyesho ya Nane Nane kanda ya Kusini yanayofanyika katika viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi Mkoani humo.


Kapinga alisema kwa sasa Taasisi hiyo bado wapo kwenye utafiti wa uzalishaji wa miche ya Mikorosho kwa kutumia majani ya Mti huo ambapo kwa kiasi kikubwa utasaidia kuzalisha miche mingi kwa wakati mmoja.


Alisema kwa kutumia njia hiyo jani moja la mti wa Mkorosho linaweza kuzalisha miche 100 ya mti huo hivyo kurahisisha namna bora ya kuandaa miche ya zao hilo.


Hata hivyo DKT. Kapinga aliongeza kuwa endapo watakamilisha utafiti huo wanaweza kuongeza uzalishaji wa mashamba mengi ya korosho kwa kupata miche mingi na mashamba kuongezeka.


"Kwa sasa bado tunaendelea na utafiti wa kuzalisha miche kwa kutumia jani la mkorosho na ukikamilika utaongeza thamani ya korosho kuanzia majani, tunda (bibo) na korosho yenyewe" alisema Dkt Kapinga.


Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa maonyesho hayo ya Wakulima Nane nae kanda ya Kusini kwa Niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (TAMISEMI) Selemani Jaffo Mkuu wa Wilaya ya Masasi Suleimani Mzee aliipongeza Taasisi hiyo kwa kugundua namna ya uzalishaji wa Miche hiyo ya mikorosho huku akiwataka watendaji wa Taasisi hiyo kuendelea kufanya utafuiti katika mazao mengine ili kuongeza tija ya uzalishaji


"Niwapongeze sana wataalamu wetu wa Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI Naliendele, kwa kuongeza Wigo katika uzalishaji wa Miche ya Mikorosho kwani wametoka kuzalisha miche kwa kutumia mbegu ya korosho na sasa wanazalisha miche kwa kutumia jani la Mti huo hongereni sana” alisema Mzee.