Wednesday, January 9, 2019

UFAFANUZI WA TANGAZO KUHUSU USIMAMIZI KWA WATOA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA

Benki Kuu ya Tanzania imetoa tangazo kwa umma kupitia tovuti yake (www.bot.go.tz) likiwataka watu na taasisi zote zinazofanya biashara ya huduma ndogo za fedha zilizoko Tanzania Bara (isipokuwa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo – SACCOS) kutoa taarifa zitakazotumika katika utayarishaji wa Kanuni za Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha. Taarifa hizo zinatakiwa kutumwa Benki Kuu ya Tanzania hadi tarehe 31 Januari 2019.


Benki Kuu inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusu tangazo hilo:


1.   Lengo la tangazo hilo siyo kuvifunga au kuvibana vikundi vya kijamii kama VICOBA, watu binafsi na taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha kama ambavyo inapotoshwa na baadhi ya watu na mitandao mbalimbali ya kijamii, bali ni kukusanya taarifa za awali kuhusu huduma hizo. 


Kama ilivyoainishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kupitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, lengo la sheria hiyo  ni kuwalinda wadau wote wanaohusika na huduma hizi (watoaji na watumiaji) kwa kuziwekea utaratibu mzuri zaidi wa uwekaji kumbukumbu, uendeshaji na uongozi kwa ujumla. Pia kuwalinda wamiliki na watumiaji wa huduma hizi dhidi ya vitendo vinavyoweza kupelekea kupoteza fedha na mali zao, pamoja na kuzuia watu binafsi, taasisi na vikundi vya kijamii kutumika kufanya uhalifu ikiwemo utakasishaji fedha haramu.
  

2.   Benki Kuu inafahamu kuwa baadhi ya watu binafsi, taasisi na vikundi vinavyotoa huduma ndogo za fedha vikiwemo VICOBA, havina usajili rasmi na hivyo havitambuliki kisheria. Kwa kutambua hilo, Sheria imeweka kipindi cha mpito cha mwaka mmoja (kuanzia sheria itakapoanza kutumika rasmi) kwa wote wanaojihusisha na utoaji huduma ndogo za fedha, kujipanga ili wawe tayari kusimamiwa pale kanuni zitakapokuwa zimetolewa rasmi. Hivyo, katika kipindi hiki cha mpito, siyo kosa kwa watu binafsi, taasisi na vikundi vya kijamii kutokuwa na usajili rasmi.  


Aidha, Wadau wote watashirikishwa kikamilifu katika utayarishaji wa Kanuni hizo, na mara zitakapokuwa tayari na kutolewa na Benki Kuu ya Tanzania, maelezo zaidi kuhusu usajili yatatolewa.


Benki Kuu inawasihi wananchi wote kutokuwa na taharuki na inasisitiza kwamba uamuzi wa kusimamia watoa huduma ndogo za fedha umechukuliwa kwa nia njema na  kwa faida ya watumiaji na watoaji wa huduma hizi.


Aidha, Benki Kuu  inautahadharisha umma kujiepusha na taarifa na miongozo inayotolewa kiholela na watu, kampuni na mashirika ambayo yanajitangaza kufanya shughuli za uandikishaji wa watoa huduma ndogo za fedha kwa wananchi kwa niaba ya Serikali au Benki Kuu. 


Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu, kampuni au shirika lolote litakalojihusisha na vitendo vya kuwakanganya wananchi kwa lengo la kupotosha au/na kujipatia mapato haramu.


Tunawahamasisha wananchi kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tangazo hili zinazoendelea kutolewa na Benki Kuu katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha Tanzania Bara.


Kwa ufafanuzi/maelezo zaidi wasiliana nasi kwa simu   022-2235585/0767503145 au barua pepe: 



au tembelea Benki Kuu Makao Makuu Mtaa wa 2 Mirambo, 11884 Dar es Salaam Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha.

SERIKALI KUSAINI MIKATABA YA UBANGUAJI WA KOROSHO JANUARI 10

Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza mpango wa serikali kusaini mikataba ya ubanguaji wa korosho wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara,  leo tarehe 8 Januari 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
............................

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Serikali imesema kuwa tarehe 10 Januari 2019 itasaini mikataba na wamiliki wa viwanda vya ubanguaji wa korosho waliojitokeza kwa ajili ya kubangua korosho za serikali za msimu wa mwaka 2018/2019 zilizonunuliwa na serikali kwa bei ya Shilingi 3300 kwa kilo.

Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 8 Januari 2019 wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara.

Alisema kuwa hivi karibuni serikali ilitangaza kuwa korosho ghafi zote zitabanguliwa nchini hivyo utekelezaji wa jambo hilo umeanza, ambapo Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko itaingia mikataba ya ubanguaji.

Pamoja na wamiliki wa viwanda kupewa kazi ya kubangua korosho lakini pia serikali imewakaribisha wananchi kujitokeza kubangua korosho za serikali kupitia vikundi au mtu mmoja mmoja. “Wananchi wenye uwezo wa kubangua tunawaomba waende Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo-SIDO) kwa ajili ya kujiandikisha ambapo mpaka sasa watu 126 kwa ajili ya ubanguaji na Tani 29 zimechukuliwa kwa ajili


ya kuanza kubanguliwa” Alisisitiza Mhe Hasunga

Katika mkutano huo Waziri huyo wa kilimo Mhe Japhet Hasunga amempongeza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kushuhudia utiaji wa saini mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) wa Bilioni 21 zitakazoiwezesha NFRA kunua mahindi kwa wakulima hivyo kuimarisha soko la nafaka nchini.

Mhe. Hasunga alisema kuwa pamoja na kuanza ubanguaji kupitia SIDO lakini serikaliimeanza mchakato wa kukufua viwanda vya ubanguaji vya serikali na watu binafsi nchini ili kuongeza ajira kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya wabanguaji wadogo wadogo.

Akizungumzia kuhusu swala la malipo ya korosho na uhakiki wa wakulima alisema kuwa tayari kiasi cha korosho ambayo imekusanywa kwenye maghala makuu ni Tani 203,938.3 wakati korosho iliyopo kwenye Vyama vikuu vya ushirika ni Tani 29,803.53 inayofanya jumla ya korosho yote iliyopokelewa kwenye vyama vya ushirika na maghala makuu kuwa Tani 233,741.83 sawa na asilimia 84.7 ya lengo lililowekwa la ukusanyaji katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani.

Kuhusu malipo ya wakulima alisema kuwa miamala ya malipo ambayo imefanyika ni 261,458 yenye jumla ya watu 203,569.

Aidha, vyama 490 vilimelipwa kati ya vyama 617, Alisema


Mkoa wa Mtwara jumla ya vyama 39 bado havijalipwa, Mkoa wa Lindi vyama vitano na Ruvuma viwili hivyo serikali imejipanga ndani ya wiki mbili vyama hivyo kuwa vimelipwa.

Waziri Hasunga amesema kuwa mpaka kufikia jana tarehe 7 Januari 2019 fedha ambazo zimeingizwa kwenye Account za wakulima ni zaidi ya Bilioni 257 huku ambazo tayari zimeingia kwenye Account za wakulima ni Bilioni 226.2 ambapo Zaidi ya Bilioni 30.7 zilizohakikiwa bado hazijaingizwa kwenye Account za wakulima kutokana na taarifa za baadhi ya wakulima hao kutofautiana majina ama vinginevyo. “Tunawaomba sana wananchi kwenda Benki kujiridhisha kama Account zao zinafanya kazi kwani


serikali ina fedha za kuwalipa wakulima wote wa korosho” Alisema

“Tena nisisitize kwa wale wanaofanya biashara ya korosho kinyume na utaratibu maarufu kama (Kangomba) wajisalimishe na kuomba radhi wenyewe kuliko kusubiri serikali iwabaini” Alisema

Vilevile, Mhe Hasunga alisema kuwa wizara yake imeweka mikakati mbalimbali ambapo hadi kufikia Januari 31 mwaka huu zoezi la uhakiki wa wakulima wanaostahili kulipwa liwe limekamilika ambapo zaidi ya asilimia 80 ya wakulima wawe wamelipwa.

Pia amewataka wananchi kupuuza taarifa mbalimbali zizotolewa na baadhi ya wananchi wasiolitakia mema Taifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa serikali hailipi wakulima badala yake amesisitiza kuwa serikali ina fedha za kutosha kulipa wakulima wa korosho isipokuwa kangomba wao hawatalipwa.
 Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara,  leo tarehe 8 Januari 2019.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo akifatilia mkutano wa Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara,  leo tarehe 8 Januari 2019.