Monday, January 23, 2017

SERIKALI YARIDHIA KUTOA BANDARINI VIFAA VYA UJENZI WA TBIII.

MIW 2

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe.Prof. Makame Mbarawa,  akionesha kitu kwa mbele (hakionekani pichani) kwa Mkurugenzi wa mradi huo, Mhandisi Mohammed Millanga, wakati alipofanya ziara kukagua ujenzi wa jengo la tatu la abiria (TBIII). Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Salim Msangi.
 MIW 1
Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, akitoa tathmini ya ujenzi wa jengo la tatu la abiria (TBIII), mara baada ya kulitembelea. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TAA (MAB), Prof. Ninatubu Lema bna kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Salim Msangi.
.....................................
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema serikali italipia haraka vifaa vya ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) vilivyokwama bandarini.

Mhe. Prof. Mbarawa alisema hayo hivi karibuni mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, ambapo alijibu moja ya changamoto zilizosomwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi kuwa vifaa vya ujenzi vimekwama bandarini.

“Hivi vifaa vitalipiwa haraka ili mradi uendelee na kumalizika kwa wakati kama ilivyosemwa utakamilika mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu 2017,” alisema Mhe. Prof. Mbarawa.

Alisema anaamini kukamika kwa jengo hili litakuwa bora kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, kwa kuwa  litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni sita kwa mwaka, na litapunguza msongamano uliokuwepo katika jengo la pili la abiria (JNIA-TBII), ambalo lilijengwa kwa ajili ya kuhudumia abiria 1.5 milioni kwa mwaka, lakini sasa linahudumia abiria 2.5 milioni kwa mwaka.

Awali, Mhe.Prof. Mbarawa alisema hii ni mara ya tatu kutembelea jengo hili, na amefanya hivyo ili kumsimamia mkandarasi kwa karibu aweze kutoa mradi mzuri usiokuwa na tatizo kwa siku za usoni.

Pia alisema serikali imejipanga kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege ili ndege yake ya Shirika la ndege (ATCL), ambayo imezindua safari zake katika baadhi ya mikoa iweze kutoa na kupaa bila tatizo.

“Huu mradi wa TBIII sio pekee, vipo viwanja 13 vitaboreshwa kwa kufanyiwa ukarabati na upanuzi, na baadhi yake ni Mwanza, JNIA TBII, KIA, Songwe, Sumbawanga, Tabora, Shinyanga na Kigoma,” alisema Mhe. Prof. Makame Mbarawa.

Awali akisoma taarifa fupi ya mradi wa TBIII, Kaimu Mkurugenzi, Bw. Msangi alisema mradi huo umekumbwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha kiasi cha Euro 121,634,888.30, ambazo serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iliahidi kukamilisha taratibu upatikanaji wa fedha mapema ili kutoathiri utekelezaji wa mradi.

Pia Bw. Msangi alisema changamoto nyingine ni uchelewaji wa malipo ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwa vifaa vilivyopo bandarini hadi sasa inadaiwa Tsh. Bil. 1,362,801,347.00, kati ya fedha hizo Tsh. Mil. 960,153,258.00 ni za kulipia vifaa maalumu vya usalama vya ukaguzi wa abiria (X-ray machine), ambavyo vinatakiwa visiathiriwe na joto.

“Hali hii ya vifaa kuchelewa kutoka inasababisha kuongeza gharama za mradi pamoja na kuchelewesha kazi zilizopangwa kufanyika, na pia hali hii itasababisha uharibifu wa vifaa ambapo serikali itabidi kuvilipia pindi itakapotokea uharibifu,” alisema Bw. Msangi.

Hatahivyo, Bw. Msangi alisema ujenzi wa jengo hilo utakaotumia gharama ya Tsh. Bilioni 560, sasa umekamilika kwa asilimia 66.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAHUSIANO CHA TAA
 MIW
Mkurugenzi wa Mradi wa Jengo la Tatu la abiria (TBIII), Mhandisi Mohammed Millanga akiendelea kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya ujenzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (aliyeshika miwani), wakati alipokagua ujenzi wa jengo hilo.

Sunday, January 22, 2017

MKOA WA PWANI HAUNA NJAA- RC NDIKILO.

Mkuu wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, akikagua masoko yaliyopomkoani humo ili  kujiridhisha na hali ya chakula katikamkoa  huo.

Na Mwamvua  Mwinyi-Pwani
 
MKOA wa Pwani, una ziada ya chakula zaidi ya tani 503,711.5 huku vyakula vikiwa vimejaa kwenye masoko hivyo hakuna njaa.

Aidha mkoa huo una mfumko wa bei za vyakula katika masoko mbalimbali kutokana na kupanda kwa gharama za nafaka katika mikoa ya Mbeya,Kagera,Iringa na Morogoro.

Hayo yalibainika ,katika ziara ya siku moja ya mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,alipotembelea soko la Mailmoja,Mlandizi na Chalinze kujionea hali ya chakula.

Katika masoko hayo mchele wa kawaida kwa sasa unauzwa kg kwa sh.1,500 hadi 2,000 ,mchele super 2,200,unga sh,1600 ,mahindi 1,100 ,maharagwe kg sh.2,000 hadi 2,400 ,na viazi mbatata gunia sh.130,000 badala ya 60,000.

Mhandisi Ndikilo alisema,msimu wa kilimo 2015/2016 mkoa ulilenga kulima hekta   205,467 za mazao ya chakula zilizotarajiwa kuzalisha tani1,039,565.

 “Mkoa pia ulilenga kulima hekta 158,242 za mazao mbalimbali ya biashara na kutarajiwa kuzalisha tani 837,108 “alisema.

Mhandisi Ndikilo,alisema hekta 144,241 za mazao ya chakula zililimwa na kuzalisha tani 773,279 huku hekta 85,850 za mazao ya biashara zililimwa na kuzalisha tani 566,283.

Alitoa angalizo kuhusiana na upungufu wa utomwili (Protini) ambao hutokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya jamii ya mikunde.

Mkuu huyo wa mkoa ,alisema upungufu wa mazao jamii ya mikunde, hauna athari kwani hufidiwa na mazao yatokanayo na mifugo, uvuvi na mazao ya jamii hiyo kutoka mikoa mingine.

Mhandisi Ndikilo,alizielekeza halmashauri za wilaya 
kuwajengea uwezo wakulima kutambua umuhimu wa uvunaji bora, utunzaji wa chakula na kiasi cha chakula kinachohitajika kaya kwa mwaka mzima.

Alisisitiza endapo kutatokea janga la njaa kwa mkoa ,basi wakulima watumie fedha walizopata kwenye mazao ya biashara kama korosho.

Alisema wakulima wa zao la biashara la korosho katika msimu unaoisha walipata sh.bil.33 kwa tani 12,000 walizouza, hivyo watumie fedha hiyo kununua chakula ili kununua chakula na kukabiliana hali hiyo.

Mhandisi Ndikilo,alikemea kutumia nafaka kwenye shughuli zisizo za lazima,ngoma na kutengeneza pombe .

Nae afisa kilimo kutoka sekretarieti mkoani hapo,Judith Mushi,alisema hali ya chakula kimkoa ni ya wastani lakini tatizo ni wananchi kulalamikia hali ngumu ya maisha.

Alihimiza kupanda mazao yanayostahimili ukame na kukomaa haraka ikiwa ni sanjali na muhogo, mtama, viazi vitamu na kunde.

Judith aliwashauri wafugaji wauze sehemu ya mifugo yao ili kujinunulia chakula badala ya kukaa na mifugo mingi bila tija.

Mfanyabiashara wa nafaka katika soko la Chalinze, Saidi Ally, alisema wafanyabiashara wanapandisha bei za vyakula kutokana na kununua bidhaa mbalimbali kutoka mikoani kwa gharama kubwa.

Alisema kwasasa pia wanagombania bidhaa hizo kwani zinashushwa magunia machache kwasababu kilimo cha vuli na masika (hasa mazao ya chakula) haukuwa mzuri .
 

Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,akiangalia hali ya chakula katika masoko mbalimbali Mailmoja,Chalinze na Mlandizi ili kujiridhisha kuwa hakuna njaa mkoani hapo.

(Picha na Mwamvua Mwinyi)