Tuesday, March 6, 2018

MARUFUKU MKAA KWENYE GARI ZA ABIRIA- DC BAGAMOYO.


Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiangalia Basi la abiria ambalo limebeba mkaa kwenye buti. 
 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiangalia Basi la abiria ambalo limebeba mkaa kwenye buti. 
...............................................

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga amepiga marufuku ndani ya wilaya yake kupita mabasi ya Abiria ambayo yamebeba Mkaa.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo kwenye oparesheni maalum ya kukagua mazao ya misitu ambayo yanasafirishwa bila ya kuwa na kibali na kukwepa ushuru hali inayopelekea kuikosesha serikali mapato.

Alisema kila mwenye kusafirisha mazao ya misitu ikiwemo Kuni, Mbao, Mkaa na Miti ya ujenzi anapaswa kuwa na kibali kinachomruhusu kuvuna na kusafirisha huku akisisitiza kuwa ndani ya vibali hivyo yapo maelekezo ya wapi muhusika anapaswa kuvuna Mbao, Mkaa au Kuni.

alisema kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ndio kutapelekea kulinda mapato ya serikali ambayo faida ya mapato hayo inarudi kwa wananchi kwa kuwatekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika Oparesheni hiyo maalum, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo amebaini mabasi kadhaa Abiria yanayobeba mkaa hali inayohatarisha usalama wa abiria.

Alisema licha ya kukiuka sheria za usalama barabarani, ubebaji wa Mkaa katika mabasi ya Abiria ni hatari kwa usalama kwakuwa baadhi ya magunia ya mkaa yanakuwa na cheche za moto hali itakayopelekea gunia la mkaa kuwaka moto na hatimae Gari lote kuungua na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia.

Aidha, aliwataka Abiria kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kubaini mabasi yote ya Abiria yanayobeba magunia ya mkaa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheia zitakazokomesha tabia ovu katika sekta ya usafirishaji.

Kwa upande wao Abiria wa mabasi hayo walisema wanakerwa vitendo vya kupakia magunia ya mkaa kwenye mabasi ya abiria kwakuwa hutumia muda mrefu kupakia mkaa njiani.

Walisema katika safari kila mtu anamahitai na umuhimu wake wa kuwahi hivyo kitendo cha kucheleshwa kwasababu ya kupakia mkaa ni kutokujali umuhimu wa safari kwa abiria.

Nao makondakta wa mabasi yanayofanya safari katika barabara ya Chalinze Segera walisema wanalazimika kupakia mkaa ili kufidia kwakuwa kuna shida ya abiria ambapo Gari hutumbea bila ya kujaza na kupelekea kushindwa hata pesa ya kujaza mafuta.

Walisema gunia moja la mkaa wanasafirisha kwa bei ya shilingi elfu kumi ambayo ukizidisha kwa magunia kumi unaweza kupata pesa ya kuongezea kipato.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, akiangalia magunia ya mkaa marefu yanayojulikana kwa jina la Shanga mbili, ambayo yapo kando ya barabara ya Chalinze Segera kwaajili ya kusubiri kupakiwa kwenye mabasi ya abiria, pamoja nae kulia ni Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFSA) Halmashauri ya Chalinze, David Ntemi, na wa pili kulia ni Kaimu meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFSA) kanda ya Mashariki, Suleiman Bulenga.
Basi hili limekutwa limepakia magunia kumi ya mkaa makubwa (shanga mbili) kutoka Kimange kuelekea Dar es Salaam, ambapo kila gunia moja hulipiwa shilingi Elfu kumi.

Monday, March 5, 2018

JK. ACHANGIA UJENZI WA SHULE KIBINDU WILAYANI BAGAMOYO.


 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete akiwasili shule ya msingi Kibindu, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga, kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete.

Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete, akizungumza katika shule ya msingi Kibindu iliyopo kata ya Kibindu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, wa kwanza kulia ni Mkewe Mama Salma Kikwete, wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga na kushoto ni Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete.
......................................................
Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete amechangia mifuko 450 ya Saruji ambapo kati ya hiyo mkewe mama Salma Kikwete amechangia mifuko 150 katika uenzi wa shule za Msingi Kibindu, Kweikonje, na Pera katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Rais huyo mstaafu wa Tanzania ametoa mchango huo baada ya kutembelea shule hizo ambazo zinaendelea na ujenzi wa kuongeza vyumba vya madarasa ili kukabiliana na msongamano wa wanafunzi ambao wamekuwa wakiandikishwa kwa wingi kila mwaka.

Akitoa mchango huo Rais huyo Mstaafu amewapongeza viongozi wa wilaya, Mbunge pamoja na wananchi kwa kujitolea katika kuhakikisha shule hizo zinaongeza vyumba vya madarasa.

Alisema shule hizo zinamahitaji ya vyumba vya madarasa hivyo ushirikiano ndio njia pekee itakayoweza kusaidia ujenzi wa madarasa hayo.

Hata hivyo ametoa ushauri kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze kuona uwezekano wa kuigawa shule ya Msingi Kibindu ili kuondoa msongamano wa wananfunzi uliopo kwa sasa.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi, kwa kutoa milioni 160 kwaajili kuchangia ujenzi wa shule mbili ikiwemo shule ya msingi Kibindu na Kweikonje.

Dkt. Jakaya alimuomba Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi, kuangalia uwezekano wa kuongeza msaada katika shule ya Msingi Kibindu ili kuwaondolea adha ya msongamano wananfunzi wa shule hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema anaipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Shule ya msingi kibindu imeanzishwa mwaka 1952 ambayo kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 1407 ambapo mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 32 na madarasa yaliyopo kwa sasa ni saba tu.
 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete akipokelewa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga mara baada ya kuwasili shule ya msingi Kibindu ambapo alienda kujionea ujenzi wa upanuzi wa shule hiyo.

 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete
akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu, huku Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akiwa saidia fundi kwa kumpa udongo Rais Mstaafu ili kazi ya ujenzi iendelee.
 Mke wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Mama Salma Kikwete, ambae pia ni Mbunge wa kuteuliwa akishiriki kujenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu.
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga, (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete (kushoto) wakibeba mawe kwaajili ya kujaza kwenye vyumba vya madarasa vinavyotakiwa kumwagwa zege la jamvi katika shule ya Kibindu.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga, akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu.

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu, wakati walipotembelea shuleni hapo pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete.

MAKATIBU WAKUU 15 KUTAFUTA SULUHU ZA CHANGAMOTO ZINAZOKABILI ZIWA MANYARA NA TISHIO LA KUKAUKA KWAKE


Baadhi ya Makatibu Wakuu wakitizama kwa mbali Ziwa Manyara.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali ,Gaudence Milanzi akiwanesha baadhi ya Makatibu Wakuu namna ambavyo athari za kimazingira zimeanza kuonekana katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara .


Mkuruenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi (Mwenye kofia) akiwaonesha Makatibu Wakuu waliotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara maeneo ya Ziwa Manyara ambayo yameanza kukauka.
Eneo moja wapo la Vivutio vya Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara likionekana kuanza kukauka kutokana na Athari za kimazingira zinazosababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo ,Kilimo Uchimbaji wa Madini katika maene ya jirani na Ziwa hilo.

Tuesday, February 27, 2018

VIONGOZI WALIOKULA FEDHA ZA WAKULIMA WA KOROSHO WARUDISHE.



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wa Vyama vya Ushirika waliokula fedha za wakulima wa korosho wilayani Masasi wazirudishe na wakishindwa mali zao zikiwemo nyumba zitauzwa ili kufidia.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa ahakikishe anawasaka viongozi wa chama Ushirika cha Msingi cha Nanyindwa wilayani Masasi ambao wamekula fedha za wakulima na kisha kutoroka.

Amesema viongozi wa vyama vya Ushirika katika wilaya hiyo si waaminifu, ambapo mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya sh. bilioni 2.3 za wakulima ziliibiwa na viongozi hao, ambapo mwaka 2017/2018 sh. bilioni 1.7 zimeibiwa.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo jana (Jumatatu, Februari 2018) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi pamoja na watumishi wa wilaya akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.

Alisema viongozi wa Ushirika wa Nanyindwa ambao wametoroka ni Michael Mkali, Yusuph Mataula, ambapo alimuagiza Bw. Byakanwa kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Pia Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuvichunguza vyama vya Msingi katika maeneo na wakikuta kuna kiongozi amekula fedha za wakulima wamkamate na kumchukulia hatua za kisheria.

Alisema wakati wa watu kuomba kuchaguliwa kuongoza vyama vya Ushirika kwa lengo la kujitajirisha umepita na Serikali imedhamilia inawasimamia wakulima wa mazao mbalimbali nchini wakiwemo wa korosho ili kuhakikisha nao wananufaika.

Waziri Mkuu alisema vyama vya Ushirika wilaya hiyo vinaongoza kwa ubadhilifu wa fedha za wakulima ambapo wiki iliyopita Bw. Byakanwa aliwakamata viongozi 36 wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) wilayani Masasi.

Viongozi hao ambao ni wenyeviti na makatibu wanakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za wakulima wa korosho ambazo ni zaidi ya sh bilioni 2.3, ambazo ni malipo ya zao hilo kwa msimu wa ununuzi 2016/2017 na 2017/18.

Alisema mbali na wafanyabiasharahao, pia Meneja wa benki ya NMB tawi la Masasi, Aidan Msuya anaye alikamatwa kwa tuhuma za kufanya muamala wa fedha za malipo ya wakulima sh milioni 45 kwa zaidi ya mara 11 kwa siku moja.

Waziri Mkuu alimpongeza  Bw. Byakanwa kwa hatua alizozichukua dhidi ya viongozi hao na kumuagiza ahakikishe viongozi wote waliosababisha ubadhirifu huo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Monday, February 26, 2018

WATOTO 6 WAWASHIWA VIFAA VYA USIKIVU (COCHLEAR IMPLANT).



Mtaalam wa Huduma ya Usikivu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mathayo Majogoro Alfred (katikati) akiunganisha kifaa cha usikivu cha nje na cha ndani ili mtoto Matilda Katobesi aweze kusikia kwa mara ya kwanza. Kulia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Pua, Koo na Masikio, Dkt. Edwin Liyombo akifuatilia na kushoto ni mama wa mtoto huyo, Angelina Cosmas.
................................

Watoto sita ambao wamewekewa vifaa vya usikivu Januari mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo wameanza kusikia kwa mara ya kwanza baada ya kuwashiwa vifaa hivyo. 

Kuwashwa kwa vifaa hivyo kumeleta furaha kwa wazazi kwani wameshuhudia watoto wao wakisikia sauti kwa mara ya kwanza na hivyo kuwajengea matumaini ya watoto hao kuanza maisha mapya.

Zoezi la kuwawashia vifaa hivyo (Switch On) limefanyika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili  kwa kushirikiana na wataalaam kutoka Medel Austria ambao ndio wasambazaji wa vifaa hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari , Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Pua,  Koo na Masikio Dkt. Edwin Liyombo amesema watoto hao walifanyiwa upasuaji wa upandikizaji kifaa cha usikivu Januari mwaka huu ambapo zaidi ya asilimia 80 ya upasuaji huo ulifanywa na watalaam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili .

 ‘’Watoto hawa wataanza maisha mapya ya kusikia sauti mbalimbali katika mazingira yanayowazunguka baada ya kuunganisha vifaa hivi na kuviwasha’’. Amesema Dkt. Liyombo.

Akifafanua amesema mbali na watoto hao sita lakini pia watoto wengine watano ambao walifanyiwa upasuaji huo mwaka jana  na  wengine sita  ambao walifanyiwa upasuaji huo nchini India nao wamekuja kufuatiliwa maendeleo yao ili kubaini changamoto zinazowakabili  na kupewa ushauri wa kitaalam.  

Akielezea ukubwa tatizo  Dkt. Liyombo amesema takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinaonesha kuwa katika watoto 1,000 wanaozaliwa,  inakadiriwa kuwa watoto watano wanazaliwa na tatizo kubwa la usikivu .
Pia amesema MNH ipo kwenye mchakato wa kuanzisha utaratibu wa kuwachunguza watoto wachanga ili kubaini mapema wenye matatizo yakutosikia. 

Kwa upande wake Muwakilishi kutoka Medel Fayaz Jafar amesema upasuji huo umekua na mafanikio makubwa kwakua  katika awamu hiyo kumekua na mabadiliko  kwani asilimia kubwa  ya upasuaji umefanywa na watalaam wa MNH  na kwamba hatua hiyo ni ya kuridhisha.

Huduma ya Upandikizaji wa kifaa cha usikivu (Cochlear Implant) ilizinduliwa Juni 7 , 2017 na  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu hivyo Tanzania imekuwa nchi ya pili kutoa huduma hiyo katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Kenya. Aidha Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hiyo  kupitia Hospitali ya Umma ambayo ni Muhimbili yenye hadhi ya ubingwa wa hali ya juu.

Mtoto Matilda kwa mara ya kwanza tarehe 24, Januari, 2018 akianza kutamka baadhi ya maneno baada ya kufundishwa na mtaalamu wa sauti kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Wazazi wa watoto wenye matatizo ya kusikia wakiwa kweny mkutano huo.

Sunday, February 25, 2018

NAIBU WAZIRI ANGELINA MABULA ASHUHUDIA UZINDUZI WA HUDUMA ZA KISASA KITUO CHA AFYA NYAMWAGA TARIME


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akiangalia vifaa vilivyopo katika kituo cha afya cha Nyamwaga kilichopo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara. 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akitoa nasaha wakati alipokwenda kushuhudia uzinduzi wa huduma za kisasa katika kituo cha Afya cha Nyamwaga kilichopo Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara.
Baadhi ya wananchi wakisikiliza nasaha zilizokuwa zikitolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula wakati wa uzinduzi wa kituo cha afya cha Nyamwaga kilichopo Tarime mkoa wa Mara.
Sehemu ya majengo ya kituo cha Afya cha Nyamwaga kilichopo Tarime mkoa wa Mara .

PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI-WANMM

NMB YASAIDIA VIFAATIBA VYA MIL. 5, HOSPITALI YA BAGAMOYO.


Meneja wa NMB kanda ya Mashariki, Aikasia Muro (wa nne kulia) akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga (mwenye suti) moja ya vifaatiba walivyotoa msaada kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, wanaoshuhudia wa pili kushoto ni mwenyekiti wa halmashauri ya bagamoyo, Ally Ally Issa na wa tatu kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Hospitali ya Wilaya Bagamoyo, Mwajuma Saidi Masaiganah.
...............................................
Benki ya NMB imesaidia vifaa tiba katika Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo vyenye thamani ya shilingi milioni tano.

Akizungumza katika kukabidhi vifa hivyo, Meneja wa NMB kanda ya Mashariki, Aikasia Muro alisema Benki hiyo imefikia hatua hiyo ikiwa ni katika mipango yake ya kurudisha faida inayopata kwenye jamii.

Alisema NMB katika mipango yake imekuwa ikishiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kusaidia katika sekta ya Elimu, kusaidia vifaa vya ujenzi, sekta ya Afya na kusaidia watu katika kipindi cha majanga kama ya mafuriko na ajali mbalimbali.

Alisema Hospitali ni sehemu ambayo kila mwana jamii anafika kupata huduma za matibabu na hivyo kupeleka msada katika hospitali ni sawa na kusaidia jamii nzima.

Aliongeza kwa kusema kuwa, Benki ya NMB ni Benki pekee yenye matawi mengi nchini na hivyo kuwa na wateja wengi hali inayopelekea kufikiria kuridisha fadhila kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa misaada mbalimbali.

Akipokea msaada huo, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid mwanga ameishukuru Benki hiyo kwa msaada huo na kusema kuwa ni kuonyesha mahusiano mema baina ya Benki hiyo na Serikali.

Alisema vifa hivyo vitasaidia kwa Hospitali ya Bagamoyo kwakuwa Hospitali hiyo inahudumia watu kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya wilaya ya Bagamoyo.

Wakati huohuo, Mkuu  huyo wa wilaya huyo amewataka madiwani katika halmashauri ya Bagamoyo kuandaa maeneo kwenye kata zao ya kujenga zahanati ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya wilaya.

Alisema kuwepo kwa Zahanati kwenye kata kutasaidia wagonjwa kutibiwa kwenye kata zao na kwamba watakaokwenda Hospitali ya wilaya ni wale ambao wameshindikana kutibiwa kwenye zahanati.

Nae Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Dkt. Salvio Wikesi alisema anatoa shukrani kwa Benki ya NMB kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vitasaidi katika kuwahudumia wagonjwa wanaofika katika Hospitali hiyo.

Alisema katika vifaa vilivyotolewa ni pamoja Delivery kit moja ambapo alisema kwenye muongozo wa wizara ya afya Hospitali ya Bagamoyo inatakiwa kuwa na Delivery kit 10 na kwamba hospitali hiyo sasa ina Delivery kit tano baada ya kupokea moja kutoka NMB.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni tano vilivyotolewa na benki ya NMB ni pamoja na Mashuka 35,  Vitanda 6 pamoa na magodoro yake, Kitanda cha kuifungulia 1, Seti 1 ya vifaa vya kujifungulia (Delivery kit) na Mashine ya kupimia BP 1.
 Meneja wa NMB kanda ya Mashariki, Aikasia Muro (wa tano kulia) akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga (wa tatu kushoto) moja ya vifaatiba walivyotoa msaada kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, (wa pili kushoto) Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally (wa kwanza kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo, Mwajuma Saidi Masiganah ( wa tatu kushoto, kwa pamoja wakimkabidhi kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Dkt. Salvio Wikesi (katikati) wa tatu kulia ni Meneja wa NMB kanda ya Mashariki, Aikasia Muro, Meneja wa NMB tawi la Bagamoyo wakishuhudia baada ya wao kukabidhi kwa Mkuu wa wilaya.
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, akitoa neno la shukrani kwa NMB mara baada ya kupokea msaada wa vifaatiba.
 Meneja wa NMB kanda ya Mashariki, Aikasia Muro, akizungumza wakati wa kukabidhi vifaatiba hivyo katika ukumbi wa Halmashauri Bagamoyo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Dkt. Salvio Wikesi, akitoa neno la shukrani kwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo kwa kutafuta wafadhili pamoja NMB kukubali kusaidia vifaatiba katika Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo.

Timu ya wasimamizi wa Afya Halmashauri ya Bagamoyo (CHMT) wakifuatilia kwa karibu makabidhiano ya vifaatiba kutoka kwa Benki ya NMB yayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Bagamoyo.
Meneja wa NMB tawi la Bagamoyo (kulia) akifuatilia makabidhiano ya vifaatiba vyenye thamani ya shilingi milioni 5, vilivyotolewa na Benki hiyo kwa hospitali ya wilaya ya Bagamoyo.

Timu ya kutoka NMB tawi la Bagamoyo wakiongozwa na Meneja wa kanda ya Mashariki, Aikasia Muro, (wa pili kulia) wakipiga picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, (wa pili kushoto) wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Afya, Mwajuma Saidi Masaigana, na wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally.
 Timu ya wasimamizi wa Afya Halmashauri ya Bagamoyo (CHMT) wakipiga picha ya pamoja na meza kuu.

Saturday, February 24, 2018

DC BAGAMOYO ATOA SIKU 3 WINDE (RAZABA)

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga,kihutubia wakuu wa idara katika Ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo Tarehe 23 February 2018.

Na Athumani Shomari 
.....................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, ametoa siku tatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, kufuatilia taarifa za watu wanaogawana viwanja katika shamba linalomilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) lililopo kijiji cha Winde kata ya Makulunge.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo hilo Tarehe 22 Februry 2018 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo, kufuatia taarifa za kuwepo watu wanaogawana viwanja ndani ya shamba hilo bila ya kujali mipaka na umiliki halali walionao RAZABA.

Alimtaka mkurugenzi kumpa taarifa za kitaalamu kuhusu mipaka ya RAZABA ili kubaini ukubwa wa eneo lililovamiwa na kuangalia hatua za kuchukua ili kunusuru eneo hilo ambalo lipo chini ya umiliki wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar .

Alisema hatua za haraka zichukuliwe ili kusitisha zoezi linaloendelea katika eneo la RAZABA na kuwaepusha watu wasie kutapeliwa kwa kuuziwa au kugaiwa eneo linalomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Mkuu  huyo wa wilaaya aliwataka wataalamu wa Ardhi Halmashauri ya Bagamoyo kufanya kazi zao kwa weledi ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili ya kazi zao.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alitoa wito kwa wananchi wanaotaka Viwanja wilayani Bagamoyo kufika ofisi za Ardhi ili kupewa maelekezo yaliyokuwa sahihi juu ya wapi hakuna mgogoro wa kiumiliki ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza kwa kupewa eneo ambalo tayari lina umiliki wa mtu mwingine.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wananchi wa kijiji cha Winde waliwasilisha malalamiko yao mbele ya Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi Wiliam Lukuvi ambapo walitaka mipaka ya RAZABA iwekwe wazi ili kutenganisha kati ya eneo la wananchi na RAZABA jambo ambalo tayari limeshafanyika.

KAULI YA CCM WILAYA YA BAGAMOYO NOVEMBA 18, 2017

Tarehe 18 Novemba 2017, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Abduli Rashidi Sharifu alisema Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Bagamoyo kinatambua uwepo wa kjiji cha Winde na kwamba hakijawahi kuvunjwa wala kuondolewa kwenye ramani ya Bagamoyo.

akizungumza katika Mkutano ulioitishwa katika kijiji cha Winde kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo, Sharifu alisema Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) ina mipaka yake na wananchi wa winde wana mipaka yao hivyo kila mmoja anapaswa kuheshimu mipaka yake.

KAULI YA HALMASHAURI YA BAGAMOYO JUNI 22, 2016.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Aliy Aliy alipiga marufuku utoaji wa hati za ardhi ikiwemo hati za kimila, katika maeneo yanayopakana na ardhi iliyohifadhiwa kama vile Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) inayomilikiwa na wizara kilimo na maliasili Zanziba, na Ranchi ya ruvu iliyopo wilayani Bagamoyo ambayo iko chini ya umiliki wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Mwenyekiti huyo wa Halmashauri alitoa kauli hiyo Juni 22, 2016. katika Mkutano Mkuu Maalum wa kijiji cha Kidomole kata ya Fukayosi Halmashauri ya Bagamoyo na kuongeza kuwa Afisa aridhi atakaebainika kutoa hati ndani ya maeneo hayo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kusimamishwa kazi.

Kauli hiyo ya Mwenyekiti huyo ilikuja kufuatia taarifa za kuuzwa kwa baadhi ya maeneo ndani ya Ranchi hizo jambo ambalo ni kinyume na sheria kwakuwa kampuni zinazomiliki maeneo hayo bado hazijavuliwa umiliki wake.

MSIMAMO WA WANANCHI WA WINDE.
  Wananchi wa kitongoji cha RAZABA Kata ya Makurunge Halmashauri ya Bagamoyo wilaya ya Bagamoyo,wakionyesha mabango yao kudai Ardhi yao ambayo kwa sasa inamilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) kwenye mkutano uliofanyika Tarehe 18 Novemba 2017, kitongoji cha RAZABA. ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abdul Rashid Sharifu.

HISTORIA YA MGOGORO KWA UFUPI
Mgogoro  wa watu wa kijiji cha Winde na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) umedumu kwa zaidi ya miaka 40 sasa huku RAZABA ikidai kuchukua eneo hilo kwa kuwalipa fidia wananchi hao toka mwaka 1977 na wananchi wa kijiji cha Winde wakidai hawajawahi kulipwa fidia.

MSIMAMO WA RAZABA.
Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) inasema RAZABA imeanzishwa rasmi mwaka 1977 mwezi wa kumi na kwa makubaliano kati ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo jumla ya  heka 77,663 zilikabidhiwa kwa serikali ya mapinduzi Zanzibar chini ya wizara ya kilimo na maliasili kwa lengo la ufugaji wa Ng'ombe na kwamba wananchi wote walilipwa fidia toka wakati huo. 
Bango linaloonyesha kwamba eneo hilo linamilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) chini ya wizara ya kilimo na maliasili ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.
Ramani ya eneo la Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA).