Wednesday, April 12, 2017

TANZANIA NCHI YA KWANZA KUWA NA RELI YA KISASA YA MASAFA MAREFU AFRIKA

A 8
Tanzania inatarajiwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na reli ya kisasa inayotumia umeme na mafuta itakayokuwa na uwezo wa kusafiri  masafa marefu kwa mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa.

Akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo ya leo huko Pugu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa reli hiyo itakuwa ya kisasa zaidi barani Afrika na itasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kuchochea fursa za biashara ndani na nje ya nchi.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo ambayo itahusisha kipande cha kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro utagharimu jumla ya shilingi trilioni 2.8 na utatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 30.

Dkt Magufuli alitoa mfano wa nchi zenye reli za mwendokasi lakini masafa mafupi barani Afrika kuwa ni Morocco ambayo inasafiri kwa mwendokasi wa kilomita 220 kwa saa na Afrika Kusini inayosafiri mwendokasi 150 kwa saa.

Dkt Magufuli alieleza kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kuwa na treni itakayosafiri masafa marefu kwa mwendokasi wa km 160 kwa saa.

Alifananua kuwa mradi huo wa ujenzi wa reli unatekelezwa kwa fedha za Tanzania ambapo tayari serikali imeshawalipa wakandarasi malipo ya awamu ya jumla ya shilingi bilioni 300.

Akizungumzia umuhimu wa ujenzi wa reli hiyo, Rais Magufuli alisema kuwa reli hiyo itasaidia kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwa haraka na kuwafikia wateja ndani ya muda mfupi.

Vilevile, reli hiyo itarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani ya Kusini.

Sambamba na hayo, Rais Magufuli alisema kuwa ujenzi wa reli hiyo utasaidia kuimarisha sekta nyingine za uchumi ikiwemo utalii, viwanda, kilimo, pamoja na kutoa ajira kwa watanzania ambapo kutakuwa na ajira muda zipatazo 600,000, na ajira za kudumu 30,000.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema kuwa reli hiyo ya kisasa inayojengwa na wakandarasi kutoka muungano  wa kampuni mbili za nchi ya Uturuki na  Ureno  itakuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo tani 10,000 kwa mara moja  na kutumia saa 2 kutoka Dar es salaam hadi Dodoma na saa 7 na dakika 40 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Naye, Mjumbe wa Bodi ya Kampuni ya ujenzi kutoka Uturuki ya Yapi Merkezi Bw.  Emre Aykar alisema kuwa reli hiyo itaimarisha zaidi uhusiano wa Uturuki na Tanzania na kuongeza kiwango cha shughuli za biashara nchini.

“Tunaahidi kujitahidi kumaliza mradi kwa wakati na katika kiwango kinachotakiwa” alisema Bwana Aykar.

Reli hiyo ya kisasa inatarajiwa kujengwa pembeni ya reli ya kati ambayo ilijengwa wakati wa utawala wa kikoloni wa Wajerumani na Waingereza miaka 112 iliyopita.

Tuesday, April 11, 2017

SERIKALI YAZINDUA USAMBAZAJI WA VIFAA VYA HOSPITALI NCHINI.

ndu2
Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai , Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy na Mkuu wa wilaya ya Kongwa Bw.Deogratius Ndejembi wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa mpango huo .
 ndu3
Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai akipokea vitanda hivyo kutoka kwa  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy , kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kongwa Bw.Deogratius Ndejembi.
ndu4
Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai ,  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy , kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kongwa Bw.Deogratius Ndejembi.wakikagua vitanda hivyo mara baada ya makabidhiano.
..................



Serikali ya awamu ya tano nchini imezindua rasmi usambazaji wa vifaa vya hospitali kwa halmashauri zote nchini  katika kutekeleza mkakati wa kuboresha huduma za afya nchini kwa kuhakikisha wananchoi wanapata huduma kwa kiwango stahiki.

Akizindua usambazaji huo  leo wilayani hapa,Waziri wa Afya,maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy mwalimu alisema serikali imetekeleza ahadi iliyotoa kwa wananchi ambapo serikali inawekeza katika afya ya wananchi  hivyo kuweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Akizungumza kwenye hadhara ya wanachi wa Wilaya ya Kongwa,Waziri Ummy alisema serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwa baadhi ya maeneo ikiwemo ya upatikanaji wa dawa ambapo bajeti ya dawa imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 251 mwaka 2016/17.

“Hatua hii imeleta mapinduzi makubwa katika upatikanaji wa dawa,vifaa na vifaa tiba kwenye vituo vya Umma vya kutolea huduma za afya,hivyo wanaomba wananchi kuhakikisha mnafika kwnye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata matibabu sahihi”.

Aidha, Waziri Ummy alisema kufuatia ahadi ya Mhe. Rais ya kununua na kusambaza vitanda kwenye vituo vya Umma ,Wizara yake kwa bajeti ya mwaka 2016/17 ilitenga kiasi cha shilingi biliuoni 4 za kuwezesha kununua pamoja na kusambaza  vifaa hivyo kwa halmashauri 184 nchini
Alivitaja vifaa vilivyonunuliwa na kuvikabidhi kwa Mhe. Job Ndungai (Mb), Mbunge wa Kongwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungazo wa Tanzania  Mhe. John Ndugai  ni pamoja na  vitanda vya hospitali (20),vitanda vya kujifungulia wajawazito (5), magodoro (25) na mashuka (50).

Vifaa vya Hospitali vitakavyopasambazwa kwenye Halimashauri zote 184 nchini ni pamoja na vitanda vya hHospitalini 3,680; vitanda vya kujifungulia akinamama wajawazito 920; magodoro 4,600; na mashuka 9,200. Thamani ya vifaa hivi ni shilingi bilioni 2,933, 125,600. Zoezi la kugawa vifaa hivi linatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 30, 2107.

Akipokea vifaa hivyo, Mhe. Ndugai ameishukuru Serikali kwa msaada wa vifaa vilivyotolewa kwa Hospitali na vituo vya Afya katika mkoa wa Dodoma ikiwemo Halmashauri Kongwa. Vifaa hivyo vitaboresha afya ya wananchi wa jimbo la Kongwa na maeneo mengine nchini na hivyo kusaidia kuwawezesha wananchi kukutumia mudao wao mwingi katika shughuli za kiuchumi.