Tuesday, October 31, 2017

MADIWANI KISARAWE WAMFUKUZA KAZI MGANGA MFAWIDHI WA ZAHANATI

BAADHI ya madiwani wa wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani ,wakionekana kusikiliza jambo  wakati wa baraza la madiwani lililofanyika mjini hapo .
Picha na Mwamvua Mwinyi

......................................
 
Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
BARAZA la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, imeazimia kumfukuza kazi mganga mfawidhi wa zahanati ya Mtakayo wilayani humo Dkt. Emmanuel Benedict.

Benedict amefukuzwa katika nafasi hiyo kutokana na kutowajibika ipasavyo,utoro na kufunga zahanati kwa siku tisa hali iliyokwamisha utoaji huduma ndani ya siku hizo .

Mwenyekiti wa halmashauri ya Kisarawe Hamisi Dikupatile akizungumza baada ya kumalizika kwa baraza la madiwani alieleza wamechukua hatua hiyo kufuatia mtumishi huyo kufanya uzembe.

Alisema maamuzi hayo yamefanyika kwa mujibu wa kanuni za utumishi ya mwaka 2003 jedwali A ,kifungu namba 42 ambapo kuna mapendekezo ya adhabu ikiwemo kushushwa cheo,kupunguziwa mshahara au kufukuzwa kazi .

Dikupatile alibainisha kwamba ,Benedict hajaitendea haki jamii ambayo ilikuwa ikihitaji huduma za afya ,hali iliyosababisha mgogoro kati ya wananchi na eneo analotolea huduma.

Alifafanua ,kutokana na hayo ndipo wakaadhimia kumfukuza kazi ili kurudisha nidhamu kazini .

“Kama Rais Dkt. John Magufuli anavyotaka kuona uwajibikaji kazini na kuhudumia wananchi na kama mtumishi awezi anatakiwa kupisha nafasi yake ama kuwajibishwa nasi tumemua kumuachisha kazi mara moja kwa kitendo chake cha kutokaa katika eneo la kazi”alieleza Dikupatile.

Hata hivyo alielezea kwasasa wanawachukulia hatua mbalimbali watumishi wenye makosa ya kiutumishi ambao wapo waliowapunguzia mishahara .

Alisema hatua wanazozichukua zinarejesha heshima kazini na kuleta tija kwa wananchi .

Dikupatile alisema baraza hilo pia limeadhimia kuwa kabla ya mwaka wa fedha 2018/2019 wakazi wa Kibong’wa wanaodai fidia yao inayofikia mil.246 ,wawe wamelipwa fidia hiyo .


Monday, October 30, 2017

TIMU YA PERA YACHUKUA USHINDI CHALINZE.



Mashindano ya Mazingira Kabumbu Cup 2017 Bagamoyo yamemalizika jana Tarehe 29 Oktoba katika mchezo wa fainali uliochezwa katika viwanja vya shule ya Sekondari Msata Halmashauri ya Chalinze kati ya Pera na Bwilingu.

Katika mechi hiyo ya fainali timu ya Pera imeibuka na ushindi wa goli moja dhidi ya Bwilingu na kuifanya timu ya Pera kuchukua Kombe la Mazingira Kabumbu Cup 2017 pamoja na zawadi ya Pikipiki ya Miguu mitatu.

Gori hilo la Pera limefungwa dakika ya 72 na mchezaji Hassani wazri ambae aliingia kipindi cha pili.

Muanzilishi wa Kombe hilo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, alisema lengo la mashindano hayo ni kuifanya jamii iwe na hamasa katika swala la kufanya usafi ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa jmahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli katika agizo lake la kutaka usafi wa mazingira ufanyike nchi nzima.

Fainali ya kwanza ilifanyika katika Halmashauri ya Bagamoyo ambapo timu ya Nianjema ilitoka na ushindi  ambapo nao walichukua kombe na zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu.

Katika mchezo huo wa fainali mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia ambapo alisema Wilaya ya Bagamoyo imekuwa mfano wa kuigwa na kwamba viongozi katika maeneo mengine wanapaswa kuiga mfano huo.

Karia aliwataka viongozi wa TFF wa mikoa na wilaya kutoa ushirikiano pindi yanapoandaliwa mashindano kama hayo ili kuibua vipaji vya vijana kutoka timu za chini.

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema Mashindano hayo yatakuwa endelevu ili kukuza vipaji vya vijana katika taaluma ya mpira.

Kikwete alisema baada ya mashindano hayo kuisha kwa kupatikana mshindi kutoka Halmashauri ya Bagamoyo na Halmashauri ya Chalinze itaandaliwa mechi kati ya mshindi wa Bagamoyo na Chalinze ili kumpata mshindi mmoja.

Aidha, aliongeza kuwa yatafuata mashindano ya mbunge pamoja na mashindano ya chini ya miaka 20. 



Kikos cha Pera
Shekhe natori, Chama iddi, Gaudensi Maarifa, Nadi Kibungo, Ramadhani Yusuph  Captain, Shaibu Jongo, Abdul Muharami, Rajab Jongo, Awadhi Mohammed, Juma Mfu na Mogera Nahau. 

Kwa upande wa Bwilingu
Mbelike Ndeule, Omary Shamte, Macelo Kipresha, Ramadhani Ngandu, Mohammed Wazir, Nyange Kaburu, Samson  Robson, Athuman  Jungu, Azishi Saimon, Kambo Zinyori na Justine Iddi.


Mashabiki wa timu ya Pera wakifurahia ushindi.
 Mchezaji wa timu ya Pera akionyesha kombe mara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bwilingu.

Katikati ni Mgeni Rasmi katika mechi hiyo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Kari, kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, na kushoto ni Mbunge wa jimbo la Chalnze Ridhiwani Kikwete.