Monday, June 3, 2024

WIZI WA MTOTO MWENYE UALBINO MULEBA, WATATU WAKAMATWA.

 

Alodia Babara, Muleba,

Noela Asimwe Novath mtoto mwenye umri wa miaka miwili na nusu mwenye ualibino  ameibwa katika mikono ya mama yake baada ya mtu mmoja  asiyejulikana kupiga hodi nyumbani kwao na kuomba msaada wa chunvi akidai amenga’twa na nyoka katika kijiji cha Bulamula kata ya Kamachumu  wilaya ya Muleba mkoani Kagera.


Mama mzazi wa mtoto huyo Judith Richard amesema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 30, mwaka huu saa 7:30 jioni wakati mama huyo akiwa amekaa ndani na mtoto wake ndipo mtu huyo alipokuja na kupiga hodi bila kutaja jina lake na kusema kuwa, amenga’twa na nyoka hivyo  anaomba msaada wa chunvi.


Judith amefungua mlango na kumuona mtu ambaye alikuwa akitembea kwa kuchechemea bila kujua kumbe alikuwepo mtu mwingine amejibanza  ukutani ambapo aliyekuwa amejibanza ukutani alimkaba koo na aliyekuwa anachechemea  aliingia ndani na kutokomea na mtoto kusikojulikana.


 “Kuna mtu alipiga hodi akaniita mama Asimwe naomba unisaidie chunvi  nikamuuliza wewe nani akajibu mie Kelvin, nikamuuliza  wa wapi? akajibu wa humu humu kitongojini Mbare awali roho ikasita baadaye nikawaza siwezi kujua atakayenisaidia nikafungua mlango nikiwa nimewasha tochi ya simu yangu nilimuona mtu amaejibanza ukutani muda huo huo alikuja haraka akanikaba shingo  dakika kama nne amenikaba na aliyekuwa anajifanya anachechemea aliingia ndani na kutokomea na mtoto wangu” amesema Richard.


Amesema baada ya mtu huyo kumwachia alianza kupiga kelele za kuomba msaada ndipo mke wa shemeji yake alitoka  na yeye kuanza kumsaidia kupiga kelele za kuomba msaada wanakijiji walikusanyika.


Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga  amesema kuwa, jeshi la polisi limeshaweka mtego kila sehemu kwa ajili ya kuwakamata watu waliofanya kitendo cha wizi wa mtoto huyo.


Dkt Nyamahanga ameitaka jamii ya wakazi wa Muleba kuendelea kuonyesha mshikamano katika kumtafuta mtoto huyo kama ambavyo walifanya toka tukio lilivyotokea.


“Sisi kama serikali kwa kushirikiana na jeshi la polisi tunaendelea kupambana na mitego yote tuliyoitega tulitoa taarifa kila kona ili kuwanasa wahalifu, maelekezo yetu kama serikali ukiona matukio haya yameanza, wameanza kutikisa kiberti kijiji chochote ndani ya wilaya ya Muleba wenye binadamu mwenye ualibino kupitia kwa maafisa ustawi wa jamii waripoti kila siku juu ya usalama wa watu hawa”


“Na nyie wanawake msiwaache watoto wenu bila mtu yeyote mkaenda kuchota maji umbali wa mita kadhaa tuwalinde kwa kila namna na kwa gharama yoyote kwa sababu ni binadamu wenzetu” amesema Dkt Nyamuhanga.


Aidha, kaimu kamanda mkuu wa jeshi la polisi mkoa Kagera Yusuph Daniel amesema wanaendelea na msako wa kutafuta wahalifu waliohusika kupora mtoto huyo na wamefanikiwa kuwakamata watu watatu washukiwa wa tukio hilo akiwemo baba mzazi wa mtoto huyo.


Kamanda Daniel amesema katika uchuguzi wanaoendelea nao bado ni mapema kusema tukio hilo la kupora mtoto mwenye Ualbino limehusisha  imani za kishirikina na bado hakuna mwananchi yeyote ambaye amethibitisha hilo.


Jeshi la polisi mkoa Kagera linatoa wito kwa wananchi  kushirikiana na polisi kata kufanya msako  kwa ajili ya kumpata mtoto huyo na kutoa taarifa za uhalifu unaotokea kwenye maeneo yao.


No comments:

Post a Comment