Wednesday, November 15, 2017

ELIMU YA MATENDE NA MABUSHA YATOLEWA KWA WAHARIRI


Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bakar Kambi akisisitiza jambo wakati wa Semina ya uhamasishaji wa wahariri na wakuu wa Idara ya Afya juu ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ilofanyika mapema leo katika ofisi za Wizara ya Afya jijini Dar es salaam, pembeni yake ni  Dkt. Janeth Mgamba
...........................................

NA WAMJW-DAR ES SALAAM.


SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto  imefanikiwa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa asilimia 90 kupitia mpango wa kudhibiti magonjwa hayo hapa nchini NTD.

Hayo yamezungumzwa na Mganga Mkuu wa Serikali  Prof. Bakari Kambi wakati alipofungua semina ya uhamasishaji wa kupambana na magonjwa hayo kwa wahariri wa vyombo vya habari na Wakuu wa idara mbalimbali wa Wizara ya Afya leo jijini Dar es salaam.

“Tumepata mafanikio kwani mpaka kufikia Oktoba  2017  huu  tumefanikiwa kupunguza  ugonjwa wa matende na mabusha katika wilaya 95 sawa na asilimia 77 kati ya wilaya 120 na hivyo tumesitisha kutoa dawa katika wilaya hizo” alisema Prof. Kambi.

Aidha Prof. Kambi amesema kuwa katika mafanikio hayo pia Serikali imefanikiwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Vikope (Trakoma) katika wilaya 58 sawa na asilimia 82 kati ya wilaya 71 hapa nchini.

Kwa mujibu wa Prof. Kambi amesema kuwa kwa maeneo ya nyanda za juu hususan katika maeneo  ya Rungwe,Kyela,ileje na Busekeleo wamefanikiwa kupima wananchi na kuonyesha kuwa maambukizi yamepungua na hivyo kuendelea katika wilaya zilizobaki.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa  wa Mpango wa kupambana na Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dkt. Upendo mwingira amesema kuwa wanajamii wanatakiwa wajitokeze katika kupata dawa za kujikinga na magonjwa hayo  kwani muitikio ni mdogo na inaweza kusababisha madhara makubwa siku za usoni.

Aidha Dkt. Mwingira amesema kuwa Semina hiyo imelenga kuwaelimisha wahariri wa vyombo vya habari ili watoe kipaumbele katika kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya dawa za kukinga magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambayo ni Matende na Mabusha, Usubi,Minyoo na Trakoma ili kuweza kutokomeza kabisa ugonjwa huo hapa nchini.

Mkurugenzi wa Blog ya Full Shangwe Bahati Bukuku akitoa mchango katika Semina ya uhamasishaji juu ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele mbele ya wahariri na wakuu wa Idara ya Afya.


Watumishi wa Idara ya Afya wakifuatilia kwa makini Semina ya uhamasishaji wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele iliyofunguliwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bakar Kambi mapema leo katika ofisi za Wizara ya Afya jijini Dar es salaam.



Monday, November 13, 2017

HAKUNA MGOMO WA BASI NOVEMBA 14, 2017.



       Chama cha Wamiliki wa Mabasi Yaendayo Mikoani (TABOA) na Umoja wa Wasafirishaji Abiria Jijini Dar es Salaam (UWADAR) wamekanusha taarifa inayosambazwa kwenye mitandao kuwa Novemba 14 mwaka huu watakuwa na mgomo wa kusitisha huduma za usafirishaji.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa UWADAR, Kismat Dhalla wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwa ajili ya kukanusha suala hilo.

Dhalla amesema kuwa taarifa hiyo iliandaliwa na vyama hivyo lakini ilishatolewa katika vyombo vya habari siku nyingi zilizopita hivyo kuna baadhi ya watu wameamua kuisambaza upya bila ridhaa ya wahusika.

“Ni kweli ile taarifa ni ya kwetu lakini tulishaitoa siku nyingi na mgomo huo haukufanyika kwa kuwa tuliahidiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) kuwa itayafanyia kazi madai yetu”, alisema Dhalla.

Dhalla ameongeza kuwa tayari SUMATRA imeandaa mkutano na wadau ambao utafanyika mnamo Novemba 15 mwaka huu kwa ajili ya kujadili kuhusiana na baadhi ya Kanuni zilizotungwa katika Sheria hiyo ya SUMATRA.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa SUMATRA, Tumaini Silaa amesema kuwa lengo la SUMATRA ni kuhakikisha kuwa usafiri unapatikana muda wote na unamfaidisha msafiri na msafirishaji ndio maana mamlaka hiyo inajitahidi kuyamaliza malalamiko ya TABOA na UWADAR pindi yanapojitokeza.

“Sisi kama SUMATRA tunaona kuwa hakuna mgogoro kati yetu na wadau wa usafiri isipokuwa ni kutoelewa Kanuni ambazo zimepitishwa na Mhe. Waziri mwenye dhamana hivyo tutakapokutana katika mkutano huo tutaeleweshana kwani tunaamini kuwa kanuni zilizoandaliwa ziko vizuri”, alisema Bw.Silaa.

Amefafanua kuwa baadhi ya watu bado wanachanganya Kanuni za mwaka 2007 ambazo zimefutwa na kanuni hizi mpya lakini wanatakiwa kufahamu kuwa kanuni mpya zimeweka usawa kwa upande wa msafirishaji, abiria, dereva na kondakta.

Pia, kanuni hizo mpya bado hazijaanza kutumika mpaka pale SUMATRA itakapotoa elimu ili kila mmoja awe na uelewa na Sheria na Kanuni zake.

Sunday, November 12, 2017

WAOMBAJI JKT WAONYWA BAGAMOYO.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaj, majid Mwanga amewataka waombaji wa nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa JKT wilayani humo,  kuacha udanganyifu wa makazi ili kutoa nafasi kwa wakazi halisi kupata nafasi hizo.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo wakati wakufunga mashindano ya Mazingira Kabumbu Cup 2017 yaliyofanyika katika uwanja wa Mwanakalenge Mjini Bagamoyo.

Alisema Rais wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John magufuli ametoa nafasi katika kila wilaya ili kila mwananchi mkazi wa wilaya husika apate nafasi hiyo hivyo si kutoka kwenye wilaya yako kuja kuomba nafasi hizo kwenye wilaya ambayo wewe sio mkazi.

Alisema katika usaili unaotarajiwa kufanyika Tarehe 15 Novemba mtu atakaebinika si mkazi wa wilaya ya Bagamoyo atakamatwa na polisi na kuwekwa mahabusu kwa kuingilia makazi ambayo si yake ili hali nafasi hizo zipo kila wilaya nchini kote.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ya bagamoyo, alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wakazi wa wilaya ya Bagamoyo kujitokeza kuomba nafasi hizo ambazo zipo kwa iwango tofauti vya Elimu.

Alisema nafas zilizopo ni 65 tu hivyo kila kata inaweza kutoa vijana watakaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa.

Aliwataka wenyeviti wa vitongoji kutoa ushirikiano katika hilo ili kuhakikisha vijana watakaoingia kwenye usaili wawe ni vijana wa Bagamoyo.