Monday, June 3, 2019

WANANCHI LINDI WASHAURIWA KUTUMIA KIFAA CHA UMETA ILI KUPATA NAFUU YA KUUNGANISHIWA UMEME.

NA HADIJA HASSANI, LINDI.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa Nishati vijijini Rea Mhandisi Amos Maganga amewashauri wananchi wa Mkoa wa Lindi kutumia kifaa cha umeme tayari UMETA Kuunganisha umeme katika Nyumba zao ili kuondokana na gharama za kuweka mfumo wa umeme.

Mhandisi Maganga ameyasema hayo leo Juni 03, 2019 mara baada ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa usambazaji wa umeme vijijiji REA katika Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi alipokuwa ameongozana na Wataalamu wa Bodi hiyo.

Maganga alisema huenda idadi ndogo ya wateja waliounganishwa kwa ajili ya kupata huduma ya Umeme inatokana na gharama kubwa ya kuweka mifumo ya umeme katika nyumba zao hivyo kupitia kifaa hicho wananchi wataweza kuunganishiwa huduma hiyo pasipo kuweka mifumo hiyo.

Alisema serikali kwa kutambua kuwa umeme huo wa Rea unaenda vijijini tena kwa wananchi walio wengi ilionelea kuwaletea kifaa hicho cha UMETA ili waweze kupata huduma hiyo ya Umeme kwa gharama nafuu zaidi.

Alisema vifaa hiyo vimetolewa 250 kwa kila mkoa ambavyo vinapaswa kuunganishwa bure kwa wateja wapya wa awali wa mradi huo wa Umeme vijijini.

Nae Msimamizi wa miradi ya Umeme Vijijini Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi Lameck Njambo alisema kifaa hicho cha Umeme tayari UMETA hakina tofauti na mfumo wa kawaida wa umeme.
Alisema kifaa hicho huwa kina uwezo wa kuwasha taa, kutumia jiko la umeme, Tv, feni, friji pasi na vifaa vingine vya umeme kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa Meneja wa Shirika la Umeme Tanesco Mkoa wa Lindi Felisian Makota alisema kuwa kati ya wateja 5000 wanaotarajiwa kuunganishiwa umeme kupitia Mradi huo wa umeme vijijini Rea ni wateja 290 Peke ndio waliounganishiwa kwa sasa.

MKUTANO WA NISHATI KWA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAANZA ARUSHA

Image may contain: 3 people, people sitting and indoor
 Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Utawala, Christopher Bazivamo, akifungua Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, Juni 3, 2019 jijini Arusha.
.............................................


Na Veronica Simba – Arusha

Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, umeanza leo Juni 3, 2019 jijini Arusha.


Akifungua Mkutano huo katika siku ya kwanza katika mkutano huo ambao unahusisha ngazi ya wataalamu wa sekta husika, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Utawala, Christopher Bazivamo, amewataka kujadili kwa uwazi changamoto zinazokabili nchi wanachama hususan upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kuainisha mikakati ya kuzitatua.


“Jamii zetu bado hazijawa na umeme wa uhakika ukilinganisha na sehemu nyingine za Dunia, hii ni changamoto ambayo tunahitaji kuitafutia ufumbuzi, tujadili kwa uwazi ili tuone wapi tunakwama na namna gani tutatue,” alisisitiza.


Akifafanua zaidi, Bazivamo alisema changamoto za nishati kwa nchi za Afrika Mashariki zinahusisha mambo mbalimbali ikiwemo nishati ya kupikia ambayo alieleza kuwa asilimia kubwa ya wanajamii wa ukanda husika bado wanatumia kuni na mkaa; hali inayochangia uharibifu wa mazingira.


Alisema haitoshi kuwaonesha wananchi kuwa nishati ipo isipokuwa kuchukua hatua za kuifanya ipatikane kwao na kwa bei wanayoweza kuimudu.


Aidha, Bazivamo amewashauri wataalamu husika, kuhakikisha wakati wanahamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa umeme, wahamasishe pia uwekezaji katika usambazaji wa nishati hiyo ili kuwezesha hali ya upatikanaji wake kwa jamii.


Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo wa 14 unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi na program katika sekta ya nishati pamoja na maagizo yaliyotolewa katika Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati.


Aidha, Mkutano huo utapokea Rasimu ya Makubaliano ya Awali (MoU) iliyoandaliwa na Sekritarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Mradi wa Umeme wa Nsongezi katika Mto Kagera unaotarajiwa kutekelezwa kwa ushirika wa nchi za Tanzania, Uganda na Rwanda ili ipitiwe na nchi husika.


Mkutano ngazi ya Mawaziri utafanyika Juni 7 mwaka huu, ambayo ndiyo siku ya mwisho ya mkutano husika.
Tanzania inawakilishwa na wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na taasisi mbalimbali zinazohusiana na nishati kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Image may contain: 4 people

 Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.
Image may contain: 6 people 

Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.
Image may contain: 4 people, people sitting    
Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.
Image may contain: 8 people 
Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.