Tuesday, December 6, 2016

KAYA 55,692 HAZISTAHILI RUZUKU YA UMASIKINI KUTOKA TASAF

unnamed
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki, akizungumza na Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam, kuhusu Kaya zilizoondolewa kwenye Mpango wa kunusuru Kaya Masikini, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Awamu ya Tatu kwa kukosa sifa. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Ikulu, Bw. Peter Ilomo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Susan Mlawi.
......................................
Serikali imeondoa kaya 55,692 katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Awamu ya tatu kutokana na sababu mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Waziri  Kairuki, alizitaja Sababu za kuondolewa kwa kaya hizo ni pamoja  kifo, kuhama kijiji/mtaa ambapo mpango haujaanza kutekelezwa, kutojitokeza mara tatu mfulululizo kupokea ruzuku, mnufaika kuwa mjumbe wa kamati mbalimbali za mpango, wastaafu, na viongozi wa watumishi wa Umma.

Alisema hayo yamebainika baada ya uhakiki ambao aliagiza ufanyike mwezi Februari 2016.

Waziri Kairuki alisema katika uhakiki huo kaya zilizokuwa na mwanakaya aliyefariki au wote kufariki zilikuwa 13, 898, kaya zilizohama vijiji/mitaa ambapo mpango haujaanza kutekelezwa 6,228.

Aliongeza kaya ambazo hazikujitokeza mara tatu mfululizo kupokea ruzuku zilikuwa 17,746, zilizothibitishwa kuwa sio masikini zilikuwa 13,468 na kaya zilizogundulika kuwa na baadhi ya wanakaya wajumbe wa kamati za usimamizi za Jamii, Halmashauri za Vijiji/Kamati za Mitaa, Viongozi na watendaji zilikuwa 4,352.

Mhe. Kairuki aliainisha kuwa kufuatia agizo lake alilotoa mwanzoni mwa mwaka huu hadi Septemba 2016 kiasi cha shilingi Bilioni 6,427,110,309 kimeokolewa kwa kaya 42, 035 zilizoondolewa kwa kipindi hicho, na kusisitiza kiasi hicho kitaongezeka kwasababu zoezi hilo linaendelea.

Waziri Kairuki alifafanua kuwa ameshauriana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuwasimamisha waratibu wa TASAF Wilaya na uchunguzi kufanyika wa jinsi walivyojihusisha kuvuruga utekelezaji wa mpango kwa kuandikisha kaya zisizo na sifa.

Kufuatia hilo, Waziri Kairuki alimwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF kuwasimamisha kazi mara moja na kuendelea na hatua za kinidhamu kwa Maafisa Washauri na Ufuatiliaji 106 walioko kwenye Halmashauri walioshindwa kufuatilia na kusimamia mpango hivyo kusababisha kaya zisizostahili kuingizwa kwenye Mpango na kuendelea kulipwa isivyostahili.

Wengine alioelekeza kusimamishwa ni Maafisa watano wa TASAF Makao Makuu wanaosimamia mpango, pamoja na Mameneja Uratibu na Mkurugenzi wa Uratibu ambao ndio wasimamizi wakuu. 

Aidha, Waziri Kairuki ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kwa kipindi kisichozidi mwezi mmoja ili kubaini ushiriki wa Maafisa hao na kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaothibitika kuhusika katika kuvuruga utaratibu wa utekelezaji wa mpango au kuwepo udhaifu katika usimamizi, ufuatiliaji na uwajibikaji.

Waziri Kairuki alielekeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya wahakikishe kuwa fedha zote zilizotolewa kwa kaya zisizokuwa na sifa zinarejeshwa ili ziwanufaishe walengwa.

Waziri Kairuki alitoa rai kwa wananchi na wadau wote wa Mfuko wa Maendeleo ya  Jamii Tanzania (TASAF) kutoa taarifa za watu wote ambao wananufaika lakini hawastahili kuwa kwenye Mpango ili malipo yasifanyike kwa wote wasiostahili.

Awamu ya Tatu ya TASAF ilianza mwaka 2012 ambapo Serikali inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini. 

Kaya zilizoandikishwa idadi yake ni Milioni moja laki moja na kumi mia sita thelasini na tano, 1,110,635, na kaya hizo huandikishwa baada ya hatua ya utambuzi ambayo jamii husika hushirikishwa katika mikutano ya pamoja kwa kuweka vigezo vya umasikini na baadaye kaya hizo hufanyiwa uhakiki kwa kutumia takwimu na viashiria vya umasikini.

 Takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania takribani asilimia 28.2 bado ni masikini sana, na serikali hadi sasa imeshatumia shilingi bilioni 391,835,484,755 zilizolipwa katika mikupuo nane kwa kaya milioni moja laki moja na  kumi mia  sita thelasini na tano, 1,110,635.

Monday, December 5, 2016

WAZIRI MKUU ASEMA KAMPUNI ZA WATUMISHI ZISIPEWE ZABUNI NDANI YA HALMASHURI ZAO.

mondu1
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Bi. Theresia Mahongo kuhakikisha kampuni zinazomilikiwa na madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo hazipewi  zabuni zinazotolewa katika maeneo yao kwa ajiliya  kuepusha migongano ya kimaslahi.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Desemba 5, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Karatu mkoani Arusha katika ukumbi bwalo la  Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Karatu akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.

“Hauzuiliwi kufanya biashara ili mradi kampuni yako isifanye kazi katika halmashauri ambayo wewe unaitumikia na una nguvu nayo ili kuepusha migongano ya kimaslahi kwani miradi yote utajilundikia,” amesema.

Pia amewataka Wakuu wa Idara katika halmashauri hiyo walisaidie Baraza la Madiwani katika kubaini vyanzo vipya vya mapato kwa lengo la kuongeza mapato ya halmashauri yao.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewataka watumishi wa halmashauri wa umma  kujitathmini na kujiridhisha kama wanafuata misingi ya utumishi katika utendaji kazi wao wa kila siku. Amewasisitiza  wawatumikie wananchi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.

“Hatuhitaji kuwa na mtumishi mvivu, asiyewajibika, mwizi, mla rushwa na asiyekuwa muadilifu mahali pa kazi.

Na  atakayeona ameshindwa kutunza na kusimamia fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi atoe taarifa hatutaki watu kufanya kazi kwa mazoea,” amesema.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa ” watumishi wa umma lazima mbadilike na muwe na nidhamu ya kazi. Muache malalamiko fanyeni kazi na msitafute  sympathy (huruma) kutoka kwa watu kwani Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ,” amesema.

Amesema katika baadhi ya ofisi za Serikali kuna ugonjwa wa watumishi wanapoona wageni wamelifika kwa ajili ya kupatiwa huduma wanawapita bila ya kuwasikiliza. ” sasa hatutaki watumishi wa namna hiyo, Jukumu lako ni kumtumikia Mtanzania na tunataka kuona mabadiliko. Hatutaki kuona watu wakizubaa maofisini,”.

Waziri Mkuu amesema Serikali ikikuta wananchi wanalalamika kutokana na kutoridhishwa na  huduma zitolewazo na watumishi wa umma itahakikisha watumishi hao wanachukuliwa hatua. Serikali ni ya Watanzania wote hivyo lazima wahudumiwe vizuri bila ya kujali uwezo wao kifedha wala itikadi zao za kidini na kisiasa.

MASHINDANO YA KUTUNISHA MISULI TANZANIA KUFANYIKA 2017.

misul2
Baadhi ya watunisha misuli wakionesha jinsi ya kutunisha misuli kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
 misul1
Katibu Mkuu wa Chama cha Watunisha Misuli Nchini Bw. Francis Mapugilo (kushoto) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mashindano ya kutafuta bingwa wa kutunisha misuli nchini Tanzania 2017 mapema hii leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Mshauri wa Ufundi wa Chama hicho Bw. Fike Wilson na mwisho kulia Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo Bw. Nilesh Bhatt
 misul4
Baadhi ya watunisha misuli wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo Bw. Nilesh Bhatt(kushoto) mapema hii leo jijini Dar es Salaam.