Thursday, March 14, 2019

RAIS MAGUFULI “AMTOA” MWANANCHI ALIYEBAMBIKIWA KESI YA MAUAJI NA POLISI

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw.Biswalo Mganga akisoma moja ya nakala ya mashtaka  wakati akizungumzia malalamiko ya Musa Adam Sadiki ya kubambikiziwa kesi ya mauaji katika mahakama ya Tabora. Kulia kwake ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.Edson Makallo na Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari-MAELEZO Bi.Zamaradi Kawawa. 
.......................................


BARUA ya wazi aliyoandikiwa Rais Dk. John Magufuli kupitia gazetini na mwananchi aliyebambikiziwa kesi ya mauaji imewezesha kuachiwa huru kwa mwananchi huyo huku Rais akiagiza hatua zaidi zichukuliwe kwa waliohusika kwenye tukio hilo linaloichafua serikali.


Mwananchi huyo Mussa Sadiki, aliandika barua ya wazi kwa rais Machi sita mwaka huu, akilalamikia kubambikiziwa kesi ya mauaji namba 8/2018 katika Mahakama ya Tabora baada ya kukamatwa na polisi ambapo baada ya rais kuisoma aliiagiza Ofisi ya Mwendesha Mashataka Mkuu wa Serikali, kuchunguza swala hilo ili kubaini ukweli.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mwendesha Mashataka Mkuu wa Serikali (DPP), Biswalo Mganga, amesema kuwa  baada ya mwananchi huyo kukamatwa, polisi walimnyang’anya sh. 778,000, simu ya mkononi na mali alizokuwa amenunua kwa ajili ya wakulima wakati akienda kwenye manunuzi.


“Kwa mujibu ya malalamiko yake aliyoyaandika gazetini, baada ya kukamatwa aliwekwa kwenye Kituo cha Polisi Tabora Mjini na kubambikizwa kesi ya kuvunja na kuiba ambapo alikaa kituoni kwa muda wa juma moja na alipopelekwa mahakamani alisomewa shtaka la mauaji,” alieleza.


DPP amefafanua  kuwa, baada ya Rais Dk. Magufuli kusoma barua hiyo, aliagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ifuatilie malalamiko ya mwananchi huyo haraka ili kujua ukweli.


Aidha amesema kuwa Ofisi ya DPP ilifuatilia suala hilo kwa kufanya mahojiano na mlalamikaji pamoja na kupitia nyaraka zilizopo katika kituo cha Polisi Tabora Mjini zinazohusiana na sakata hilo.


“Katika kufuatilia malalamiko hayo, ofisi ya DPP imebaini malalamiko hayo ni ya kweli. Hii ni kwa sababu kitabu cha kuzuia wahalifu (detention register) kilichopo katika kituo hicho cha polisi, kinaonyesha kuwa mwananchi huyo alikamatwa Juni 21 mwaka jana kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba na aliingizwa mahabusu ya polisi saa tisa alasiri.


Hata hivyo amaesema kuwa  kitabu hicho kinaonyesha kuwa Juni 29 mwaka jana, mlalamikaji alitolewa mahabusu saa mbili asubuhi na kupelekwa mahakamani.


Mwendesha Mashtaka Mkuu alieleza kuwa, tarehe hiyo hiyo mwananchi huyo alifunguliwa kesi ya mauaji namba 8/2018 ikionyesha Mei sita mwaka jana katika barabara ya Kazima Tabora Mjini, alimuua Jackson Thomas.


Ameeleza  kuwa wakati wa kufuatilia malalamiko hayo, ofisi ya DPP ilibaini Julai mosi mwaka jana, alikamatwa Edward Matiku kwa makosa ya kuvunja nyumba usiku na kuiba lakini Julai 16 mwaka jana, naye aliunganishwa katika shauri la mauaji namba 8/2018 kuhusika na mauaji ya Jackson Thomas.


“Baada ya kuyabaini hayo, Machi nane mwaka huu, niliwafutia washtakiwa wote wawili mashtaka hayo na mahakama ikawaachia huru.


DPP  ameeleza kuwa baada ya Rais Dk. Magufuli kupokea ukweli wa malalamiko hayo na hatua zilizochukuliwa, anampongeza Mussa Sadiki kwa ujasiri aliouonyesha kwa kuweka wazi malalamiko yake.


Aidha amesema kuwa Rais anavishauri vyombo vingine vya habari kuchunguza na kuchapisha habari zenye ukweli kwa kuzingatia maslahi ya taifa.


“Mheshimiwa Rais ameagiza hatua zaidi zichukuliwe kwa wote waliohusika na tukio hilo kwa lengo la kukomesha tabia kama hizo zinazoichafua serikali kwa wananchi wake na dunia nzima,” amesisitiza
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw.Biswalo Mganga akisikiliza maswali kutoka kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari juu ya malalamiko ya Musa Adam Sadiki ya  kubambikiziwa kesi ya mauaji katika mahakama ya Tabora. Kulia kwake ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.Edson Makallo na Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari-MAELEZO Bi.Zamaradi Kawawa.

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw.Biswalo Mganga akizungumza na waandishi wa habari juu ya malalamiko ya Musa Adam Sadiki ya  kubambikiziwa kesi ya mauaji katika mahakama ya Tabora.Kulia kwake ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.Edson Makallo na Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari-MAELEZO Bi.Zamaradi Kawawa.

MIGOGORO YA ARDHI YAMRUDISHA WAZIRI LUGOLA MKOANI MOROGORO

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugolawa Mamb
………………………………………

Na Felix Mwagara, MOHA.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelazimika kuwasili kwa mara nyingine Mkoani Morogoro leo, kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi ambayo imeibua mifarakano baina ya wananchi Mkoani humo.


Waziri Lugola, wiki iliyopita alimaliza ziara yake Mkoani humo iliyokuwa na lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi kuhusiana na utendaji kazi wa Taasisi za Wizara yake.


Lugola katika ziara yake Mkoani humo, alifanya mikutano ya hadhara ambapo alikutana na migogoro mbalimbali lakini kero kubwa kati ya hizo ni kuhusiana na ardhi ambayo inapelekea wananchi kuwekeana chuki, kujeruhiana, kufikishana Polisi pamoja na kuuana.


Kati ya Wilaya tatu alizozitembelea alipokuwa Mkoani humo, ni Morogoro, Mvomero na Kilosa, licha ya wananchi kutoa kero zao mbalimbali, mgogoro wa ardhi uliibuka kwa sehemu kubwa hasa katika Wilaya ya KIlosa.


Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Waziri Lugola alisema alipokuwa Wilaya ya Kilosa, alikutana na mgogoro wa ardhi ambapo umeleta mgawanyiko miongoni mwananchi hivyo akawaahidi kurejea tena Wilayani humo kwa ajili ya kutatua kero zao baada ya kukutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.


Lugola alisema mipango yote ipo sawa, hivyo anatarajia kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kilosa Kesho Machi 15 Wilayani humo ili kuwapa majibu ya kero zao pamoja na kumaliza mgogoro wa ardhi unaowakabili.


“Migogoro mingi inaletwa vituo vya polisi hasa Wilaya ya Kilosa, na wananchi katika mikutano yangu ya hadhara wanalalamika kuhusiana na ardhi, baadhi wanawalaumu polisi wangu kutokuwatendea haki na wengine pia wanawapongeza kwa kazi nzuri, na wengi wao wanalalamikia kuwa matajiri ndio wananyang’anya ardhi zao wakitumia fedha kwa wakiwahonga Polisi,” alisema Lugola.


Aliongeza kuwa, alipokuwa katika mkutano wake wa mwisho katika Tarafa ya Kimamba, Wilaya ya Kilosa Mkoani humo, kuliibuka na hoja nyingi za migogoro ya ardhi, kutokana na usugu wa tatizo hilo, aliwaahidi wananchi wa Wilaya hiyo atarejea tena kwa ajili ya kutatua mgogoro huo.


“Ziara yangu niliikatisha katika Mkoa huo, kwa ajili ya kwenda Dar es Salaam kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri, hata hivyo, niliwaahidi wananchi nitakutana na Waziri wa Ardhi, ili tushirikiane kutatua mgogoro huu ambao unaweza ukaleta vurugu kubwa pale Kilosa na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla,” alisema Lugola.


Lugola anatarajia kufanya mkutano mwingine wa hadhara kuleta majibu ya ahadi alizowaahidi wananchi hao pamoja na kusuluhisha mgogoro huo ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za maendeleo kama kawaida.


Waziri huyo alisema, hawezi kukaa ofisini huku wananchi wakiwa wanapata matatizo mitaani, hivyo atazunguka nchi nzima kuzungumza na wananchi na kupokea kero mbalimbali zinazowakabili.

  
“Wananchi wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii, na hakika Serikali ya Dokta Magufuli inawajali wananchi wake ndio mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso kwa uso,” Alisema Lugola.


Lugola alisema Taasisi zilizopo ndani ya Wizara yake ambazo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na Idara ya Probesheni na Huduma kwa Jamii, zifanye kazi za kiweledi bila kuwaonea wananchi.

Siku ya figo duniani:fanya mazoezi angalau nusu saa kwa siku, punguza matumizi ya Chumvi,kula matunda na mbogamboga kwa wingi.