Sunday, March 24, 2019

MSAKO KWA WAGANGA WA KIENYEJI SUMBAWANGA.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alipokuwa akiongea na wananchi wa mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite Sumbawanga mjini.
.................................


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Mathias Nyangi kuhakikisha anafanya msako wa waganga wa kienyeji katika mkoa na kuwakamata wale wote wanaofanya uganga wa kienyeji bila ya kuwa na leseni halali za kuwaruhusu kufanya shughuli hizo.


Ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza vilio vya wananchi wakati wa mkutano ulifanyika mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga, wananchi waliokuwa wakiomboleza vifo vya watoto wawili na mmoja kubaki mahututi katika hospitali ya rufaa ya mkoa baada ya mganga wa kienyeji kuwateka na kuwaficha katika gari lake chakavu tangu watoto hao kupotea tarehe 21.3.2019 na wawili kupatikana wakiwa wamefariki tarehe 23.3.2019 baada ya mmoja aliyepona kutoroka na kuwajulisha wananchi kilichotokea.


Amesema kuwa msako huo wa waganga wa kienyeji ufanyike katika wilaya zote tatu za mkoa ili kuwahakikishia wananchi amani na utulivu ambayo imekuwepo kwa miaka yote na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha wanawafagia waganga hao wanaonyesha dalili za kuvuruga utulivu uliopo katika mkoa.


“RPC fanya Operesheni kali ya waganga wa Kienyeji ndani ya Mkoa huu, wale ambao wana leseni tutajua hukohuko kwamba huyu ana leseni n ani halai au siyo halali na kama sio halali basi huyo ni halali yako, na kama kuna mganga wa kienyeji asiye na leseni, huyo ndio kabisa halali yako zaidi, kuanzia sasa hivi bonde la ziwa Rukwa kule Nkasi, Kalambo, Sumbawanga yenyewe hapa kote, opresheni ipite ya kamatakamata waganga wa kienyeji, tumechoka,” Alisisitiza.


Wakati wakitoa malalamiko yao kwa mkuu huyo wa mkoa, wananchi hao walisema kuwa vifo vya watoto hao vinahusishwa na Imani za kishirikina ambapo kumekuwa na wimbi la vijana wanaoonekana wakila, wakinywa na kuvaa vizuri bila ya kujulikana shughuli zao maalum wanazofanya jambo mbalo limekuwa likiwaumiza kichwa wananchi hao na kukosa majibu.


Mmoja wa wananchi hao Debora Maenge alisema 
“Nasikitika kwa tukio hili lililotokea mtaa wa Vuta, huyu mtu tunaishi nae jirani sana, tunajua ni mtu mwema, kumbe ni mtu ambae sio mwema na hafai kabisa katika jamii, cha kushanga alikuwa na vibali ambavyo alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ni mganga wa jadi, vibali hivi vinatolewa serikalini, Je serikali yetu mtaendelea kutoa vibali hivi ili watu waendelee kuuawa kiasi hiki? serikali angalieni mnapotoa vibali je ni waganga Kweli?” Aliuliza.


Mh. Wangabo alitembelea eneo la nyumba ya mganga huyo wa kienyeji ambayo gari alilowafichia watoto ilikuwamo na kukuta nyumba hiyo ikiwa imevunjwa na gari la mganga huyo kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali.


Watuhumiwa James Kapyela (52) pamoja na mtoto wake Michael Martin (14) wa tukio hilo la mauaji ya watoto Nicolous Mwambage (7) pamoja na Emanuel Juma (4) hivi sasa wanashikiliwa na polisi huku uchunguzi wa awali ukionyesha watoto hao walifariki kwa kukosa hewa baada ya kufungiwa ndani ya gari chakavu aina ya Chaser Saloon iliyokuwa haitumiki na vioo vya gari hiyo kufungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akionyesha eneo katika nyumba iliyokuwa haijamalizika ambapo maiti za watoto hao zilipatikana baada ya kutupwa na mtuhumiwa James Kapyela ambae ni mganga wa kienyeji.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa pole kwa wazazi waliofiwa na watoto wao alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mara tu baada ya kupata taarifa ya vifo vya watoto wawili na mmoja kuwa mahututi baada ya kupatikana tangu kupotea kwao tarehe 21.3.2019.

Eneo la Nyumba ya mtuhumiwa ambaye ni Mganga wa Kienyeji wa mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite mjini Sumbawanga baada ya nyumba hiyo kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kubaini kuwa mganga huyo amesababisha vifo vya watoto wawili na mmoja kuwa mahututi.

ZAO LA MUHOGO SASA NI MALI KWA WAKULIMA.

Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata muhogo kilichopo katika kijijiji cha Mbalala Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani lindi.
...........................................................
 
NA HADIJA HASSAN, LINDI

WAKULIMA wa zao la Muhogo Nchini sasa kuwa na soko la uhakika katika Zao hilo baada ya kuzinduliwa kwa Kiwanda kikubwa na cha kisasa Cha kuchakata unga wa muhogo katika kijiji cha Mbalala  Halmashauri ya wilaya ya Lindi Mkoani Lindi.

Kiwanda hicho kimezinduliwa na Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa, Machi 22 mwaka huu 2019, katika kijijiji cha Mbalala Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani lindi

Akizindua kiwanda hiko Majaliwa alisema viwanda vinavyojengwa Nchini vitahitaji Muhogo mwingi zaidi na ili kutosheleza mahitaji ya viwanda hivyo  ni vyema kwa wakulima kuongeza kasi ya uzalishaji wa mihogo iliyo bora 

" Ni dhahiri kwamba wakulima wetu wa Muhogo wanapaswa kulima kitaalamu kwa lengo la kuongeza uzalishaji hivyo Wizara ya kilimo ihakikishe wakulima wetu wanapata utaalamu wa kilimo cha kisasa cha Muhogo" alisema Majaliwa

Hata hivyo Majaliwa alisema  licha ya kiwanda hicho Serikali imefanikiwa kupata soko la zao hilo Nchini china ambapo mpaka kufikia January 2019 jumla ya Kampuni 5 zinazojihusisha na biashara ya Muhogo zimetambulishwa Nchini 

Alisema hadi kufikia februari 2019 , kampuni ya Dar cantoni Ivestment imesafirisha tani 187 za Muhogo mkavu(Makopa) kwenda Nchini China na wanatarajia kusafirisha tani 2,060 ifikapo juni 2019

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo ya Cassava Starch Tanzania Coparation(CSCT) Christophe Gallen alisema kuwa kiwanda hicho cha muhogo kinauwezo wa kuzalisha unga wa muhogo tani 1 kwa saa na tani 6000 kwa mwaka na kimeajili wafanyakazi zaidi ya 400 ambapo kati ya hao asilimia 97 ya wafanyakazi ni Watanzania

Alisema pamoja kiwanda hicho Kampuni hiyo inatarajia kujenga  kiwanda kingine cha kusindika Wanga lengo likiwa ni kukuza Mazao yenye ubora wa hali ya juu katika mashamba Makubwa yenye ufanisi yatakayosimamiwa na CSTC pamoja na kusindika mazao yote katika kiwanda kilichopo eneo la karibu

Kwa upande wake, naibu waziri wa kilimo Omary Mkumba alisema kutokana na utabili wa hali ya Hewa kueleza kuwepo kwa Mvua Chache alitumia fulsa hiyo pia kuwataka wananchi kulima mazao ambayo yanastahimili ukame kama vile Mihogo, uwele na Mtama.
 
Muonekano wa kiwanda cha kuchakata muhogo kilichopo kijijiji cha Mbalala Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani lindi.



Friday, March 22, 2019

MAGAZETI YA LEO IJUMAA TAREHE 22.03.2019

re:






U

Thursday, March 21, 2019

Waziri Mkuu awaita Wananchi kushiriki mapambano dhdi ya ukatili wa Mwanamke na mtoto...




Imeelezwa kuwa Watoto wa kike ndio waathirika wakubwa wa ukatili wa ukeketaji na mimba za utotoni na ndoa kwa mujibu wa utafiti(TDHS)2015/16 ambao umeonesha kuwa asilimia 36 ya wanawake waliolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 15,  hivyo Kuna umuhimu wa wadau kuungana na kupata nguvu ya pamoja ili kukomesha ukatili wa Mwanamke na mtoto.



Hayo yamebainishwa na WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa Kongamano la kitaifa la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto jijini Dar es Salaam
 Majaliwa amesema Ili kukabiliana na ukatili huo, sasa ni wakati wa Serekali, Asasi za kiraia ,Mashirika, Halmashauri pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kuzitilia mkazo na kuzifanyia kazi tafiti mbalimbali zinazofanywa wadau kwa lengo la kuongeza nguvu katika vita vya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.



Aidha amesema kwa upande wa Serikali tayari imeshatoa mwongozo na utaratibu wa kuunda kamati za kushughulikia matukio hayo,lakini pia ameziagiza Halmashauri na mikoa zipange bajeti za kuimarisha kampeni za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.



Alisema mwongozo huo utatoa utaratibu wa usimamizi na ufuatiliaji  kuhusu uundwaji wa kamati mbalimbali za mfumo wa mawasiliano na uwasilishaji wa taarifa jambo litakalosaidia kuwezesha kampeni ya utoaji wa elimu kwa jamii dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto. 
 

Mhe Majaliwa ameongeza kuwa kutakuwa na kamati za kijinsia na ustawi wa wanawake na serikali Inaunga mkono na kutambua jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali  kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na ndoa za utotoni ikiongozwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa mtoto (CDF).


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la jukwaa la utu wa mtoto (CDF)Bw. Koshuma Mtengeti ameiomba serikali kutoa ushirikiano pamoja na kutenga bajeti ya kutosha katika kuendesha mikakati ya kupinga ukatili wa kinjisia nchini.

“Mwezi Mei mwaka 2018, mwalimu wa shule ya msingi hapa jijini Dar es Salaam alituhumiwa kuwadhalilisha kingono wanafunzi wake wanne wa kike wa darasa la saba kwa kuwageuza kuwa wake zake na kufanya nao ngono,”amesema Mtengeti.

Tunakushukuru sana Mh. Raisi John P. Magufuli kwa salamu zako kutoka kwa Waziri Mkuu, Mh. Kassim Majaliwa. Tumefarijika kujua kwamba uko nasi bega kwa bega katika kongamano hili la kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye amesema Suala la Ukatili dhidi ya Watoto na Wanawake ni nyanja pana, ni tatizo linalozikabili nchi zote Duniani ingawa viwango vya Ukataili hutofautiana.

Ripoti mbalimbali za haki za binadamu zimeweza kuonyesha kuna ongezeko kubwa la ukatili dhidi ya watoto kwa kipindi cha mwaka 2018 ukilinganishwa na mwaka 2017 nchini.

Aidha, kongamano hilo litatoa fursa kwa washiriki kudadavua ukubwa wa sura za ukatili yanayowasibu wanawake na watoto na litasaidia juhudi za kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia, kukabili na kuanzisha utaratibu wa kuboresha huduma kwa watoto na wanawake waathirika wa ukatili.