Friday, May 12, 2017

WAWEKEZAJI TOKA AFRIKA YA KUSI NI WAKARIBISHWA KUWEKEZA TANZANIA.

MEN4
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wafanyabiashara wa nchi za Afrika Kusini na Tanzania uliofanyika Alhamisi Mei 11, 2017 Jijini Dar es Salaam, ambao ulijadili fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara zilizopo baina ya Mataifa hayo.
.............................


RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika Kusini kujitokeza na kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania ina mazingira yaliyo salama, bora na fursa wezeshi.
 
Rais Magufuli ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini mkutano wa wafanyabiashara wa nchi hizo mbili uliojadili fursa na vivutio vya uwekezaji katika mataifa hayo. 

Rais Magufuli amesema Tanzania ina vivutio mbalimbali vya uwekezaji vyenye kutoa fursa kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Afrika Kusini kuwekeza katika sekta yoyote nchini kwani uwekezaji huo una uhakika wa kuzaa matunda mazuri.

 “Napenda kuwahakikishia wafanyabiashara wanaotaka kuwekeza Tanzania kuwa nchi hii ina amani tangu tupate uhuru mnamo mwaka 1961,ina mazingira mazuri ya kibiashara,utulivu wa kiasiasa pamoja na uchumi unaotabirika hivyo nawasihi wafanyabiashara wa Afrika Kusini kuwekeza nchini kwetu,”alisema Dkt. Magufuli.

 Ameongeza kuwa Tanzania ina soko kubwa la kuuzia bidhaa na kutoa huduma mbalimbali kwani tumezungukwa na nchi nane ikiwemo ya Burundi, Congo, Malawi, Rwanda, Uganda na Zambia kwa kiasi kikubwa zinashirikiana na Tanzania katika kufanya biashara za kimataifa hivyo wakiwekeza Tanzania watapata soko la nchi nyingi. 

Kwa upande wake Rais wa Afrika Kusini. Jacob Zuma amesema kuwa wamekubaliana na Rais Magufuli kukuza ushirikiano hasa wa kiuchumi wa nchi zote mbili ikiwa ni moja ya kichocheo kitakachosaidia kuleta faida na kutunza ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya nchi hizo mbili. 

“Hadi sasa kuna zaidi ya Makampuni 200,000 kutoka Afrika Kusini ambayo yamewekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, mawasiliano, sekta za fedha, ujenzi, madini na utalii lakini kwa kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya kuwezesha ukuaji wa uchumi tunaamini kampuni hizo zitaongezeka,”alisema Rais Zuma.

Ametoa rai kwa nchi hizo mbili kuacha kujikita katika bidhaa pekee kwani sio endelevu na haitengenezi ajira za uhakika na badala yake kuwekeza nguvu katika uzalishaji.
 MEN1

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania (TPSF) Reginald Mengi na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye NA Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mhandisi Raymond Mbilinyi wakati wa mkutano wa Mkutano wa Wafanyabiashara wan chi za Afrika Kusini na Tanzania uliofanyika Alhamisi Mei 11, 2017 Jijini Dar es Salaam.
 MEN2

Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mwenyeji wake, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma wakifuatilia kwa makini hotuba za Viongozi mbalimbali wa Serikali za nchi hizo wakati wa mkutano wa Wafanyabiashara wa Mataifa hayo uliofanyika leo Alhamisi Mei 11, 2017 Jijini Dar es Salaam.
MEN3
Baadhi ya Wafanyabiashara kutoka nchini Afrika Kusini wakifuatilia kwa makini hotuba za Viongozi mbalimbali wa Serikali za nchi hizo wakati wa mkutano wa Wafanyabiashara wa Mataifa hayo uliofanyika leo Alhamisi Mei 11, 2017 Jijini Dar es Salaam.
MEN5
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akizungumza jambo na Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa mkutano wa Wafanyabiashara wa Mataifa hayo uliofanyika Alhamisi Mei 11, 2017 Jijini Dar es Salaam.


Thursday, May 11, 2017

CHALINZE YAPONGEZWA KWA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM.

Image may contain: 2 people, people standing
KAIMU Katibu wa Jumuia ya Umoja wa Vijana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Shaka Hamdi Shaka, akizungumza na viongozi mbalimbali wa chama na watendaji wa serikali katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
.................................... 
 
Na Omary Mngindo.
Chalinze.

KAIMU Katibu wa Jumuia ya Umoja wa Vijana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Shaka Hamdi Shaka ameziagiza Halmashauri, Manispaa na Majiji yote nchini kwenda kujifunza uendeshaji wa shughuli zao katika halmashauri ya Chalinze namna ya kuwatumikia wananchi wao.

Shaka ametoa kauli hiyo Mei 10 alipokuwa akizungumza na viongozi wa Halmashauri hiyo, Madiwani, watendaji mbalimbali pamoja na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Bagamoyo chini ya Mwenyekiti Almass Masukuzi, Katibu Kombo Kamote, Mwenyekiti wa Halmashauri Said Zikatimu, pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Edes Lukoa na viongozi wengine.

Kauli ya Shaka imefuatia taarifa iliyotolewa na Zikatimu kuhusiana na namna ilivyotekeleza majukumu yake katika kipindi cha miezi minane tangu kuanzishwa rasmi mwezi wa saba mwaka 2016 ikitokea Bagamoyo ambapo katika kipindi hicho imefanikiwa kuwalipa posho ya sh. 30,000 Wenyeviti wa vijiji wapatao 64.

"Mbali ya kuwalipa posho Wenyeviti wetu, pia kuanzia Julai Mosi mwaka 2016 tunasafirisha bure wagonjwa wote wanaopewa uhamisho kimatibabu kutoka kwenye Zahanati, Vituo vya afya na Hospitali ambao hawalipi hata sentano, mbpo awali walikuwa wanachangia sh. 60,000 kwa ajili ya mafuta wanapotoka eneo moja kwenda lingine," alisema Zikatimu.

Kuhusu ujenzi wa Zahanati katika vijiji vyote, Zikatimu alisema kwamba wameshaanza zoezi hilo katika baadhi ya vijiji na kwamba imani yao ni kuwa kila kijiji kitapata zahanati yake ikiwa ni kuunga mkono sera ya Serikali Kuu ya kutaka kila kijiji kuwa na Zahanati na Vituo vya afya ngazi za Kata.

"Sanjali na hayo tumeweza kurejesha asilimia 10 ya makusanyo yetu ya ndani kwa vijana na wanawake, zaidi ya sh. Mil. 160 tumekopesha vikundi pia tunataraji wakati wowote tutakwenda tena kugawa hundi kota ya nne, hayo ni mafanikio ya urejeshwaji wa asilimia hiyo ambapo Wenyeviti na wananchi wanasimamia vema mapato," alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha, Shaka alianza kwa kuwapongeza viongozi hao huku akisema ni mfano wa kuigwa na kwamba viongozi wa Halmashauri zote, Manispaa na Majiji nchini kwenda Chalinze kujifunza namna ya ukusanyaji mapato na Utawala bora na kwamba wametekeleza kwa vitendo azima ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuwataka viongozi kuwatumikia wananchi wao katika kuwapatia maendeleo.

"Niwaombe waandishi andikeni hili, nawataka Maofisa wote wa Halmashauri, Majiji na Manispaa zote nchini kuna Chalinze kujifunza namna ya ukusanyaji mapato kwani wamejiongoeza wenyewe katika kuwalipa posho Wenyeviti, nimetembea nchi nzima ndio kwanza mambo haya nimeyakuta hapa," alisema Shaka.