Thursday, August 25, 2016

BALOZI WA PALESTINA NCHINI TANZANIA ACH ANGIA DAMU MUHIMBILI.

Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Hazem Shabati akijisajili kabla ya kuchangia damu leo katika hospitali hiyo. Kushoto ni Msajili wa damu, Titus Mhokole.
.............................................................................................


Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Hazem Shabati amewataka Watanzania kuwa na tabia ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu.

Balozi Shabati amefika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili kuchangia damu na kuwahamasisha watu wajitokeze kwa wingi ili kuchangia damu.

Amesema kila mtu ana wajibu wa kuchangia damu kwa kuwa ni muhimu kwa maisha ya wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ya kiafya.

Pia, Balozi Shabati amesema lengo la kuchangia damu ni kudumisha uhusiano kati ya Tanzania na nchi yake ambao ni wa muda mrefu na wa kihistoria.

 Katika hatua nyingine, Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Neema Mwangomo amesema kwa wastani hospitali hiyo inakusanya chupa 40 hadi 50 kwa siku, lakini mahitaji kwa siku ni chupa 80 hadi 100.

Amesema makundi makubwa yanayohitaji damu kina mama wajawazito, watoto wenye saratani, majeruhi wa ajali na wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji.

Mwangomo amesema mwanaume mwenye umri wa miaka 18 hadi 65 ndiye anapaswa kuchangia damu wakati mwanamke ni miaka 18 hadi 62.

Amesema kigezo cha pili ni mtu anayechangia damu anapaswa kuwa na uzito wa kilo 50 na kuendelea na kwamba mtu anapaswa kuwa na wingi wa damu kuanzia asilimia 85.

Mwanamke anaweza kuchangia damu mara tatu kila baada ya miezi minne wakati mwaume mara nne kila baada ya miezi mitatu.



WATAALAMU WA TEHAMA WATAKIWA KUSIMAMIA MAADILI.

 

Naibu Waziri  Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani  akiongea na wanahabari  hawapo pichani wakati wa uzinduzi wa mkutano wa siku moja wa wataalamu hao uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.

 Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano Prof. Faustine Kamuzora  akiongea na wataalam wa Tehama wakati wa uzinduzi wa mkutano wa siku moja wa wataalamu hao uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
 

Naibu Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani ameiagiza Tume ya Teknolojia ya Habari na  Mawasiliano nchini kuhakikisha wanatengeneza misingi ya uadilifu wa kitaaluma na misingi hiyo itumike kuwadhibiti wale ambao wanatumia utaalamu huo kwa nia mbaya.

Mhandisi Ngonyani aliyasema hayo  wakati akizindua mkutano wa kwanza ambao umeandaliwa ma Tume mpya ya Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa  Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Alisema Mkutano huo una lengo la kuwakutanisha wataalamu wa TEHAMA kutoka katika sekta za umma na sekta binafsi ili kuweza kujadiliana ni kwa namna gani taaluma hiyo inavyoweza kutumika zaidi kwa faida ya ukuaji wa uchumi nchini Tanzania.

“Wapo baadhi ya watu wanatumia taaluma ya TEHAMA kwa manufaa mbalimbali ya kujenga uchumi na maendeleo, lakini wapo wachache ambao wanatumia utaalamu wao kwa manufaa  binafsi ikiwemo kuwadhalilisha watu wengine na kuwaibia fedha zao katika mitandao” Alisema Mhandisi Ngonyani.

Alisema Tume hiyo ya Teknolojia ya Habari na  Mawasiliano inatakiwa  kuja na sheria kali ambazo zitawabana wale wote ambao wamekua na tabia ya kutumia mitandao katika kufanya vitendo viovu badala ya kutumia katika kujiletea maendeleo.

Awali akizungumza katika mkutano huo,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano upande wa sekta ya Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora alisema uanzishwaji wa Tume ya Teknolojia ya Habari na  Mawasiliano nchini ni jitihada za makusudi za serikali  katika kukuza Mawasiliano .

Prof,Kamuzora alisema kuwa tume hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa na hivyo kuwasihi watendaji hao kuwaelimisha zaidi wananchi  kujikita zaidi katika kufuata maadili ya taaluma hiyo ili kulifikisha Taifa katika mafanikio ya sekta  ya mawasiliano.

Alisema Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano itasaidia kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kukua kwa sekta ya TEHAMA na kuchochea uzalishaji ,ukuaji wa sekta zingine kiuchumi na usambazaji wa huduma za jamii.