Monday, October 22, 2018

RC. TABORA APIGA MARUFUKU WATOTO WASIOSOMA DARASA LA AWALI KUANZA DARASA LA KWANZA.

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri.
 
NA TIGANYA VINCENT,RS TABORA.

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amewaagiza Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kuhakikisha hakuna mtoto anayeanza Darasa la Kwanza bila kuwa amepitia darasa la Awali.

Hatua hiyo inalenga kuondoa tatizo la kuwa na wanafunzi wanaoingia Darasa la Kwanza ambao hawajui kusoma, kuhesabu na kuandika.

Mwanri alitoa kauli hiyo hivi wakati akifungua mkutano wa kutathmini masuala ya elimu mkoani humo na kuhimiza walimu kuhakikisha wanaondoka tatizo la KKK shuleni kwao.

 “Msingi mzuri wa mtoto lazima uanzie elimu ya awali na ndio maana nasistiza kuwa mtoto asiingie la kwanza kama akupitia Chekechea …kule ndipo mtoto anapoandaliwa kuwa na maendeleo mazuri kitaaluma …ukikosea toka hapo basi mtoto anaweza kutokuwa na maendeleo mazuri darasani” alisema.

Alisema vitendo vya baadhi ya walimu kutozingatia hilo na kuchukua watoto ambao hawakupita elimu za awali ndiko kunakosababisha baadhi yao wanapofanya mitihani ya kujipama ya Darasa la Nne matokeo yao sio mazuri kwa sababu ya kuanza la kwanza hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Aidha Mwanri aliwapongeza walimu wa Shule za Awali na msingi kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuwatengenezaea msingi mzuri watoto hao ili wanapoendelea na masomo yao waweze kufanya vizuri.

Katika hatua nyingine amewataka wamiliki na walimu wa Shule za Awali kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri kwa watoto hao ili wapende kwenda shule.

Alisema maeneo hayo lazima yawe na vivutio wa michezo mbalimbali ya watoto wadogo ili pamoja na kujifunza wawe na muda wa kucheza kama sehemu ya burudani na elimu kwao.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora ametoa wito kwa wazazi na wadau wengine kuweka mazingira mazuri ambayo yatawavutia  walimu hasa wale ajira mpya kupenda kufanya kazi katika maeneo yao.

Alisema mazingira hayo ni pamoja na kuwawekea vivutio kama vile kuwapa maeneo ya kulima , nyumba za kuishi kama hakuna nyumba za shule na wakati mwingine kuwapa chakula cha kuanzia maisha.

Mwanri alisema kuna baadhi ya maeneo hapa nchini yamefanikiwa kielimu kutokana na wazazi kuweka vivutio ambavyo vimewafanya walimu wanaporipoti kutofikia kuhama katika shule walizopangiwa.

“Tujenge utamaduni wa kuweka motisha kwa walimu wetu…kwa mfano mnaposikia leo kuna mwalimu mpya anaripoti katika shule yetu , mnaweza kukusanyika na kumlaki ili ajiene kuwa amefika nyumbani na sio ugenini” alisema.


MAJINA YALIYOTANGAZWA NA TFF, WAJUMBE WAPYA KAMATI YA UCHAGUZI, NIDHAMU NA MAADILI.

Kamati ya Utendaji iliyokutana Jumamosi Oktoba 20,2018 Makao Makuu ya TFF Karume, Ilala ilipitia masuala mbalimbali ikiwemo kuchagua wajumbe wa kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Nidhamu na Rufaa Maadili.

Pia Kamati ya Utendaji imepitisha tarehe ya Mkutano Mkuu wa TFF wa mwaka ambao unatarajiwa kufanyika Jijini Arusha Disemba 29,2018
Mkutano huo unafanyika kwa mujibu wa Katiba ya TFF na umepata siku 60 za kutangazwa kabla ya kufanyika katika kikao hicho cha Kamati ya Utendaji kimepitisha mabadiliko madogo kwenye kamati ndogo ndogo za TFF.

Mabadiliko hayo yametokana na baadhi ya Wajumbe kujiuzulu na Wajumbe wengine kukabiliwa na majukumu mengi.

MABADILIKO YA KAMATI ZA  TFF YAPO HAPA CHINI
KAMATI YA UCHAGUZI.

1.MALANGWE ALLY -Mwenyekiti

2.Mh . MOHAMED MCHENGELA  -M/Kiti

3.BENJAMINI KARUME   –  Mjumbe

4.MOHAMED GOMBATI  –  Mjumbe

5/HAMISI ZAYUMBA  – Mjumbe

KAMATI YA NIDHAMU

1.KIOMONI  KIBAMBA – Mwenyekiti

2.PETER HELLA – M/Mkiti
 
3.KASSIM DAU – Mjumbe
 
4. HANDLEY MATWENGA – Mjumbe
 
5.  TWAHA MTENGERA – Mjumbe

KAMATI YA RUFAA MAADILI

1.RICHARD MBARUKU – Mwenyekiti

2.THADEUS KARUA  -M/Kiti

3.MH . MUSSA ZUNGU -Mjumbe

4.ASP BENEDICT NYAGABONA-Mjumbe

5.LUGANO HOSEA -Mjumbe

RIDHIWANI KIKWETE ASHIRIKI MAZISHI YA MSANII MASHAKA.

MBUNGE wa jimbo la chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete akiwa makaburini, akiungana na wasanii mbalimbali kumzika msanii Mashaka.

Na Shushu Joel, Dar.

MBUNGE wa jimbo la chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete ameungana na wasanii wa kada mbalimbali katika kumzika msanii maarufu wa maigizo nchini Ramadhani Ditopile aliyewai kuwa msanii wa kundi la sanaa la kaole.

Mashaka alifariki juzi asubui wakati akiwa anapata matibabu katika hospital ya Amana Ilala jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Ridhiwani alisema kuwa pengo la msanii huyo ni ngumu kuliziba kwa kipiondi hiki kutokana na jinsi alivyokuwa akifanya kazi zake kwa weredi.

“Mashaka alikuwa si msanii tu kwangu bali alikuwa ni mjomba wa mfano kwani alikuwa akinipatia ushauri mkubwa juu ya kazi zangu za siasa hivyo nimepoteza mtu wa muhimu sana kwangu”Alisema Ridhiwani.

Aliongeza kuwa anawapongeza wote waliofika katika kuhakikisha tunamzika ndugu yetu,kwani maziko ni wajibu wetu sote kwani ni ibada.

Aidha mbunge huyo alisema kuwa marehemu mashaka atakumbukwa kwa kupitia kipaji chake cha uigizaji ambapo katika uhai wake aliwai kutamba na kundi la kaole kupitia tamthilia za mambo hayo,kidedea,jumba la dhahabu na nyingine nyingi.

Kwa upande wake msanii maarufu wa uigizaji nchini Mzee chilo alisema kuwa Mashaka alikuwa ni mtu wa pekee katika tasinia ya kuigiza kutokana na kupenda kutumia kipaji chake kuwaelekeza wenzake pindi mnapokuwa katika kazi.

Aliongeza kuwa ni pengo kubwa katika fani yetu lakini kutokana na kuwa hapa duniani tunapita hakuna budi kumuombea kwa Mungu ili apumzike kwa amani.

Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu Abdallah Ditopile,baba yake aliugua ghafla usiku wa kuamkia juzi na kisha kupelekwa hospital ya Amana ambapo alilazwa kabla ya kufariki akiendelea kupatiwa matibabu.

Aidha alisema kuwa baba yake alizidiwa na kupewa rufaa ya kwenda mloganzila lakini wakiwa wanasubili gari ili waelekee huko baba alipoteza maisha”Alisema Abdalaah.

Aliongeza kuwa anawashukuru watnzania wote waliojitokeza kwenye makaburi ya kifamilia yaliyoko Tabata Kinyelezi kwa ajili ya kumzika baba sina la kuwalipa ila Mungu atawalipa kwa wema mliotufanyia wanafamilia.


DK.KAWAMBWA AWATOA HOFU WATAKAOPITIWA NA MRADI WA BARABARA YA MAKOFIA -MLANDIZI

MBUNGE wa jimbo la Bagamoyo, mkoani Pwani, Dk.Shukuru Kawambwa.
 
NA MWAMVUA MWINYI, BAGAMOYO.

MBUNGE wa jimbo la Bagamoyo, mkoani Pwani, Dk.Shukuru Kawambwa, amewatoa hofu wananchi watakaopaswa kupisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Makofia -Mlandizi kwa kiwango cha lami kuwa watalipwa fidia utekelezaji utakapoanza. 

Aidha amewaeleza, wakala wa barabara (TANROADS) bado haijawa tayari katika utekelezaji huo lakini wale wanaopitiwa na bomba kuu linaloelekea Bagamoyo ,kuanzia eneo la Sunguvuni -Sanzale watarajie kulipwa fidia zao na DAWASA hivi karibuni . 

Akitolea ufafanuzi suala hilo kwa wakazi wa Chasimba na Magoza, kata ya Yombo wakati wa ziara yake ya kata kwa kata, Kawambwa alisema walengwa wanaoguswa na miradi hiyo wavute subira. 

Aidha alieleza, ahadi ya malipo ambayo DAWASA  italipa anaendelea kufuatilia ili kupata taarifa zaidi ya malipo hayo . 

“Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara mbalimbali, hii barabara nayo ipo katika utekelezaji wa ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi, “

“Tanroads na DAWASA wamekubaliana wakati ikisubiriwa kufikia ujenzi wa  barabara hiyo, imeingiliana na mradi wa bomba kuu la maji ambapo DAWASA italipa wale  watakaopitiwa na ujenzi huo “alifafanua Kawambwa. 

Kuhusu barabara ya Yombo-Kiegea ,mbunge huyo alisema inatafutwa fedha ili iweze kuboreshwa kwa kiwango cha changalawe .

“Kwa bajeti ya mwaka 2018/2019 TARURA haina fedha hivyo kwasasa ni matengenezo madogo madogo wakisubiri utengenezaji mkubwa baadae endapo kukipatikana fedha”alibainisha .
Akijibu suala la ukosefu wa umeme huko Chasimba na Magoza alisema maeneo hayo yameingizwa katika mradi wa Peri Urban na mkandarasi atakapopatikana watarajie kunufaika na mradi huo mpya. 
Awali wakazi wa Chasimba, Magoza kata ya Yombo walisikitishwa umeme kuwekwa mijini na vijiji kusahaulika kwa miaka mingi. 
Walisema ,wanatumia solar kila siku kwa gharama ya sh.3,000, gharama ambayo ni kubwa kwao kwa maisha ya sasa .

HIFADHI YA SAADANI WATOA OFA KWA WATAKAOTEMBELEA HIFADHI HIYO.

Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akisoma kijarida cha Hifadhi ya Taifa ya Saadani alipotembelea banda la maonesho la Hifadhi hiyo katika Tamasha la 37 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo alipokuwa analifunga rasmi Oktoba 20,2018. Kulia ni Mhifadhi Utalii wa Saadani Bi. Apaikunda Mungure.
………………….

Ofa ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Saadan kwa Tsh 91,000 tu
BAGAMOYO:
Hifadhi ya Taifa ya Saadani kupitia Tamasha la 37 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo limetangaza ofa kwa Watanzania na wasio Watanzania kutembelea hifadhi hiyo kuanzia Oktoba 25, 26 na 27 mwaka huu kujionea vivutio mbalimbali vya Utalii.

Akizungumza Mhifadhi Utalii, Hifadhi ya Saadani, Bi. Apaikunda Mungure alisema ofa hiyo ni maalum kwa msimu huu wa tamasha la Sanaa Bagamoyo  ambapo kwa kiasi cha Tsh. 91,000   ni gharama kwa Raia wa Tanzania pamoja na Afrika Mashariki huku wageni kutoka nje ya Afrika Mashariki hao watalipia US$120 tu.

“Ofa hii itanda kwa muda wa siku tatu. Oktoba   25, 26 na 27. Wageni wataenda Saadani na kurudi hapa Bagamoyo. Kwa kiasi hicho cha Tsh. 91,000 inajumlisha usafiri wa magari ya Kitalii, usafiri wa kuzunguka na boti kwenye makutano ya Mto Wami na bahari ya Hindi.

Pia watapata kifungua kinywa, chakula cha mchana na vinywaji na kutembelezwa kwa safari za kuangalia wanyama na magari” alieleza  Bi. Apaikunda Mungure.

Ameongeza kuwa kwa familia itakayokuwa na motto atamlipia Tsh. 71,000.
Saadani  ni hifadhi ya kipekee ambapo Nyika na bahari  vinakutana pamoja. Ndani ya hifadhi hiyo ina aina mbalimbali za wanyama pori, fukwe ya bahari ya hindi.

Iko katika mkoa wa Pwani na Tanga
Watanzania ambao wapo Bagamoyo na miji jirani ya Dar es Salaam ni fursa ya kujitokeza kwenda kujionea Utalii wa ndani wenye kila aina ya vivutio vya Wanyama na safari zitakuwa kila siku kwa wageni kuanzia saba ambao wao kila mmoja atakaa kwa siti tena dirishani (window seat).