Sunday, March 17, 2019

LUGOLA AKAGUA NA KUPIMA ULEVI MADEREVA WA MABASI, MALORI MJINI MOROGORO.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola (kulia) akiangalia zoezi la upimaji wa kilevi kwa dereva wa basi la Kimbinyiko, Omary Sauli (katikati). Dereva huyo hakuwa na kilevi chochote na aliruhusiwa aendelee na safari yake
 ..........................................


Na Felix Mwagara, MOHA, Morogoro.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amefanya operesheni kubwa ya kukagua na kupima ulevi wa pombe kwa madeveva wa mabasi na malori mjini Morogoro, leo.


Lugola pia alizungumza na abiria wa mabasi hayo, pamoja na viongozi wa madereva waliopo stendi kuu ya mabasi Msamvu, mjini humo, ambapo walimwelezea kero mbalimbali zinazowakabili.


Ukaguzi wa mabasi na malori hayo ulifanyika barabara kuu itokayo Dodoma kuja Morogoro-Dar es Salaam ambapo Waziri huyo akiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo (RPC), Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa huo (RTO), alisimamisha vyombo hivyo vya moto vilivyokuwa vinaingia Mizani iliyopo eneo la Kihonda, nje kidogo ya Mji wa Morogoro.


Akizungumza na madereva, kondakta, wapiga debe na abiria mara baada ya kufanya ukaguzi huo, Lugola alisema ni wajibu wake kufanya hivyo katika hatua ya kupunguza kwa kasi ajali mbalimbali zinatokana kwa uzembe wa madereva nchini.


“Mimi ni Waziri wa vitendo, nikiagiza nataka nitekelezwe, na pia nikiahidi lazima nilifuatilie, niliwaambia nitakua nakuja kufanya ukaguzi muda wowote ambao hamuujui, na ninafanya hivi kwa lengo moja tu, kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa ikiwa ni hatua ya kumaliza kupunguza au kumaliza kabisa ajali za barabarani hapa nchini,” alisema Lugola.


Aliongeza kuwa, kwasasa ajali zimepungua nchini, hasa Mkoa wa Morogoro, kwasababu ya askari wa usalama barabarani kufanya kazi zao kiweledi, na pia madereva kufuata sheria za usalama barabarani.


Lugola aliwataka madereva nchini, kuacha uendeshaji wa mashindano, kuwa na leseni na pia kuhakikisha wanapokuwa barabarani wanakua makini kwasababu ya kuwabeba abiria au mizigo mbalimbali wanayoisafirisha sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi.


“Madereva wa mabasi na malori ambao nimefanikiwa kuwapima kilevi leo, ambao wasiopungua sita, sijawakuta na kilevi, wapo makini na hii inaleta nguvu na imani kuwa madereva wanaelewa na kuzingatia sheria za usalama barabarani, na pia ndani ya mabasi niliyokuwa nayakagua nimezungumza na abiria wakaniambia madereva wanaendesha vizuri na pia niliwakuta wamevaa mikanda, naamini safari yetu ya kuondoa ajali za barabarani tunazidi kufanikiwa,” alisema Lugola.


Wakizungumza kwa wakati tofauti katika stendi kuu ya mabasi, madereva walilipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, kwa usimamizi mzuri ambao umewaunganisha na kuwafanya waifurahie kazi wanayoifanya.


Dereva Juma Rashidi wa basi linalosafiri kutoka Ifakara kuja Morogoro, alisema wanajisikia furaha kubwa kwa uongozi mpya wa Jeshi la Polisi ulioletwa Mkoani Morogoro hivi karibuni. 


“Naomba niseme ukweli, RPC na RTO hakika wanatuongoza vizuri, hakuna kero za ajabu kama zamani, tupo huru kufanya kazi zetu, hii inaonyesha viongozi hawa wanataka tufanye kazi ili tuweze kupata riziki zetu kwa njia halali bila usumbufu wa kusumbuana kama ulivyokuwa siku za nyuma,” alisema Rashidi.


Lugola alifanya ziara katika kituo hicho, na baadaye kutoka nje ya kituo hicho kuyakagua mabasi na malori, mara baada ya kumaliza ziara yake aliyoifanya Wilayani Kilosa ya kutatua migogoro ya ardhi ya wananchi wa Tarafa ya Kimamba wilayani humo, juzi.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akiwauliza maswali abiria wa basi la Kimbinyiko kuhusiana na mwendokasi wa dereva wa basi hilo, na pia kuwapa elimu kuhusiana na kujua haki zao wanapokuwa safarini. Abiria hao walimweleza Waziri huyo dereva huyo yupo makini na pia walimshukuru kwa kufanya ukaguzi kwa mabasi mbalimbali nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akitoka ndani ya basi la Kimbinyiko kufanya ukaguzi na kuzungumza na abiria wa basi hilo, mjini Morogoro, leo. Abiria hao walimweleza Waziri huyo dereva huyo wa basi hilo yupo makini na pia walimshukuru kwa kufanya ukaguzi kwa mabasi mbalimbali nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola (wapili kulia) akiwa ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu, mjini Morogoro, wakati alipokuwa anafanya ukaguzi na kupima kilevi kwa madereva wa mabasi kituoni hapo pamoja na wa malori katika barabara ya Morogoro-Dodoma. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola (kushoto) akizungumza na madereva wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu, Mjini Morogoro, leo, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kituo hapo kwa ajili ya kukagua na kupima kilevi kwa madereva wa mabasi kituoni hapo. Pia Lugola aliwapima madereva wa malori barabara kuu ya Morogoro Dodoma. Wapili kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

KAMATI YA BUNGE YATAKA MALIPO YA KOROSHO YALIYOBAKI YAHARAKISHWE.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Kamati ya kudumu ya Bunge , kilimo, mifungo na Maji imeishauri serikali kuharakisha mchakato wa kuwalipa wakulima wa korosho waliosalia baada ya kumalizika zoezi la uhakiki febduari 15 mwaka huu ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza


Kauli ya kamati hiyo ya bunge imetolewa jana katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kilichowakutanisha , wakulima kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara, Waziri na Naibu Waziri wa kilimo, Wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa idara kilimo, Mifugo Uvuvi na Maji


Kauli ya kamati hiyo imekuja baada ya kuibuka maswali kutoka kwa wakulima ya kutaka kujua ni lini Serikali itawalipa wakulima hao baada ya kumalizika kwa uhakiki wa zao hilo


Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo mbunge wa  viti maalumu  Mkoa wa Ruvuma Sikudhani Chikambo alisema kuwa kitendo cha Serikali kuchukuwa muda mrefu bila ya kuwalipa wakulima kunaweza kuzua migogoro baina ya wakulima na Serikali na hata kupelekea Wananchi  kukosa imani na Serikali yao


“ilipotoka kauli ya Rais ya kutaka kununua korosho zote kwa sh.3300 bila shaka ilikuwa na nia mzuri ya kuwasaidia wakulima ila mashaka yangu juu ya jambo lile inawezekana tumeshindwa katika utekelezaji wa zoezi wakati linafanyika na hiyo ndio inayosababisha zoezi hili kuchukuwa muda mrefu”


Kauli hiyo ya chikambo iliugwa mkono pia na Mbunge wa viti maalumu wa Mkoa wa Dar-es-salaam Lucy mageseli ambapo alisema kuwa hakuona sababu ya wakulima hao kucheleweshewa fedha zao kwa kuwa Serikali ilishasema kuwa inafedha za kutosha kuwalipa wakulima  ambapo alimtaka Waziri wa Kilimo wakati akijibu maswali ya wakulima hao awahakikishie kama fedha za kuwalipa wakulima hao zipo ama laa


“Mimi nashangaa hili swala la uhakiki limetokea wapi? Kwanini misimu iliyopita haukufanyika? Au kwa sababu msimu huu Serikali ndio imenunua na kama mlisema tayari fedha mnazo za kutosha kuwalipa wakulima wote kwanini mnachelewa kuwalipa? mimi nadhani labda mnavutamuda ili kutafuta hiyo fedha ya  kuwalipa wakulima” Alisema Mgeseli


Nae mbunge wa Shauri moyo Zanzibar Maftar Salim alitumia fulsa hiyo kuishauri Serikali  kuanza maadalizi ya uhakiki kwa wakulima hao mapema wakati wa kuelekea msimu ujao wa kilimo 2019/2020 ili kuepuka usumbufu uliojitokeza kwa msimu huu


Wakiongea kwa masikitiko makubwa mbele ya kamati hiyo ya bunge iliyoambatana na waziri wa kilimo, wamesema kwa kuwa uhakiki umeshakamilika ni vyema wakaharakisha malipo yao kwani muda wa kuanza maandalizi ya msimu ujao umeshafika ili wafanye mapema 


Nae  Issa  Mkombwe kutoka chama cha msingi Rutamba alisema kuwa kama wakulima wakubwa wa zao hilo changamoto kubwa wanayokumbana nayo kwa wakati huu ambao wanasubiri malipo wengi wao wanaishi kwa  hofu ya kutaifishwa mali zao kutokana na kuchelewa kwa marejesho ya mikopo yao katika taasisi mbali mbali za kifedha lakini hata kwa vibarua wadogo wadogo ambao waliwatuma kupalilia mikorosho yao pamoja na wakati wa kuokota korosho  ambapo walitakiwa kulipwa baada ya kupata fedha hizo


“ kabla ya kuingia katika dhahama hii mimi sikuwahi kuugua presha lakini toka mwezi januari nimegundulika nina presha ya kushuka kama unataka waziri hata vyeti ninavyo hii ni kutokana na mawazo niliyonayo kwanza nadaiwa kiasi kikubwa na Bank na deni hilo linazidi kukua siku hadi siku, lakini mbaya zaidi nanyimika raha usiku silali vizuri kila siku hodihodi za wale vibalua walionisaidia kuokota korosho wakitaka niwalipe ela zao mimi nazitoa wapi? Mtatuuwa wenzenu” alisema mzee huyo


Kufuatia hatua hiyo waziri wa kilimo Japhet Hasunga ameahidi kuwalipa wakulima hao waliosalia huku akiwapa wiki mbili bodi ya mazao mchanganyiko pamoja na benki ya maendeleo ya kilimo TADB  kuhakikisha malipo hayo yanakamilika kwa wakati