Tuesday, June 18, 2024

CTI YASEMA BAJETI ITASISIMUA UKUAJI WA VIWANDA


 Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda nchini (CTI), limepongeza bajeti kuu ya serikali kwa kuweka mambo muhimu ambayo yatachochea ukuaji wa viwanda nchini.


 


Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga, wakati akizungumza na waandishi wa habari.


 


Amesema serikali imekuwa sikivu kwa wenye viwanda na kila wanapokuwa na jambo wamekuwa wakifunguliwa milango ya majadiliano na kwamba hakuna jambo la wenye viwanda ambalo linakwama.


 


Amesema wenye viwanda wamefurahia sana bajeti ya serikali kwa kuzingatia uendelezaji wa miradi ya kimkakati kama reli ya kisasa SGR ambayo alisema itasiadia kwa kiwango kikubwa kukuza viwanda vya  ndani kuzalisha kwa wingi bidhaa.


 


Amesema miradi kama SGR inasaidia kukuza uchumi kwani viwanda vitazalisha kwa wingi na bidhaa kusafirishwa kwa urahisi tofauti na sasa ambapo usafirishaji umekuwa ukisababisha bei kupanda.


 


“Nchi ambayo iko makini inaendeleza miradi mikubwa kama ya ujenzi wa reli, barabara, miradi ya maji kama kuendeleza miradi ya kimkakati barabara maji, bandari kwasabbau huwezi kuendeleza viwanda kama huna umeme au unamatatizo ya usafirishaji,” alisema tenga


“Mfano bei ya mfuko wa saruji hapa Dar inaweza kuwa shilingi 16, 000 au 17,000 lakini bei ya kuubeba mpaka Mwanza ni kati y ash 10,000 hadi 12,000 kwa hiyo mtu ananunua mfuko wa saruji hapa kwa 16, 000 lakini mpaka kuufikisha Mwanza unauzwa shilingi 28,000,” alisema


“SGR itapunguza gharama ya usafirishaji na bei ya bidhaa itapungua sana na itasaidia sana viwanda vya ndani kukua na kuongeza mapato na ni vizuri serikali inapofanya vizuri sekta binafsi tuseme kwamba inafanya vizuri,” alisema.


Tenga alisema bajeti ya mwaka huu inakusudia kuhamasisha mapato ya ndani zaidi ikilinganishwa na bajeti ya 2023/24.


Amesema jambo muhimu katika bajeti ya mwaka huu ni Serikali kufanya mageuzi mbalimbali ya muundo wa kodi, ada, tozo na marekebisho ya sheria na kanuni ili kuboresha mazingira ya biashara.


 


Amesema marekebisho ambayo yamependekezwa kuhusiana na sekta ya viwanda ni katika ongezeko la thamani VAT, ushuru wa bidhaa, ada na tozo za wakala pamoja na ushuru wa forodha.


 


Tenga amesema baadhi ya hatua chanya ni pamoja na kuanzishwa kwa tozo ya maendeleo ya viwanda kwa bidhaa zinazotoka nje yenye lengo la kulinda viwanda vya ndani, kuchochea uwekezaji na kuongeza mauzo ya nje; kupunguza ada na tozo zinazotolewa na vyombo vya udhibiti ili kupunguza gharama za uzalishaji.


 


Amesema pia wamefurahishwa na kupunguzwa kwa ushuru wa forodha kwenye malighafi za viwandani na pembejeo za uzalishaji ili kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kutozwa ushuru wa VAT kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa pamba inayolimwa hapa nchini ili kuchochea uwekezaji katika viwanda vya nguo vya ndani.


 


Amesema hatua za kodi zilizopendekezwa hapo juu zinalenga kusaidia viwanda vya ndani katika kupunguza gharama za uzalishaji, kuhimiza matumizi ya vifaa vya ndani, kuongeza ushindani, na kukuza ukuaji wa uchumi.




 

No comments:

Post a Comment