Saturday, July 13, 2019

KAMISHNA MHIFADHI WA MISITU PROF. DOS SANTOS SILAYO AWASILI MAKAO MAKUU YA TFS JIJINI DAR ES SALAAM

Image may contain: 1 person, standing and outdoor
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Tehama, Harold Chipanha akimpigia saluti Kamishna Mhifadhi wa Misitu Prof. Dos Santos Silayo mara baada ya kuwasili makao makuu ya Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu kuvishwa cheo hiko cha kijeshi Julai 9,2019 wilayani Chato mkoani Geita
......................................... 


Kwa mara ya kwanza tangu avishwe cheo cha Kamishna Mhifadhi wa Misitu na Mhe. Dkt Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii na hatimaye kula Kiapo cha Utii na uadilifu mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Julai 9, 2019, Kamishna Prof. Dos Santos Silayo amewasili makao Makuu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), jana, Julai 12 jijini Dar es salaam na kupokelewa na Viongozi Waandamizi na watumishi wa TFS.


Akizungumza na watumishi wake mara baada ya kuwasili ofisini hapo, Kamishna Prof. Silayo alisema mabadiliko yanayotokea katika sekta ya maliasili yamepelekea pia kubadili mfumo wa usimamizi na utendaji wetu toka ule wa Kiraia kwenda Jeshi Usu.


Hatua hiyo ikapelekea kuvishwa cheo cha Kamishna Mhifadhi wa Misitu na Mhe Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii na kula Kiapo cha Utii mbele ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. John Pombe Magufuli siku ya tarehe 9 Julai 2019.


“Mabadiliko hayo yanalenga kujenga uwezo wa taasisi, uwezo wa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwajengea ari, uzalendo, weledi na ujasiri katika kusimamia rasilimali za misitu na nyuki,” alisema Kamishna Prof. Silayo.


Kamishna Prof. Silayo alisema uwezo wa watumishi wa TFS utaenda sambamba na weledi katika matumizi ya mbinu na vifaa vya kisasa vinavyoweza kumudu mabadiliko ya changamoto za uhifadhi kuanzia usalama wao pamoja na usalama wa mali zenyewe unaotokana na kuongezeka kwa mbinu za kihalifu kila wakati.


Aidha Prof. Silayo alitoa shukurani kwa Mheshimiwa Rais na viongozi wote wa wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua hiyo waliyofikia ambayo anaamini itasaidia kukuwa kwa sekta ya misitu nchini na kuongeza ushirikiano na wadau wengine hususani wananchi katika kusimamia misitu yetu.


Akiongea kwa njia ya simu Naibu Kamishna wa Huduma Saidizi, Emmanuel Wilfred alisema mabadiliko hayo yamepelekea kubadili mfumo wa usimamizi na utendaji wa TFS toka ule wa Kiraia kwenda Jeshi Usu na hivyo kulazimu watumishi wote kwenda kwenye mafunzo.


“Tunaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wachache waliobaki na kwa wale waliokwishakwenda kwenye mafunzo tunakamilisha taratibu ili Kamishna aweze kuwatunuku vyeo vyao, lakini niwatake wafanyakazi wote kuenda sambamba na mabadiliko kwa kasi hitajika,” alisema Kamishna Msaidizi huyo.


Rosemary Sabida mmoja wa watumishi wa TFS anasema mabadiliko hayo yataisaidia TFS kukabiliana na changamoto mbalimbali za uhifadhi nchini.


Jumla ya Makamishna wanne, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Dkt Allan Kijazi, Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu toka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof Dos Santos Silayo na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Dkt. James V. Wakibara pamoja na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Freddy Manongi walivishwa vyeo vya kijeshi Julai 9, 2019 katika sherehe za Uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato zilizofanyika wilayani Chato mkoani Geita.
 Image may contain: 10 people, people standing, tree and outdoor

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Tehama, Harold Chipanha akimuongozo Kamishna Mhifadhi wa Misitu Prof. Dos Santos Silayo kwenda kwenye ukumbi wa mikutano wa Ngorongoro uliopo makuu ya Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuzungumza na watumish.
Image may contain: 18 people, people smiling, people standing 
Kamishna Mhifadhi wa Misitu Prof. Dos Santos Silayo akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa jeshi usu.


Friday, July 12, 2019

WAJASIRIAMALI PWANI WATAKIWA KUBUNI BIDHAA MPYA.



Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akikagua vikundi vilivyokopeshwa na Halamashauri hiyo, kushoto mwenye miwani ni Diwani wa kata ya Magomeni Bagamoyo, Bi Mwanaharusi Jarufu.
...............................

Na Selestian James.

Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, amewataka wajasiriamali mkoani humo kubuni Bidhaa mpya ili kukabiliana na ushindani katika masoko ya bidhaa za wajariamali.


Mgalu ameyasema hayo katika Halmashauri ya Bagamoyo wilayani humo, alipokuwa akikagua vikundi vilivyokopeshwa na Halmashauri hiyo ili kujiridhisha kama mjumbe wa mikopo kuona kama fedha hizo zimefika kwa walengwa na kufanyiwa kazi zilizokusudiwa.


Alisema wajasiriamali wengi wanalalamika bidhaa zao kukosa soko hali inayopelekea kukata tamaa ya kuendelea kuzalisha kwakuwa mitaji haikuwi kutokana na mauzo hafifu.


Aliwasihi kubuni bidhaa za aina mbalimbali na hasa kutumia fursa ya vitu ambavyo havipatikani katika eneo husika, vitu vinavyoendana na utamaduni wa watu wa eneo husika, kuangalia bidha ambayo haipo katika eneo husika itengenezwe pamoja na kuzingatia ubora wa bidha.


Alisema katika kipindi hiki ambacho mifuko ya plastic imepigwa marufuku na wananchi kutumia mifuko mbadala ni kipindi cha kutumia fursa ya kubuni mifuko mbadala inayoendana na mazingira na utamaduni wa watu wa Pwani ili kukidhi mahitaji ya wateja na kupanua wigo wa ubunifu katika ujariamali.


Akitolea mfano, Mgalu, alisema watu wa Pwani wanaasili ya kutumia vikapo hivyo wajasiriamali watengeneze vikapo kwa wingi ili kwenda sambamba na mahitaji, na kwamba wasipotumia fursa hiyo watu wa pwani watanunua vikapo kutoka mikoa mingine jambo ambalo litawafanya washindwe kuingia kwenye ushindani wa bidhaa.


Subira Mgalu ambae pia ni Naibu Waziri wa Nishati amewataka wananchi wilayani Bagamoyo kujitokeza kuchukua fomu za kuunganishwa umeme ili kutumia fursa ya punguzo la bei katika kuunganishwa umeme ambao kwa sasa ni shilingi elfu ishirini na saba tu 27,000.


Awali akisoma taarifa, Afisa Maendeleo ya Jamii anaeshughulikia mfuko wa vijana wilaya ya Bagamoyo, Halima Shabani, alisema Halmashauri ya Bagamoyo imetoa zaidi ya milioni 92 kwa vikundi vya wanawake na milioni 70 zimetolewa kwa vijana katika kipindi cha mwaka wa fedha wa mwaka 2018/2019 na hivyo kufanya jumla fedha zilizotolewa mwaka huu ni zaidi ya milioni 162.


Aidha, alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 milioni 53 zimetolewa kwa vikundi vya vijana na milioni 59 kwa vikundi vya wanawake ambapo mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya milioni 136 zimetolewa kwa vikundi vya vijana na vikundi vya wanawake milioni 134, huku mwaka wa fedha 2017/2018 shilingi milioni 131 kwa vikundi vya wanawake na milioni 114 kwa vikundi vya vijana.


Akiwa katika ziara hiyo, Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Mgalu  alifanikiwa kukagua vikundi vya kata za Magomeni, Nianjema, na Kiromo ambapo alijiridhisha kuwa vikundi vyote vilifikiwa na fedha.


Kwa upande wao viongozi wa vikundi hivyo vilivyokopeshwa wameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwajali wanawake na vijana katika kujikwamua kiuchumi.


Aidha, walisema kwa sasa hawana sababu ya kuingia kwenye vikundi vya mitaani ambavyo wanaweza kutapeliwa na badala yake wanapata mikopo kwa fedha za serikali ambazo hazina riba.
  
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akikagua vikundi vilivyokopeshwa na Halamashauri hiyo,
  
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akikagua vikundi vilivyokopeshwa na Halamashauri hiyo, kushoto mwenye miwani ni Diwani wa kata ya Magomeni Bagamoyo, Bi Mwanaharusi Jarufu.
 
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, akiwa katika picha pamoja na vikundi vya wajasiriamali Halmashauri ya Bagamoyo.

Picha zote Na Selestian James.

Thursday, July 11, 2019

SHULE WILAYANI RUANGWA ZABUNI MIRADI KUONGEZA KIPATO.

Na Hadija Hassan, LINDI.

Kutokana na Changamoto ya uchache wa fedha za Elimu Bure kutokidhi mahitaji Baadhi ya Shule za Msingi wilayani Ruangwa Mkoani Lindi zimebuni Miradi mbali mbali ya maendeleo ili kuweza kujiongezea kipato.


Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Ng'ombe wa Maziwa katika Shule ya Msingi Matope na Mradi wa Shamba la Miembe ya muda mfupi katika Shule ya Msingi Chilangalile.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Walimu wakuu wa Shule hizo mbili , mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtope, Zunu Kigomba na Bakari Hamimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chilangalile, walisema kuwa kutokana na mahitaji waliyonayo katika shule zao fedha hizo zinazotolewa na Serikali haziendani na idadi ya wanafunzi waliokuwepo.


Nae Zuna kigomba alisema kuwa kutokana na Mradi wa Ngombe waliouanzisha baada ya kupata fedha za Elimu ya kujitegemea (EK) kutoka EQUIP T ulioghalimu Tsh. 15,000,000. umeweza kupunguza michango mbali mbali kutoka kwa wazazi kwa ajili ya kuandaa mitihani hasa kwa wanafunzi wa Darasa la Nne na Darasa la Saba.


“faida tuliyoipata kutoka katika huu Mradi tumekuwa tukipata fedha za kuchapa Mitihani bila kuhusisha fedha ya kapitesheni ya Shule, tumeweza kununua baskeli ya Shule , Sufuria kwa ajili ya kupikia chakula cha Wanafunzi, unatusaidia pia kununua vifaa vya kufundishia kama vile chaki na manila bila ya kukopa kopa maeneo Mengine "Alisema.


Aliongeza kuwa kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuendeshea shule kutotosheleza mahitaji wanalazimika kukopa kutoka Katika vyanzo vingine vya mapato ili kuendesha shughuli za Shuleni hapo.


Kwa upande wake Mratibu elimu Kata wa Kata ya Makanjiro Katherini Mbinga alisema kuwa Mradi wa miti ya Miembe ambapo pia umetokana na Mpango wa Elimu ya kujitegemea (EK) kupitia Mpango wa EQUIP T uliobuniwa katika Shule ya Msingi Chilangalile wenye gharama ya Tsh. 15,000,000, na Shule Zingine katika kata hiyo utaweza kuwasaidia katika utekelezaji wa Mikakati ya kuinua taaluma Ngazi ya Kata inayofanywa katika Halmashauri hiyo.


Alisema Mikakati mingi ya kupandisha ufaulu katika maeneo yao inakwama kutokana na changamoto ya kukosa fedha ya kutosha ya kutekeleza mikakati hiyo.


“tunapokaa na walimu kupanga namna ya kuinua taaluma lazima tuhitaji pesa, pesa ambayo mashuleni ukilinganisha fedha inayofika ni kidogo ambayo sisi kama ngazi ya kata kama ni kufanya mitihani, kufanya ziara za kimasomo, tunashindwa kutekeleza kwa sababu fedha haitoshi kwa hivyo kupitia huu mradi baada ya kuanza kuvuna mazao ni matarajio yangu shule hizi zitakuwa na kipato binafsi tofauti na ile fedha ambayo inaingia kutoka serikali kuu” 

  
Alifafanua Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chilangalile Bakari Amimu alisema kuwa Shamba hilo la Miembe Lina ukubwa wa Nusu hekta na lina miche 120 ambapo kila mche mmoja unatarajiwa kuzaa maembe 20 ambapo kwa mara ya kwanza wanataraji kuvuna maembe hayo ifikapo mwaka 2020.


Hata hiyo Abdull Nangomwa Ofisa Elimu Taaluma wa Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi akizungumza kwa Niaba ya Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo Alikili kuwepo kwa Miradi ya Maendeleo katika Baadhi ya Shule Wilayani hapo itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato ambayo itapelekea Kufanya ujazilizi katika fedha zinatoka Serikalini kwa ajili ya kufanya mambo mbali mbali katika Shule Zao