Thursday, May 18, 2017

ZANZIBAR HAIBAGULIWI KATIKA EAC.

719A6500
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Balozi Ramadhani Muombwa, akimkaribisha Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota kutoa mada kwenye semina ya mtangamano inayoendelea Kisiwani Pemba. Ushiriki na mwitikio katika semina hiyo umekuwa mkubwa kwa washiriki ambapo wameonekana kuvutiwa sana na semina hii pia wamekuwa wadadisi wazuri wa kutaka kujua zaidi fursa zinazo patikana kwenye mtangamano huo.
 
Bw. Chodota akitoa mada kwenye semina ya mtangamano inayoendelea Pemba.
 
Sehemu ya washiriki wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa ikitolewa na Bw. Chodota (hayupo pichani).
 
Bw. Chodota akiendelea kutoa mada yake.
Mmoja wa washiriki Bi. Kauthari akiuliza swali mara baada ya mada kumalizika kutolewa na Bw. Chodota hayupo pichani.
 
Washiriki wakisikiliza kwa makini mada na maswali yaliyo kuwa yakiulizwa na washiriki wengine.
 
Mhe. Mbarouk Salim Ali Mbunge wa Jimbo la Wete akiuliza swali kwenye semina. Pembeni yake ni Mbunge wa Jimbo la Konga, Mhe. Mbarouk Ali akisikiliza kwa makini.
 
Meneja wa TRA kwa upande wa Kisiwani Pemba Bw. Habibu Saleh naye akiuliza swali kwa mtoa mada, Bw. Suleimani (hayupo pichani).
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Zanzibar haibaguliwi katika EAC,

Serikali ya Zanzibar inashiriki moja kwa moja bila ukomo katika masuala yote ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivyo Wazanzibari wamehimizwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Jumuiya hiyo na kuondokana na dhana kuwa eti, Serikali yao inabaguliwa.
  
Akiwasilisha mada leo kuhusu ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye semina ya masuala ya  mtangamano wa EAC inayofanyika Pemba, Afisa wa Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Bw. Suleima Haji alitoa ufafanuzi wa kina kuonesha namna Zanzibar inavyoshiriki katika EAC.

Bw. Haji alieleza kuwa  licha ya Zanzibar kuwa  sehemu ya muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ushiriki wake umedhihirika katika mgawanyo wa miradi ya maendeleo ya EAC, hususan miradi ya Miundombinu.  Alisema Zanzibar iliwasilisha mapendekezo ya miradi 10 kwenye Sekretarieti ya EAC na kutokana na vipaumbe vilivyowekwa miradi 3 imekubaliwa na mchakato wa kuitekeleza unaendelea. Miradi hiyo ni ujenzi wa Bandari ya  Marhubi kisiwani Pemba, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na ununuzi wa meli kubwa zitakazosafirisha abiria na mizigo kwenye nchi wanachama wa EAC.

 Aidha, kwenye miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Zanzibar haijasahaulika. Zanzibar inanufaika na miradi inayofadhiliwa na taasisi inayojihusisha na masuala ya kukuza biashara na kupunguza umasikini katika nchi za EAC inayoitwa "East Africa Trademark" (TMEA).  TMEA ambayo ni mdau mkubwa wa EAC inafadhili mradi ambao unawawezesha Wazanzibari kufanya maombi kwa njia ya mtandao ili kupata cheti cha uasili wa bidhaa. Cheti hicho ni muhimu kwa wafanyabiashara kwani kinatambulisha bidhaa yako ilipotengenezwa na kupata msamaha wa kodi ya forodha inapoingia nchi nyingine za EAC.

Mradi mwingine unaofadhiliwa na TMEA huko Zanzibar ni ule wa kuwasilisha malamiko kwa njia ya mtandao au ujumbe mfupi wa simu pale inapotokea mfanyabiashara amekumbana na vikwazo visivyo vya forodha katika kusafirisha bidhaa zake ndani ya Jumuiya. Ujumbe huo utakapopokelewa, kikwazo kilicholalamikiwa kitafanyiwa kazi na taasisi husika mara moja.
  
Benki ya dunia pia inaendesha mradi wa kutathmini utekelezaji wa Soko la Pamoja kwa upande wa Zanzibar. Kama inavyotambulika soko la pamoja lina vipengele vingi vikiwemo; usafirishaji huru wa bidhaa, huduma, mtaji na watu. Hivyo kuna umuhimu wa kupima namna nchi wanachama zinavyotekeleza vipengele hivyo.

Ushiriki wa Zanzibar unapatikana pia kwenye uenyeji wa taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zanzibar imebahatika kuwa mwenyeji wa Kamisheni ya  Kiswahili ya EAC. Kuwa mwenyeji wa taasisi kuna faida kubwa zikiwemo kujitangaza na ajira. Kwa upande wa ajira, Bw. Haji alisema sio tu Wazanzibari wanafaidikia na ajira za  Kamisheni ya Kiswahili, bali wanapata ajira hata katika Sekretarieti ya EAC na kutolea mfano kuwa Mhasibu Mkuu wa kwanza wa Sekretarieti hiyo alikuwa Mzanzibari.
  
Vile vile, Zanzibar imekuwa mwenyeji wa vikao mbalimbali vya taasisi za Jumuiya. Mwaka 2010 Mahakama ya Afrika Mashariki ilifanya kikao chake Zanzibar, Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) lilifanya kikao chake Zanzibar mwaka 2016 na mwezi Agosti mwaka huu utafanyika mkutano mkubwa wa masuala ya Kiswahili mjini Zanzibar. Aliendelea kusema kuwa katika Bunge la EALA la kipindi hiki,  Zanzibar ina wabunge watatu, wawili wakitokea CCM na mmoja CUF.

Alihitimisha mada yake kwa kuwasihi Wazanzibari waache fikra potofu za kujihisi kubaguliwa badala yake waunganishe nguvu kuchangamkia fursa lukuki za kibiashara zilizopo kwenye mtangamano wa EAC. Alisema Serikali ya Zanzibar inashiriki katika kila jambo ikiwemo kushiriki mikutano ya Marais. Mawaziri na Wataalamu ili kutetea maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
  

 -Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 18 Mei, 2017



HALMASHAURI KUNUFAIKA NA BILIONI 250 ZA MRADI WA MAJI VIJIJINI .

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Fatuma Omari Latu, akiangalia msimamo wa Halmashauri yake katika usafi wa mazingira kupitia mradi wa Nipo Tayari chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwenye semina inayofanyika mjini Morogoro.
 
Mratibu wa mradi wa usafi wa mazingira uitwao Nipo Tayari Juliana Kitira akimuonyesha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kakonko, Kigoma, Elinatha Elisha takwimu za hali ya usafi wa mazingira katika halmashauri yake kwenye semina inayofanyika Morogoro.
Mradi huo pia unahamasisha uwepo wa vyoo bora na kunawa mikono na maji safi baada ya kutoka chooni.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Simanjiro mkoani Manyara Yefred Myenzi akiapa kuwa yupo tayari kutekeleza kwa vitendo kampeni ya nchi nzima ya usafi wa mazingira iitwayo Nipo Tayari kwenye semina inayofanyika mjini Morogoro.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Sabas Damian Chambasi akiapa kuwa yupo tayari kutekeleza kwa vitendo kampeni ya nchi nzima ya usafi wa mazingira iitwayo Nipo Tayari kwenye semina inayofanyika mjini Morogoro.

 .......................

Halmashauri za wilaya zimetakiwa kuongeza ufanisi katika kusimamia miradi ya maji kwa kuchangamkia fursa ya fedha za kitanzania bilioni 250 zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji safi na salama vijijini (2016-2020).

Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Injinia Jackson Mutazamba aliwaambia wakurugenzi Halmashauri za wilaya katika semina inayofanyika mjini Morogoro, kuwa ni halmashauri chache tu ndio zimeanza kupata fedha hizo mara baada ya kukidhi vigezo vinavyotakiwa na wafadhili.

“Kuna fedha za kutosha katika mradi huu ukilinganisha na mwamko wa Halmashauri katika kuchangamkia fursa hii ya kuongeza mtandao wa maji katika maeneo yao,” alisema na kuongeza kuwa, fedha hizo zinaweza kuzisaidia halmashauri kuanzisha miradi mipya na kukarabati ile ya zamani ili iweze kutoa maji kwa wakati wote wa mwaka.

Alisema moja ya sharti la upatikanaji wa fedha hizo ni ufanisi katika utekelezaji wa miradi iliyopita na ubora wa ripoti za kila mwezi kama ambavyo programu hii inavyozitaka halmashauri. 

Alisisitiza kuwa, Kigezo hicho ni muhimu sana katika kuvuka hatua moja hadi nyingine na kupata fungu kubwa zaidi la fedha ambalo litawezesha kutekeleza miradi mikubwa zaidi katika Halmashauri husika.

Alisema Halmashauri zinaweza kupokea aina mbili za malipo kama vile paundi za kiingereza 50 kwa ajili ya kuendeleza kituo cha maji na kwamba kiasi hicho kinaweza kuongezeka hadi paundi 1,500 kulingana na ufanisi wa utekelezaji katika hatua ya mwanzo.

“Ukipata paundi zaidi ya 1,500 kwa mara moja kwa miradi ya vijijini ni nyingi sana katika kuiboresha na kuifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wakati wote. 

Na pia fedha hizi zinaweza kutumika kuanzisha vituo vipya vya kusambazia maji hivyo kufanya mtandao wa maji kuwa mkubwa zaidi katika eneo husika,” alisema.

Alibainisha kuwa, ni Halmashauri 57 tu ambazo ziliweza kuvuka vigezo viwili vya mwanzo kwa mwaka jana na kuweza kupata fungu kubwa zaidi la kiasi cha paundi za uingereza 5,000, fedha ambazo kwa miradi ya maji vijijini zinaweza kusaidia sana katika upatikanaji wa maji wakati wote wa mwaka.

Aidha, aliwahimiza wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya kuchangamkia fursa hiyo ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mingi ya maji na kuifufua ile iliyokufa iweze kufanya kazi tena na kuongeza mtandao wa maji kuwa mkubwa zaidi ili kufikia azma ya serikali ya asilimia 95 wa watu wanaopata maji katika miaka michache ijayo.

Injinia Mutazamba aliongeza kwa kusema kuwa, lengo la kuwakutanisha wakurugenzi wote nchini katika semina hiyo ni kuweza kuwaeleza kwa kina kuhusu fursa hiyo ya fedha za wafadhili ambazo bado zipo nyingi na zinaweza kusaidia kupunguza na hata kumaliza kabisa tatizo la maji hasa sehemu za vijijini.

Alisema programu hiyo ya kuongeza mtandao wa maji vijijini unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya shirika la kimataia la DFID la uingereza na serikali ya Tanzania.