Monday, May 13, 2019

SERA YA UGATUAJI IMEKWAMA WAPI

Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akifungua kikao cha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa cha kupitia rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper Jijini Dodoma.
...........................


Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

Kutokuwepo kwa Sera ya Ugatuaji Madaraka iliyojengwa kwenye mfumo wa Sheria ni moja ya changamoto iliyofanya Serikali kufanya mapitio ya sera hiyo.
 
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo(Mb) wakati wa kufungua kikoa kazi kilichokutanisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kutoka Mikoa yote 26 kwa ajili ya kutoa maoni na mapendekezo kwenye Rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji Madaraka ya 2019.
 
Alisema kuwa changamoto moja wapo ni kutokuwepo kwa sera ya ugatuaji iliyojengwa kwenye mfumo wa kisheria inayoelekeza mipaka, majukumu na utaratibu wa utekelezaji wake, jambo ambalo linafanya ionekane kama ni hiari na utashi (Voluntary and Willingness).
 
Jafo alisema changamoto nyingine ni kuwepo kwa mitazamo inayokinzana kati ya watendaji na viongozi wa kisiasa katika ngazi ya vijiji, kata na halmashauri katika kuweka vipaumbele na kutekeleza miradi ya maendeleo.
 
Aliongeza kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekuwa zikitegemea fedha kwa kiasi kikubwa kutoka Serikali kuu na kutolea mfano kwa mwaka 2018 zilitegemea zaidi ya asilimia 88 ya mapato.
 
“ Wizara za Kisekta kuandaa sera na sheria na kupeleka halmashauri kwa ajili ya utekelezaji bila kuambatanisha rasilimali fedha, vifaa na watu.”
 
Waziri Jafo alibainisha kuwa uelewa mdogo wa dhana ya Ugatuaji wa Madaraka (D by D) kwa baadhi ya Wizara za Kisekta na hivyo Sera hii kuonekana kama ni suala ya OR-TAMISEMI kwa kiasi kikubwa imechangia kufanya Sera hii kutotekelezeka kwa kiwango kilichotegemewa.
 
Jafo aliongeza: “Kwa ujumla hatujafikia kiwango cha mafanikio kilichotarajiwa kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeaza na ndio maana Serikali imeamua kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji ili kupata suluhisho la changamoto zilizojitokea.
 
Aidha, Jafo amewataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kutoa maoni na mapendekezo hayo ili kuboresha rasimu hiyo kwa maslahi mapana ya wananchi, wadau na taifa kwa ujumla.
 
Aidha Mhe. Jafo alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuhakikisha wanasimamia kwa ukabilifu fedha na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa hospitali za wilata, ujenzi wa mabweni, madarasa, vyoo katika shule za msingi na sekondari ambayo tayari fedha zake zimeshatolewa na serikali.
 
Naye Mwenyekiti wa wakuu wa mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Eng. Evarist Ndikilo aliahidi kushiriki mzuri wa wawakuu hao kwa kuwa wao ndio wanaotoka kwa wananchi.
 
Pia alimhakikishia Waziri Jafo kuwa watasimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwa itakamilika katika muda uliopangwa na kwa ubora unaotakiwa.
 
Naye Mwakilishi wa UNICEF, Pius Chaya alisema agenda ya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji Madaraka imekuja wakati muafaka, kwasababu Serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma wanazostahili na ambazo zinawafikia kwa wakati.
 
Aidha, Chaya alisema wadau wa maendeo ambao pia wameshiriki katika machakto wa mapitio ya sera hiyo wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuwaletea wananchi wake maendeleo
Sera ya Ugatuaji wa Madaraka ni dhana ya Kupeleka Madaraka, Majukumu na Rasilimali kutoka Serikali Kuu kwenda kwa Wananchi kupitia vyombo vya kidemokrasia na Kisiasa ambavyo, wajumbe wake huchaguliwa na kuwajibika kwa Wananchi na vimepewa Mamlaka ya kutoa Maamuzi na kusimamia rasilimali (yaani vina uhuru, vinajitawala, na vina hadhi ya kisheria).
 
Sera hii ilianza kutekelezwa mwaka 1998 kupitia mpango wa maboresho ya Serikali za Mitaa ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi kushiriki shughuli za Maendeleo katika maeneo yao na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.

 

UWT PWANI WAANDAA KONGAMANO LA KUMPONGEZA RAIS DK. MAGUFULI KWA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM 2015 -2019

Mbunge wa viti maalumu wa kuteuliwa, Mama Salma Kikwete akizungumza katika kikao cha maandalizi ya kongamano la kumpongeza Rais Dk.John Magufuli na serikali kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2015 – 2018, kushoto ni mwenyekiti wa UWT mkoani Pwani,Farida Mgomi.( Picha na Mwamvua Mwinyi)
............................


NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA.

UMOJA wa wanawake Tanzania (UWT), mkoa wa Pwani umefanya mkutano maalumu wa maandalizi ya kongamano la kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kufuatia utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM 2015 – 2019 katika mkoa huo, ambapo unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.


Mwenyekiti wa Uwt Mkoa wa Pwani, Farida Mgomi, akielezea juu ya kongamano hilo alisema, wamekutana wajumbe wa kamati maalumu kwa ajili ya kuzungumza namna bora jinsi ya kujipanga katika maandalizi hayo.


Aidha alisema, Rais Dk. Magufuli ni jemedari na kiongozi asiyeyumbishwa na mtu katika kulijenga Taifa kuelekea kwenye uchumi wa kati, amefanya mengi katika mkoa huo hasa  miradi mikubwa ya ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR), utengenezaji wa barabara za lami, ujenzi wa bwawa la umeme eneo la Rufiji, ujenzi wa viwanda na mradi mkubwa wa umeme.


“Sisi uongozi wa umoja wa wanawake wa Tanzania (UWT) wa chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani  tumepata wasaa wa kufanya mazungumzo na kupata namna nzuri ya kuandaa kongamano letu, ukiachia kumpongeza Rais Magufuli lakini pia kuwakutanisha wanawake wa mkoa huu na kupeana mbinu mbalimbali za kiuchumi”


“Lakini kupitia kongamano hilo pia wabunge wa viti maalum wa mkoa akiwemo Subira Mgalu, Hawa Mchafu na Zaynab Vullu watapata fursa ya kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kuanzia 2015 hadi 2019 kwa mkoa wetu wa Pwani”alielezea.


Hata hivyo Farida alifafanua kwa kusema kuwa, kinamama pia watapata elimu juu ya namna ya kutumia fursa za viwanda na mradi mkubwa wa Stigler's Gorge , katika kujikwamua kiuchumi .


Mbunge wa viti maalum wa kuteuliwa mama Salma Kikwete alikuwa miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Pwani ambae aliupongeza uongozi wa jumuiya hiyo kwa kuamua kufanya kikao kwa ajili ya maandalizi ya kongamano kubwa la kumpongeza Rais.


Aliahidi na kuwahakikishia jumuiya hiyo kuwa pamoja nao katika kuhakikisha kongamano hilo linafanyika na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

TASAF LINDI WABUNI MRADI WA KUPANDA MIKOROSHO KUNUSURU KAYA MASKINI.

NA HADIJA HASSAN 12/05/2019 LINDI.

Wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi wamefanikiwa kupanda Miche 3,039 ya Mikorosho katika mashamba yenye ukubwa wa hekari 121 na kufanikiwa kujipatia ujira wa Tsh. Milioni 437.6

Hayo yameelezwa na Mratibu wa TASAF wa manispaa hiyo Dativa kysima alipokuwa anatoa taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika Halmashauri yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi Mwishoni mwa wiki alipokwenda kutembelea pamoja na kuzungumza na walengwa wa Mpango huo katika halmashauri hiyo.

Kysima alisema walengwa hao ni wale ambao wanatekeleza mradi huo kupitia mpango wa ajira za muda mfupi.

Aidha Kysima aiitaja mitaa iliyotekeleza mradi huo wa kupanda miche ya Mikorosho kuwa ni Mitumbati ambapo wamefanikiwa kupanda miche 45 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 2 na kufanikiwa kupata ujira wa Tsh. 10.777,800.00, mtaa wa kiduni ambapo umepanda miche 208 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 8 na kupata ujira wa kiasi cha Tsh.10,959,500, mtaa wa Chikonji Kaskazini miche 307 kwa shamba lenye ukubwa wa hekta 12 na kupata ujira wa 23,740.600 na mtaa wa Chikonji Kusini miche 307 kwa shamba lenye ukubwa wa hekta12 na kupata ujira wa Tsh.12,045,100

Aliitaja mitaa mingineni kuwa ni Mtaa wa Kikwetu ambao umepanda miche 333 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 13 na kupata ujira wa Tsh.5,448,700, 00, mtaa wa Mingoyo miche 122 katika shamba lenye hekta 5 huku wakipata ujira wa Tsh.18,018,200,00, mtaa wa Mawasiliano ambao umepanda Miti 178 katika shamba lenye ukubwa wa Hekta 7 na kupata ujira wa Tsh.14,524,500,00.

Mitaa mingine iliyotekeleza mradi huo ni Nanyanje ambao wao wamepanda miche 320 katika shamba lenye ukubwa wa Hekta 13 na kupata ujira wa Tsh.8,429,500.00, Mtaa wa Jangwani miche 120 katika shamba lenye ukubwa wa Hekta 5 na kupata ujira wa fedha ya Tsh.13,298,600.00 na mwisho ni Mtaa wa ambao umepanda miche 1100 katika shamba lenye ukubwa wa Hekta 44 na kupata ujira wa Tsh. 20,382,600.00

Awali Mkurugenzi wa Manspaa ya Lindi Jomary Satura alisema kuwa kabla ya kubuni mradi huo wa mashamba wanufaika hao wa TASSAF ambao wanatekeleza mradi wa ajira za muda walikuwa wanawatumia katika kufanya usafi kwenye maeneo yao ya mitaa pamoja na meneo ya Umma kama vile maeneo ya sokoni , katika hospitali na zahanati pamoja na stendi

“walikuwa wanafanya shughuli hizo na baadae tunawalipa lakini tukaona hiyo sio sawa kwa kuwa shughuli zile tulikuwa tunapaswa kufanya wenyewe kama Halmashauri ndipo tukabuni huu mradi wa mashamba ya mikorosho ambapo tulikubaliana na wanufaika hawa kufanya usafi katika mashamba hayo pasipo kuwaambia kuwa baadae mashamba hayo yatakuwa yakwao” alisema Satura.

Satura aliongeza kuwa Baada ya mashamba hayo kufanyiwa usafi pamoja na kupanda miche ya Mikorosho sasa yatakuwa yanamilikiwa na wanajamii wa maeneo husika ambao wamekuwa katika mpango huo wa kunusuru kaya maskini

Nae mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga alisema kuwa Lengo kuu la mpango huo ni kuwafanya wanufaika hao kuondokana na umasikini Alisema ni wazi kuwa baada ya miaka kadhaa mikorosho hiyo itakapoanza kuzalisha wananchi hao hawatakuwa maskini tena

Akizungumza na wanufaika hao wa Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii TASSAF Mkuu wa Mkoa wa Lindi aliupongeza uongozi wa Halmashauri hiyo kwa mawazo mazuri ya kuanzisha kitega uchumi kikubwa ambacho kitakwenda kuwasaidia wananchi hao katika kujiongezea kipato pamoja na kuwapongeza wanufaika hao kuupokea mradi huo na kuutekeleza

Zambi alisema ni muhimu kwa halmashauri zote za mkoa huo kuiga mfano uliofanywa na Halmashauri hiyo huku akimuagiza katibu Tawala kuwaandikia Barua Wakurugenzi hao juu ya kutekeleza jambo hilo

Zambi alisema ifike mahala sasa fedha hizo zinazotolewa na Serikali ziwe zinaleta tija kwa wanufaika ikiwa pamoja na kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuinua uchumi wa wanajamii ambao wamekuwa katika Mpango huo.