Monday, July 25, 2016

MAADHIMISHO SIKU YA MASHUJAA TANZANIA LEO JULAI 25.



Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Christina Mndeme akiwasha Mwenge wa uhuru katika mnara wa mashujaa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ambayo inaadhimishwa leo 25 Julai, hafla iliyofanyika Saa Sita Kamili usiku ya tarehe 25 julai 2016 Mkoani Dodoma.
 
Mwenge wa uhuru mara baada ya kuwashwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mh. Christina Mndeme, Tarehe 25 julai 2016 Saa Sita Kamili usiku Mkoani Dodoma.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Jordan Rugimbana akiongea na baadhi wa viongozi wa serikali waliohudhuria tukio hilo la uwashwaji wa Mwenge na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuupa heshima Mkoa wa Dodoma ambapo maadhimisho hayo yanafanyika mkoani humo.
 
Wanajeshi wa Kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiimba wimbo wa Taifa mara baada ya kuwashwa kwa Mwenge usiku wa saa sita, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yanayofanyika hii leo tarehe 25 julai 2016 Mkoani Dodoma.
 
Baadhi ya Viongozi mbalimbali wa Serikali wakishuhudia uwashwaji wa Mwenge katika mnara wa Mashujaa usiku wa saa sita mkoani Dodoma. 
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiongea na baadhi wa viongozi wa serikali waliohudhuria tukio hilo la uwashwaji wa Mwenge na kutoa rai kwa watanzania kuwa wazalendo na nchi yao bila kujali itikadi ya mtu kama walivyofanya wazee wetu waliopigania uhuru wa nchi.
.................................................................................................................................................................
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama amesema kuwa kufanyika kwa maombolezo ya kumbukumbu za Mashujaa inawakumbusha watanzania kuwa wazalendo.

Akizungumza wakati wa maombolezo ya kumbukumbu za Mashujaa sambamba na kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru katika mnara wa kumbukumbu za Mashujaa, leo usiku katika viwanja vya Mashujaa vilivyopo mjini Dodoma, Waziri Mhagama alisema kuwa kufanyika kwa maombolezo ya Mashujaa mkoani Dodoma ni heshima kwa wananchi wa Dodoma na watanzania wote kwa ujumla.

“Kufanyika kwa maombolezo haya inatukumbusha watanzania kuwa wazalendo na kupigania bila kuchoka, bila kujali makabila yetu na tujifunze kwa Mashujaa hawa waliopigania uhuru wetu” alisema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama aliwaomba watanzania kutumia siku ya kumbukumbu ya Mashujaa ambayo ni Julai 25, kwa namna mbalimbali ikiwemo kufanya maombi ya sala kwa Mashujaa wote walifariki katika harakati mbalimbali za kupigania uhuru wa Taifa la Tanzania.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimwa Jordan Rugimbana aliishukuru Serikali kwa uwamuzi wa kuadhimisha kumbukumbu za mwaka huu za Mashujaa mkoani Dodoma, na kusema kuwa kufanyika kwa tukio hilo la kihistoria linakumbusha uwajibu wa watanzania na Mkoa wa Dodoma utaienzi heshima hiyo.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Mheshimiwa Christina Mndeme aliwasha Mwenge wa Uhuru katika kilele cha mnara wa mashujaa mnano saa 6 kamili usiku ikiwa ni sehemu ya maombolezo ya kumbukumbu ya Mashujaa.

Mnara wa Mashujaa uliopo mkoani Dodoma ni kati ya vituo 4 vilivyopo nchi nzima ambavyo vimekuwa na makaburi ya Mashujaa mbalimbali waliopigania uhuru wa nchi ya Tanzania. Vituo vingine vipo meneo ya Mtwara, Dar es Salaam na Kagera.

Maadhimisho ya kumbukumbu za Mashujaa kwa mwaka huu yanafanyika leo julai 25, mkoni Dodoma ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli atakuwa mgeni rasmi.

CCM BAGAMOYO, KUMPOKEA JK. LEO TAREHE 25 JULAI.




MWENYEKITI mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Jakaya Kikwete ameandaliwa mapokezi makubwa na wanaCCM wilayani Bagamoyo leo baada ya kukabidhi wadhifa huo, kwenye Mkutano Mkuu Maalum Dodoma.

Akielezea kuhusu mapokezi hayo mjini Dodoma, Katibu Mwenezi wa CCM, Wilaya ya Bagamoyo,Kassim Gogo (Brenya) alisema kuwa mapokezi hayo yataanzia Chalinze hadi Bagamoyo.

Alisema kuwa wanaCCM wa wilayani Bagamoyo wanajisikia furaha sana kuona Jakaya Kikwete ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Msoga, wilayani humo, amemaliza salama uongozi wake ndani ya chama baada ya kukitumia chama na serikali kwa miaka kumi. 


Alisema kuwa jambo lingine linalowapa faraja ya kuandaa mapokezi hayo ni kwamba Jakaya Kikwete amemaliza uongozi wake kwa kukiacha chama salama na nchi ikiwa salama pia.

Gogo, alisema kuwa katika mapokezi hayo watakuwepo madiwani wote wa wilaya hiyo, viongozi wa CCM, wabunge wote wa Mkoa wa Pwani na wananchi kwa ujumla. 


Alisema kuwa wakati wa hafla hiyo pia Mwenyekiti mstaafu, Kikwete atakabidhiwa zawadi mbalimbali ikiwemo kumvisha gwanda ili awe mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani.

Katika sherehe za mapokezi zitakazofanyika mbele ya Makao Makuu ya Ofisi za CCM za wilaya hiyo zilizopo Bagamoyo Mjini, patakuwepo ngoma za asili ya makabila ya Wakwere, Wazaramo na Wazigua pamoja na wasanii mbalimbali pia watatumbuiza. 


Alisema kuwa Kikwete akiwa amepumzika baada ya kumaliza muda wake, watapata wasaa wa kuchota hekima na burasa zake ya jinsi ya kukiongoza chama hicho na serikali kwa ujumla.

Saturday, July 23, 2016

RAIS MAGUFULI ASEMA SERIKALI ITAHAMIA DODOMA.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha Serikali inahamishia makazi yake mjini Dodoma.

Alisema hayo leo, wakati alipokuwa akihutubia wajumbe wa Chama cha Mapinduzi(CCM) katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti.

“Nitahakikisha katika awamu ya uongozi wangu, Serikali inahamia Dodoma, najua viongozi wengine wote nao watanifata, kwa kuwa sasa miundombinu ya Dodoma inaweza kukidhi mahitaji yote” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliendelea kusema kuwa katika kipindi cha miezi nane ya uongozi wake chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ameweza kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuanza kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Akiongelea maeneo ya utekelezaji katika kipindi chake Dkt. Magufuli alisema kuwa mpaka sasa Serikali imefanikiwa kusimamia suala la utoaji wa elimu bure kwa shule za Msingi na Sekondari nchini na kuwezesha udahili kuongezeka zaidi tofauti na miaka iliyopita.

Aidha Dkt. Magufuli alisema kuwa Serikali yake pia imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji wa mapato ya serikali hali itakayosaidia kuimarisha utoaji wa huduma muhimu za jamii.Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano imeagiza ndege mbili mpya zinazotarajiwa kuwasili nchini Septemba mwaka huu,

Rais Dkt. Magufuli aliongeza kuwa Serikali yake kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda wamefanikiwa kujenga bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima katika ziwa Alberti nchini Uganda kwenda bandari ya Tanga ambapo mafuta hayo yatasafirishwa sehemu mbalimbali duniani na bombahilo litazalisha zaidi ya ajira 20,000.

Vile vile, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali yake imeweza kurudisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma na kuweza kuondoa watumishi hewa waliokuwa na waliokuwa wamefikia 12,500,na kuongeza kuwa kwa mwaka huu Serikali imetenga fedha za matumizi jumla ya shilingi trilioni 29.5, ambapo asilimia 40 ya fedha hizo zitapelekwa katika kutekeleza shughuli za maendeleo.

Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ulihudhuriwa na wajumbe zaidi 2,000 ulimpitisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa mshindi na Mwenyekiti wa Chama hicho kwa kura 2398 kati ya kura 2398 zilizopigwa ikiwa ni sawa na asilimia 100.

Rais Magufuli anakuwa Mwenyekiti wa awamu ya Tano baada ya kupokea uongozi huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama hicho anayemaliza muda wake Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka 10.

HIFADHI YA WAMI MBIKI YAHITAJI ULINZI KUNUSURU MALIASILI.

Kiboko akiwa  ndani ya mto Wami ambao umepita kwenye Hifadhi ya Wami Mbiki.


Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga kulia, wa pili kutoka  kulia ni Meneja msaidizi Wakala wa Misitu Tanzania TFS wilaya ya Bagamoyo, Joel Liyangala walipotembelea hifadhi ya Wami Mbiki  kwa upande wa Bagamoyo.

Serikali wilayani Bagamoyo, inaandaa mkakati wa kuinusuru hifadhi ya Wami Mbiki ambayo inashirikisha wilaya tatu za Bagamoyo, mvomelo na Morogoro vijijini, ili kulinda misitu na wanyama waliomo ndani yake kwa manufaa ya Taifa.

Mkakati huo umeelezwa na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga, katika ziara aliyoifanya kwenye hifadhi ya Wami  Mbiki inajumuisha wanyama  na misitu.

Katika  ziara hiyo iliyowajumuisha Wakala wa Hifadhi za Misitu Tanzania TFS, na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Bagamoyo ililenga kubaini madhara yaliyopatikana katika hifadhi hiyo ya Wami mbiki  na  kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Mkuu  huyo wa wilaya alisema  ili kuweza  kudhibiti mipaka ya  hifadhi hiyo  na kulinda maliasili zilizomo ndani yake ni muhimu kuimarisha ulinzi wa mipaka katika vijiji vinavyozunguuka hifadhi hiyo.

Alisema wilaya  ya Bagamoyo inaandaa mkakati ambao utawashirikisha wakuu wa wilaya zote tatu zinazozunguuka hifadhi hiyo ambazo ni Bagamoyo, Mvomelo na Morogoro vijijini.

Aliongeza kuwa , kufuatia maliasili  zilizomo ndani ya hifadhi hiyo, Taifa linaweza  kufaidika ikiwa utawekwa ulinzi utaimarishwa na ukawekwa utaratibu mzuri wa  watu mbalimbali kutembelea hifadhi hiyo kwa kulipa kiingilo.

Meneja msaidi wa TFS wilaya ya Bagamoyo, Joel Liyangala.
Kwa upande wake meneja msaidizi wakala wa hifdhi za misitu  Tanzania TFS, wilaya ya Bagamoyo, Joeli Liyangala, alisema, hifadhi hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo nguvu ndogo ya ulinzi ukilinganisha na ukubwa wa eneo lenyewe.
Alisema  lengo la  kutembelea hifadhi hiyo pamoja kamati ya ulinzi na usalama ni kuangalia namna  ya kupanga mikakati ya ulinzi ili kudhibiti uharibifu  unaofanywa  katika hifadhi hiyo ikiwemo uvunaji wa mbao na uchomaji mkaa huku wanyama waliopo katika hifadhi hiyo wapo hatarini kutoweka kwa kukosa ulinzi wa kutosha.
Liyangala alisema, hifadhi ya Wami Mbiki ina wanyama wengi wanoishi humo huku wakifanya njia kuu ya kutoka  mbuga mbalimbali kuelekea Seluu.
Askari wa hifadhi ya Wami Mbiki wakiwa kwenye ulinzi.
Aliongeza kwa kusema, hifadhi ya Wami Mbiki ina ukubwa  wa hekta 2500 ambapo inajumuisha vijiji 24 vinavyozunguuka hifadhi hiyo, kutoka katika wilaya 3 za Bagamoyo, Mvomelo na Morogoro vijijini.
Askari wanaolinda  hifadhi ya Wami Mbiki, wakimueleza mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid hemed Mwanga, hayupo pichani, changamoto wanazokabiliana nazo

Kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Bagamoyo, ambayo iliambatana na mwenyekiti wa kamati hiyo mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga walipotembelea hifadhi ya wami Mbiki kwa upande wa Bagamoyo.