Friday, April 5, 2019

NAIBU WAZIRI MGUMBA AIALIKA KAMPUNI YA MBOLEA (OCP) KUTOKA MOROCCO KUJENGA KIWANDA CHA MBOLEA NCHINI

 Naibu Waziri Kilimo Omary Mgumba akiwa pamoja na Mgeni wake Makamu wa Rais wa Kampuni ya OCP Afrika Mashariki, Bwana Faysal Benameur (Kulia kwake) pamoja na Watendaji wa Kampuni ya OCP Barani Afrika na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara ya Kilimo mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wao, Jijini Dodoma, jana Aprili 04, 2019.
...................................


Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe. Omary Mgumba amewaeleza Wawekezaji kutoka nchini Moroco ambao ni Kampuni ya Mbolea ya Taifa (OCP) ya nchini kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi za kuendeleza kilimo na amewahakikishia kuwa Serikali itahakikisha inawasaidia ili wafanikishe azma yao ya kujenga kiwanda cha mbolea mkoani Lindi katika wilya ya Kilwa.


Naibu Waziri Mgumba akiwa pamoja na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya kilimo Jijini Dodoma amemwambia Makamu wa Rais wa Kampuni ya OCP Afrika Mashariki, Bwana Faysal Benameur mapema leo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kumwinua Mkulima wa Tanzania ambapo mkazo umewekwa katika kuongeza uzalishaji na tija kwenye mazao ya chakula na biashara na kwamba ujenzi wa Kiwanda cha mbolea nchini utachochea katika ongezeko la uzalishaji na tija.


Waziri Mgumba amesema nchi zote zilizoendelea, zimepiga hatua kubwa katika Sekta ya Kilimo kwa kuwa zinazingatia matumizi makubwa ya mbolea yanaenda sambamba na eneo la uzalishaji pamoja na kutibu hitaji la mapungufu ya virutubisho vilivyo kwenye udongo na si ilimradi kutumia mbolea tu.


Naibu Waziri wa Kilimo Mgumba ameongeza kuwa uwiano wa matumizi ya mbolea na eneo la kilimo hapa nchini upo chini sana, ukilinganisha na nchi za Afrika na zile zilizoendelea, akitoa mfano amesema, hapa Tanzania, matumizi ya mbolea ni kilo 20 kwa hekta, Ethiopia na nchi nyengine za Afrika ni kilo 100 kwa hekta wakati nchini Marekani na nchi nyingine, zilizoendelea matumizi yao ya mbolea ni kilo 1,000 (Sawa tani 1) kwa hekta.


“Kwa uwiano huu, hatuwezi kuzalisha kwa kiwango kikubwa na ndiyo maana tija ipo chini, nitoe mfano, kwenye uzalishaji wa mahindi, Tanzania tunazalisha tani mbili (2) kwa hekta huku Ethiopia ikizalisha tani sita (6) kwa hekta wakati Marekani, wanazalisha tani kumi (10) hadi kumi na mbili (12). Amekaririwa Mhe. Mgumba.


“Napenda Wakulima wa Tanzania wafahamu kuwa suala la muhimu si kutumia tu mbolea, lazima tujenge mazingira mazuri ya kufahamu mahitaji halisi ya virutubisho vinavyokosekana kwenye udongo, ardhi yetu imelimwa na mababu na mababu, na wazazi wetu, na wao wameshafariki, hatutaweza kuzalisha kwa tija bila kutumia mbolea”. Amesisitiza Naibu Waziri Mgumba.


“Nawapongeza Kampuni ya OCP kwa kuliona jambo hilo na huo ndiyo msimamo wao na watatusaidia kwa kuwa wanavifaa vya kufanya tathmini ya udongo kabla ya kuwauzia Wakulima mbolea.” Amekaririwa Mhe. Mgumba.


Naye Meneja wa Kampuni ya Mbolea ya OCP (Tanzania) Dkt. Mshindo Msolla amesema Kampuni hiyo inataraji kujenga Vituo vya kufanya majaribio ya kuonyesha namna zoezi la upimaji wa udongo linavyofanyika, matokeo baada ya kupima na matumizi ya mbolea za OCP kulingana na matokeo ya taarifa hizo na kuongeza kuwa tarehe 8 Aprili wanataraji kuzindua Kituo kimoja Mkoani Songwe.


Waziri Mgumba amesisitiza kuwa Vituo (Ward Resources Centre) kama hivyo vinapaswa kujengwa katika ngazi ya Tarafa ambapo Serikali ilishajenga vituo hivyo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Kwanza (ASDP I) na kuongeza sasa ni wakati muhafaka wa kuviendeleza.


Kampuni ya Mbolea ya OCP ipo katika mazungumzo ya kujenga kiwanda cha mbolea katika mkoa wa Lindi Wilaya ya Kilwa ambapo jumla ya dola bilioni 1.7 zinataraji kuwekezwa katika mradi huo mkubwa ambapo kwa kuanzia Kampuni ya OCP imeanza kujenga mashine ya kuchanganya virutubisho vya madini mbalimbali ili kupata mbolea za iana tofauti hapa nchini.


Imeelezwa kuwa ujenzi wa Kiwanda hicho cha mbolea utasaidia kupunguza gharama ya bei ya mbolea kwa zaidi ya asilimia 30 hadi 40.
 

Naibu Waziri Omary Mgumba akiwa pamoja Meneja wa Kampuni ya OCP Tanzania, Dkt. Mshindo Msolla katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya kilimo Jijini Dodoma, jana tarehe 4/4/2019.

Naibu Waziri Omary Mgumba akiwa pamoja Mgeni wake Makamu wa Rais wa Kampuni ya OCP Afrika Mashariki, Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara ya Kilimo pamoja na Watendaji wa Kampuni ya OCP Barani Afrika katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya kilimo Jijini Dodoma.

NYUMBA 20 ZA POLISI ZAJENGWA PWANI.

 Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo akijadiliana jambo na kamanda wa polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)  Wankyo Nyigesa.
............................


NA MWAMVUA MWINYI, PWANI

ASKARI wa jeshi la polisi mkoani Pwani, wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa makazi ya kuishi, hali inayosababisha kushindwa kuwahi wakati wakihitajika haraka katika dharula za majukumu yao ya kikazi.


Kutokana na hali hiyo, kwasasa jeshi hilo linajenga nyumba 20 za makazi ya askari polisi hao, zitakazogharimu milioni 500 ili kukabiliana na hali hiyo.


Akizungumza wakati alipotembelea ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa Kibaha Mjini, Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alitaka ujenzi huo ,ukamilike ifikapo June 30 mwaka huu, kama Amiri jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ,Dkt. John Magufuli alivyoelekeza.


Alisema ,askari wanapaswa kulinda mali za wananchi na kulinda usalama wa raia hivyo wanatakiwa waishi kwenye mazingira yaliyo bora.


“Kanda maalum ya kipolisi Rufiji imepatiwa milioni 500, pamoja na jeshi la polisi Pwani milioni 500, jumla ni Bilioni moja, ambazo zimetolewa na serikali kuhakikisha askari wanajengewa makazi ya kuishi “


“Hivyo ni wajibu wa jamii, wenye viwanda kushirikiana na serikali na jeshi la polisi kujenga mazingira bora ya askari hawa waweze kutulinda kwa moyo na upendo “alifafanua Ndikilo.

  
Awali akitoa taarifa fupi kwa mkuu wa mkoa huyo juu ya ujenzi unavyoendelea, Kamanda wa polisi Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa, alibainisha, kutokana na ufinyu wa bajeti wamepewa milioni 500 na kwa wastani kila nyumba itagharimu milioni 25 mpaka kukamilika kwake.


Aliwashukuru wadau waliojitokeza kusaidia akiwemo Said Salim Bakhresa, jeshi la wananchi wa Tanzania kupitia kikosi cha usafirishaji (KJ 95) ambao waliwapatia lowbed kwa ajili ya kubeba buldoza kutoka bakhresa sugar company huko Bagamoyo.


Wengine ni Chila mkurugenzi wa Creative Intertraders ltd ambae ametoa mifuko 100 ya saruji na Twyford Ceramics (KEDA )ya Chalinze na wengine ambapo amewashukuru na kuomba wadau wengine waendelee kuwashika mkono.


Mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa ambayo , Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Magufuli akiwa anazindua nyumba za askari polisi mkoani Arusha ,april 7 mwaka 2018, alitoa maelekezo kwa mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP) kwamba atatoa fedha kwa ajili ya makazi ya askari ,ambapo mkoa huo umeanza utekelezaji baada ya kupokea fungu hilo.
 
Kamanda wa polisi Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa, akimuonyesha Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, hali ya ujenzi inavyoendelea.
 
 Muonekano wa kazi ya ujenzi wa nyumba 20 za makazi ya askari polisi unavyoendelea Kibaha Mkoani Pwani.