Sunday, May 5, 2019

JUMAA AISHUKURU TAMISEMI, AISHAURI.

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, (kulia) akiwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Butamo Ndalahwa, wakikagua majengo hayo, Picha na Omary Mngindo.
...................................... 

Na Omary Mngindo, Mlandizi 


MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, ameishukuru Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa fedha kiasi cha sh. Bil. 1.5 zinazojenga hospitali ya wilaya. 


Jumaa ametoa shukrani hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea ujenzi wa hospitali hiyo, inayojengwa katika Kitongoji cha Disunyala, Kata ya Kilangalanga, akiambatana na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Butamo Ndalahwa ambapo amejionea maendeleo mazuri ya ujenzi huo. 


Aidha Jumaa ameishauri Wizara hiyo kwamba inapozipatia fedha halmashauri, basi iziache zijipangie wenyewe namna watavyojenga majengo, kulingana na eneo walilonalo, ikiwa wataweza kujenga ghorofa au majengo yatakayoendana na ardhi ya sehemu husika. 


"Mfano wa ushauri wangu nautolea hapa, hili eneo ni kubwa lakini kutokana na kujengwa majengo mbalimbali, hapa katikati imeachwa sehemu ambayo kimsingi haina faida, kwani haiwezi kutumika kwa ujenzi wowote, tungeachiwa tungejenga ghorofa ardhi kubwa ingebaki," alisema Jumaa. 


Aidha mbunge huyo ameridhishwa na kasi ya ujenzi, japokuwa kunajitokeza changamoto za hapa na pale, zinazochangia kusuasua kwa ujenzi huo unaoelekea ukingoni, huku akiwataka wanaosimamia kazi hiyo kuendelea na kazi ili ikamilike kwa wakati muafaka.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Butamo Ndalahwa aliwambia waandishi wa habari kwamba, wameitumia siku ya upandaji miti, ambapo katika eneo hilo amepanda miti 1,200 lengo ni kuweka mipaka ya eneo lenya eka 42. 


Akizungumzia ujenzi huo, Ndalahwa alisema kuwa baada ya serikali kuwapatia kiasi cha sh. Bil. 1.5 za ujenzi wa majengo matano ya awali, tayari wameshapaua maabara, chumba cha mionzi wakati duka la dawa wanasubiri vifaa maalumu vinavyotunzia ubaridi. 


"Majengo ya Utawala, wagonjwa wa nje, kufulia na wodi kwa ajili ya wazazi hayo tunataraji kuyapauwa wiki ijayo, juu ya changamoto za upatikanaji wa vifaa, tumeshaifanyiakazi kwa kuvileta eneo la tukio wiki moja kabla ya kuhitajika," alisema Ndalahwa. 


Mkurugenzi huyo alimalizia kwa kusemaa kwamba, kazi hiyo ya upauaji inataraji kumalizika kwa wakati ambapo mwezi huu wa tano itakuwa imekamilika, huku akiwashukuru mafundi na wasimamizi wa kazi hiyo kwa juhudi zao.
 
 MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, akitumia futi kamba kupima urefu wa ukuta wa moja ya majengo ya Hospitali ya wilaya ya Kibaha wakati alipotembelea kukagua ujenzi unavyoendelea.
    
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, akipima urefu wa dari ili umbali utakaofungwa feni katika moja ya majengo ya Hospitali ya wilaya ya Kibaha wakati alipotembelea kukagua ujenzi unavyoendelea.

Saturday, May 4, 2019

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUACHA KUSHABIKIA NDOA ZA JINSIA MOJA

 Na Ahmed Mahmoud Arusha

JESHI la polisi mkoa wa Arusha, limewataka wanahabari nchini kutokushabikia au kuunga mkono  ndoa za Jinsia moja ambazo ni vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu havikubaliki na ni kinyume cha maadili .


Rai hiyo imetolewa May 3 na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha Jonathan Shana, alipokuwa akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya vyombo vya habari Duniani lililoandaliwa na Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Arusha APC kwenye ukumbi wa hotel ya Golden rose ya jijini Arusha.


Amesema kuna harakati zinazoendelea Ulimwenguni za kutaka kuungwa mkono ndoa za jinsia moja ,wanahabari wasiunge mkono vitendo hivyo na badala yake waungane pamoja kupiga vita  hata kama tutatengwa na Jumuia za kimataifa  vitendo hivyo ni kinyume cha maadili.


Amewataka wanahabari kutambua kuwa hakuna uhuru usio kuwa na mipaka hivyo akawataka wazingatia uzalendo katika kazi zao ili kuhakikisha habari zinazoandikwa zisiwe zinachafua nchi  au mkoa na Uhuru uliopo utumike  kuwalinda wanahabari wenyewe na watu wengine.


Amesema lipo tatizo  la watoto  kubakwa na kulawitiwa mkoani Arusha na wazazi huwa wanayamaliza kienyeji kwa kupitia vikao amesema anaomba wanahabari na wananchi kuwafichua watu wa aina hiyo na jeshi la polisi limewasha moto wa  kupambana na vitendo vyote vya ukatili huo.


Amewahakikishia  ulinzi wa wanahabari wanaokumbana na madhira wakati wa kutekeleza majukumu yao na kuwalinda dhidi ya vitendo vyote vya uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa haki za binadamu  ikiwemo wakati wa chaguzi za serikali za mitaa zitakazofanyika nchini kote mwaka huu.


Amewataka wanahabari kutokukubaliwa kutumiwa na watu wenye nia mbaya kuvuruga amani ya nchi na kusisitiza kuwa Arusha ni Geneva ya Afrika na anataka ibakie kuwa Geneva ya kweli kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele katika kutimiza majukumu yao ya kila siku .


Awali mwenyekiti wa APC,Claud Gwandu, amesema kwa siku za karibuni kumekuwepo na migogoro kati ya wanahabari na serikali na vyombo vyake hali ambayo inaondoa uhusiano uliokuwepo na badala yake kujenga chuki .


Amesema haoni sababu ya kugombana kati ya wanahabari na serikali na vyombo vyake,na matokeo yake ni wanahabari kukamatwa na vyombo vya dola na hivyo kuibua migogoro ambayo haina ulazima.


Kauli mbiu ya mwaka huu inasema Jukumu la UTPC na Klabu za waandishi  wa habari  kuchangia uchaguzi huru na haki .

BAGAMOYO WAICHANGIA YANGA ZAIDI YA LAKI SABA

Muweka hazina wa Yanga Tawi la Bagamoyo, Hanga january (katikati) akiweka kumbukumbu sawa walipokuwa wakijumlisha kiasi cha fedha zilizokusanywa kwenye harambee ya kuichangia yanga kwa wilaya ya Bagamoyo, harambee hiyo imefanyika leo Mei 04, 2019 katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuBa) kushoto ni Mjumbe wa uhamisishaji na Mwenyekiti wa usafiri, Mwanahamisi Kondo

  .......................................
 
Harambee ya kuchangia timu ya Yanga wilayani Bagamoyo imefanyika leo Mei 04, 2019 katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuBa) na kufanikiwa kupata kiasi cha shilingi laki saba na elfu themanini 780,000/= ikiwa pesa taslimu pamoja na ahadi.


Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG, Muweka hazina wa Yanga Tawi la Bagamoyo, Hanga january alisema fedha taslimu zimefikia shilingi laki tano na kiasi kilichobaki ni ahadi ambapo jumla ni laki saba na themanini.


Hanga alisema licha makusanyo hayo wilaya ya Bagamoyo imepokea kadi sita zilizoandaliwa maalum kwaajili ya kuchangia Yanga ambapo kila kadi moja ina thamani ya shilingi milioni moja na kwamba tayari kadi hizo zimechukuliwa na matawi ya Bagamoyo kwaajili ya kuwasilisha kiasi hicho cha fedha.


Alifafanua kuwa, Tawi la Lugoba wamechukua kadi moja, Matimbwa na Yombo kadi moja, Msata kadi moja huku mdau mmoja akiahidi kuongeza laki tano na itapatikana milioni moja na laki tano kutoka Msata.


Matawi mengine yaliyochukua kadi hizo ni Kerege, Zinga na Mapinga kwa pamoja wakichukua kadi moja huku Tawi Bagamoyo mjini likichukua kadi mbili.

 Viongozi wa Yanga Bagamoyo wakiwa meza kuu kwaajili ya kuendesha zoezi la Harambee ya  kuichangia yanga, harambee hiyo imefanyika leo Mei 04, 2019 katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuBa)
Muweka hazina wa Yanga Tawi la Bagamoyo, Hanga january, akiweka sawa kumbukumbu za mahesabu wakati wa harambee ya kuichangia timu ya Yanga, harambee hiyo imefanyika leo Mei 04, 2019 katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuBa)